Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 06 Januari 2015 14:06

Umoja wa umma wa Kiislamu, vizuizi na changamoto

Umoja wa umma wa Kiislamu, vizuizi na changamoto

Hivi sasa tumo katika Wiki ya Umoja kati ya Waislamu ambayo ilitangazwa na hayati Imam Khomeini kutokana na hitilafu za mapokezi kuhusu siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (saw). Wiki hiyo inaanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal. Makala hii inazungumzia Umoja wa Umma wa Kiislamu, Vizuizi na Changamoto.
Umoja wa Umma wa Kiislamu ni lengo muhimu na aali ambalo wanafikra na maulamaa wa Kiislamu wamekuwa wakifanya jitihada kubwa tangu zama za awali za Uislamu kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Hadi sasa kumetolewa fikra nyingi na kuitishwa vikao na mikutano chungu nzima kujadili kadhia ya udharura wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya Waislamu wote.
Udharura wa umoja na mshikamano wa Kiislamu umesisitizwa mno katika maandiko ya kidini na hoja za kimantiki na kiakili. Hata hivyo inasikitisha kwamba Waislamu wanapokaribia kuungana na kuimarisha umoja na mshikamano wao hujitokeza vizuizi chungu nzima ambavyo kunahitajika juhudi kubwa, tadbiri na mwamko wa Waislamu ili kuweza kuviondoa na kukabiliana navyo. Baadhi ya vizuizi na vikwazo vya umoja wa Waislamu vinatokana na hitilafu za ndani ya Umma wa Kiislamu japokuwa hapana shaka kwamba wakoloni na madola ya kibeberu daima yamekuwa yakifanya njama za kuzusha hitilafu na mifarakano katika Umma wa Kiislamu.
Umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu ndio nguvu kubwa isiyoshindika ya umma huu ambayo inaweza kutumiwa na Waislamu kukabiliana na madola yanayoingilia masuala yao na kutaka kupora utajiri na maliasili zao. Pamoja na hayo yote tunapaswa kuelewa kwamba, lengo kuu la wakoloni na madola ya kibeberu ni kuuondoa Uislamu katika maisha ya kawaida na kuidhoofisha dini hiyo inayopambana na dhulma na uonevu ambayo daima imekuwa kizuizi kikubwa dhidi ya siasa za kibeberu na tamaa za madola kikoloni.
Maadui wa Uislamu wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali katika kuzuia umoja na mshikamano wa Kiislamu. Maadui hao hufanya jitihada za kutia chumvi na kukuza hitilafu ndogondogo za kimitazamo zinazotokea kati ya Waislamu na baadaye kuzitumia kwa ajili ya kuzusha mifarakano kati yao. Maadui hao hutumia hitilafu au tofauti za kimadhehebu, kilugha, kikaumu na kikabila na kadhalika kama nyenzo za kuzusha fitina na kuwatenganisha Waislamu. Ni wazi kuwa jiografia ya ulimwengu mkubwa wa Kiislamu inajumuisha makabila, kaumu, lugha, madhehebu na mataifa tofauti. Hata hivyo tofauti hizo za kimaumbile au hitilafu ndogondogo hazipaswi kuwa tatizo kubwa au kizuizi cha umoja na mshikamano.
Katika upande mwingine nchi za Magharibi zinaanzisha au kuhamasisha makundi yenye misimamo ya kupindukia na bandia katika ulimwengu wa Kiislamu kama lile la Daesh kwa lengo la kuzuia umoja na mshikamano wa Waislamu. Kwa mfano sisi sote tunaelewa ni kwa kiwango gani makundi mawili ya Kiwahabi na Kibahai yalivyowasababishia Waislamu matatizo na mashaka makubwa mno katika kipindi cha karne mbili zilizopita.

>>>

Historia ya sasa ya dunia ya Kiislamu inaonesha kwamba madola ya kikoloni mara nyingi huwatumia watu ambao kidhahiri ni Waislamu lakini hakika yao ni watu waliopotoka na wanaotumiwa kuzusha mifarakano na hitilafu katika Umma wa Kiislamu. Watu wa aina hii wamekuwa wakijitokeza wakiwa na anwani na sura mbalimbali, lakini sifa inayowakutanisha pamoja wote ni kuzua itikadi zinazokwenda kinyume na misingi ya awali ya Uislamu ambazo lengo lake kuu ni kuzusha mfarakano na hitilafu. Watu hawa wenye mitazamo potofu na isiyokuwa sahihi wanapatikana katika nchi mbalimbali.
Baada ya kukithiri mitandao ya intaneti na kanali mbalimbali za televisheni za satalaiti katika miaka ya hivi karibuni mwenendo wa kuzusha mijadala na kueneza itikadi zisizokuwa sahihi dhidi ya Uislamu na kukuza maudhui zinazozusha mfarakano na hitilafu, imeongeza zaidi. Hii ni moja ya mbinu zinazotumiwa na wakoloni kwa ajili ya kueneza hitilafu na kuzuia umoja na mshikamano kati ya Waislamu.
Wataalamu wa masuala ya ulimwengu wa Kiislamu wanaamini kuwa vizuizi vya umoja ndani ya ulimwengu wa Kiislamu vinaweza kuwa na madhara na hatari kubwa hasa pale zinapotumiwa vibaya na madola ambayo daima yananyemelea fursa kama hiyo kutoa pigo na dharba kali kwa Umma wa Kiislamu. Wataalamu hawa wanasema kuwa, njama hizo zinaweza kuzimwa kirahisi hasa kwa kutilia maanani kwamba, Waislamu wa madhehebu zote wanashirikiana katika mambo mengi ya kimsingi kama itikadi ya Mungu Mmoja, Mtume Mmoja, kitabu kitakatifu kimoja cha Qur'ani, kibla kimoja na masuala mengi ya kisheria na kiibada. Si hayo tu, bali wanafikra wengi wa masuala ya Kiislamu wanasisitiza kuwa, hata tofauti za kimadhehebu haziwezi kuwazuia Waislamu kuwa na umoja na mshikamano kwa kuzingatia nguvu kubwa na mambo mengi ya kimsigi yanayowakutanisha pamoja kama itikadi tulizozitaja punde kidogo.
Kimsingi maana ya umoja na mshikamano kati ya Waislamu si kuwataka wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu kutupilia mbali itikadi zao, bali lengo kuu ni kujenga maelewano na mshikamano mbele ya adui wao wa pamoja. Naam, tofauti hizo za kimadhehebu zinaweza kujadiliwa kwa njia za kimantiki na busara katika vikao vya mijadala ya kielimu vya wanazuoni na maulamaa wa Kiislamu na kufikia nukta za wazi. Hapana shaka kuwa makelele na malumbano yasiyokuwa ya kielimu katika vikao vya umma kuhusu masuala ya kitaalamu hayawezi kuwa na matunda ya kuridhisha. Tunaweza kusema hapa kuwa moja ya vizuizi vya umoja na mshikamano katika umma ni kutolewa mijadala kama hiyo ya kielimu na kitaalamu kuhusu masuala ambao Waislamu wanatofautiana juu yake katika vikao vya umma na kwa njia ya kichochezi.

>>>

Dini tukufu ya Kiislamu inawalingania wafuasi wake wote kutumia akili na kutafakari na kuzidisha maarifa na elimu yao kadiri inavyowezekana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuwa na maarifa na elimu huzuia mifarakano na ukosefu wa maelewano. Inasikitisha kuona kwamba katika zama za sasa za mawqasiliano na utandawazi Waislamu wa madhehebu moja hawajui kabisa au wana maarifa finyu kuhusu itikadi za ndugu zao wa madhehebu nyingine ya Kiislamu. Upungufu huu wa maarifa kuhusu itikadi za madhehebu tofauti za Kiislamu umekuwa moja ya vizuizi vya umoja na mshikamano wa Kiislamu na umekuwa ukisababisha mambo mengi ya kusikitisha katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu Ustadh Murtadha Mutahhari anasema: "Tishio linalowakabili Waislamu kutokana na hali ya kutofahamiana na kudhaniana vibaya ni kubwa zaidi kuliko lile linalotokana na tofauti zao za kimadhehebu." Ustadh Shahid Mutahhari anasema kuhusu taathira mbaya za kutofahamiana kati ya Waislamu na mchango wake katika kukuza hitilafu kwamba: "Tofauti za kimadhehebu na kiitikadi ni jambo ambalo limekuwepo katika zama zote lakini jambo linalobadilika kila wakati na katika kila zama ni ukosefu wa maelewano na kutofahamiana kwa pande husika. Kwa sababu hiyo, moto wa ugomvi, malumbano na mifarakano huchochewa zaidi na zaidi."
Kutofahamiana na ukosefu wa maelewano kati ya wafuasi wa madhehebu tofauti hufuatiwa na tuhuma zisizokuwa na msingi kati ya pande husika. Tuhuma hizo hujibiwa kwa tuhuma mfano wake, suala ambalo huchochea zaidi moto wa hitilafu na ukosefu wa maelewano. Ni jambo lililowazi kwamba maadui wa dini ya Kiislamu hutumia hali hiyo na kufanya jitihada za kushadidisha zaidi anga ya ukosefu wa maelewano na hitilafu kati ya Waislamu. Hali hiyo inapoambatana na taasubi na fikra finyu huwa na maafa makubwa zaidi.
Sheikh Muhammad Abu Zahra ambaye alikuwa miongoni mwa maulamaa wa chuo cha al Azhar cha Misri amesema: "Tofauti na hitilafu zilizoko kati ya Waislamu zimepenya na kuingia zaidi katika fikra, hisia na nyoyo zao kutokana na taasubi na chuki za kikaumu na kimadhehebu kwa kadiri kwamba Muislamu mmoja humuangalia Muislamu mwenzake anayehitilafiana naye kifikra kama adui aliyeko mafichoni dhidi yake na si kama mtu mwenye mitazamo tofauti kama yeye anayefanya jitihada za kujua hakika ya sheria za Mwenyezi Mungu."

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)