Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 04 Januari 2015 21:29

Matibabu ya ugonjwa wa figo

Matibabu ya ugonjwa wa figo

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi chenu hiki cha Ijue Afya Yako. Wiki iliyopita tulieleza kwa urefu kuhusu ugonjwa wa figo na kufafanua jinsi mtu anavyoweza kuugua ugojwa huo. Wiki hii pamoja na mambo mengine tutaeleza jinsi ugonjwa huo unavyoweza kutibika. Basi msiondoke kando ya redio zenu ili muweze kufahamu namna ya kutibu ugonjwa huo. &&&&&&&&
Tulisema kwamba dalili ya kwanza ya kuugua ugonjwa wa figo ni kupungua kwa kiasi cha mkojo. Dalili nyingine ni maji kujaa mwilini, madini za mwili kuwa juu hasa ya potasiamu, asidi nyingi, na mgonjwa kujisikia au kuwa na matatizo katika moyo na anaweza pia kuwa na matatizo katika ubongo. Mgonjwa pia anaweza kukosa hamu ya kula chakula chochote na hali hiyo kumfanya au kusababisha adhoofike mwili. Nyongeza za dalili za mtu kuugua ugonjwa wa figo hasa kwa wale wagonjwa ambao hawagunduliki mapema ni kuvimba macho mara tu baada ya kuamka wakati wa asubuhi na uvimbe kupungua baadaye. Dalili kubwa nyingine ni mgonjwa kupungukiwa na damu mwilini.
Tiba ya figo
Mojawapo ya njia za matibabu ya figo ni kukisaidia kiungo hicho kufanya kazi kama kawaida kwa kutumia mashine za kitiba kunakojulikana kama dialysis. Dialysis ni usafishaji wa figo unaohusiana na utoaji wa maji yaliyojaa mwilini, uchafu, pia sumu zinazotokana na vyakula au dawa. Tiba ya 'dialysis' ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji kuipata, hutakiwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha huku akitakiwa kuipata tiba hiyo mara nyingine hata mara tatu kwa wiki. Kwa mfano nchini Tanzania mwenye matatizo ya figo huhitaji shilingi laki 3 kila wiki kwa ajili ya tiba hiyo ambayo hufanyika mara tatu hadi nne kwa mwezi. Mgonjwa akifikia hali inayohitajia matibabu haya, huhitaji huduma hii ya kusafishwa damu kwa mashine kwa umri wake wote, kama hatopandikizwa figo nyingine. Dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitajika kutoka kwenye damu, mchakato unaofanywa kwa mashine maalumu zinazounganishwa kwa mgonjwa baada ya figo kushindwa kufanya kazi. Hii ni kwa sababu ni lazima damu isafishwe na kuondolewa taka hizo zilizoingia kwenye mfumo wa damu kwani zikibakia huhatarisha maisha. Kwa kawaida figo hufanya kazi ya kuchuja uchafu katika mwili, lakini baadhi ya wakati figo hushindwa kufanya kazi yake hiyo muhimu kutokana na sababu mbalimbali tulizozizungumzia huko nyuma. Usafishaji wa figo hufanyiwa wagonjwa ambao figo zao zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na maradhi ambapo tiba hiyo huwa ni ya dharura. &&&&&&&&&&&
Wakati wa kufanyiwa tiba ya dialysis mgonjwa hutundikiwa mipira maalumu, huku kwenye mashine kukiwa na figo ya bandia ambayo kazi yake ni kupitisha damu, kuisafisha na kuirudisha mwilini. Kwenye mashine maalumu kunakuwepo na mipira kadhaa ikiwemo ya kupitishia damu kupeleka kwenye figo bandia inayofanya kazi kama ya mwilini, na mirija mingine ambayo ni mikubwa kiasi inayotumika kutoa maji yasiyohitajika mwilini na sumu, huku mingine ikitumika kurudisha damu safi mwilini. Mgonjwa hulala kitandani wakati wa kufanyiwa tiba hii kwa masaa manne, bila kuchomwa sindano ya usingizi, kwa kuwa dialysis haina maumivu makali. Vilevile mgonjwa hutobolewa eneo maalumu mwilini kwa ajili ya kupitishia mipira, kuna wanaotobolewa shingoni au mkononi kulingana na anavyotaka mgonjwa. Hata hivyo, tiba hii licha ya kuwa na gharama kubwa ambazo wagonjwa wengi huwa hawazimudu hasa katika nchi masikini, haina uhakika wa kupunguza tatizo kwa asilimia 100, bali kwa asilimia 40 hadi 50 pekee. Suala hili linasisitiza umuhimu wa kuzitunza vyema figo zetu na kujiepusha na mambo yanayosababisha figo kuharibika. Sio vibaya ukijua mpenzi msikiliza kuwa, mwili wa binadamu una uwezo wa kumudu kazi zake kwa kutumia figo moja tu, licha ya mwanadamu kuumbwa na figo mbili. Hii ndio sababu mtu huanza kuhisi matatizo ya figo pale inapokua figo zote mbili zimeshindwa kufanya kazi na kuharibika. Na pia ndio sababu watu wanaweza kusaidia wagonjwa figo moja na kubakia wakiishi kwa kutumia figo moja iliyobakia bila matatizo yoyote.
Tiba nyingine ya ugonjwa huu ni ya kupandikiza figo inayojulikana kitaalamu kama kidney transplant. Tiba hii hufanywa hasa kwa mgonjwa ambaye figo yake imekufa na haiwezi kufanya kazi kwa msaada wa dialysis ambapo hupandikizwa au kuitikwa figo ya mtu mwingine mwilini mwake. Tiba hii ya figo ina gharama kubwa sana na ni ngumu kufanyika hasa kwa kuzingatia kuwa figo inayotakiwa kupandikizwa mgonjwa hutoka kwa mtu mwingine. Pia ni vigumu kupatikana mtu atakayejitolea figo yake na abakiwe na figo moja, na hata akipatikana baadhi ya wakati huwa hailingani au haiendani na figo ya mgonjwa suala ambalo hupekekea kufanyika tiba hiyo kuwa kugumu na mafanikio yake kuwa madogo. Pia tiba hiyo huwa na madhara kiafya hasa kwa walio kwenye hatua ya tano ya tiba hiyo. Madhara hayo ni pamoja na maradhi ya moyo, miguu kukaza na maumivu ya kifua. &&&&&&&
Wapenzi wasikilizaji, miongoni mwa sababu zinazodhuru figo baadhi huweza kuepukika. Miongoni mwa mambo yanayosababisha figo kuharibika ni ulevi, kuvuta sigara na matumizi holela ya dawa za maumivu. Kwa ajili hiyo jamii inashauriwa kuepuka kunywa pombe, kuvuta sigara na kutumia hovyo dawa za maumivu. Pia tunashauriwa kufanya uchunguzi wa miili yetu mara kwa mara au kwa ibara ya kitaalamu check-up, na pale tunapobaini figo zetu zimeanza kuathirika basi tuanze matibabu mapema na kuzuia kuharibika kabisa viungo hivyo muhimu mwilini. Pia tunashauriwa tuonapoona dalili tulizozitaja kuhusiana na ugonjwa wa figo basi haraka twende hospitali au tukamuone daktari. &&&&&&&&&&&&&&&&&
Tunakiendeleza kipindi chetu kwa kutoa ushauri wa lishe na ulaji kwa watu mwenye ugonjwa wa figo. Ulaji wa mtu mwenye ugonjwa huu unapaswa kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa kwani figo huwa haziwezi tena kutoa mabaki ya protini, maji, chumvi na potassium kwa urahisi vinapozidi mwilini. Vyakula vyenye chumvi na potassium nyingi viepukwe ikiwa ni pamoja na kuzingatia mambo yafuatayo:
Kupunguza kiasi cha nishati-lishe au calories. Kiasi cha nishati-lishe na protini kinapozidi mwilini huzipatia figo ambazo zimeathirika kazi kubwa. Pia kupunguza kiasi cha vinywaji au vimiminika, ili kupunguza kujaa kwa maji mwilini ambako husababishwa na kushindwa kwa figo kutoa maji mwilini. Maji yakizidi mwilini husababisha kushindwa kupumua, shinikizo kubwa la damu, kuvimba mwili na huweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi.
Pia mtu mwenye matatizo ya figo anapaswa kupunguza kiasi cha sodium au chumvi anayokula. Kiasi cha maji mwilini hudhibitiwa na sodium na pale madini hiyo inapozidi mwilini husababisha maji kubakia mwilini. Hali hii huweza kusababisha ongezeko la uzito ghafla, kuvimba kwa viungo vya mwili, shinikizo kubwa la damu, kushindwa kupumua na hatimaye kusababisha ugonjwa wa moyo. Vyakula vyenye sodium kwa wingi ni vyakula vilivyosindikiwa kwa chumvi kama nyama, samaki na soseji za makopo. Mgonjwa anapaswa kujenga tabia ya kutoongeza chumvi kwenye chakula wakati wa kula. Vilevile anapaswa kupunguza kiasi cha potassium katika mlo wake. Madini ya potassium yanapozidi mwilini husababisha misuli kuwa dhaifu na mapigo ya moyo kubadilika na yakizidi sana huweza kusababisha kifo cha ghafla. Ni muhimu kudhibiti kiasi cha potassium kwa ukaribu. Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maparachichi, ndizi mbivu, maboga, machungwa, peach, peasi, matunda yaliyokaushwa na maharagwe. Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kidogo ni pamoja na zabibu, machenza, mahindi mabichi, cauliflower, na matango. Unaweza kupunguza kiasi cha potassium kwenye chakula kwa kuchemsha na kumwaga maji ya ziada.
Pia mgonjwa wa figo anapaswa kupunguza kiasi cha phosphorus. Uwiano wa calcium na phosphorus mwilini ni muhimu kuwezesha afya njema ya mifupa, misuli na neva. Phosphorus inapozidi mwilini mifupa huwa myepesi na rahisi kuvunjika suala linatokana na mwili kushindwa kuhifadhi na kuitoa calcium kwenye mifupa. Vyakula ambavyo vina phosphorus kwa wingi ni pamoja na maziwa na vyakula vya jamii ya maziwa, nyama, shellfish, vyakula ambavyo havijakobolewa, maharage, karanga, korosho na chokoleti. Wagonjwa wa figo pia huhitaji vitamini na madini ya nyongeza kutokana na kutokula aina mbalimbali za vyakula na hivyo kuweza kusababisha upungufu wa baadhi ya virutubishi. Damu inapochujwa kwa njia ya dialysis pia huondoa vitamini kwenye damu kwa hivyo vitamin hizo ambazo ni dharura kwa mwili hupaswa kufidiwa kwa kula virutubishi vya nyongeza au supplements. Virutubishi vya nyongeza vinapaswa kutolewa kwa mgonjwa wa figo baada ya ushauri wa daktari. &&&&&&&&&

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …