Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 15 Januari 2014 14:17

Uenezaji mawimbi ya hitilafu kupitia kanali za habari

Uenezaji mawimbi ya hitilafu kupitia kanali za habari

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujumuika nami katika kipindi kingine cha Makala ya Wiki ambacho leo kitazungumzia umuhimu wa umoja wa Waislamu na njama za maadui za kuvunja safu hiyo ya umoja. Karibuni....

Bwana Hempher, jasusi wa Uingereza ambaye alifanya harakati kubwa Mashariki ya Kati katika karne ya 18, anaandika katika moja ya kumbukumbu zake kama ninavyo nukuu: "Kabla ya safari kuelekea nchini Iraq, nilikuwa na kikao na mmoja wa viongozi wa Uingereza na aliniambia hivi: "Jukumu kubwa ulilonalo katika safari hii ni kuhakikisha unazusha hitilafu kati ya Waislamu, hitilafu ambazo zitawapelekea kutengana wao kwa wao. Hii ni kwa sababu haiwezekani sisi Waingereza kupata maendeleo na kuboresha hali ya ustawi wa jamii kwa asilimia 100 isipokuwa kwa kuwasha moto wa fitina na hitilafu katika makoloni yetu yote. Wakati kutakapoibuka tofauti na hitilafu kati yao na kugawika nguvu na muhimili wa makoloni hayo, sisi ndipo tutakapoweza kuzikoloni nchi hizo kwa urahisi." Mwisho wa kunukuu.

******

Hii ni kauli mbiu ya tangu zamani ya wanasiasa wa Uingereza na Magharibi inayosema "Zusha hitilafu utawale." Mpango wa kuibua hitilafu kati ya wafuasi ya madhehebu za Kisuni na Kishia, ni siasa zilizoandaliwa na mabeberu kwa njia tofauti kwa kipindi cha miaka mingi iliyopita. Kupigia upatu nukta za tofauti kati ya madhehebu za Kiislamu na kufumbia macho nukta zinazoziunganisha pamoja madhehebu hizo ni miongoni mwa njama za kuwasha moto wa fitina kati ya Waislamu duniani zinazotekelezwa na maadui. Kwa bahati mbaya baadhi ya Waislamu waliodanganyika wamekuwa mamluki na watekelezaji wa malengo ya mabeberu ya kuzusha fitina na mifarakano baina ya Waislamu. Mfano wa wazi kabisa wa suala hilo, ni wa waendeshaji wa kanali za televisheni matangazo kwa njia ya satalaiti zinazoonekana kidhahiri kuwa ni za kidini, kanali ambazo hazina lengo jingine ghairi ya kuzusha hitilafu kati ya madhehebu za Kiislamu. Nyaraka zilizoko nyuma ya pazia la baadhi ya kanali hizo zinaonyesha kuwa, gharama kubwa mno zinazotumika kuendesha kanali hizo, zinadhaminiwa na baadhi ya nchi zikiwemo Marekani, Saudi Arabia na Uingereza. Kwa hakika ushawishi wa kanali hizo unaweza kuwaathiri Waislamu wa madhehebu za Kisuni na Kishia. Bila shaka Mawahabi nao wanaitumia kikamilifu fursa hiyo kueneza itikadi zao potofu kwa kutumia jina la Ahlus Sunna, hali ya kuwa itikadi zao zinapingana na madhehebu hiyo. Aidha katika kanali hizo huwa hakutangazwi jambo jingine ghairi ya kutusi madhehebu za Kiislamu, kuzifanyia istihzai na kutoa maneno machafu yasiyofaa dhidi ya Waislamu wengine kwa kupitia matangazo ya moja kwa moja (Live) katika kanali hizo. Kwa kutoa mfano, kanali ya televisheni iitwayo (Ahlu Bayti) inayojiarifisha kuwa ya Kishia, katika kuzusha hitilafu na mifarakano, huwa inazitusi itikadi za Waislamu wa madhehebu ya Kisuni sanjari na kuzikuza na kuzipigia upatu hadithi zinazozusha mifarakano kati ya Waislamu.

Licha ya kanali hiyo kujiarifisha kuwa ya Kishia, inapinga vikali Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku ikiwakejeli maraajii wakubwa wa Kishia kama vile, Imam Khomein (MA) Mwasisi wa taifa hili na hali kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ali Khamenei. Hii ni kwa sababu viongozi hao wa Kishia daima walikuwa na wamekuwa wakisisitizia sana juu ya umoja kati ya Waislamu. Mkurugenzi na muendeshaji matangazo wa kanali hiyo ambaye ni shekhe kijana lakini mwenye elimu ndogo, huwafanyia kejeli na stihzai Maraajii wakubwa wa kidini ili kudhoofisha hadhi na haiba zao. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba, kanali hiyo si tu kwamba, inarusha matangazo yake kutoka nchini Marekani, bali inapata uungaji mkono wa kifedha wa serikali ya nchi hiyo. Aidha nukta nyingine ni kwamba, kanali hiyo inaendesha shughuli zake nchini Marekani katika hali ambayo nchini humo kuna sheria ya kudhibiti vyombo vya televisheni ambapo inapotokea kanali yoyote ile kufanya kitendo kidogo kabisa cha kuyavunjia heshima matukufu ya madhehebu yoyote au tapo lolote la kifikra au kijamii, kanali hiyo hufungiwa na leseni yake ya urushaji matangazo hufutwa. Hapa linajitokeza swali hili kwamba, kwa nini kanali hiyo inayoitwa 'Ahlu Bayti' haifungiwi licha ya mienendo yake ya kuzitusi madhehebu nyingine za Kiislamu? Jibu la swali hilo liko wazi kabisa. Hii ni kwa sababu serikali ya Marekani, ni muungaji mkono mkubwa wa watu wanaozusha hitilafu kati ya madhehebu za Kiislamu au wale wanaopinga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa upande mwingine ni kwamba, wakati wimbi la kuibua hitilafu za kimadhehebu kupitia kanali za televisheni lingali linaendelea, kuna kanali zenye taasubi na kufurutu ada kama vile kanali ya 'Kalimah' ambayo inajiarifisha kuwa ya madhehebu ya Kisuni katika hali ambayo kanali hiyo inamilikiwa na Mawahabi. Ukiiangalia tovuti ya habari ya kanali ya televisheni ya 'Kalimah' na masuala yanayojadiliwa katika vipindi vya kanali hiyo, utabaini kuwa kanali ya 'Kalimah' yenye makao yake nchini Sudan, haina kazi nyingine ghairi ya kuzusha tofauti za kimadhehebu baina ya Waislamu. Kanali ya 'Kalimah' inaendesha shughuli zake kwa uungaji mkono wa kifedha wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia chini ya msaada wa fikra wa Marekani na Uingereza. Lengo kuu la kanali hiyo ya televisheni ni kuwachochea Waislamu wa Kisuni ili wawachukie wenzao wa Kishia kwa manufaa ya Mawahabi. Masheikh wa Kiwahabi wenye misimamo ya kufurutu ada hutoa mada zao kali za uchochezi kupitia kanali hiyo, mada ambazo zinapingwa na kukosolewa vikali na maulamaa wote wa Kisuni wenye insafu na wanaotetea umoja baina ya Waislamu duniani. Mara nyingi mashekhe wa Kiwahabi wanaozungumza katika kanali ya 'Kalimah' hutaka kuonyesha kuwa madhehebu ya Shia ni madhehebu bandia na iliyo mbali na Uislamu. Kupitia kanali hiyo ya Kalimah, Mashekhe wa Kiwahabi hutoa hadithi dhaifu na zisizo na mashiko yoyote ambazo zinapingwa pia na maulama wenyewe wa Kishia wakati huo huo kutumia maneno makali na ya matusi dhidi ya madhehebu hiyo ya wafuasi wa watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) 'yaani Ahlul-Bayti' na kuitaja madhehebu hiyo kuwa ni bandia na ya kubuni. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, bajeti ya mwaka ya kanali hiyo ni zaidi ya dola milioni saba, fedha ambazo baadhi yake hutoka moja kwa moja katika bajeti ya makundi ya kidini nchini Saudia. Kwa upande wa kiufundi kanali hiyo ya 'Kalimah' husimamiwa na wafanyakazi wa kanali ya al-Arabiyyah yenye mafungamano na serikali ya Saudia.

*******

Mbali na kanali ya Kalimah,  kanali za Nur, Fadak, Wiswal Farisi na Salam, ni miongoni mwa kanali nyengine zinazotekeleza mkakati wa kuzusha hitilafu kati ya Waislamu duniani, huku zikiwa zimejivisha vazi la Usuni na Ushia katika Ulimwengu wa Kiislamu. Nukta ya kutoa mguso ni kwamba, kanali hizo kama vile Fadak inarusha matangazo yake kutokea nje ya mipaka ya nchi za Kiislamu na aghlabu hurusha matangazo hayo kutoka mjini London, Uingereza na Marekani. Kwa upande mwingine ni kwamba, kanali hizo na kwa kutumia propaganda za urongo, hutangaza kuwa, zinaendeshwa kwa kutegemea misaada ya fedha za Waislamu.

Kuhusiana na suala hilo, Marjan Husseini mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na mkuu wa idara ya 'Monitoring' ya kurushia matangazo ya Shirika la Redio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB anasema kama ninavyo mnukuu: "Aghlabu ya kanali hizo huwa hazitangazi matangazo ya biashara katika hali ambayo ili ziweze kupata mawimbi ya Frequency ya satalaiti ya Hot Bird, zinatakiwa kulipia kiasi cha dola elfu 28 kwa mwezi, huku zikilipia dola elfu 60 kwa ajili ya matumizi mengine. Kiwango hicho ni kwa ajili ya kurusha matangazo tu kwenda kwenye satalaiti na kutoka kwenye satalaiti kuja ardhini. Hii ni katika hali ambayo ikiwa tutaongeza gharama za mishahara ya wafanya kazi wa kanali hizo, kwa hakika tutapata kiwango kikubwa cha fedha kinachotumiwa kwa mwezi. Kanali hizo zisizokuwa na matangazo ya biashara (ambayo kwa kawaida ndio chanzo cha mapato ya televisheni) zinapata wapi kiwango chote hicho cha fedha? Hakuna shaka kwamba, suala hilo ni uthibitisho tosha wa uwepo wa mahusiano ya karibu kati ya kanali hizo na dola chafu za utawala wa Marekani. Huku zikisikitika kuwa hazina fedha , ubora wa kanali hizo unazidi kupanda siku hadi siku  na wigo wa urushaji matangazo yake unazidi kupanuka...." Mwisho wa kunukuu.

*******

Katika hali ambayo suala la umoja kati ya madhehbu za Kiislamu hususan Suni na Shia, limekuwa likipewa umuhimu wa aina yake na maulama wa pande mbili, maadui wa Uislamu hutumia kanali hizo zinazojiarifisha katika sura ya kidini, kuchochea hisia za Waislamu na kuzusha hitilafu kati ya Suni na Shia kwa kukejeli matukufu ya kila moja kati ya madhehebu hizo. Kwa upande wao maulama wenye uchungu wa dini, wa madhehebu za Kisuni na Kishia wamekuwa wakisisitizia sana juu ya umoja baina ya Waislamu na kuwausia Waislamu kutoangalia kanali hizo zenye kuzusha hitilafu baina yao. Akiashiria njama za maadui za kutaka kuzusha hitilafu baina ya Waislamu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei anasema kama ninavyomnukuu: "Wametambua vyema kwamba, ikiwa madhehebu za ulimwengu wa Kiislamu zitatofautiana na kuanza mivutano baina yao, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel utaweza kupumua kwa raha. Kwa sababu hiyo wameasisi makundi ya kitakfiri ambayo si tu kwamba yanawakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Kishia, bali yanawakufurisha pia Waislamu wengine wa madhehebu za Kisuni. Wakati huo huo kuna kundi lingine la vibaraka ambalo limewekwa kwa minajili ya kuchochea moto wa hitilafu hizo kama mnavyoona.... Wanawapatia vyombo vya mawasiliano ya umma na vya habari. Ni wapi? Marekani! Ni wapi? Mjini London. Ushia huo unaotangazwa kwa ajili ya walimwengu kutoka mjini London na Marekani, Ushia wa namna hiyo hauna nafasi katika ulimwengu wa Kiislamu. Viongozi wa Kishia na hasa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu kama vile Imam Khomeini na wengineo, wamekuwa wakisisitizia sana juu ya umoja wa umma wa Kiislamu. Lakini badala yake linakuja kundi jingine na kuwasha moto wa fitina na kuzusha hitilafu na mapigano." Mwisho wa kunukuu.

Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu cha makala ya wiki kinaishia hapa kwa leo. Ni matumaini yangu kuwa mmenufaika vya kutosha sanjari na kufahamu umuhimu wa umoja baina ya Waislamu duniani mkabala na njama za kuwagawa kupitia kanali za televisheni. Msikose kuungana nami tena katika kipindi kingine cha makala ya wiki katika siku kama hii. Kwaherini.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)