Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 17 Disemba 2014 15:01

Jinsi ya Kujikinga na Madhara ya Jua

Jinsi ya Kujikinga na Madhara ya Jua

Assalam Aleykum wasikilizaji wapenzi na karibuni katika kipindi kingine cha Ijuwe Afya Yako. Wiki hii kama tulivyoahidi katika kipindi chetu kilichopita tutazungumzia jinsi ya kujikinga na madhara ya jua na pia namna ya kutunza ngozi kwa ujumla. Tafadhalini msiondoke kando ya redio zenu hadi mwisho wa kipindi.

&&&&&&

Kama tulivyosema katika kipindi kilichopita sababu kuu ya saratani ya ngozi ni miale ya jua. Kwa ajili hiyo ni muhimu kujifunza tangu utotoni kuhusu kujikinga na madhara ya kupigwa na jua. Kwa mujibu wa Taasisi ya Kansa ya Ngozi, watu wengi hupigwa na asilimia 80 hivi ya kiasi cha jua wanachohitaji maishani kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Kuunguzwa sana na jua na kupatwa na malengelenge mara moja tu utotoni, huzidisha maradufu uwezekano wa kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi baadaye maishani. Hii ni kwa sababu kansa ya ngozi inaweza kuchukua miaka 20 au zaidi kujitokeza. Australia ina kiwango cha juu cha kesi za ugonjwa wa kansa ya ngozi, hasa ile inayoathiri chembe za ndani ya ngozi. Hii ni kwa sababu, wakazi wengi wa nchi hiyo ambao walihama kutoka Ulaya Kaskazini wana ngozi yenye rangi hafifu, na wengi wao huishi kwenye pwani na fuo zenye jua. Uchunguzi waliofanyiwa wahamiaji hao unadokeza kwamba, wale wanaohamia Australia wakiwa wachanga hukabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kansa inayoathiri chembe za ngozi za ndani, jambo linaloonesha umuhimu wa kujifunza tangu utotoni kuhusu madhara ya kupigwa na jua. Serikali ya Australia imeanzisha kampeni kali ya kuwafunza watu kuhusu hatari za jua kwa kuwasihi wavae nguo ndefu, kofia na kujipaka losheni ya kujikinga na jua. Mabadiliko hayo madogo katika mtindo wa maisha yamekuwa na matokeo makubwa katika kuzuia kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi kati ya vijana nchini humo.
Losheni ya kujikinga na jua inayofaa ni ile inayoweza kukinga miale ya mnururisho ya UVA na UVB. Ni muhimu kujipaka losheni hiyo hata siku zenye mawingu mengi, kwa kuwa asilimia 85 ya mnururisho wa miale ya jua inaweza kupenya mawingu na vilevile maji. Baadhi ya wataalamu wanapendekeza losheni ya kujikinga na jua yenye kinga (SPF) ya angalau namba 15. Ili kujua losheni hiyo inaweza kukukinga kwa kiasi gani, hesabu dakika ambazo kwa kawaida wewe huchukua kukaa juani kisha uzizidishe kwa 15. Mtu anapaswa kujipaka losheni hiyo angalau baada ya kila masaa matatu, kwa kuwa kufanya hivyo hakuzidishia maradufu muda ambao utakuwa umekingwa na jua.
Isitoshe, kitabu cha The Skin Cancer Answer kinaonya kwamba, hupaswi kufikiri kwamba uko salama eti kwa sababu tu unatumia losheni ya kujikinga na jua. Hakuna losheni ya kujikinga na jua inayoweza kuzuia kikamilifu kuunguzwa na jua, wala kuzuia kansa ya ngozi. Kwa hakika, kutumia losheni kama hizo kunaweza kuongeza uwezekano wa kupatwa na kansa ya ngozi kwa njia isiyo ya moja kwa moja, ikiwa kuzitumia kutamfanya mtu akae muda mrefu zaidi kwenye jua. Kitabu hicho kinasema, njia pekee ya kujikinga ni kufuata maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na madhara ya kupigwa na jua. Imeonekana kuwa, kuvaa mavazi ya kujikinga na miale ya jua na kukaa ndani ya nyumba wakati jua linapokuwa kali, ni miongoni mwa mbinu zenye faida za kujikinga na kansa ya ngozi. Vilevile ili kujiepusha na madhara ya miale ya jua tunashauriwa tusikae kwenye jua sana hasa kati ya saa 4 asubuhi na saa 10 jioni, wakati kuna mnururisho mwingi wa miale hatari ya jua. Pia tunashauriwa kuchunguza ngozi zetu kuanzia unyayo hadi utosini angalau mara moja kila miezi mitatu. Unapokuwa nje, unashauriwa kutumia losheni ya kujikinga na jua yenye kinga (SPF) namba 15 au zaidi. Jipake losheni nyingi dakika 30 kabla ya kujianika juani na baada ya kila saa mbili. Watoto walio chini ya umri wa miezi sita hawapaswi kupakwa losheni ya kujikinga na jua. Tunashauriwa kuwafunza watoto pia jinsi ya kujikinga na jua wakiwa wangali wadogo, kwa kuwa madhara ambayo husababisha kansa ya ngozi kwa watu wazima huanzia utotoni. Kuvaa nguo za kujikinga kama vile suruali ndefu, shati zenye mikono mirefu, kofia pana, na miwani inayoweza kuzuia miale ya jua husaidia sana kuikinga ngozi na madhara ya jua.

&&&&&&&&&&

 

Namna ya kutunza ngozi wakati wa uzeeni

Umri ni kigezo kikubwa kinachoweza kusababisha mabadiliko katika ngozi. Mabadiliko makubwa zaidi huonekana wakati wa kuelekea uzeeni, kuanzia miaka 40 na kuendelea. Katika kipindi hiki mabadiliko makubwa yanaweza kuonekana ikiwa ni pamoja na ngozi kukunjamana na hata kupoteza mng'ao wake wa asili uliokuwapo wakati wa ujana. Vilevile ngozi huwa kavu na kupauka mno. Endapo tutaanza kuona hali hiyo, tunapaswa kuepuka kupambana nayo kwa kutumia vipodozi vyenye kemikali. Ingawa ni vigumu kukabiliana na hali ya uzee, lakini tunaweza kuzifanya ngozi zetu kuwa na muonekano mzuri, licha ya kuwa na umri mkubwa. Zifuatazo ni dondoo tunazoshauriwa kufuata ili kuhakikisha ngozi zetu zinabaki na mvuto licha ya uzee au kukaribia hali ya uzeeni. Kwanza tunapaswa kuzingatia mlo kamili kwa kula zaidi matunda, mboga za majani, maziwa na maji walau lita 3 kwa siku. Pia tunashauriwa kuepusha ngozi zetu za uso kupigwa na mionzi ya jua mara kwa mara, kwani hilo huchangia kwa kiasi kikubwa kudhoofika ngozi na hatimaye kukunjamana. Katika kipindi hiki, pia tunashauriwa kuepuka kutumia vipodozi bila kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa masuala ya ngozi, kwani wao ndio wanaoweza kushauri aina gani ya vipodozi inayoweza kuwa salama kwa ngozi. Vilevile tunashauriwa kutotumia losheni zilizo na kemikali au kavu kupita kiasi kwani wakati wa uzee ngozi huwa kavu. Ni bora kupaka losheni itakayokuwa na mafuta yatakayolainisha na kung'arisha ngozi.

&&&&&&

Kuchomeka kwa miale ya jua

Pengine wengine huona ni raha kuota jua, lakini unaweza kuunguza ngozi au kupata saratani ya ngozi kutokana na suala hilo. Kwa ajili hiyo tunashauriwa kila mara tuzikinge ngozi zetu na madhara ya jua kwa kupaka losheni yenye SPF 15 au zaidi pale tunapokuwa nje, hata wakati wa baridi au kukiwa na mawingu. Ni bora kujiepusha kuota jua sana kati ya saa 4 hadi saa 10 mchana, kwani wakati huu miale ya jua huwa mikali na ni rahisi kuunguza ngozi. Iwapo utachomwa kwa miale ya jua, unaweza kujitibu nyumbani kwa njia zifuatazo. Baada ya kuoga jipake mafuta ya aloe-vera, yanasaidia kuponya. Ukihisi maumivu, meza aspirini au dawa nyingine za kuondoa maumivu na jipake mafuta yaliyo na benzini, (benzolaine) camphor, au menthol. Tazama kiambato kwenye mafuta au uliza mfamasia akusaidie kutambua mafuta yenye mada hizo. Pia weka pamba au kitambaa chenye unyevu ulipoungua na funika sehemu iliyoungua kwa kitambaa unapokwenda nje.
Unashauriwa kumuona daktari kwa majeraha mabaya ya miale ya jua iwapo utaona dalili zifuatazo. Iwapo unahisi kichefuchefu, kizunguzungu na homa. Kama una malengelenge yaliyosababishwa na jua, vipele au ngozi ikigeuka rangi na kuwa zambarau na iwapo majeraha yatatapakaa kote mwilini siku moja baada ya kuunguzwa na jua.
Mpenzi msikilizaji, tunaweza kusema kuwa ngozi yako ni kama "Ukuta wa Jiji". Hii ni kwa sababu wakazi wa miji ya zamani walijenga kuta ili kuzuia uvamizi. Ukuta wa jiji ulikuwa ngome ya kuzuia adui na kulinda jiji. Mwili wako vilevile una "ukuta" ambayo ni ngozi yako ambayo unapaswa kuitunza vizuri ili ikulinde ipasavyo. Lakini je, ngozi yako hukulindaje? Sehemu ya juu ya ngozi ina bakteria na vijiumbe tofauti, na vingine vinaweza kusababisha maambukizo na magonjwa pale inapopatikana fursa kama vile kudhoofika kinga ya mwili. Ngozi yako si kinga tu bali pia ndani yake kuna protini zinazolinda mwili kwa kuua vijidudu. Baadhi ya protini hizo hufanya kazi daima na nyingine hujitokeza pale ngozi inapojeruhiwa au kudhurika. Aina mbili za protini ambazo huua vijidudu katika ngozi zinaitwa defensin na cathelicidin, na huwa tayari kulinda mwili nyakati zote. Protini hizo hutokeza katika chembe zilizo kwenye tabaka la juu la ngozi wakati ngozi inapojeruhiwa au kuvimba. Protini hizo huangamiza vijidudu haribifu kwa ngozi kwa kuvitoboa.

&&&&&&

Tutaishia hapa kwa leo lakini usikose kutegea sikio kipindi chetu kijacho, ambapo pamoja na mambo mengine tutazungumzia vyakula vinavyosaidia kulinda na kuimarisha ngozi. Hadi wakati huo, tuzilinde afya zetu.

&&&&&&&&&

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …