Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 07 Januari 2015 12:10

Mwanamke bora katika mtazamo wa Kiislamu na nafasi yake katika kuleta umoja

Mwanamke bora katika mtazamo wa Kiislamu na nafasi yake katika kuleta umoja

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji katika kipindi hiki maalumu kinachojadili mitazamo tofauti inayopindukia mipaka kuhusiana na mwanawake na pia mtazamo wa Kiislamu kuhusiana na kiungo hiki muhimu katika jamii ya mwanadamu. Kama tunavyojua, nusu ya jamii ya kila nchi huundwa na wanawake. Leo kuna mitazamo tofauti duniani kuhusiana na nafasi ya mwanamke katika jamii. Kundi moja la watu lina mtazamo hasi na finyu sana kuhusiana na mwanamke ambapo linaamini kwamba mwanamke ni kiumbe wa daraja la pili na kwa msingi huo anapaswa kuzuiwa kujihusisha na shughuli zozote za kijamii. Katika upande wa pili kuna kundi jingine lililo na fikra za kupindukia mpaka ambapo linaamini kwamba mwanamke amedhulumiwa na kunyimwa haki zake za kimsingi katika historia na kwa hivyo anapaswa kuwekwa kwenye daraja moja na mwanaume na ikibidi apewe nafasi iliyo juu zaidi kuliko mwanaume. Kuhusu suala hili, Uislamu una mtazamo wa wastani unaompa mwanamke heshima na haki zake zote za kiutu na kimaumbile. Tutajadili suala hili kwa kutilia maanani nafasi ya umoja ya mwanamke wa Kiislamu katika familia na jamii, tukisisitiza juu ya sira na mafundisho ya Mtume Mtukufu kuhusiana na suala hili, karibuni.
********
Katika zama za kale baadhi ya jamii na mataifa yalikuwa na fikra potofu na za kupindukia mipaka kuhusiana na mwanamke ambapo alikuwa akichukuliwa kuwa kiumbe wa daraja la pili na ambaye hakupasa kupewa haki zozote za kiutu katika jamii. Kwa msingi wa fikra za mataifa na watu hao mwanamke ni mtu ambaye hakuwa na haki zozote za kiutu na wala hangeweza kufikia ukamilifu wa kimaanawi. Kwa mfano Aristotle, mwanafalsafa wa Ugiriki ya zamani, alikuwa akiamini kwamba mwanamke ni kiumbe aliye na kasoro katika maumbile yake na kwa hivyo hana sifa za kiutu zinazofanana na za mwanaume. Fikra hii potofu ilienea sana katika pembe tofauti za dunia katika zama hizo. Ni wazi kuwa fikra hii bado inaonekana katika baadhi ya nchi duniani ambapo mwanamke amenyimwa haki zake za kiraia na wala haruhusiwi kushiriki katika masuala ya kisiasa wala kijamii. Kwa mfano watafiti wa masuala ya kijamii wanafananisha hali ya wanawake katika baadhi ya nchi za Kiarabu na ile iliyokuwa ikitawala katika mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Hii ni kwa sababu katika mifumo ya nchi hizo bado kuna kiwango kikubwa cha ubaguzi unaofanywa dhidi ya wanawake ambapo hunyimwa haki za kimsingi na kubanwa katika kupewa nafasi za kazi na suhula za kuendeshea maisha. Makundi ya kigaidi ya Taliban, Daesh na Boko Haram ambayo hupiga nara zinazoonekana kidhahiri kuwa za Kiislamu leo hii yamekuwa tishio kubwa kwa haki za wanawake katika nchi za Afghanistan, Iraq, Syria na Nigeria.
Katika upande wa pili, na ikiwa ni katika kukabiliana na fikra hii ya kupindukia mipaka katika historia ndefu ya wanawake kunyimwa haki zao za kimsingi katika nchi za Magharibi, kuna baadhi ya wanawake na wanaume waliojitokeza katika nchi hizo mwanzoni mwa karne ya 20 kwa lengo la kufidia na kurejesha haki hizo zilizoporwa na kukanyagwa na wanaume wa ulimwengu wa Magharibi. Ili kufikia lengo hilo harakati inayojulikana hii leo kama harakati ya Feminism ilianzishwa. Fikra hiyo inawataka wanawake kusimama na kupigania haki zao walizoporwa na wanaume. Katika kampeni zake harakati hiyo imekuwa ikifuatilia malengo ya kimapinduzi kama vile ya kupigania usawa wa kijinsia, kupuuza misingi ya ndoa na thamani za mama, kutetea uhuru wa ngono, kuavya mimba na kumshajiisha mwanamke apuuze thamani za maadili na mifungamano ya kifamilia. Mwenendo huu wa kupindukia mpaka wa harakati ya ufeministi licha ya kuwa umejaribu kumuondolea mwanamke baadhi ya matatizo aliyokuwa nayo lakini umemletea yeye na jamii nzima kwa ujumla, matatizo mengine chungu nzima. Kuhusiana na suala hili Ustadh Murtadha Muttahari, mwanafikra wa Kiislamu wa Iran anasema hivi katika kujaribu kukabiliana na fikra hii potofu ya ufeministi: "Zamani utu wa mwanamke ulisahaulika na katika zama hizi hali yake ya kuwa mwanamke imesahaulika." Suzan Faludi mwandishi wa Marekani pia anaamini kwamba kulikuwa na ujumbe mwingine maalumu uliokuwa umejificha nyuma ya furaha ya kuadhimishwa ushindi huu wa kidhahiri wa wanawake. Ujumbe huu ulikuwa ukiwaambia wanawake: "Hivi sasa mko huru na sawa lakini hakuna wakati ambao mumekuwa na hali mbaya kama hii."
Wafeministi wenye misimamo ya kupindikia mipaka zamani walikuwa wakipinga vikali nafasi ya kimsingi ya mwanamke, kuwa kwake mama na kumlea mwanawe na kudai kuwa nafasi hizo zilikuwa zikimzuia kujiendeleza katika jamii. Hii ni katika hali ambayo hii leo wafeministi wengi wanakiri wazi kwamba mwanamke kuwa mama ni kilele cha furaha yake maishani. Kwa msingi huo fikra mpya za kutetea haki za mwanamke, kutetea haki yake ya kuwa mama ni msingi muhimu na zama hizi zinatajwa kuwa zama za mwanamke kurejea katika umama. Kuhusiana na suala hili Toni Grant mwandishi wa Marekani anasema: "Mwanamke wa leo bado ana hamu ya kulinda nafasi yake ya kuwa mama na anafanya juhudi kubwa ya kudhihirisha hali hiyo."
Mitazamo hii miwili ya kupindukia mipaka kuhusiana na mwanamke imepelekea kupuuzwa na kutotumika vizuri nafasi yake ya kuleta utulivu na umoja katika jamii. Mbali na mitazamo miwili hii ya kupindukia mipaka kuna mtazamo mwingine wa wastani kuhusiana na mwanamke ambao unatokana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Katika mtazamo huu, licha ya kuwa mwanamke na mwanaume wana tofauti za kimwili na kiroho lakini wakati huohuo wana haki sawa za kiutu. Kwa mtazamo wa Kiislamu, mwanamke kama alivyo mwanadamu mwingine yeyote, anaweza kutumia nafasi yake ya asili na kushiriki kwa njia tofauti katika shughuli za kijamii. Nafasi hii ya juu ya mwanamke katika Uislamu inaonekana wazi katika sehemu tofauti za maneno na mafundisho ya Mtume wetu Mtukufu Muhammad (saw), Mtume ambaye aliheshimu sana nafasi ya mwanamke na kumpa hadhi kubwa katika jamii. Daima alikuwa akiusia watu kuwaheshimu na kuamiliana vyema na wanawake na kuwaonyesha huruma. Alikuwa akisema: "Hawawakirimu wanawake isipokuwa Wakarimu na hawawadhalilishi wanawake isipokuwa watu waovu."
Muamala wa Mtume na wake zake pia ulikuwa wa kuvutia sana na uliojaa mapenzi, huruma, heshima, uadilifu na usawa. Muamala wake uliojaa upendo na heshima na binti yake Fatima (as) pia ni wa kupigiwa mfano. Mara nyingi alikuwa akiubusu mkono wa binti yake na kusimama na kumuacha sehemu aliyokuwa ameketi ili binti yake huyo apate kuketi. Kuhusu binti yake huyo mtukufu na mpendwa, Mtume (saw) alikuwa akisema: "Fatima ni sehemu ya mwili wangu. Kila mtu anayempenda huwa amenipenda na kila anayemuudhi huwa ameniudhi mimi."
Mtume pia alifanya juhudi kubwa za kuwapa wanawake nafasi za kijamii na kuwawezesha kuainisha mustakbali wao. Kwa msingi huo alikuwa akiruhusu wanawake wahudhurie vikao vyake vya beia na misafara ya hijra.
Nafasi ya mwanamke katika familia akiwa kama msimamizi na mwendeshaji wa masuala ya nafsi, huruma na kiroho wa familia hiyo huwa na umuhimu mkubwa katika kuleta mazingira ya utulivu na usalama wa kiroho wa mume na watoto wake nyumbani. Kama mwanamke hataweza kuandaa na kuleta mazingira hayo ya utulivu nyumbani na kwenye familia basi ni wazi kuwa familia hiyo itakabiliwa na pengo kubwa la mapenzi na utulivu wa kiroho jambo ambalo bila shaka mwishowe litakuwa na athari hasi katika jamii.
Moja ya nukta muhimu za wanawake wakiwa walinzi na walezi wa jamii ni kuleta umoja na mfungamano katika jamii hiyo. Mwanamke ni msingi na nguzo kuu ya familia. Iwapo mwanamke ataelewa vyema nafasi hii na kuilea familia yake kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu ni wazi kuwa anaweza kuwa mfano bora wa kuigwa na watoto wake. Iwapo mwanamke kama huyo atazingatia masuala ya umoja na kuondoa hitilafu kati ya jamaa wa familia, ni wazi kuwa atawalea watoto vizuri na kuwakabidhi kwa jamii, ambapo watu kama hao wanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuondoa hitilafu tofauti zikiwemo za kimadhehebu kwenye jamii. Watu kama hao bila shaka wanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha umoja wa Waislamu na hivyo kuandaa uwanja unaofaa kwa ajili ya kulindwa Uislamu usije ukadhuriwa na maadui. Kwa ufupi ni kuwa, mwanamke wa Kiislamu aliye na msimamo na mwamko sahihi wa Kiislamu anaweza kuelea familia nzuri iliyosimama juu ya misingi na mafundisho sahihi ya Kiislamu na hatimaye kuweza kuleta mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kimaadili kwenye jamii.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki maalum. Basi hadi wakati mwingine tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema kwaherini

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)