Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 27 Disemba 2015 06:52

Rais kufungua Mkutano wa Umoja wa Kiislamu leo

Rais kufungua Mkutano wa Umoja wa Kiislamu leo

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran asubuhi hii anatazamiwa kutoa hotuba katika ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unaofanyika hapa mjini Tehran.

Manouchehr Mottaki, Msemaji wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu inayoandaa mkutano huo amewaambia waandishi habari kwamba, mbali na hotuba ya Rais Rouhani, kikao hicho cha ufunguzi pia kitahutubiwa na wanazuoni na maafisa wa ngazi za juu wa nchi za Kiislamu. Amesema mkutano huo ambao unafanyika kwa mnasaba wa Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Wiki ya Umoja wa Kiislamu utahudhuriwa na wageni zaidi ya 300 kutoka nchi 70 duniani. Ameongeza kuwa mkutano wa mwaka huu utajadili mada kuu ya "Migogoro ya Sasa Katika Ulimwengu wa Kiislamu". Mottaki ameongeza kuwa mkutano wa mwaka huu utakuwa na kamati 12 ambazo zitajadili masuala kama vile sayansi na teknolojia, vyuo vikuu, utatuzi wa migogoro, tathmini ya migogoro katika ulimwengu wa Kiislamu na njia za kujikwamua, muqawama, familia, wanawake, biashara na vijana.

Mottaki ameashiria pia hali ya Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa na jeshi la nchi hiyo na kusema: "Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaki." Amesema Jumuiya hiyo inaitaka serikali ya Nigeria isitishe ukandamizaji wa Waislamu nchini humo na kuwachukulia hatua waliotenda jinai dhidi ya Waislamu katika mji wa Zaria.

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)