Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 27 Disemba 2014 08:43

Uislamu Chaguo Langu (97)

Uislamu Chaguo Langu (97)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru maishani yaani Uislamu. Katika makala yetu ya leo tutamuangazia mwanamke Mmarekani aliyesilimu. Karibu kujiunga nami hadi mwisho.
@@@
Twahira ni mwanamke Mmarekani aliyesilimu na ambaye sasa ni mama mzazi wa mtoto wa kiume aliyepewa jina la Hafidh na mtoto wa kike aliyepewa jina la Sabira.
Bi. Twahira alizaliwa katika jimbo la New York na aliikubali dini tukufu ya Kiislamu mwaka 2007. Mwaka mmoja baada ya kusilimu alipata taufiki ya kuwa mfuasi wa madhab ya Shia Ithnaashari. Bi. Twahira alizaliwa katika familia ya Kikristo na kutokana na kuwa mfanyakazi wa Wizara ya Afya ya Marekani alipata fursa ya kusafiri katika maeneo mbali mbali ya dunia.
Bi. Twahira anabainisha alivyopata taufiki ya kusilimu ifuatavyo: "Katika mwaka wa mwisho wa masomo ya shule ya sekondari nchini Marekani huwa kuna somo la kuarifisha dini muhimu zaidi duniani. Nakumbuka tukifundishwa kuhusu misingi ya dini ya Kiislamu na kwa mujibu wa tuliyoyasoma dini hii ilikuwa ngumu sana kuifuata. Wakati huo nilikuwa Mkristo aliyekuwa na imani thabiti na baba yangu alinifunza misingi yote ya Ukristo. Mwaka 2007 nilifunga safari na kuelekea Afrika. Ilikuwa ni katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na nilihudumu kama mfanyakazi wa afya katika nchi za Kiislamu za Somalia, Djibouti na nchi ya Eritrea yenye idadi kubwa ya Waislamu. Kitu ambacho kilinishangaza ni kuwa, licha ya Waislamu wa nchi hizo kuwa ni watu masikini na wenye maisha magumu lakini walifungamana kikamilifu na mafundisho ya Uislamu. Hali ya hewa katika nchi hizo ni ya joto la juu sana lakini Waislamu walikuwa wakifunga kikamilifu kula na kunywa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani huku wakitekeleza ibada nyinginezo kama vile kuswali. Suala hili la kufungamana Waislamu na mafundisho ya dini yao katika hali ngumu kama hiyo ni jambo ambalo lilinipelekea nifanye utafiti zaidi kuhusu Uislamu."
Mwanamke huyu Mmarekani aliyesilimu anaendelea kusema: "Baada ya kuvutiwa na namna Waislamu wanavyofungamana na dini yao, niliporejea Marekani nilianza kusoma vitabu vya Kiingereza kuhusu Uislamu. Katika kipindi hicho niliweza kujuana na Mwislamu ambaye aliweza kunifunza mengi zaidi kuhusu mafundisho ya Uislamu. Kwa hakika nilivutiwa sana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu na niliweza kupata majibu ya maswali mengi ambayo nilikuwa nayo. Nilianza kuenda katika msikiti na kujifunza lugha ya Kiarabu ili niweze kuisoma Qur'ani Tukufu kwa lugha yake asili yaani Kiarabu. Utafiti na uchunguzi wangu ulinivuta zaidi katika Uislamu. Hatua kwa hatua nilianza kufahamu kuwa Uislamu ndiyo dini bora na kamili zaidi ya Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo niliamua kusilimu," anasema Bi. Twahira.
@@@
Baada ya kusilimu Bi Twahira alijitahidi sana kutekeleza mafundisho ya Kiislamu na alifanikiwa katika hatua alizozichukua. Hapa anafafanua zaidi kwa kusema: "Nilianza kuandika mafundisho ya Kiislamu na nilijitahidi kuyatekeleza katika maisha yangu. Katika sehemu niliyokuwa nikifanya kazi wengi walistaajabu kuona nikitekeleza ibada za Kiislamu. Wakati wa kuswali nilikuwa nikitumia chombo maalumu kutafuta qibla. Kwa muda mrefu mkurugenzi wangu hakuwa amefahamu kuwa mini ni Mwislamu na kwamba nilikuwa nikiswali kazini. Baadaye ilimbainikia kuwa mimi, mwanamke Mmarkenai Mzungu, nimesilimu jambo ambalo lilimshangaza sana. Alikuwa na dhana potofu kuwa Uislamu ni dini ambayo wanaume wanaoifuata huwapiga ovyo wanawake na hivyo alipinga ibada niliyokuwa nikifanya. Kwa bahati nzuri mkurengezi huyo aliondolewa na mahala pake akaja mtu mwenye mantiki ambaye aliweza kunidiriki na hivyo aliniruhusu kufanya ibada katika wakati maalumu. Kwa muda mrefu baada ya kusilimu sikuwa nikivaa hijabu kwani hali yangu ya kikazi haikuniruhusu kufanya hivyo. Fauka ya hayo nguo tulizokuwa tukivaa zilikuwa ni za mikono mifupi. Lakini baada ya kupata maelezo kamili kuhusu umuhimu na ulazima wa kuvaa Hijabu, nilianza kuvaa vazi hilo la stara," anasema Mmarekani aliyesilimu, Bi. Twahira.
Kwa mtazamo wa wanafikra na wanazuoni, adhama ya dini ambayo risala yake ililetwa na Mtume Mohammad SAW ni nukta mbili. Awali ni Qur'ani Tukufu ambayo ni burhani inayosomwa kwa lugha yake asili. Pili ni shakhsia kubwa na ya kipekee ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mohamad Al Mustafa SAW. Kwa hakika mtukufu huyo ni nyota ya kipekee inayoangaza dunia. Ni nyota ambayo inaendelea kuleta nuru na karama kila mahala. Moja ya sifa za kipekee za Mtume Mtukufu wa Uislamu ni elimu inayoenda sambamba na maadili, hekima, uafilifu na heshima. Hivi sasa baada ya kupita zaidi ya miaka 1,400 tokea alipozaliwa, Mtume Muhammad SAW anaendelea kuvutia idadi kubwa ya wanaadamu. Mmarekani aliyesilimu Bi. Twahira anabainisha mtazamo wake kuhusu baadhi ya sifa za kipekee za Mtukufu Mtume kwa kusema: "Mtume Muhammad SAW alikuwa shakhsia mwenye malengo ya juu na ya kipekee. Ameweza kutoa masomo yenye thamani za juu kwa wanaadamu. Uhusiano wa Mtume wa Uislamu na Mayahudi wa zama zake ni jambo ambalo liliniathiri sana. Nukta nyingine iliyonivutia katika shakhsia ya Mtume Mtukufu ni ibada yake katika pango la Hiraa."
Mmarekani aliyesilimu Bi. Twahira anaongeza kuwa nukta nyingine iliyompelekekea asilimu ni utamaduni tajiri wa kifikra katika Uislamu. Anasema Waislamu wana umaanawi wa kina ambao hauko tena katika nchi za Magharibi. Bi. Twahira anasema baada ya kusilimu aliolewa na Mwisllamu na hapo akaweza kuujua zaidi Uislamu. Anaongeza kuwa hatua kwa hatua alipata taufiki ya kuujua utamaduni wenye thamani wa Ahul Bayt wa Mtume SAW ambao amewataja kuwa kigezo cha maisha bora na sahihi ya Kiislamu. Mmarekani huyu aliyesilimu ambaye sasa anafuata madhehebu ya Shia Ithnaashari anasema: "Ningali ninakumbuka vizuri majlisi ya kuomboleza kuuawa shahidi Imam Hussein AS. Nilikuwa sijawahi kupata tajriba kama hiyo. Baada ya kuchunguza maisha ya Ahul Bayt wa Mtume SAW niliweza kuufahamu Uislamu kikamilifu". Anaelezea zaidi kuhusu namna alivyoyakubali madhehebu ya Shia Ithnaashari kwa kusema: "Ushia ulinivutia sana kutokana na utamaduni wake wa kujitolea muhanga. Kwa hakika utamaduni wa kufa shahidi ni mkabala ya kujipenda." Mmarekani huyu aliyesilimu anasema katika kuimarisha maarifa yake alisoma kitabu kilichoandikwa na Ayatullah Sistani chenye anwani ya "Sheria za Kiislamu". Aidha alisoma kitabu cha Imam Ghazali chenye anwani ya "Kuhuisha Sayansi za Dini" au Ihya Ulumu Din, kitabu cha Ayatullah Amini kuhusu 'Mwanaadamu Kujijenga Nafsi' na kitabu maarufu cha Sheikh Mufid chenye anwani ya Al Irshad au Muongozo.
Mmarekani huyo aliyesilimu pia amevutiwa sana na malenga na wanafasihi Waislamu. Anaongeza kuwa: "Kabla ya kusilimu nilisoma athari za malenga Wairani Waislamu kama vile Maulana, Attar, Hafidh na Saadi. Umaridadi wa Irfani katika mashairi ya Kifarsi ni nukta iliyonivutia katika Uislamu." Anasema mvuto wa mashairi ya lugha ya Kifarsi ni moja ya sababu zilizompelekea ampe mtoto wake jina la Hafidh, ambaye alikuwa malenga maarufu Muirani.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …