Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 18 Oktoba 2014 06:23

Saratani ya shingo ya kizazi (Cervical Cancer)

Saratani ya shingo ya kizazi (Cervical Cancer)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine cha Ijue Afya Yako. Tutakiendeleza kipindi chetu kwa kuzungumzia matatizo na magonjwa ya wanawake hasa ugonjwa wa saratani. Kwa leo tutazungumzia ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ambao huwaathiri wanawake duniani kote.

&&&&&&&&&

Shingo ya kizazi au cervix ni njia ya kizazi kati ya uke na mji wa mimba. Sehemu hii ina kazi nyingi kukiwemo kupitisha mbegu za kiume kuelekea katika mirija ya uzazi ili kupevusha yai, kupitisha damu ya hedhi na pia ndio mlango anaopitia mtoto wakati wa kuzaliwa. Kama zilivyo sehemu zingine za mwili, sehemu hii nayo inaweza kupata maradhi ikiwemo kansa. Ugonjwa huu huwaathiri wanawake wengi wa rika zote walio katika umri wa kuzaa. Miaka ya nyuma kabla ya maambukizi ya Ukimwi kansa ya shingo ya kizazi ilikuwa ikiwapata zaidi wanawake wenye umri wa miaka 45 na kuendelea. Lakini miaka ya hivi karibuni mwanamke yeyote aliye katika umri wa kuzaa anaweza kupata tatizo hili. Saratani ya shingo ya kizazi ni mabadiliko ya chembe chembe hai zilizo juu au zinazofanana na shingo ya uzazi ambapo huchukua miaka mingi hadi kujitokeza kwake. Ugonjwa huu huchukua zaidi ya miaka 15 mpaka 20 kugundulika lakini kabla ya kujitokeza bayana hutokea mabadiliko kadhaa yanayoweza kugundulika mapema na kufanikiwa kuzuilika katika hatua za mwanzoni. Utafiti uliofanywa na timu ya wataalamu wa ugonjwa huo umebainisha mabadiliko ambayo hujitokeza kabla ya maradhi haya katika sehemu ya kizazi kabla ya kujitokeza saratani yanayoitwa kitaalamu Precancerous lesion. Mabadiko hayo yanaweza kuendelea na kujirudia na mwishowe kuwa ugonjwa. Hata hivyo yapo mambo ambayo yameonekana kusababisha ugonjwa huo kwa wanawake ambapo baada ya kufanyika uchunguzi duniani kote imebainika kuwa ugonjwa huo husababishwa na sababu tofauti. Uchunguzi huo uligundua kuwa saratani hiyo ya shingo ya kizazi husababishwa na kuanza ngono mapema katika umri mdogo chini ya miaka 18, kuwa na wapenzi wengi na kuvuta sigara. Pia miongoni mwa mambo yanayochangia kupata saratani ya shingo ya kizazi ni pamoja na historia ya kubeba mimba nyingi na unywaji pombe kupindukia huku watu walioathirika na virusi vya Ukimwi wakiwa katika hatari zaidi ya kupata maradhi hayo.

 

SABABU YA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

Ugonjwa huu husababishwa na virusi vinavyoitwa Human papilloma, ambapo mtu anaweza kupatwa na virusi hawa wakati wa kujamiana na mtu mwenye maambukizi. Human Papillomavirus aina ya 16 na 18 husababisha kansa ya aina hii kwa asilimia 75 duniani kote huku aina ya 31 na 35 zikisababisha maambukizi kwa asilimia 10. Watu walio katika hatari ya maambukizi ya ugonjwa huu ni kwa ujumla wanawake wote lakini zaidi wale wasiokwenda kufanyiwa uchunguzi wa kila mwaka kuhusiana na ugonjwa huu unaojulikana kitaalamu kama pap smear, wanawake walioathirika na virusi vya human papillomavirus HPV au genital warts, wanaovuta sigara, wenye ukimwi na wasiokula vyakula bora hasa wasiozingatia mboga na matunda katika lishe zao. Kutokana na uchunguzi huo, timu ya wataalamu wa ugonjwa huo imeeleza sababu zinazochangia kupata saratani ya shingo ya kizazi na kubainisha dalili ambazo huonekana kwa mtu ambaye anasumbuliwa na ugonjwa huo. Kimsingi mabadiliko ya awali ya saratani hii hayatoi dalili yoyote ya moja kwa moja hadi mwanamke afanyiwe uchunguzi au vipimo vingine vya ugonjwa huo. Dalili zinazoonesha kuwepo kwa saratani ya shingo ya kizazi ni pamoja na kutokwa na damu ambayo si ya hedhi, kutokwa na uchafu, majimaji au usaha sehemu za siri. Hata hivyo dalili nyingine ni pamoja na kuhisi maumivu makali wakati wa kujamiiana na kusababisha kutokwa na damu baada ya tendo hilo ambapo pia ni pamoja na maumivu ya tumbo chini ya kitovu sambamba na maumivu ya kiuno.
Kufanyiwa uchunguzi wa pap smear ili kubaini ugonjwa huu kuna nafasi kubwa katika kuzuia watu kupatwa na saratani ya shingo ya kizazi. Uchunguzi wa awali wa saratani ya shingo ya kizazi unatakiwa kufanyiwa wanawake walio katika mahusiano ya ndoa na pia wanatakiwa kupima mara kwa mara hadi wanapofikia umri wa miaka 69. Mwanzoni uchunguzi huu unatakiwa ufanyike mara kwa mara kwa muda wa miaka mitatu mfululizo. Ikitokea katika miaka mitatu mfululizo uchunguzi huo haujatoa dalili zozote za kuwepo saratani basi mwanamke anaweza kuendelea kufanyiwa uchunguzi mara moja kila baada ya miaka miwili na mitatu hadi pale atakapofikisha umri wa miaka 69.

&&&&&

Wapenzi wasikilizaji tunapaswa kujua kuwa, uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi ni rahisi na hauna maumivu yoyote tofauti na dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa huambatana na maumivu yanayotokana na uchunguzi huo na unaweza hufanyika katika chumba cha daktari au nesi mtaalamu kwa muda wa dakika chache tu. Pap-Smear ni kipimo ambacho hutumika kuchunguza mabadiliko ya chembe zilizopo katika mlango wa kizazi (cervix) ili kugundua mabadiliko yanayotokea katika chembe hizo mapema na hivyo kuyakabili mapema, kwani saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutibika iwapo itagundulika mapema. Kipimo hicho huangalia shingo ya mfuko wa kizazi kwa kutumia kemikali iitwayo acetic acid, ambayo huwekwa kwa kutumia pamba na mabadiliko ya rangi ya chembe chembe hai zilizopo ndizo zitakazobainisha kuwepo kwa dalili za ugonjwa huo. Endapo kipimo hicho kitaonesha dalili za mwanzo za ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi, kitachukuliwa kipimo kutoka katika sehemu iliyoathirika kwa ajili ya uchunguzi zaidi.


TIBA YA SARANI YA SHINGO YA KIZAZI
Kansa ya shingo ya kizazi inatibika iwapo itagundulika mapema ikiwa katika hatua za mwanzo. Hii ni katika hali ambayo ugonjwa huu unapogundulika katika hatua za mwisho, uwezekano wa kutibika huwa mdogo na gharama za matibabu kuwa kubwa. Kuna njia za kutibu saratani ya shingo ya kizazi ambayo haijaanza kuonesha dalili ikiwa ni pamoja na kutumia barafu maalumu na pia njia ya upasuaji mdogo wa kuondoa uvimbe. Pamoja na njia hiyo ya kutibu saratani ya awali pia ipo tiba maalumu ya saratani ya shingo ya kizazi ambayo ni pamoja na upasuaji katika hatua ya mwanzo ya ugonjwa, mionzi pamoja na njia ya dawa inayohusisha matumizi ya kemikali maalumu za kutibu saratani au chemotherapy. Matibabu ya mionzi na dawa hutegemea umri, afya na hatua ambayo ugonjwa umefikia. Baadhi ya wakati wagonjwa hutolewa kizazi wakati wa upasuaji ili kutibu aina hii ya saratani hasa wakati ikiwa imesambaa kwenye kizazi chote.
Hata hivyo saratani ya shingo ya kizazi huweza kuzuilika kwa kutumia njia kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi mara kwa mara, mke au mume kutokuwa na wapenzi wengi, kutoanza tendo la ndoa katika umri mdogo, kutozaa sana na kutovuta sigara. Kutokana na hali hiyo wataalamu wa afya wanashauri kuwepo utaratibu wa kuchukua tahadhari mapema endapo dalili za ugonjwa huo zitagundulika. Pia ugonjwa huu huweza kuzuilika kwa chanjo inayojulikana kana HVP vaccine, ambayo hupunguza hatari ya kutokea mabadiliko ya seli na kuwa saratani. Chanjo hii hupewa wasichana walio kati ya umri wa miaka 9 hadi 26 na inategemea mazingira. Wataalamu wa masuala ya afya wanasema kuwa, asilimia 50 ya wagonjwa wana uwezo mkubwa wa kupona kabisa ugonjwa huu, lakini pengine ikiwa saratani ya shingo ya kizazi haitochukuliwa na jamii za kimataifa kuwa tatizo kubwa huenda miaka ijayo ukawa ni ugonjwa mkubwa kuliko hata ukimwi na malaria.

&&&&&&&

Naam wasikilizaji wapenzi, kama wanavyosema wahenga kinga ni bora kuliko tiba, basi tufahamu kuwa kwa kujikinga tunaweza kujiepusha na magonjwa mengi na hata ya saratani. Moja ya kinga hizo ni kulinda tabia zetu na kutofanya ngono zembe. Hadi wakati mwingine panapo majaaliwa, tukutane tena katika kipindi kingine cha Ijuwe Afya Yako na daima tusisahau kuzilinda afya zetu!

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …