Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 05 Januari 2015 14:53

DAESH; wachafuaji wa sura safi ya Uislamu wa asili wa Bwana Mtume SAW

DAESH; wachafuaji wa sura safi ya Uislamu wa asili wa Bwana Mtume SAW

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kuadhimisha Wiki ya Umoja. Katika kipindi chetu cha leo mbali na kubainisha umuhimu wa kujenga umoja baina ya Waislamu tutazungumzia pia nafasi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika kuchafua jina na sura ya Uislamu na kukwamisha kupatikana umoja kati ya jamii za Kiislamu. Endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi.
MUZIKI
Tumo kwenye masiku ya Wiki ya Umoja baina Waislamu. Kulingana na hadithi iliyopokelewa na Ahlu Sunna, tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal ndiyo siku aliyozaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Wafuasi wa madhehebu ya Shia wanasema tarehe 17 Rabiul Awwal ndiyo siku aliyozaliwa nabii huyo wa rehma. Hitilafu kama hizi sio chache kati ya madhehebu za Kiislamu; lakini muhimu ni kwamba Waislamu wote wanaiamini Qur'ani moja na mafundisho ya Mtume wao mmoja. Hitilafu hizo si sababu ya kuwepo uadui, chuki na mifarakano baina ya madhehebu za Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kipindi cha baina ya siku zinazohitilafiana hadithi zilizopokelewa na Masunni na Mashia kuhusu siku aliyozaliwa Bwana Mtume kimepewa jina la Wiki ya Umoja. Imam Khomeini (R.A) marjaa mkubwa katika ulimwengu wa Kishia na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa akiuzungumzia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni ushindi wa Waislamu wote duniani na kurejea izza ya Uislamu na wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu. Kwa mantiki hiyo kuunga mkono harakati zote za Kiislamu bila kujali ni za madhehebu gani ni miongoni mwa misingi ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Na ndiyo maana tunashuhudia kuwa japokuwa wananchi wa Palestina ni wafuasi wa madhehebu ya Ahlu Sunna lakini malengo matukufu ya wananchi wa Palestina na kukombolewa masikiti wa Al Aqsa kutoka kwenye makucha ya Wazayuni ni miongoni mwa misingi mikuu ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu. Aidha kama ambavyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaiunga mkono kwa uwezo wake wote Hizbullah ya Lebanon ambayo ni ya wafuasi wa madhehebu ya Shia na moja ya mihimili mikuu ya muqawama katika kupambana na utawala ghasibu wa Kizayuni, inaiunga mkono pia harakati ya Hamas ya wafuasi wa madhehebu ya Sunni ambayo ni mhimili mkuu wa muqawama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Katika anga kama hiyo baada ya kugonga mwamba hatua zote za madola ya Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni mnadi na mlinganiaji wa umoja katika ulimwengu wa Kiislamu, madola hayo yameamua kupambana na fikra za Uislamu wa asili wa Bwana Mtume kupitia ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa kuchafua sura ya rehma, amani, urafiki na kutetea haki na uadilifu ya Uislamu. Ni katika zama hizi ambapo tunashuhudia kuibuka kwa harakati za kufurutu mipaka katika Ulimwengu wa Kiislamu. Harakati ambazo japokuwa cheche zake zimewahi kushuhudiwa katika zama zote za historia ya Uislamu, lakini hazijawahi kuvuma duniani wala kufanya jinai kwa kiwango kama hiki kinachoshuhudiwa hivi sasa. Jinai nyingi za makundi yenye kufurutu ada kama lile la Daesh hazijawahi kushuhudiwa hata katika zama za Karne za Kati kwa kimombo Middle Ages wakati wingu la vitisho na mauaji lilipokuwa limetanda katika bara zima la Ulaya. Suali la kujiuliza, ni kwa nini harakati za kufurutu mpaka na kigaidi zinaibuka katika Ulimwengu wa Kiislamu katika karne ya 21 na katika zama ambapo dunia iko mithili ya kijiji kimoja? Hivi kweli ingeliwezekana kuibuka na kushamiri makundi haya pasina kupata misaada na uungaji mkono wa nchi zinazojidai kuwa zimeendelea na kustaarabika?
MUZIKI
Suala la hitilafu baina ya Waislamu haliko baina ya madhehebu moja na nyengine tu bali hata maulama wa madhehebu moja wanahitilafiana pia. Kwa mfano katika madhehebu ya Shia, hutokezea mujtahidi wawili wakatoa fatwa mbili zinazotafautiana kikamilifu juu ya maudhui moja. Hata hivyo hitilafu hizo katu hazijawa sababu ya kuwepo chuki na uadui baina yao. Bali ni kinyume chake, kwamba yeyote kati ya maulama hao hao wenye rai zinazotafautiana humfuata alimu mwenzake na kusali nyuma yake katika Sala za jamaa. Hali iko hivyo hivyo pia kati ya maulama wa Kisuni juu ya hukumu na masuala mengi ya dini. Kabla ya maadui kuchochea moto wa mifarakano baina yao, wafuasi wa madhehebu tofauti za Kiislamu wamekuwa wakiishi kwa amani na masikilizano baina yao bali na hata wasiokuwa Waislamu kwa miaka na miaka bali kwa karne kadhaa. Kwa sababu kuheshimu imani na itikadi za wasiokuwa Waislamu ilikuwa ndio sira ya Bwana Mtume na Ahlu bayt zake. Kwa hivyo pale suala hili la mahusiano na kuishi kwa amani na masikilizano linapohusisha Waislamu wenyewe kwa wenyewe wanaounganishwa na mafundisho ya Mtume wao mmoja na kitabu chao kimoja cha Qur'ani, kuheshimiana huko huwa na umuhimu maradufu. Kwa kuzingatia Sunna za Bwana Mtume na Ahlu bayt zake, Imam Khomeini (R.A), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wanasisitiza juu ya umoja baina ya madhehebu za Kiislamu licha ya hitilafu zote zilizoko baina ya madhehebu hizo. Ukweli ni kwamba mambo yanayoziunganisha pamoja madhehebu mbalimbali za Kiislamu ni mengi kuliko yanayoleta hitilafu baina yao. Kama ni hvyo kuna sababu gani ya kuwepo chuki na uadui kama ule unaofanywa kwa jina la Uislamu na makundi ya kitakfiri na kigaidi kama Daesh? Qur'ani tukufu inauelezea Uislamu kuwa ni dini ya rehma na kuishi kwa amani na masikilizano; na yeye mwenyewe Bwana Mtume Muhammad SAW ametufunza kwamba Muislamu, ni yule ambaye watu huwa katika salama na amani kutokana na shari ya mkono wake na ulimi wake. Mwenyezi Mungu Mtukufu amemtambulisha Mtume wake huyo kuwa ni rehma kwa walimwengu. Na kila anayetamka shahada mbili anahesabika kisharia kuwa ni Muislamu; na hili jambo wanalokubaliana wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu. Kwa hivyo vitendo vinavyofanywa na kundi la Daesh havina uhusiano wowote na mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW.
MUZIKI
Moja ya nukta ambazo Maimamu wote watoharifu wa kizazi cha Bwana Mtume SAW waliitilia mkazo ni kulindwa heshima na haki za wanadamu wote. Kwa mfano, katika kipindi kifupi cha utawala wa Imam Ali (AS), mtukufu huyo alisisitiza na kulitilia mkazo suala la kulinda haki, si za Waislamu pekee, bali hata za wale wote wasiokuwa Waislamu ambao walikuwa wakiishi katika ardhi zilizoko chini ya mamlaka ya utawala wa Kiislamu. Lakini kundi la kitakfiri la Daesh linamkufurisha kila asiyekuwa na fikra sawa na za kundi hilo na kila asiyefuata imani na itikadi batili na potofu kuhusiana na mafundisho ya Uislamu lilizonazo kundi hilo, na kumwona kuwa ni mtu anayestahili kuuawa. Hali ya kuwa, madamu mtu au kundi la watu halijabeba silaha kupiga vita imani na itikadi za Kiislamu au kuvamia ardhi na kuhujumu matukufu ya Waislamu, Uislamu hautoi ruhusa kwa wafuasi wake kuchukua hatua yoyote dhidi ya mtu au kundi hilo. Tabia na mwenendo wa Bwana Mtume na Ahlu bayt zake ni ithbati na ushahidi tosha wa suala hili. Ukweli ni kwamba ukatili na jinai za kinyama zinazofanywa dhahiri shahiri na kundi la Daesh pamoja na makundi mengine ya kigaidi katika katika ardhi za Iraq na Syria na za nchi nyengine za Kiislamu, na sisitizo la serikali na vyombo vya habari vya Magharibi la kuvihusisha vitendo hivyo na Uislamu havina lengo jengine ghairi ya kuzusha hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu na kuchafua sura ya Uislamu.
Hatua ya madola ya Magharibi ya kuyaunga mkono na kuyasaidia kwa zana makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na ya kitakfiri katika nchi za Kiislamu inalenga kudhibiti na kupotosha mkondo wa wimbi la mwamko wa Kiislamu katika eneo. Lengo la maadui wa Waislamu katika kuyaunga mkono makundi hayo ni kuvunja nguvu na uwezo wa vuguvugu la mwamko uliojitokeza katika nchi za Kiislamu na kulisahaulisha vuguvugu hilo na masuala ya asili yanayoukabili Ulimwengu wa Kiislamu likiwemo la kitisho cha utawala wa Kizayuni. Akiashiria nukta hiyo katika kuifanyia upembuzi dhati halisi ya makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na ya kigaidi katika nchi za Kiislamu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei amesema:"Badala ya kikundi cha matakfiri kushughulishwa na utawala khabithi wa Kizayuni, kinatumia jina la Uislamu na sheria zake kukufurisha akthari ya Waislamu na kuandaa mazingira ya kuzusha vita, machafuko na hitilafu; na ni kwa sababu hiyo, kuwepo kwa tapo hili la kitakfiri ni bishara njema kwa maadui wa Uislamu".

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anaashiria sehemu ya aya tukufu ya Qur'ani inayoashiria sifa ya Waislamu kwamba ni اَشدّاء علیَ الکُفّارِ رُحَماء بَینَهُم, yaani wakali kwa makafiri na wanaohurumiana wao kwa wao, na kueleza kama ninavyomnukuu:"Tapo la kitakfiri linaipuuza amri hii ya wazi kabisa ya Mwenyezi Mungu na kuwagawa Waislamu wenyewe baina ya 'Waislamu na makafiri na kuwapiganisha wao kwa wao'. Ayatullah Khamenei anahoji:"Kwa hali hii mtu anaweza kuwa na shaka yoyote kwamba kuwepo kwa harakati hii na misaada ya fedha na silaha inayopata hakutokani na vyombo vya usalama na vya kikhabithi vya madola ya kiistikbari na kuwa harakati hii ni kibaraka wa madola hayo?"
Ukweli wapenzi wasikilizaji ni kwamba kundi la kitakfiri na kigaidi la Daesh ni silaha na wenzo unaotumiwa na Magharibi kueneza wimbi la sumu ya hofu na uadui juu ya Uislamu. Kwa hivyo Wiki ya Umoja na vikao na makongamano mbalimbali yanayofanyika katika wiki hii katika nchi za Kiislamu, ni fursa kwa maulama wa Kiislamu na shakhsia wenye fikra huru wa kila madhehebu katika Ulimwengu wa Kiislamu kuwataalamisha na kuwaelimisha Waislamu kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW na kitabu kitukufu cha Qur'ani ni nguzo na mihimili mikuu ya umoja na mshikamano baina ya Waislamu, na kwamba vitendo vinavyofanywa na makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka na ya kigaidi kama Daesh vinalenga kuchafua jina na sura ya Uislamu, ambayo ni dini ya amani na ya kutetea haki na uadilifu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)