Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 08 Januari 2015 21:01

Ulimwengu wenye migogoro unahitajia mafundisho ya Mtume wa Rehma (saw)

Ulimwengu wenye migogoro unahitajia mafundisho ya Mtume wa Rehma (saw)

Ilikuwa miaka mingi ambapo watu walikuwa wakiishi katika taasubi, itikadi batili na khurafa.  Kwa amri yake Mwenyezi Mungu SWT, katika usiku usiosahaulika, rahma zake zilishuka Hijaz na ulimwengu ukashuhudia kuzaliwa Muhammad Al Mustafa SAW. Kwa kuzaliwa Mtume Mtukufu SAW, jangwa la ujahili na taasubi liligeuka na kuwa bustani ya ukarimu na kutafakari. Mtume huyo mtukufu alizaliwa katika mji Mtakatifu wa Makka katika familia ya waumini wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu. Alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal na hivyo kuijaza dunia kwa nuru yake yenye baraka. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za pongezi kwa mnasaba wa Maulid ya Nabii wa Rahma SAW.

@@@

Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu ni kumbukumbu ya baraka na neema zisizo na kikomo katika maisha ya mwanaadamu.  Bwana Mtume aliweza kuleta machipuo katika maisha ya mwanaadamu sambamba na kujaza nyoyo za watu na mafunzo ya Tauhidi au kumpwekesha Mwenyezi Mungu.  Aliweza kuvunja itikadi batili, ukabila na taasubi na badala yake kueleta urafiki, ubinaadamu na umoja sambamba na kuwaelekeza wanadamu katika ukweli kuhusu maumbile ya dunia na maarifa ya Mwenyezi Mungu SWT. Kwa msingi huo tunaweza kusema uzawa huu uliojaa baraka uliweza kuizawadia jamii ya wanaadamu tauhidi na uadilifu.

Kutokana na hima ya Mtume Muhammad SAW, katika miaka ya awali ya kudhihiri Uislamu kulishuhudiwa mabadiliko adhimu kwa misingi na vigezo vyenye thamani za juu. Mihimili muhimu ya mapinduzi hayo ilikuwa ni pamoja na kuondoa ubaguzi wa kijamii, kuelekea katika maadili bora, kuzingatia heshima ya mwanadamu, uadilifu na uhuru. Mtukufu huyo alikuwa mjini Madina kwa muda wa miaka 10 ambayo imetajwa kuwa muongo ulionawiri zaidi wa utawala  katika historia ya mwanaadamu. Hizo zilikuwa ni zama ambapo mfumo wa Kiislamu uliasisiwa na Mtume  SAW kuweza kuwasilisha kigezo  cha utawala wa kidini. Hicho ni kigezo ambacho kinaweza kutumika katika maeneo na zama zote. Kwa hakika mapinduzi aliyoleta Bwana Mtume  SAW  na mfumo wake wa utawala ulikuwa ramani ya njia kwa ajili ya wanaadamu wanaotaka kufikia ubora na ambao wanataka kufuata dini bora na iliyo wazi zaidi. Mtume SAW aliweza kuwasilisha mfano bora wa utawala wa kiserikali huko Madina na kuwazawadia wanaadamu.

Mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani Bibi Annemarie Schimmel anasema hivi kuhusu adhama ya kazi kubwa aliyoifanya Mtume wa Uislamu: "Mtume wa Uislamu alikuwa na nafasi ya aina yake katika mabadiliko ya kiroho ya mwanadamu. Alihuisha roho ya mwanadamu. Alizikomboa fikra za wanadamu na kuziondoa katika minyororo ya kijahili."  Bibi Annemarie Schimmel anaendelea kusema: "Nabii Muhammad aliwafundisha wanadamu jinsi ya kutumia vyema jicho, sikio, elimu na akili na akawapa bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba mwanadamu anaweza kudhibiti jua, mwezi na mbingu." Annemarie Schimmel anamalizia kwa kusema: "Kwa msingi huo kumtukuza kiongozi adhimu kama huyu humpa kila mwanadamu saada na hadhi kubwa."

Ukweli wa dunia ya sasa unaonyesha kuwa, mwanaadamu anahitajia utulivu na furaha ya kweli. Ongozeko la uzalishaji wa silaha haribifu, vita vya kujitanua, ubaguzi wa rangi, ukosefu wa uthabiti katika masoko ya dunia, umasikini njaa nk ni mambo ambayo yanahatarisha usalama na amani duniani. Ingawa tunaishi katika zama za ustawi mkubwa na wa kasi wa sayansi na teknolojia lakini bado tunashuhudia kuongezeka dhulma, ukatili na hujuma dhidi ya mataifa mbali mbali duniani.

Katika hali hii ya migogoro, ili dunia irejee katika utulivu na maadili mema inahitaji mafundisho ya kidini. Haya ni mafundisho ambayo Mwenyezi Mungu SWT aliwaletea wanaadamu kupitia Mtume wake wa mwisho Mohammad Al Mustafa SAW. George Bernard Shaw msomi nwa mwandishi mashuhuri wa Uingereza anasema: "Ili dunia ya leo itatue matatizo magumu yaliyopo inahitaji shakhsia kama vile Muhammad SAW ili iweze kutulia." Bernard Shaw katika sehemu nyingine ya matamshi yaliyo katika kitabu alichoandika mwaka 1936 chenye anwani ya ‘Genuine Islam' anasema: ‘Natabiri kuwa Uislamu utakumbatiwa na bara Ulaya katika siku za usoni. Dini ya Mohammad itaweza kuleta amani na saada duniani."

Mtume Muhammad SAW kama mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu aliteremshiwa Wahyi ili aweze kuwafahamisha na kuwafunza walimwengu kuhusu yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola Muumba. Kwa kubainisha njia ya kutekeleza mafundisho ya Mwenyezi Mungu, Mtume SAW alilenga kumletea mwanaadamu utulivu wa kiroho na pia ustawi wa kimaisha duniani. Utulivu wa kiroho ni kitu ambacho mwanaadamu wa leo anakihitaji sana. Mtume Mtukufu alitoa muongozo na Qur'ani Tukufu nayo pia imetoa nasaha kwa wanaadamu na iwapo watatekeleza miongozo na nasaha hizo, basi wataweza kuwa mbali na mifadhaiko na masaibu yaliyopo. Mafunzo ya Kiislamu kama vile utakasifu, kutosheka, ucha Mungu, kutawakali au kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuwasaidia wasiojiweza, subira, kujisitiri, kusamehe, kuwaheshimu wengine, kuishi kwa amani, kuwaheshimu wengine, kupambana na madhalimu, kuwasaidia wanaodhulumiwa, kutoa misaada, kuwa na hulka njema, kuwa na fikra huru, kutetea uadilifu na maadili mema ni kati ya nukta zilizojaa nuru katika mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Sira ya Mtume wa Rahma. Haya ni mambo muhimu ambayo mwanaadamu wa sasa anayahitaji hasa kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya migogoro ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni katika dunia. Mafundisho ya Qur'ani na Sira ya Mtume SAW ni chanzo cha kumletea mwanaadamu uhai mpya.

Katika Aya ya 157 ya Surat Al-A'Raaf katika Qur'ani Tukufu tunasoma namna Mtume SAW alikuja kuondoa mzigo mzito waliokuwa nao wanaadamu. Aya hiyo inasema:

"Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiyesoma wala kuandika, wanayemkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anayewaamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomuamini yeye, na wakamheshimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa."

Wapenzi wasikilizaji, ujahili, ukatili, ukabila na utumiaji mabavu, kupenda mali ya dunia na kuondoka umaanawi katika maisha ni kati ya mizigo mizito katika mabega ya mwanaadamu na ili kuweza kuondoa mizigo hiyo anahitaji mafundisho yaliyojaa nuru ya Mitume wa Mwenyezi Mungu na  bora zaidi kati ya mfundisho hayo ni mafundisho ya Mtume Mtukufu wa Uislamu.

Imam Ali AS anasema: "Muhammad, ni chaguo la Mwenyezi Mungu, ni balozi wa Wahyi, ni Mtume wa Rahma…Kwa hakika inatosha kumtanguliza Mtume SAW…ni Mtume aliye mtakasifu zaidi. Mfuateni kwani njia yake ni kigezo kwa kila mtu anayemfuata kwa uhakika. Mja bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule ambaye atamchukua Mtume kuwa kigezo na kufuata nyayo zake."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema Maulid ya Mtume SAW ni bishara ya rahma ya Mwenyezi Mungu kwa wanaadamu. Anaongeza kuwa: "Katika Qur'ani, uwepo wa Mtume umetajwa kuwa ni 'Rehema kwa walimwengu wote". Rehema hii haina kikomo; inajumuisha malezi, utakasifu, mafundisho na kuwaongoza wanaadamu katika njia nyoofu na kuwastawisha katika nyuga za misha ya kimaada na kimaanawi. Ni rahma ambayo si ya zama alizoishi bali ni ya zama zote za historia. Njia ya kufikia malengo hayo ni kutekeleza mafundisho ya Kiislamu ambayo mwanaadamu ameainishiwa.

Kwa maelezo hayo mwanaadamu wa zama hizi anahitajia mafundisho ya Kiislamu yenye umaanawi na uhai. Wanazuoni wana jukumu zito la kuwakumbusha walimwengu kuhusu mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Sira ya Mtume SAW. Kwa kufuata mafundisho ya Kiislamu mwanaadamu ataweza kuokoka na kuepuka mkondo wa maangamizi ya ustaarabu. Kwa hakika iwapo katika maisha yetu Mtume SAW atakuwa ruwaza njema au 'Uswatun Hasanah' kama alivyotajwa katika Qur'ani Tukufu, 'na tumuige katika imani yake, kutawakali kwake, ikhlasi na ushujaa wake, nidhamu na unadhifu wake na maisha yake yaliyotakasika basi maisha yetu yatashuhudia mabadiliko makubwa sana na nuru itakayoenea kila mahala.

Kwa mara nyingine tena tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za pongezi kwa mnasaba wa Maulid ya Nabii wa Rahma SAW.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)