Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 03 Disemba 2014 10:12

Saratani ya Ngozi (Melanoma)

Saratani ya Ngozi (Melanoma)

Ahlan wa Sahlan wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine cha Ijuwe Afya Yako. Kama mnakumbuka wiki iliyopita tulianza kujadili magonjwa yanayoshambulia ngozi ambapo tulizungumzia juu ya ugonjwa wa mba na pia matibabu yake. Wiki hii katika muendelezo wa kuzungumzia magonjwa yanayoathiri ngozi tutajadili ugonjwa wa saratani ya ngozi.

&&&&&&&&&&

Kansa ya Ngozi Ni Tatizo Kubwa Leo

Jarida la The Merck Manual limeeleza kwamba kansa ya ngozi ndiyo kansa inayopata watu wengi zaidi ulimwenguni. Nchini Marekani, mtu mmoja kati ya kila watu 6 hadi 7 hupatwa na aina fulani ya kansa ya ngozi. Lakini idadi ya watu wanaopatwa na kansa hiyo inaongezeka. Katika kitabu The Skin Cancer Answer, Dakta I William Lane anasema: "Sasa inakadiriwa kwamba asilimia 50 ya watu ambao hufikisha umri wa miaka 65 hupatwa na aina fulani ya kansa ya ngozi." Kulingana na Taasisi ya Magonjwa ya Ngozi ya Marekani, kansa ya ngozi inayoathiri chembe za ndani za ngozi husababisha vifo 7,500 hivi kila mwaka nchini humo na idadi hiyo inazidi kuongezeka. Si rahisi kwa watu wenye ngozi nyeusi kupatwa na kansa ya ngozi, lakini wao pia wamo hatarini.
Kwa nini kansa ya ngozi imeenea hivyo? Ingawa huenda ikasababishwa na mambo mengi kama vile mwinuko kutoka usawa wa bahari, latitudo, kiasi cha mawingu, na hali ya tabaka la ozoni, lakini huenda kisababishi kikuu kikawa ni kupigwa na jua kwa muda mrefu. Mitindo ya maisha nayo imebadilika. Imekuwa rahisi kwa watu wengi wanaofanya kazi maofisini kwenda likizo kwenye fuo na kufurahia tafrija kama vile kupanda milima na kuteleza kwenye barafu bila kuzingatia ni kiasi gani ngozi zao zinaathirika na miale ya jua. Mitindo ya mavazi pia imebadilika. Ingawa zamani wanaume na wanawake walikuwa wakivaa nguo ndefu za kuogelea, siku hizi nguo za kuogelea hazifuniki sehemu kubwa ya mwili. Kwa sababu hiyo kansa ya ngozi imeongezeka. Huenda hii ndiyo sababu watu wanaoishi majangwani kama vile Wabedui wanatambua athari mbaya za jambo hilo na kuamua kuvalia kanzu ndefu na vilemba.
Melanoma ni aina ya saratani inayoshambulia ngozi ambayo ingawa hutokea mara chache sana ikilinganshwa na saratani nyinginezo lakini ni hatari sana ikiwa haitogunduliwa mapema. Saratani ya ngozi husababisha vifo kwa asilimia 75 ya watu wanaoathirika, na mwaka 2012 ilisababisha vifo vya watu 55,000 kati ya watu laki mbili na 32 elfu waliopatwa na ugonjwa huo duniani kote. Nchi za Australi na New Zealand zinaripotiwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaopatwa na ugonjwa huu wa saratani ya ngozi na kwa miaka 20 iliyopita imeshuhudiwa sana kwenye meneo hayo ambayo wakaazi wake wengi ni wenye asili ya Caucasian. Melanoma ni aina ya kansa ya ngozi ambayo hutokea katika seli zenye rangi katika ngozi zinazojulikana kama melanocytes. Kwa wanawake mara nyingi saratani hii hutokea katika miguu ambapo wanaume hupatwa zaidi eneo la mgongoni. Lakini ili kuelewa vyema saratani hii kwanza tueleze muonekano wa kawaida wa ngozi na pia kazi yake. Ngozi ni sehemu muhimu sana mwilini. Ngozi ya mwanamume ina urefu wa meta mraba 1.8 na ile ya mwanamke ina urefu wa meta mraba 1.6. Ina vipokezi ambavyo hufanya mtu ahisi uchungu, mguso, na halijoto. Ndicho kiungo cha kwanza kukinga mwili hasa dhidi ya joto, baridi, majeraha, na vilevile sumu, kemikali, na vichafuzi. Hata hivyo, ngozi inaweza kudhuriwa na jua. Ngozi ina kazi nyingi kama vile, kufunika vifaa vingine vyote vilivyo ndani ya mwili na kusaidia kuvilinda visidhurike. Ngozi ni kizuizi cha vijidudu kama vile bakteria na pia huzuia mwili kupoteza maji sana na vimiminika vinginevyo. Vilevile husaidia kudhibiti joto la mwili, kuzuia mwili usidhurike na miale hatari ya jua na kusaidia mwili utengeneze vitamin D. Ngozi ina sehemu kadhaa lakini Melanoma ni kansa inayoanzia katika seli za melanocytes. Jina lingine la saratani hii ni malignant melanoma na cutaneous melanoma. Kwa kuwa seli nyingi za melanoma hutengeneza melanin, uvimbe wa melanoma kwa kawaida huwa na rangi ya kahawia au nyeusi lakini kwa seli zile ambazo hazitengenezi melanini tezi hizo hugeuka na kuwa pinki au kwa jina jingine rangi ya waridi, zilizoungua na hata nyeupe.

&&&&&&

Melanoma ni saratani hatari sana kwa maisha ya mwanadamu. Saratani hii huwapata watu wachache lakini inapotokea mtu akapata saratani hii basi maisha yake huwa hatarini. Saratani hii si rahisi kugundulika ikilinganishwa na saratani nyingine za ngozi. Siyo tu kwamba saratani hii ni ngumu kidogo kutambulika bali pia husambaa haraka zaidi kuliko saratani nyingine za ngozi. Melanoma huweza kusambaa na kushambulia viungo vingine zaidi ya ngozi kama mifupa na ubongo. Inapofikia hatua hii saratani hii huwa ngumu sana kutibika.
Ni nani wanaoweza kupata kansa ya ngozi? Mbali na watu ambao wamewahi kupigwa na jua kwa muda mrefu sana, au wale wanaojianika juani kwa vipindi virefu, wale walio na ngozi nyeupe, nywele na macho ya rangi hafifu, wenye mabaka na madoadoa, na wale ambao mtu fulani katika familia yao amekuwa na ugonjwa huo, wanaweza kuupata. Watu weupe hupatwa na kansa ya ngozi zaidi kuliko watu weusi. Lakini je, hii inamaanisha kwamba kadiri ngozi yako inavyounguzwa na jua na kuwa nyeusi ndivyo inavyokuwa vigumu kupatwa na kansa ya ngozi? Sivyo, kwa sababu ingawa ngozi hujigeuza rangi na kuwa nyeusi ili kujikinga na mnururisho wa miale ya jua, lakini inapofanya hivyo huathirika, na inapoathirika mara nyingi huwa kuna uwezekano mkubwa wa kupata kansa ya ngozi.
Dalili za Melanoma
Kuna dalili nyingi za saratani hii na ni vyema kila mtu azifahamu. Dalili ya kwanza kabisa ambayo inabidi kila mtu aifahamu ni kubadilika kwa ukubwa, rangi au ule muundo wa ngozi ambayo umekuwa nayo kwa muda mrefu au umezaliwa nayo. Alama hii ni ile ambayo ina rangi nyeusi zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine ya ngozi. Mabadiliko haya si lazima yawe yanatokea haraka haraka yanaweza kuwa yanatokea taratibu katika kipindi cha miezi lakini cha muhimu zaidi ni kuonekana mabadiliko kwenye alama hiyo ya ngozi. Mabadiliko mengine ni kama yafuatayo, alama hiyo inayojitokeza kwenye ngozi inaweza kuwa inavimba, kingo zake kupoteza mzingo wake wa kawaida na alama kua zaidi kwa mfano kutoka mzingo wa milimita 4 na kuzidi milimeta 6. Dalili nyingine ni alama kuanza kuwasha na kama mgonjwa atachelewa kugundua tatizo basi zitajitokeza alama nyingine kwenye ngozi ambayo itapasuka na kuwa kidonda. Alama hiyo baadaye inaweza kutoa damu na kuwa na maumivu.
Kama matibabu hayatafanyika basi saratani hii ya ngozi husambaa na dalili zifuatazo kuonekana:- Tezi za mwili za kwenye makwapa na kwenye nyonga huvimba, mgonjwa kutokwa na uvimbe kwenye ngozi, kupoteza uzito kwa kasi bila kujua sababu, kupata kikohozi kisichoisha, kupoteza fahamu au kupata kifafa, na pia kuumwa na kichwa.

&&&&&&&&&&&

Hayo yote yakiwa ni tisa, kumi ni matibabu ya saratani hiyo. Ingawa Melanoma ni kansa hatari zaidi ya ngozi lakini inaweza kutibiwa na kupona iwapo itagundulika mapema. Uthibitisho wa kansa ya ngozi hufanywa kwa kipimo cha biopsy ya ngozi na baada ya hapo timu ya madaktari hujadili njia ya tiba iliyo bora zaidi kwa mgonjwa kulingana na jinsi ugonjwa ulipofikia na kusambaa na kwa kuzingatia mambo mengine kama umri na afya jumla ya mgonjwa. Aina ya kwanza ya kutibu saratani ya ngozi ni kuondoa tishu zilizoathirika, na njia inayotumika katika matibabu hayo ni kukata na kuondoa tezi za ngozi zilizoathirika. Kumepigwa hatua kubwa katika upasuaji wa aina hii katika miongo ya hivi karibuni, na tishu chache zaidi huondolewa ikilinganishwa na huko nyuma. Aina hii ya upasuaji huitwa resection na imeonekana kuwa wagonjwa huvumilia zaidi aina hii ya tiba na pia huacha makovu machache. Aina hii ya upasuaji pia huweza kufanywa katika ofisi ya daktari na kwa kutumia dawa ya kuzuia kuhisi maumivu mwili mzima. Kwa wagonjwa wenye kansa ya ngozi ambayo imesambaa katika maeneo mengine ya mwili, lymph nodes na viungo vinginevyo, matibabu mengine huweza kufanywa kama tiba ya mionzi (Radiotherapy) au dawa za kutibu saratani (Chemotherapy), tiba ya kuimarisha au kudhoofisha mfumo wa kinga ya mwili inayojulikana kama immunotheraphy na pia tiba ya molekuli. Aidha saratani ya ngozi aina ya melanoma huweza kutibiwa kwa dawa.
Na tunakomea hapa kwa leo wapenzi wasikilizaji. Ungana nasi tena wiki ijayo ambapo tutazungumzia jinsi ya kujikinga na madhara ya jua ili kuepusha kansa ya ngozi. Hadi wakati huo kwaherini.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …