Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 29 Septemba 2014 15:42

Uvimbe katika mfuko wa uzazi (Fibroid)

Uvimbe katika mfuko wa uzazi (Fibroid)

Assalam Aleykum wasikilizaji wapenzi na karibu kujiunga nami katika kipindi kingine cha Ijue Afya Yako. Leo tutaendelea kujadili magonjwa yanayowasumbua wanawake ambapo tutazungumzia uvimbe katika mfuko wa kizazi au Fibroid. Ni matumaini yangu kuwa mtajumuika nami hadi mwisho wa kipindi.

&&&&&&

Uvimbe katika mfuko wa kizazi wa mwanamke hujulikana kama uterine myoma au fibroid. Uvimbe huu hutokea kwenye misuli laini ya mfuko wa uzazi. Tatizo hili huwakumba wanawake wengi ambapo huwapata kwa asilimia tano wanawake wenye umri kati ya miaka 20 hadi 30, asilimia karibu 20 kwa wanawake wenye umri kati ya miaka 30 hadi 40, na zaidi ya asilimia 40 kwa wale wenye umri zaidi ya miaka 40. Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa myoma ni aina ya uvimbe unaowapata wanawake wengi hasa katika umri wa miaka ya uzazi. Hii inamaanisha kuwa kadiri umri unavyokuwa mkubwa mwanamke ana nafasi kubwa ya kupata ugonjwa huu, pia ni tatizo ambalo linashuhudiwa sana katika jamii kwa sasa na pengine ni kutokana na jinsi watu wanavyoishi. Kuna aina kuu 3 za fibroids, kwanza ni uvimbe unaotokea kwenye tumbo la kizazi na unaweza kuwa ndani ya kizazi unaojulikana kama submucosal fibroids. Aina ya pili ni uvimbe unaotokea ndani ya nyama ya kizazi yaani intramural fibroid, na aina ya tatu ni ule unaotokea nje kwenye ukuta wa kizazi ambao hujulikana kitaalamu kama subserol fibroids.
Uvimbe katika mfuko wa uzazi huwapata zaidi kina mama ambao wako katika umri wa kuweza kuzaa (reproductive age). Uvimbe huwa wa ukubwa tofauti huanza kwa mdogo na baadaye kuwa mkubwa sana na hata baadhi ya wakati mwanamke kuonekana kama ni mjamzito. Uvimbe huu unaweza kuwa mmoja lakini baadhi ya wakati hutokea uvimbe zaidi ya mmoja amboa hutanda katika mfuko wa uzazi.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wanawake wa asili ya Kiafrika hupata zaidi tatizo hili kuliko wazungu. Pia huwapata zaidi wanawake ambao hawajazaa kabisa au wamekaa muda mrefu bila ya kuzaa, wanawake wanene, na pia wale ambao wana ndugu wa karibu aliyepatwa na ugonjwa huu. Wengine walio katika hatari ya kupata ugonjwa huu wa fibroids ni pamoja na wale wanaopata hedhi mapema.
Inafaa kuelewa kuwa, fibroids sio kansa bali ni uvimbe wa kawaida tu ambao hukuwa kwa kutegemea kichocheo au hormone ya estrogen na ndio maana wakati wa kupata uvimbe huo ni kuanzia kubalehe mpaka kukoma kwa hedhi. Hata hivyo ingawa fibroids si saratani, lakini uvimbe wa aina hii umekuwa tishio kwa wanawake wengi duniani na kusababisha wengi wao kuondolewa vizazi. Pamoja na kuwa sababu kuu ya uvimbe katika kizazi haijajulikana, lakini zipo sababu ambazo zimehakikiwa kusababisha mwanamke kupata uvimbe wa fibroid. Sababu inayopewa kipaumbele zaidi ni wingi wa vichocheo vya estrogen ambavyo vipo katika miili ya wanawake na vichocheo hivi ndivyo hufanya kazi katika mwili wa mwanamke na kumsababishia kupata siku zake.
Mara nyingi uvimbe huu huwa unaongezeka kukua sana hasa wakati wa ujauzito kwani vichocheo hivi huongezeka wakati huu ili kulinda makuzi ya mtoto. Unapaswa kujua kuwa, kwa watu waliofikia kikomo cha hedhi au menopause huwa hawapati fibroids na kama wakipata basi huwa na hatari ya kuwa kensa.

&&&&&&

Dalili za uvimbe katika kizazi

Uvimbe katika kizazi cha mwanamke ukiwa mdogo unaweza usiwe na dalili zozote na dalili hutegemea sehemu ulipo kwenye mfuko wa uzazi na pia ukubwa wake. Hata hivyo dalili za ugonjwa huu mara nyingi ni kutokwa damu nyingi kwa muda mrefu wakati wa hedhi ikiambatana na mabonge mabonge isivyo kawaida, au kutokwa damu isiyo ya kawaida katikati ya mwezi au hedhi zisizokuwa na mpango. Dalili nyingine ni kupata maumivu ya kiuno hasa wakati wa hedhi, kutokana na ugonjwa kubana viungo vingine vya mwili (pressure symptoms). Wengi hupata maumivu makali ya tumbo, maumivu wakati wa tendo la ndoa, maumivu ya mgomgo na kukojoa mara kwa mara kwani uvimbe hukandamiza kibofu cha mkojo. Dalili nyingi za fibroid ni pamoja na kutotunga mimba au mimba kuharibika na kutoka, na wakati mwingine ugumba. Tatizo la uvimbe katika kizazi mara nyingi huambatana na maradhi mengine. Maradhi hayo ni kama, upungufu wa damu, kufunga choo, matatizo ya figo na mara chache huweza kuwa saratani. Pia uvimbe wa fibroid unapokua mkubwa unaweza kusababisha dalili zifuatazo, mkojo kubaki kwenye kibofu, haja kuwa ngumu, miguu kuvimba na kupungukiwa damu.
Uchunguzi
Ni rahisi kwa mtaalamu kugundua ugonjwa huu au uvimbe katika mfuko wa uzazi kwa kumkagua, au kumpima mgojwa (bimanual examination). Daktari anaweza kuhisi uvimbe kwa kutumia mikono miwili anapokuwa ana pima tumbo, hata hivyo kipimo cha Ultrasound ya nyonga hutumika kugundua uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke. Kipimo cha MRI pia huweza kutumika kupata usahihi wa ukubwa na eneo uvimbe ulipo.
Fibroids zinaweza kuzuia kupata mtoto kwa njia tofauti. Kwanza kabisa uvimbe huu unapokuwa sana hukandamiza mirija ya kupitisha mayai kutoka kwenye ovari au sehemu mayai yanapotengenezwa. Uvimbe huu pia unaweza kuzuia yai lililorutubishwa kujishikiza kwenye kizazi hasa ikiwa ni submucosal fibroids. Pia hufanya mfuko wa kizazi ukaze na hivyo kushindwa kusukuma mbegu kwenda kwenye mishipa ya kupitisha mayai.

&&&&&

MATIBABU

Matibabu ya tatizo hili yanaweza kulenga kutibu dalili au kupunguza uvimbe. Hata hivyo kama ugonjwa huu hauna dalili unaweza kuwa ukifuatiliwa tu bila kuchukuliwa hatua zozote. Tunapaswa kujua kuwa, mwanamke anapokoma siku zake tatizo hili nalo hutoweka. Wanawake wengi wana fibroids ndogo ndogo lakini kwa sababu hazina dalili huwa hawaendi hospitali na pengine hubainika pale wanapofanyiwa ultrasound. Lakini iwapo watabeba ujauzito uvimbe huu huongezeka kwa sababu ya vichocheo kuongezeka. Kwa ajili hiyo tunashauriwa kuwa na mazoea ya kufanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara ili kuweza kushughulikia haraka matatizo kama haya.
Uvimbe ambao ni mkubwa wenyewe hutibiwa kwa namna zifuatazo:
1. Dawa ambazo kwanza ni kwa ajili ya kurekebisha kiwango cha vichocheo vinavyosababisha uvimbe huu kwa mfano danazol na aina ya pili ya dawa ni vidonge vya maumivu ili kutuliza maumivu yanayosababishwa na fibroids.
Vidonge vingine vinavyoweza kutumika ni vya kuzuia damu kama tranexamic acid na pia dawa za uzazi wa mpango.
2. Njia ya pili ni upasuaji, ambao hutegemea na ukubwa wa uvimbe na wingi wa fibroids. Kuna aina mbili za upasuaji : 1. Myomectomy - njia hii hutumika ikiwa kuna uvimbe mmoja na si mkubwa sana, na iwapo mwanamke ni kijana anayehitaji kuendelea kuzaa na kwa wale wenye uvimbe mmoja ulio katika sehemu nzuri. Operesheni hii ni kwa ajili ya kutoa uvimbe tu na kuacha kizazi. Hata hivyo katika upasuaji wa aina hii kuna uwezekano mkubwa wa uvimbe kujirudia.
2. Total abdominal hysterectomy – Hii ni aina ya upasuaji ambapo kizazi chote hutolewa na hufanyika ikiwa kizazi kina uvimbe mmoja mkubwa sana au vivimbe vingi.
Sio vibaya kujua kuwa aina ya upasuaji wa uvimbe katika kizazi hutegemea pia umri wa mgonjwa, idadi ya watoto na maamuzi binafsi ya mgonjwa. Baadhi ya wakati pia hata baada ya kufanyiwa operesheni uvimbe hujirudia iwapo vichocheo vinavyosababisha hali hiyo havitasawazishwa.
&&&&&&
Wasikilizaji wapenzi magonjwa yanayowasumbua wanawake ni mengi hasa yanayohusiana na masuala ya uzazi na kwa ajili hiyo wataalamu wa afya ya uzazi wanashauri wanawake kwenda kufanyiwa uchunguzi mara kwa mara ili kubaini maradhi ambayo mengine yanaweza kutibika au kuzuilika. Hadi wakati mwingine, na katika kipindi kingine cha afya, kwaherini.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …