Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 27 Disemba 2015 18:32

Umoja; Siri ya Uwezo na Nguvu za Ulimwengu wa Kiislamu

Umoja; Siri ya Uwezo na Nguvu za Ulimwengu wa Kiislamu

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji. Karibuni kuwa nami katika mfululizo mwengine wa vipindi hivi maalumu vinavyokujieni kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja ya kuadhimisha Maulidi, yaani kuzaliwa kwa Nabii wa rehma na mbora wa viumbe, Bwana Mtume Muhammad SAW. Kipindi chetu cha leo kitauzungumzia umoja kama siri ya nguvu na uwezo wa Ulimwengu wa Kiislamu. Endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kuhusiana na maudhui hiyo.

Leo hii Waislamu duniani wanaandamwa na dhoruba za hujuma na mashambulio ya kila upande ya maadui, kutokana na mifarakano, hitilafu ndogo ndogo na kushindwa kuwa na umoja baina yao. Mashariki ya Kati, ambayo ni kitovu cha kijografia cha dini ya Uislamu imekabiliwa na wimbi la mauaji, vitendo vya ukatili na vya kufurutu mpaka vinavyotokana na hatua za Wazayuni, pamoja na makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka yakiwemo ya Taliban, Al-Qaeda pamoja na Daesh. Ugaidi wa kiserikali wa Kizayuni, kwa miaka kadhaa sasa unaendelea kuteketeza roho na maisha ya Waislamu wasio na hatia wa Palestina. Kwa upande mwengine, idiolojia na itikadi za kufurutu mpaka, na magaidi ambao wenyewe wanayanasibisha wayafanyayo na Uislamu wamekuwa wakifanya ukatili na jinai za kutisha katika eneo hili. Mauaji ya halaiki na ukatili usio na mfano unashuhudiwa katika Mashariki ya Kati katika hali ambayo watu wenye idiolojia ya kufurutu mpaka wanazitumia nembo za Kiislamu na hata mafundisho yanayokubaliwa na Waislamu wa mataifa ya eneo hili kuwakufurisha Waislamu hao na kufikia hadi hata ya kuwachinja na kuwakata vichwa vyao. Na kwa upande mwengine pia, utawala wa Kiwahabi wa ukoo wa Aal Saud, ambao ni miongoni mwa waungaji mkono wa kimaanawi na kimaada wa makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh, umeanzisha wimbi jipya la mauaji ya Waislamu nchini Yemen. Maafa ya Mina na kupotea roho za karibu mahujaji 8,000 katika ardhi ya wahyi wakati wa msimu wa Hija, ni maafa mengine ambayo hayawezi kusahaulika kirahisi ndani ya nyoyo na fikra za Waislamu.
Huko barani Afrika pia Waislamu hawajanusurika na hatari ya makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka kama Boko Haram, Al-Shabab na Anti Balaka. Mauaji ya kinyama na ya kutisha ya hivi karibuni ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria, ni mfano mwengine wa maafa na masaibu yanayowapata Waislamu wa bara hilo. Vitendo vya watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka, wakiwemo magaidi wakufurishaji wa kundi la Daesh vimeenea hadi nchi za Magharibi ikiwemo Ufaransa na kusababisha wimbi la vitendo vya ukatili na ubaguzi dhidi ya Waislamu. Misikiti mingi, vituo vya Kiislamu na hata makaburi ya Waislamu hayajasalimika na hujuma na mashambulio ya makundi ya watu wabaguzi na wenye misimamo ya kufurutu ada ndani ya nchi za Magharibi. Katika nchi hizo, heshima na hadhi ya kiutu ya Waislamu haithaminiwi, bali Waislamu wenyewe, mali zao na hata maharimu zao wanaandamwa na hujuma mbalimbali. Katika miamala ya kijamii pia, kuwa Muislamu tu ni kosa tosha la kumfanya mtu akabiliwe na anuai za ubaguzi na uonevu.

Kama tutaiangalia hali ya sasa ya Ulimwengu wa Kiislamu, itatudhihirikia wazi kwamba adui amefanikiwa vyema kutekeleza kampeni ya umwagaji damu na uteketezaji roho za Waislamu. Wazayuni, wameifanya jamii ya Waislamu kuwa ndiye adui yao mkuu; nayo makundi ya ukufurishaji, kutokana na idiolojia yao bandia yanawaangalia Waislamu kama adui yao pia. Leo sura chafu, ovu na ya kikatili ya kundi la kigaidi la Daesh inaarifishwa na kutambulishwa ulimwenguni kuwa ni nembo ya wafuasi wa dini tukufu ya Uislamu. Lakini la ajabu ni kwamba Madaesh hao hao wanaojitangaza kuwa Waislamu wanamwaga damu za Waislamu katika nchi za Kiislamu.
Uislamu wapenzi wasikilizaji ni dini ya amani, upendo na udugu; na Mtume wake ni dhihirisho la rehma, huruma na upendo kwa walimwengu wote. Lakini pamoja na hayo dini na misingi ya utu pamoja na haki za mataifa zimekuwa mawindo ya uchu wa watu walioendekeza matamanio ya nafsi zao katika kufanya ushenzi na ukatili unaotokana na idiolojia na itikadi potofu. Samuel Huntington, mwananadharia mashuhuri wa Marekania ameyasema haya kuhusiana na nadharia yake ya "Mgongano wa Staarabu" kwa kimombo "The Clash of Civilizations": "Katika dunia mpya, Uislamu, ukiwa ni tishio kuu la kistratijia katika zama za baada ya Vita Baridi umechukua nafasi ya dola kuu la Ukomunisti. Kwa hivyo Magharibi inajikuta imetangulia mbele katika hali ya makabiliano na Ulimwengu wa Kiislamu. Moja ya hatua kuu za utanguliaji huo wa Magharibi katika kukabiliana na Mwamko wa Kiislamu ni kuanzisha hitilafu za kikaumu, kimadhehebu, kisiasa n.k. Uzushaji hitilafu wa kambi ya Uistikbari kati ya mataifa ya Waislamu, utakuwa ni wa kuzidhoofisha nchi ambazo kutokana na nguvu ya nishati na jiopolitiki, zitakuwa na nafasi kuu katika mustakabali wa dunia".

Kuendelea kwa hali tuliyoielezea wapenzi wasikilizaji, bila ya shaka ni kwa madhara ya Waislamu wote duniani, kutakakopelekea kutengwa, kunyimwa haki zao za binafsi na za kijamii na hatimaye kusambaratika moja kwa moja. Kwa hivyo njia pekee ya uokovu na ya kuwapa izza na nguvu Waislamu ni umoja na mshikamano wao. Na kwa kweli umoja na mshikamano si moja ya mambo ya ulazima mkubwa tu kwa sasa bali kuendelea kwa maisha yao kunafungamana moja kwa moja na jambo hili muhimu. Leo hii hisia hasi dhidi ya Waislamu ambazo zimefikia kilele katika Ulimwegu wa Magharibi kwa upande mmoja, kutojihisi Waislamu kuwa na mas-ulia baina yao kwa upande mwengine na vile vile moto wa fitna, mauaji ya halaiki yanayotokana na chuki, pamoja na mashambulio angamizi ya silaha za kisasa yanayoziandama nchi za Waislamu katika anga ya kimya kizito cha jamii ya kimataifa, ni mambo yanayolifanya suala la umoja na kuwa kitu kimoja Ulimwegu wa Kiislamu liwe na udharura na umuhimu mkubwa zaidi, na kupiga kengele ya indhari ya mtawalia kwa Waislamu kwamba maisha yao na izza yao hivi sasa vinategemea umoja wao tu na si vinginevyo.
Katika Qur'ani tukufu, Mwenyezi Mungu amewaamuru Waislamu washikamane na wawe wamoja. Umoja ni neema itokayo kwa Mola ambayo ilipotunzwa na kudumishwa katika zama za mwanzoni mwa Uislamu, iliwapa nguvu Waislamu na kuwawezesha kuwashinda maadui zao. Katika aya ya 103 ya Suratu Aal-Imran Mwenyezi Mungu anasema:" Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka". Shahidi Murtadha Mutahhari (R.A) amesema:"Waislamu, ni watu ambao wanamwabudu Mungu mmoja, na wanakiri na kuuamini Utume wa Nabii Mtukufu (SAW). Kitabu chao wote ni Qur'ani, na kibla chao wote ni Al-Ka'aba. Wanatekeleza pamoja na kwa namna moja Hija, wanasali namna moja, wanafunga saumu namna moja, wanafunga ndoa, wanafanya miamala ya biashara, wanalea watoto wao na wanazika maiti zao pia namna moja... Kwa hakika Waislamu wana mtazamo mmoja juu ya ulimwengu, wana utamaduni wa pamoja, ustaarabu mmoja na historia moja inayong'ara."
Mambo mengine yanayowaunganisha Waislamu na kuleta mshikamano baina yao ni msikiti, Sala za jamaa, Sala ya Ijumaa, Hija pamoja na lugha ya pamoja ya dini yao. Kuhudhuria kwenye minasaba hii, kwa kuzingatia lengo la pamoja la Waislamu ambalo ni kumwabudu Mwenyezi Mungu, kuna taathira kubwa mno katika kujenga na kuratibu umoja baina yao kuanzia ngazi ya shina, kieneo, kitaifa hadi kimataifa.
Lakini ni muhimu pia kuelewa kwamba umoja baina ya Waislamu haumaanishi asilani suala la wao kuwa na madhehebu moja. Makusudio ya umoja huo ni mshikamano baina ya wafuasi wa madhehebu tofauti, ambao licha ya hitilafu zao za kimadhehebu, wako kitu kimoja kukabiliana na ajinabi na adui wa pamoja wa dini yao. Madhumuni ya Umoja wa Kiislamu si kuzikusanya madhehebu zote kwa kuanzisha madhehebu moja au kuchanganya pamoja yale yanayokubalika na madhehebu zote na kuyatupilia mbali yale yanayozitafautisha. Bali madhumuni hasa ni kuwapanga na kuwaunganisha Waislamu katika safu moja ya kukabiliana na adui yao wa pamoja.
Umoja na mshikamano wa Waislamu ndio siri ya nguvu na uwezo wa Umma wa Kiislamu. Umoja wao ndio unaokithirisha mara mia bali hata mara elfu nguvu, zao za kukabiliana na maadui na kuwafanya watukuke na kuwa na nguvu na izza isiyo na mfano. Kwamba umoja ndio unaoleta ushindi, hii ni kanuni kuu na isiyo na shaka. Ikiwa mataifa ya Waislamu hayatoungana pamoja, Waislamu watasambaratika na watamezwa; na heshima na adhama yao itapotea. Na ndiyo maana Mwenyezi Mungu anatuambia katika aya ya 46 ya Suratul-Anfal ya kwamba:" Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri."
Qur'ani tukufu imezitaja hitilafu na mifarakano kuwa ni miongoni mwa adhabu za Mwenyezi Mungu kwa watu, kama inavyoeleza aya ya 65 ya Suratul-An'am ya kwamba:" Sema: Yeye ndiye Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu, au kukuleteeni fujo la mfarakano, na kuwaonjesha baadhi yenu jeuri ya wenzao. Tazama vipi tunavyo zieleza Aya ili wapate kufahamu."
Bwana Mtume Muhammad SAW amesema:"Kuwa pamoja (umoja) kwa umma wangu ni sababu ya kupata rehma, na kufarikiana ni sababu ya kupata adhabu".
Ukweli ni kwamba umoja na kuwa na msimamo mmoja kidini ni ngome imara ya kukabiliana na madola ya kidhalimu, na kuyafanya yashindwe kufikia malengo yao ya kikoloni. Ikiwa Waislamu, ambao wana maliasili chungu nzima za ardhini na vyanzo visio na mfano vya kiuchumi, watashikamana kikweli na dini yao na kuishikilia barabara kamba ya umoja wa Kiislamu, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, hakutokuwa na dola lolote lile, si la Mashariki wala Magharibi litakaloweza kuwanyongesha na kuwatawala. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndipo kwa hekima na busara kubwa, Imam Khomeini (M.A) akaitangaza wiki ya baina ya mwezi 12 hadi 17 Mfunguo Sita (Rabiul-Awwal) kuwa ni Wiki ya Umoja, ili kuwazindua Waislamu warejee kwenye umoja na mshikamano wao utakaowapa tena nguvu na izza waliyokuwa nayo. Tuhatimishe kipindi chetu hiki kwa maneno ya busara ya mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu umuhimu wa umoja baina ya Waislamu. Imam Khomeini amesema:"Enyi Waislamu wa dunia nzima! Imekuwaje, nyinyi ambao katika zama za mwanzoni mwa Uislamu, licha ya kuwa wachache mliyashinda madola makubwa na kujenga umma mkubwa wa Kiislamu na kibinadamu, hivi sasa licha ya kufikia karibu watu bilioni moja, na kuwa na hazina kubwa za utajiri ambao ni silaha kubwa kabisa, lakini mumekuwa duni na dhaifu kiasi hiki mbele ya adui? Je mnajua kwamba masaibu yenu yote yanatokana na mifarakano na hitilafu baina ya viongozi wa nchi zenu na kuishia baina yenu? Inukeni hapo mlipo, ikamateni Qur'ani Tukufu na itiini amri ya Mwenyezi Mungu ili mrejeshe tena utukufu wenu na adhama ya Uislamu azizi. Njooni msikilize mawaidha haya ya Mwenyezi Mungu pale anaposema:" Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja;". Simameni nyote kwa mapambano; mpambane kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; mpambane mmoja mmoja kukabiliana na majeshi ya shetani wa batini za nafsi zenu; na mpambane nyote pamoja kukabiliana na madola ya kishetani".
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)