Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 27 Disemba 2015 16:27

Umoja wa Kiislamu kwa mtazamo wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Umoja wa Kiislamu kwa mtazamo wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Waislamu wanaweza kujenga "Umma Mmoja wa Kiislamu" kwa kuwa na umoja na mshikamano.

Rais Rouhani amesema hayo Jumapili ya leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran. Katika hotuba yake hiyo Rais Rouhani ameashiria chimbuko na chanzo cha kuibuka vitendo vya utumiaji mabavu na mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu na kusema kuwa, utumiaji mabavu chimbuko lake ni fikra na aidiolojia ya makundi ambayo yana ufahamu na welewa usio sahihi kuhusiana na dini ya Kiislamu. Rais Rouhani amesema kinagaubaga kwamba, kuna haja ya kusimama na kukabiliana na fikra hizi mbovu za utumiaji mabavu. Amesema, kuna udharura wa kufutwa taswira hii bandia kuhusu na kuwaonesha walimwengu sura halisi na ya kweli ya Uislamu na Waislamu.

Hii leo hata waungaji mkono wa ugaidi wanaungama na kukiri kwamba, ugaidi na uchupaji mipaka ndio changamoto kubwa zaidi katika karne ya 21; hata hivyo kubainisha ukweli huo sio dawa mujarabu ya tatizo hilo, bali kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kivitendo za kukabiliana na mushkeli huo. Pamoja na hayo swali la kimsingi la kujiuliza ni kwamba, je ugaidi na uchupaji mipaka unaweza kutokomezwa kwa vita na mabomu, au kuna haja ya kutambua chimbuko la fikra zenyewe na kisha kufunga njia zake kupitia mazungumzo?

Ukweli wa mambo ni kwamba, makundi ya kigaidi kama al-Qaeda, Daesh, Boko Haram, al-Shabab na mengineyo ni matokeo ya fikra ghalati na potofu za makundi ambayo hayana mpaka wowote katika kutenda jinai zao; na himaya na uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati kwa makundi hayo havijawa na natija nyingine ghairi ya kuuangamiza Umma wa Kiislamu.

Ukweli ni kuwa, fikra na aidiolojia za kitakfiri zimekuwa sababu ya kukanyaga misingi ya utu na ubinadamu na hivyo fikra za uchupaji mipaka kuchukua wigo mpana zaidi. Hii ni katika hali ambayo, dini tukufu ya Kiislamu inasisitiza kwamba, wanadamu wote ni sawa katika misingi ya ubinadamu bila kujali rangi, dini, utaifa, maeneo yao ya kijiografia au madhehebu na itikadi zao. Inasikitisha kuwa, ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa kujua au kwa kutojua kuna watu wanatumiwa kama wenzo wa kutekeleza njama za kuzusha fakachi na mifarakano baina ya Waislamu na kuwagonganisha vichwa Waislamu wa Kisuni na Kishia, na hii ni hatari kubwa ambayo leo hii inaukabili Ulimwengu wa Kiislamu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwenye mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, Rais Hassan Rouhani ameashiria ukweli mwingine nao ni huu kwamba, hii leo adui ameanzisha njama nyingine mpya nayo ni kupotosha ukweli kuhusiana na dini ya Uislamu.

Kama alivyosisitiza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu katika mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran ni kuwa, hakuna hilali ya Kishia wala ya Kisuni; lakini baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati kama Saudi Arabia kwa kuwa na fikra za kuzusha mifarakano na kuchukua hatua katika uwanja huo, zimeandaa uwanja wa kujitokeza makundi kadhaa ya kimadhehebu na hivyo kupelekea kuweko tofauti za kijamii, kiutaifa na mipaka bandia baina ya Umma wa Kiislamu.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)