Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 03 Disemba 2014 16:17

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ukimwi

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ukimwi

Assalam aleykum wapenzi wasikilizaji popoto pale mlipo. Tarehe Mosi Disemba ni Siku ya Kimataifa ya Ukimwi ambayo huadhimishwa duniani kote ili mbali na kuwaunga mkono wanaoishi na virusi vya HIV, walimwengu waweze kuhamasishwa ili wachukue hatua zaidi za kukabiliana na ugonjwa huo hatari ambao bdo unaua mamilioni ya watu duniani. Kwa mnasaba huo tumewaandalia kipindi maalumu ili kuzungumzia ripoti mbalimbali kuhusiana na ugonjwa huo, mafanikio yaliyopatikana na pia mikakati iliyowekwa kwa ajili ya kukabiliana na Ukimwi.

&&&&&&&&&

Sote tunafahamu kuwa ugonjwa wa Ukimwi unawaumiza vichwa wataalamu wa tiba na madaktari duniani kote, kwani bado haujapatiwa dawa mujarabu wala tiba ya uhakika na umeendelea kusababisha mamilioni ya watu wapoteze maisha huku wagonjwa wengi wakisumbuliwa na maumivu na matatizo mbalimbali yanayosababishwa na maradhi hayo. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) katika Siku ya Kimataifa ya maadhimisho ya Ukimwi Disemba Mosi, watu milioni 35 walikuwa wakiishi na virusi vya HIV mwaka 2013 duniani kote. Kulikuwa na maambukizo mapya ya virusi vya HIV kwa watu milioni 2.1 huku wengine milioni 1.5 wakiwa wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ukimwi. Hii ni katika hali ambayo bara la Afrika bado linaongoza kwa kuwa na waathirika wengi zaidi wa ugonjwa huo hasa katika nchi za chini ya Jangwa la Sahara. Lakini kundi linaloongoza kampeni dhidi ya HIV la ONE campaign limesema kuwa, dunia hatimaye imeanza kuhitimisha mfumuko wa Ukimwi ambao umewaathiri na kuua mamilioni ya watu katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Imeonekana kuwa idadi ya kesi mpya za watu walioambukizwa virusi vya HIV mwaka uliopita ilikuwa ndogo kuliko watu waliokuwa tayari na ugonjwa huo wanaopatiwa matibabu ya kurefusha maisha. Hata hivyo imetahadharishwa kuwa, hali hiyo haimaanishi kuwa Ukimwi utatokomezwa hivi karibuni.
Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Ukimwi yamefanyika huku miito mbalimbali ikitolewa kwa ajili ya kutoa elimu na maarifa zaidi hasa kwa rika la vijana kuhusiana na maradhi ya Ukimwi na kusisitizwa kuwa, bado dawa ya kutibu maradhi hayo haijapatikana. Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetoa wito wa kuweko uwekezaji zaidi katika kuwakinga na kuwatibu watoto. UNICEF imesema kuwa, inakadiriwa kupungua maambukizo ya watoto milioni 1.1 walio na umri wa hadi miaka 15, lakini kwamba kutotolewa tiba ipasavyo kunazuia jitihada zinazofanywa ili kufikia malengo ya dunia ya kupunguza maambukizo mapya kwa watoto kwa asilimia 90 duniani kote ifikapo mwaka 2015. Shirika hilo aidha limesema kuwa, maambukizo mapya ya virusi vya HIV kwa watoto yalipungua kwa zaidi ya asilimia 50 kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2012, kutokana na kupanuliwa mkakati wa kuwawezesha mamilioni ya mama wajawazito wanaoishi na virusi vya Ukimwi kupata huduma za kuzuia wasiwaambukize watoto wao ugonjwa huo. Mfuko wa Kuwahudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, malengo ya dunia ya kupunguza maambukizo ya HIV kwa watoto kwa asilimia 90 bado hayajafikiwa. Ukweli ni kuwa, mwaka 2013 ni asilimia 67 tu ya mama wajawazito wanaoishi na virusi vya HIV katika nchi zenye kipato cha kati na cha chini ndio waliopata huduma na dawa za kuongeza umri ili kuzuia watoto wao wasiambukizwe Ukimwi.
Miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya HIV katika nchi zinazoendelea, watu wazima ndio wanaoweza kupata zaidi dawa za kurefusha umri za Ukimwi kuliko watoto. Mwaka 2013, asilimia 37 ya vijana wenye umri wa miaka 15 na zaidi walipata matibabu ikilinganishwa na asilimia 35 ya watoto waliokuwa na umri wa chini ya miaka 14. Maambukizi mapya ya virusi vya HIV miongoni mwa watoto yalipungua zaidi kati ya mwaka 2009 na 2013 katika nchi 8 za Afrika. Nchi hizo ni Malawi, Ethiopia, Zimbabwe, Botswana, Namibia, Msumbiji, Afrika Kusini na Ghana.
UNICEF imesisitiza kuwa, vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana pia ni jambo la kuzingatiwa. Katika hali ambayo vifo vinavyotokana na magonjwa yanayosababishwa na Ukimwi vilipungua katika makundi yote kwa karibu asilimia 40 kati ya mwaka 2005 na 2013, vifo viliongezeka tu kwenye kundi la vijana waliokuwa na umri wa miaka 10 hadi 19.

&&&&&&&&&&&

Miongoni mwa tafiti zilizotangazwa hivi karibuni kuhusiana na ugonjwa wa Ukimwi ni ule unaotujuza kuwa, dawa za kurefusha umri za ugonjwa huo za ARV zinaweza kuzuia pia upofu. Utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Marekani cha Kentucky umeonesha kuwa, dawa za kuongeza umri zinaotumiwa na waathirika wa Ukimwi zinaweza kuzimua protini mwilini na hivyo kuzuia seli zisizeeke na hivyo kuzuia upofu. Wataalamu wa macho katika utafiti huo wamesema kuwa, wanapanga kufanya majaribio ya kitiba katika miezi ijayo na kwamba inahitajika kwa uchache miaka miwili hadi mitatu ili kutambua iwapo dawa hizo zinaweza kweli kutibu kuzorota utendaji wa seli kunakosababisha wazee kupoteza uwezo wa kuona. Uchunguzi mwingine kuhusiana na Ukimwi uliotangazwa hivi karibuni ni ule unaohusiana na dawa za kuzuia Ukimwi zinazotumiwa na mama wajawazito wenye virusi vya HIV. Utafiti unatujuza kuwa, dawa hizo zinaweza kusababisha matatizo ya muda mrefu ya mioyo ya watoto ambao mama zao walitumia dawa hizo walipokuwa tumboni.
Uchunguzi huo uliofanywa na Kituo cha Tiba cha Detroit umebainisha matatizo muhimu katika misuli na utendaji wa mioyo ya watoto ambao hawana Ukimwi, lakini mama zao walitumia dawa za kuzuia ugonjwa huo wakati watoto hao walipokuwa tumboni. Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliochapishwa katika jarida la AIDS, wataalamu walichunguza ukuaji na utendaji wa muda mrefu wa mioyo ya watoto 412. Waalioshiriki walikuwa ni watoto ambao hawakuathirika kutoka kwa mama zao waliokuwa na virusi vya HIV waliozaliwa kati ya mwaka 2007 hadi 2012. Uchunguzi huo umeonesha kuwa, kuna uhusiano kati ya kuzorota utendaji a misuli ya moyo na uwezo wa kusukuma damu katika watoto waliozaliwa na mama ambao wana virusi vya Ukimwi, waliotumia dawa za kuzuia watoto wao wasipatwe na virusi vya HIV walipokuwa wajawazito.
Ingawa dawa za kuzuia Ukimwi zimekuwa na nafasi kubwa katika kupunguza maambukizo ya virusi vya HIV kwa watoto kutoka kwa mama wakati wa ujauzito, timu ya wachunguzi imesisitiza kuwa, utafiti zaidi unapaswa kufanywa kuhusiana na athari ya muda mrefu ya dawa hizo kwa siha ya mioyo ya watoto. Hata hivyo, mpango wa kuzuia mama wasiwaambukize watoto wao Ukimwi unaojulikana kama PMTCT umekuwa na mafanikio makubwa kuhusiana na ugonjwa huo.
Kupima mara kwa mara virusi vya HIV, kuzingatia matibabu kwa wale walioathirika na pia kufuatilia na kuangaliwa vyema watoto wanaoishi na virusi vya Ukwimi kunaweza kusaidia watoto waathirika kuishi muda mrefu bila kuwa na matatizo ya kiafya.

&&&&&&&&

Wapenzi wasikilizaji si vibaya tukikumbusha kuwa, ugonjwa wa Ukimwi husababishwa na virusi vya HIV, ambavyo hushambulia bila huruma mfumo wa kulinda mwili na kuudhoofisha kiasi kwamba, maisha ya muathirika huwa hatarini hata kwa kupatwa na maradhi madogo madogo ya kawaida. Virusi vya HIV vina uwezo mkubwa wa kusababisha maambukizo ya kasi na kwa watu wengi katika jamii. Hii ni kwa sababu, tangu virusi hivyo vinapoingia katika mwili wa muathirika, inaweza kupita miaka mingi kabla ya mwili kuonyesha dalili za ugonjwa, na katika kipindi hicho mtu aliyeathirika huweza kuwaambukiza wenzake virusi hivyo bila kujua. Kwa ajili hiyo watu wote katika jamii wanashauriwa kupima afya zao mara kwa mara na kuhakikisha kuwa hawana ugonjwa huo unaoweza kukaa kimya mwilini bila muathirika kujua kwa muda mrefu. Pia pale inapojulikana kuwa mtu ameathirika inashauriwa kwenda hospitalini na kuanza tiba haraka kwa kutumia vidonge vya kurefusha maisha vya wagonjwa wa Ukimwi venye uwezo wa kukabiliana na makali ya virusi vya HIV na kuvizuia visizidi kushambulia mfumo wa kulinda mwili.
Ingawa kuna baadhi ya taarifa zenye kutia moyo kuhusiana na kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi, lakini hatupaswi kulegeza nguvu zetu katika mapambano dhidi ya gonjwa hilo hatari. Ni wazi kuwa bado tuna safari ndefu hadi kuweza kufanikiwa kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Ukimwi na pia kuhitimisha ubaguzi katika kutoa matibabu, kuwangalia na kuwasaidia wagonjwa wa Ukimwi. Serikali zote na taasisi za kimataifa zinapaswa kushirikiana haraka iwezekanavyo ili kuweza kuung'oa ugonjwa wa Ukimwi na kusaidia kuwaokoa walimwengu na ugonjwa huo hatari.
Na kufikia hapo hatuna la ziada. Ni matumaini yetu kwamba mmefaidika vya kutosha na daima tukumbuke kuwa, kinga ni bora kuliko tiba basi tuchukue tahadhari kwani UKIMWI UNAUA!

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …