Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 28 Disemba 2015 11:28

Umoja katika mtazamo wa Imam Khomeini (MA) na Ayatullah Khamenei

Umoja katika mtazamo wa Imam Khomeini (MA) na Ayatullah Khamenei

Uislamu umeufanya umoja kuwa jambo la wajibu na lazima miongoni mwa Waislamu na waumini na dini nyinginezo za mbinguni zinazomwamini Mwenyezi Mungu Mmoja. Uzito wa jambo hili unaonekana wazi katika aya za Qur'ani Tukufu na riwaya zilizopokelewa kutoka kwa Maimamu Maasumu (as). Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 103 ya Surat Aal Imran kitabu hicho kitakatifu: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu.
Historia ya Kiislamu inaonyesha wazi kuwa kila mara Waislamu wa madhehebu tofauti wanapochukua uamuzi wa kuungana na kushirikiana katika ngome moja dhidi ya audui, jamii ya Kiislamu huwa ni tukufu na yenye nguvu na maadui kuwa dhaifu, lakini Waislamu wanapoghafilika na kusahau amri hiyo muhimu ya Mwenyezi Mungu, hukabiliwa na misiba mingi ukiwemo wa kudhibitiwa na maadui na kuhatarishwa kizazi na jamii nzima ya Kiislamu. Qur'ani Tukufu inasema katika aya ya 46 ya Surat al- Anfaal: Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu.
Katika karne hii, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mfano bora wa dhihirisho la nguvu ya Umma wa Kiislamu ambayo imepatikana kutokana na imani na umoja wa wananchi. Wananchi hao waliokuwa mikono mitupu lakini waliokuwa na nyoyo zilizojaa imani ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, walisimama imara mbele ya utawala wa kitaghuti wa Shah uliokuwa umehijami vilivyo kwa kila aina ya silaha za kisasa na kupata uungaji mkono wa kila upande kutoka kwa madola ya kibeberu na kiistikbari ya Magharibi. Hatimaye wananchi walijipatia ushindi wa kishindo kutokana na mshikamano na ushirikiano wao imara kwa ajili ya kuung'oa mzizi wa upotovu nchini.
Iran ni nchi ambayo ina madhehebu na makabila mengi. Hata kama Mashia ndio walio wengi nchini, lakini Masunni pia wanaunda asilimia kubwa ya Waislamu wa nchi hii. Mbali na madhehebu haya mawili kuna wafuasi wa dini nyinginezo kama vile Mayahudi na Wakristo. Jambo la kuvutia hapa ni kwamba licha ya kuwepo tofauti hizi zote za kimadhehebu, kidini, na kikabila lakini wananchi wote wa Iran katika vipindi vyote vya mapambano dhidi ya uistikabari walisimama pamoja na kushirikiana bega kwa bega dhidi ya utawala dhalimu wa Shah huku wakitambuana kama ndugu. Hivi sasa pia kutokana na misingi muhimu ya utamaduni wa umoja iliyoandaliwa nchini na Imam Khomeini (MA), wafuasi wa dini na madhehebu mbalimbali wanaishi pamoja kwa amani, ushirikiano na udugu. Katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Masuni walipigana bega kwa began na wenzao Mashia dhidi ya utawala huo wa Kibaathi na kutoa mashahidi wengi kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Wakristo na Wakalimi wa Iran pia walishiriki vilivyo katika medani ya vita na kufuatilia kwa uwezo wao wote malengo ya Jamhuri ya Kiislamu na kuuawa shahidi kwenye njia hiyo.
Kutokana na uongozi shupavu na wa busara wa Imam Khomeini (MA), Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameweza kudhihirisha muujiza wa umoja katika karne hii. Kwa kufuata kikamilifu miongozo ya Qur'ani Tukufu ambayo inawataka Waislamu kuwa na umoja na pia kuungana na wafuasi wa dini nyinginezo zinazompwekesha Mwenyezi Mungu, Imam Khomeini (MA) alitoa wito wa kuwepo umoja miongoni mwa madhehebu zote za Kiislamu na hata wafuasi wa dini nyingine, kushirikiana kwa pamoja chini ya kivuli cha Mapinduzi ya Kiislamu. Ni wazi kuwa umoja hapa hauna maana ya wafuasi wa madhehebu na dini tofauti kuacha imani zao na kufuata itikadi moja lakini una maana ya kwamba licha ya kuwepo tofauti za kiimani na kiitikadi lakini wote wanapasa kuimarisha umoja na kushirikiana kwa msingi wa kuheshimiana na kuzingatia udugu baina yao. Tofauti zilizopo zinapaswa kuchunguzwa na kujadiliwa si kwa njia za kawaida na za kijuu juu tu bali kwa mbinu za kielimu, kitaalamu na katika mazingira yaliyo mbali na dharau, matusi na kukufurishana ili ukweli wa mambo upate kufahamika.
Kwa kuwa na mtazamo wa kina na mwamko wa kupigiwa mfano na katika hali ambayo ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa umedhoofishwa pakubwa na hitilafu za kikabila na kimadhehebu, Imam Khomeini (MA) alifanikiwa kulifahamisha taifa la Iran udharura wa kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu na hivyo kuzuia kutokea mgawanyiko katika jamii hii ya kimapinduzi, kupitia hotuba zake za hamasa na mwamko. Alisema: 'Leo ni siku ambayo makundi yote ya Kiislamu yamesimama mkabala na nguvu za kishetani ambazo zinataka kufuta msingi wa Uislamu, nguvu ambazo zimetambua kwamba kitu ambacho ni hatari kwao ni Uislamu na umoja wa mataifa ya Kiislamu. Leo ni siku ambayo Waislamu wa nchi zote za dunia wanapasa kushikamana.' Imam Khomeini (MA) alikuwa akisema: 'Katika Uislamu, lugha, kabila na sehemu havitambuliki (havipewi umuhimu). Waislamu wote, wawe ni Masuni au Mashia, ni ndugu na wote ni sawa, na wote wananufaika na fursa na haki za Kiislamu. Usuni na Ushia haujadiliwi kwenye Uislamu wala Mkurdi na Mfursi, wote ni ndugu."
Si taifa la Iran tu, bali Imam Khomeini aliwataka Waislamu wa mataifa yote bali wanyonge wote wa ulimwengu bila kujali dini zao kuwa na umoja mbele ya uistikbari wa dunia. Hata hivyo alitilia mkazo sana umoja baina ya Shia na Suni katika nchi za Kiislamu. Aliamini kuwa jambo lililowadhoofisha Waislamu wengi na kuwafanya wadhalilishwe duniani ni mfarakano ulio baina yao. Alikuwa akisema: 'Hitilafu zinazoletwa nchini Iraq, Iran na nchi nyigine za Kiislamu zinapasa kutiliwa maanani na viongozi wa serikali za Kiislamu na kutambua kwamba hitilafu hizo zitafuta nguzo yao. Wanapasa kutambua kwa kutumia akili na busara kwamba wanataka kuufuta Uislamu kwa kisingizio cha madhehebu na Uislamu. Mikono miovu ambayo inazua hitilafu miongoni mwa Mashia na Masuni katika nchi hizi sio Mashia wala Masuni halisi. Hii ni mikono ya wakoloni ambayo inataka kudhibiti nchi za Kiislamu kupora utajiri wao na kuanzisha masoko ya magendo katika nchi zinazotajwa kuwa zimeendelea.'
Tokea mwanzoni, Mapinduzi ya Kiislamu yamewanyooshea Waislamu na wapwekeshaji wote wa Mwenyezi Mungu mkono wa udugu na urafiki. Mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alikuwa akisema: Sisi na Waislamu wa Ahlu Sunna ni ndugu. Ikiwa mtu atatamka maneno ambayo yatachochea mfarakano na tofauti kati ya Waislamu, basi jueni ya kuwa mtu huyo atakuwa ima ni jahili au ni miongoni mwa watu wanaotaka kuleta hitilafu miongoni mwa Waislamu. Hapa hakuna kabisa suala la Ushia wala Usuni bali sisi sote ni ndugu.' Fikra ya umoja ilibadilika na kuwa stratijia muhimu katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambapo uhusiano wake na nchi nyingine za Kiislamu ulisimama na ungali unasimama juu ya msingi huu wa udugu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitofautishi kati ya Shia na Suni katika kutetea Uislamu na Waislamu wanaodhulumiwa katika sehemu yoyote ile ya dunia na kama ambavyo inatetea kwa maneno na vitendo Mashia wa Lebanon ndivyo hivyohivyo inavyotetea na kuwaunga mkono Waislamu wa Kisuni wa Palestina wanaodhulumiwa na kukandamizwa na utawala ghasibu wa Israel. Katika miongo minne iliyopita tokea ijipatie ushindi, Jamhuriya Kiislamu ya Iran imethibitisha wazi kwamba inaamini na kuzingatia umoja miongoni mwa Waislamu kuwa msingi muhimu kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya Uislamu ulimwenguni.
Ayatullah Ali Khamenei, ambaye alichukua nafasi ya kuongoza Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kuaga dunia Imam Khomeni pia husisitiza mara kwa mara juu ya umuhimu wa kuimarishwa umoja wa Waislamu na kuainisha siasa kuu za mfumo wa Kiislamu wa Iran lwa msingi huo. Anasema katika moja ya hotuba zake ambapo anaashiria moja ya manufaa wanayoyapata maadui wa Uislamu kutokana na mfarakano wa Waislamu kwa kusema: 'Kuna watu bilioni moja duniani ambao wana imani moja kuhusu Mwenyezi Mungu, Mtume Mtukufu (saw), Swala, Hija, Al-Kaaba, Qur'ani Tukufu na mambo mengine mengi katika dini na kuhitilafiana katika baadhi ya mambo. Je, ni mantiki kwa watu kama hawa kutumia hitilafu hizi chache kwa lengo la kuanzisha vita baina yao na hivyo kuwapa watu wasiomwamini kabisa Mwenyezi Mungu, Mtume (saw), dini na mambo mengine yote ya msingi fursa ya kuuhujumu Uislamu na Waislamu? Anasema katika sehemu nyingine: 'Moja ya maamrisho ya Qur'ani ni kumtaka kila mtu katika Umma wa Kiislamu kuzingatia umoja na kushirikiana na wenzake. Mwenyezi Mungu anasema shikamaneni na kamba yake na wala msifarakiane. Ni nani wanaokusudiwa kwenye maneno haya? Maneno haya yanatuhusu sisi, ni maneno yanayolihusu taifa la Iran, nchi na mataifa ya Kiislamu na ni maneno yanayowahusu waumini wote wa dini ya Kiislamu kote duniani. Je, tunafanya kama tulivyoamrishwa? Nukta iliyo kinyume cha mafundisho haya ya Qur'ani ni mafundisho ya kikoloni yaani ya kuleta na kuzua hitilafu kati ya Waislamu, ili kundi moja lilikufurishe jingine, kulaani na kujitenga na jingine. Hili ndilo jambo linalofuatiliwa na ukoloni hii leo ili tusiwe pamoja.'
Ulimwengu wa Kiislamu hii leo unahitaji kuwa na umoja kuliko wakati mwingine wowote. Mfarakano na utakfiri ni balaa kubwa linalowakabili Waislamu ambao wote wanaswali kuelekea kibla kimoja, wana kitabu kimoja cha mbinguni, wanamwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja na wote wanampenda Mtume wa Mwisho. Leo maadui wa Uislamu wanapiga ngoma ya kuwatenganisha Waislamu kwa nguvu kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote na kuota ndoto ya kuzidhibiti nchi za Kiislamu. Katika hali kama hiyo umoja wa Kiislamu ni dawa mujarabu ambayo Mwenyezi Mungu amewataka waja wake wema waitumie. Kuitikia wito huo wa Mwenyezi Mungu bila shaka kutafungua njia ya saada na utukufu kwa Waislamu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)