Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 28 Disemba 2015 09:53

Mkutano wa 29 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu

Mkutano wa 29 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu

Mkutano wa 29 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unaendelea hapa mjini Tehran katika siku yake ya pili leo ukishirikisha wanazuoni, wanafikra na wasomi kutoka nchi 70 duniani. Mkutano huo unafanyika wakati ulimwengu wa Kiislamu ukikabiliana na changamoto kubwa ya ugaidi na haja kubwa ya kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Waislamu.

Katika sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo hiyo jana, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliashiria sababu za kujitokeza ukatili na migawanyiko katika ulimwengu wa Kiislamu na kusema kuwa, jibu la wito wa Mtume mtukufu wa Uislamu, Muhammad bin Abdullah (saw) wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya Waislamu ni kujiepusha na vitendo vya utumiaji mabavu na kueneza upendo wa Kiislamu.

Rais Rouhani amesema ukatili na vitendo vya kutumia mabavu vinavyoshuhudiwa katika ulimwengu wa Kiislamu ni matokeo ya ufahamu usio sahihi na potofu kuhusu Uislamu na kuongeza kuwa: Haiwezekani kuchukua maamuzi kuhusu mustakbali wa taifa lolote kwa kutumia mabomu na makombora, wala haiyumkini kuangamiza ugaidi kwa kutumia mabomu bali kwa njia ya mazungumzo.

Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu nchini Iraq, Ammar Hakim ambaye pia amehutubia kikao cha Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unaoendelea mjini Tehran amesema kuna udharura wa kupambana na wale wote wanaotumia vibaya hitilafu za mitazamo ya kifiqhi na kiitikadi kwa ajili ya kuzusha fitina na kuwapotosha vijana.

Kwa upande wake Sheikh Naeem Qasin ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria tatizo la ugaidi na makundi yanayowakufurisha Waislamu katika eneo la Mashariki ya Kati katika hotuba yake kwenye Mkutano wa 20 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu na ametahadharisha kuhusu njama za maadui za kutaka kuwa na ushawishi katika vituo vya kuchukua maamuzi muhimu katika mataifa ya Waislamu. Sheikh Naeem Qasim amesema: Tatizo hili litaondolewa kwa kushikamana barabara chini ya uongozi wa Faqihi Mtawala.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu, Ayatullah Muhsin Araki ambaye pia amehutubia kikao cha mkutano wa Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran amesema mgogoro mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu kwa sasa ni mifarakano na mapigano ya ndani. Ayatullah Araki ameongeza kuwa, matatizo yanayolenga utambulisho wa Uislamu katika zama hizi yanapaswa kushughulikiwa ipasavyo na viongozi, wanafikra na wasomi wa Kiislamu.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Dakta Ibrahim Jaafari amesema njia pekee ya kupata ushindi na mafanikio ulimwengu wa Kiislamu katika mazingira ya sasa ni umoja na mshikamano baina ya nchi za Waislamu.

Mufti Mkuu wa Syria, Sheikh Ahmad Badreddin Hassoun ambaye pia anashiriki Mkutano wa 29 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran amesema kuwa, ulimwengu wa sasa wa Kiislamu unahitajia fikra zinazotokana na sira na mwenendo wa Mtume Muhammad (saw) na kwamba maulama wa Kiislamu waliokusanyika katika mkutano huo wanapaswa kuhubiri sira hiyo watakaporejea katika nchi zao.

Mkutano wa 29 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulioanza jana hapa mjini Tehran unahudhuriwa na washiriki 500 kutoka nchi 70 duniani. Mkutano huo utakamilisha shughuli zake keshi.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)