Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 07 Oktoba 2014 16:23

Uvimbe katika mayai ya mwanamke (Ovarian Cyst)

Uvimbe katika mayai ya mwanamke (Ovarian Cyst)

Assalam aleykum wasikilizaji wapenzi na karibuni katika kipndi kingine cha Ijue Afya yako. Wiki hii tutazungumzia uvimbe katika mayai ya mwanamke au kwa maneno mengine ovarian cyst, ikiwa ni katika muendelezo wa kujadili magonjwa ya wanawake ambao tuliuanza huko nyuma. Karibuni kujumuika nami hadi mwisho wa kipindi.

&&&&&&&&&

Uvimbe kwenye mayai ya mwanamke (ovary) hutokana na mkusanyiko wa majimaji yanayozungukwa na kuta nyembamba ndani ya mayai ya mwanamke. Uvimbe huu ambao hupatikana ndani ya mayai ya mwanamke ndio unaojulikana kama ovarian cyst. Uvimbe huu hutokea kwa wanawake wa umri wowote ule na mara nyingi huonekana kwa wanawake waliofikia kikomo cha umri wa kupata ujauzito. Lakini kwanza hebu tuelezee juu ya mayai ya mwanamke. Kwa kawaida mwanamke anakuwa na mayai mawili katika mwili wake. Yai moja upande wa kulia na yai jingine upande wa kushoto kwake. Mayai haya hupatikana pembezoni mwa mfuko wa uzazi (uterus). Mayai haya ya mwanamke huanza kuzalisha mayai ya uzazi yanayojulikana kama ovum na mayai hayo ya uzazi hukuwa ndani ya mayai ya mwanamke (ovary) kwa kuchochewa na baadhi ya homoni. Katikati ya mwezi, siku ya kumi na nne, masaa 24-36 baada ya kiwango cha kichocheo aina ya Luteinizing Hormone kuwa juu, mayai ya uzazi hutolewa katika kila ovari na hii ndio hujulikana kama ovulation au kufikia kilele upevukaji mayai. Mayai haya ya uzazi huishi kwa masaa machache hadi masaa 24 ikiwa hayatorutubishwa na mbegu kutoka kwa mwanamume. Mabaki ya mfuko wa mayai ya uzazi yanayojulikana kama follicle ndani ya ovari, hugeuka na kuwa corpus luteum ambao huhusika na utoaji wa kichocheo au homoni aina ya progesterone kwa wingi. Homoni hii ya progesterone ndio inayosababisha mfuko wa uzazi kujiandaa kwa kujikita yai (implantation) lililorutubishwa kwa mbegu ya kiume ndani ya mfuko wa uzazi kwa kuongeza unene kwenye kuta zake. Yai hili husafiri hadi kwenye mfuko wa uzazi ambako hukua na kuwa mtoto. Kama upachikwaji wa yai liliorutubishwa hautafanyika, basi ndani ya wiki mbili, corpus luteum huanza kusinyaa na kupotea na kusababisha kushuka kwa kiwango cha homoni aina ya progesterone na estrogen. Kushuka kwa viwango vya vichocheo hivi ndio husababisha mfuko wa uzazi kuanza kutoa mabaki ya kuta zake pamoja na yai la uzazi na hii ndiyo pale mwanamke anapotoka damu ukeni inayojulikana kama hedhi. Unaweza ukajiuliza, ni kwa nini nimeanza na maelezo haya, lakini jibu ni kutaka kuonyesha umuhimu wa mayai ya uzazi kwa mwanamke pamoja na kazi yake.

&&&&

Kuna aina ngapi za uvimbe kwenye mayai ya mwanamke?
Kuna aina nyingi za uvimbe kwenye mayai ya mwanamke lakini aina hizi saba ndio huonekana sana kwa wanawake wengi ambazo ni kama ifuatavyo:
I. Follicular cyst ni uvimbe ambao hutokea wakati ovulation isipotokea au baada ya corpus luteum kuanza kusinyaa na kupotea yenyewe baada ya kutopachikwa kwa yai kwenye kuta za mfuko wa kizazi. Uvimbe huu unakuwa na wastani wa inchi 2.3 kwa upana. Upasukaji wa uvimbe huu husababisha maumivu makali sana katikati ya mzunguko wa hedhi yaani siku ya ovulation. Maumivu haya huonekana kwa robo ya wanawake wenye aina hii ya uvimbe. Kwa kawaida, uvimbe huu hauna dalili zozote na hupotea wenyewe baada ya miezi kadhaa.
II.Corpus Luteum cyst- ambao ni uvimbe unaotokana na kutopachikwa kwa yai la uzazi lililorutubishwa na mbegu ya kiume kwenye mfuko wa kizazi. Kwa kawaida corpus luteum husinyaa na kupotea yenyewe, au wakati mwengine inaweza ikajaa maji na hivyo kusababisha uvimbe wa aina hii. Uvimbe huu huonekana kwenye upande mmoja (kushoto au kulia) wa mwanamke na hauna dalili zozote zile.
III. Hemorrhagic cyst- Uvimbe huu hutokea wakati kukiwa na uvujaji wa damu ndani ya uvimbe wa aina yoyote ule ambao umeshajitengeneza tayari. Huambatana na maumivu makali kwenye upande mmoja wa ubavu wa mwanamke (kushoto au kulia).
IV. Dermoid cyst- Uvimbe huu ambao sio saratani na pia hujulikana kama mature cystic teratoma, huathiri wanawake wadogo walio katika umri wa kushika mimba na huweza kukua na kufikia inchi 6 kwa upana na ndani yake huweza kuwa na mchanganyiko wa nywele, mfupa, mafuta na cartilage. Uvimbe wa aina hii huweza kuwa mkubwa zaidi au kujizungusha na hivyo kuathiri usambazaji wa damu kwenda kwenye uvimbe huu na hivyo kusababisha maumivu makali sana maeneo ya tumboni.
V. Polycysitic appearing cyst- Uvimbe wa aina hii unakuwa ni mkubwa sana na huwa umezungukwa na vijivimbe vyengine vidogo vidogo na huonekana hata kwa wanawake wenye afya njema au wale wenye matatizo ya homoni.
VI. Cystedenoma-Ni aina ya uvimbe unaotokana kwenye tishu za ovary na hujazwa na majimaji yenye kuvutika. Uvimbe wa aina hii huweza kuwa mkubwa sana hata kufikia inchi 12 au zaidi kwa upana.
VII. Endometriomas /Endometrial Cysts- Husababishwa na uwepo wa aina mojawapo ya kuta za mfuko wa kizazi unaojulikana kama endometrium kwenye mayai ya mwanamke. Huathiri wanawake waliofikia kikomo cha umri wa kupata ujauzito na huambatana na maumivu sugu ya nyonga wakati wa hedhi. Uvimbe huu unakuwa na damu ya rangi nyekundu inayoelekea kuwa kahawia na ukubwa wake ni kuanzia inchi 0.75 hadi 0.8.

&&&

Nini husababisha tatizo hili la uvimbe kwenye mayai ya mwanamke?
Vihatarishi vya tatizo la uvimbe kwenye mayai ya mwanamke ni;
kwanza kabisa historia ya awali ya ovarian cyst. Kwa maana kuwa, wanawake ambao wazazi wao au watu wao wa karibu wamekuwa wakisumbuliwa na ugonjwa huo kuna uwezekano mkubwa nao pia wakapatwa na tatizo hilo. Sababu nyingine inayoweza kusababisha uvimbe katika mayai ya mwanamke ni kuwa na mzunguko wa hedhi usiokuwa na mpangilio maalum au kama tunavyouita kwa kimombo, irregular menstruation cycle. Kihatarishi kingine ni kuwa na mafuta mengi kwenye sehemu ya juu ya mwili na hii ni kwa wale wanawake wanene. Ugumba na kuvunja ungo au kubaleghe mapema ni sababu nyingine ambapo mtoto wa kike anapobaleghe akiwa na miaka 11 au chini ya hapo huweza kupatwa na uvimbe katika mayai yake. Vilevile kukosekana uwiano sawa wa vichocheo au homoni mwilini au ugonjwa wa hypothyroidism na pia dawa ya kutibu saratani ya matiti ya Tamoxifen husababisha tatizo hilo.
Dalili na viashiria vya Ovariancyst.
a)Maumivu makali, ambayo hayana mwanzo maalum na yanayochoma, ambapo maumivu hayo yanaweza yakawa yanakuja na kupotea au yakawepo moja kwa moja. Pia mtu anaweza kupata usumbufu na kutojisikia vizuri kwenye maeneo ya chini ya kitovu, kwenye nyonga, uke, kwenye mapaja na mgongoni upande wa kwa chini. b) Kuhisi tumbo kuwa zito, kujaa au kuvimba.
c) Maumivu kwenye matiti na hedhi isiyokuwa na mpangilio maalum.
d) Maumivu ya muda mrefu kwenye nyonga wakati wa hedhi na ambayo huweza kuhisiwa sehemu ya chini mgongoni. Maumivu haya yanaweza kuanza muda mfupi tu baada ya kuanza hedhi, wakati wa hedhi au mwisho wa hedhi.
e) Maumivu ya nyonga baada ya kufanya kazi ngumu, mazoezi au baada ya kujamiiana. Kuhisi kichefuchefu, kutapika na kutokwa na matone ya damu ukeni. Dalili nyingine ni ugumba na kuhisi uchovu, mabadiliko ya haja ndogo yaani kukojoa mara kwa mara, kujikojolea au kushindwa kutoa mkojo wote kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kupata haja ndogo.
Vilevile mabadiliko ya haja kubwa ambayo ni kupata haja kubwa kwa shida sana kutokana na presha kwenye maeneo ya nyonga.
n) Nywele kukua kwa kasi na kuongezeka kuota kwa nywele kwenye uso au sehemu nyingine za mwili. Dalili nyingine za uvimbe katika mayai ya mwanamke ni kuumwa kichwa, kuongezeka uzito, maumivu ya kwenye mbavu, kutokewa na uvimbe chini ya ngozi na kuvimba mara kwa mara.
Vipimo vya uchunguzi:- Kwanza kabisa ni mgonjwa kufanyiwa Endovaginal Ultrasound ambayo hufanywa kwa kuingiza mpira maalum kupitia ukeni na kuangalia mfuko wa uzazi na mayai ya mwanamke. Kwa kutumia kipimo hiki, ni rahisi kwa daktari kugundua kama uvimbe kwenye mayai ni wa aina gani na kujua kama ni maji tu (fluid filled sac), au ni maji pamoja na mchanganyiko wa vitu vigumu kwa mana ya complex, au ni vitu vigumu pekee ambapo huitwa completely solid. Kipimo kingine kinachochukuliwa kuchunguza ugonjwa huu ni Abdominal Pelvic Ultrasound ambayo ni Ultrasound ya kawaida. Husaidia kujua ni aina gani ya uvimbe uliopo kwenye mayai ya mwanamke.
Wapenzi wasikilizaji tunaishia hapa kwa leo lakini bado hatujamaliza kuelezea vipimo vyote anavyochukuliwa mwanamke mwenye uvimbe katika mayai. Tuataendelea wiki ijayo ambapo pia tutaelezea tiba ya ugonjwa huo. Hadi wakati huo tusisahau kulinda afya zetu.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …