Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 25 Oktoba 2014 10:29

Uislamu Chaguo Langu (91)

Uislamu Chaguo Langu (91)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru katika maisha ya dunia na akhera yaani Uislamu.
Katika makala yetu ya leo tutamwangazia raia wa Romania aliyesilimu Bi. Maria. Karibu kujiunga nami hadi mwisho.
@@@
Maria si mashuhuri wala hajaandika kitabu kinachomfanya awe mwandishi mtajika lakini yeye ni shakhsia mwenye kutafuta ukweli. Ingawa alizaliwa katika mazingira yaliyotawaliwa na umaada, lakini ili kufikia ukweli na maarifa halisi, alichukua mkondo uliokuwa tafauti na mazingira aliyokuwa akiyaishi. Maria anafafanua zaidi kwa kusema: "Nilikuwa na umri wa takribani miaka 12 hivi ambapo nilihisi shinikizo kubwa la kiroho na kisaikolojia. Nilikuwa na hamu kubwa ya kumjua Mwenyezi Mungu. Lakini la kusikitisha ni kuwa hapakuwa na mtu wa kujibu maswali yangu. Sikupata jibu lolote katika Ukristo na hivyo nilikimbilia kusoma vitabu mbali mbali umri wangu ulivosonga mbele nilianza kuvutiwa na dini za Mashariki lakini pia sikuweza kupata faraja hapo."
Kwa miaka kadhaa Maria aliishi maisha yaliyojaa shaka na mfadhaiko wa nafsi. Kipindi hicho pia kulijiri matukio makubwa duniani na moja ya matukio hayo ni Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979. Televisheni ya Romania ilionyesha taswira kuhusu matukio ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Maria anasema hivi kuhusu aliyokuwa akiyaona katika televisheni: "Kwa mara ya kwanza niliona taswira ya Imam Khomeini katika televisheni. Nyanya yangu alisema hivi kuhusu suala hili: 'Huyu mtu anapoinua mkono wake juu anawasiliana kiroho na kisaikolojia na watu na si kila mtu ana uwezo kama huo.' Nyanya yangu alikuwa akisema, 'huyu mtu ataitikisa dunia'. Wakati huo mimi sikuweza kudiriki maneno ya nyana yangu." Maria aliendeleza masomo yake na kuingia chuo kikuu. Hapo aliweza kupata uzoefu wa dunia mpya kwani katika maisha yake alishuhudia mabadiliko makubwa. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Katika chuo kikuu nilikutana na watu wa aina mbali mbali wakiwemo Waislamu. Kipindi hicho kilisadifiana na kuenea fikra za Imam Khomeini MA kote duniani. Hapa ninapaswa kukiri kuwa kuenea Uislamu Ulaya Mashariki kulitokokana kwa kiasi kikubwa na Uongozi wa Imam Khomeini."
Ukweli alioutaja Maria ni ukweli ambao hauwezi kupingika. Kujiri Mapinduzi ya Kiislamu Iran kwa uongozi wa Imam Khomeini MA ni tukio ambalo lilipelekea uhakika wa Uislamu uweze kubanika na hivyo kuhuisha dini hii tukufu. Sifa za kipekee za harakati ya Hadhrat Imam ni kuwa Uislamu ndio uliokuwa chimbuko la harakati yake. Kwa msingi huo, madola makubwa ya Kimagharibi yalitambua uwezo mkubwa wa Uislamu uliokuwa umefichika pale yalipokumbana na Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini. Kuhusu hili, Gazeti la 'The Times' la Uingereza liliandika: 'Mwamko wa kidini umeibuka nchini Iran kwa uongozi wa Imam Khomeini MA. Mwamko huo ulienea kote duniani. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliwapelekea Wamagharibi wautambue Uislamu...." Kwa hakika Imam Khomeini na Mapinduzi ya Kiislamu ni vitu viwili ambavyo haviwezi kutenganika. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliweza kufanikiwa kutokana na fikra na nadharia za Imam Khomieni. Kwa msingi huo kuyachambua Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pasina kuitambua shakhsia ya Imam Khomeini ni jambo lisiliowezekana. Itikadi za kisiasa za Imam Khomeini zimejengeka katika msingi wa imani imara ya mafundisho ya Kiislamu ya kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu SWT. Wamagharibi hawajaweza kufahamu na kudiriki kikamilifu fikra na nadharia za Imam Khomeini. Kwa maneno sahihi zaidi ni kuwa, fikra za kisiasa za Imam Khomeini ambazo zilikuwa msingi asili wa kuanza na kuendelea harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu ni natija ya kimantiki ya kufasiri kwake mafundisho ya Mwenyezi Mungu SWT kuhusu maumbile ya dunia na nafasi ya mwanaadamu katika maumbile hayo.
Imam Khomeini MA alifanikiwa kutumia mafundisho ya Kiislamu katika medani ya siasa za kimataifa na si tu kuwa aliongoza harakati ya dunia ya Mapinduzi ya Kiislamu bali pia aliweza kuleta fikra mpya na ya kidini kabisa sambamba na kubatilisha na kuibua changamoto katika nadharia za kibinaadamu na kimaada hasa za Wamagharibi. Fikra za Imam Khomeini zilikuwa tiba kwa matatizo mengi na tunaweza kusema kuwa aliweza kuleta mabadiliko ya kimsingi katika firka za kisiasa katika zama hizi. Ni kwa msingi wa fikra hizo ndio tukashuhudia mapinduzi makubwa zaidi katika karne ya 20. Hayo ni mapinduzi ambayo baada ya ushindi wake, wataalamu wa masuala ya kimataifa waliyataja kuwa yasiyoweza kulinganishwa na mapinduzi mengine makubwa duniani. Kwa hakika Imam Khomeini alikuwa mfano kamili wa Mwislamu na kigezo cha kiongozi wa Kiislamu ambaye aliuletea Uislamu heshima na kuinua bendera ya Qur'ani kote duniani. Imam Khomeini pia alihuisha thamani za kimaadili duniani sambamba na kupambana na madhalimu na kuwatetea waliodhulumiwa duniani.
Mromania aliyesilimu anasema baada ya kusikia habari za matukio ya Iran, aliathiriwa pakubwa na shakhsia ya Imam Khomeini MA pamoja na fikra zake. Hali hiyo ilimpelekea aanze kufanya utafiti wa kina kuhusu Uislamu kama dini ambayo ilikuwa chanzo cha ilhamu ya Imam Khomeini na hivyo kuleta ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Maria anabainisha zaidi kuhusu hili kwa kusema: "Imam Khomeini MA aliuletea Uislamu uhai mpya na hivyo kupelekea idadi kubwa ya watu kusilimu. Nilitaka sana kufanya utafiti kuhusu Uislamu. Hivyo nilisoma vitabu kadhaa ikiwemo tarjama ya Qur'ani Tukufu ambapo nilipata maarifa mengi mapya. Nukta muhimu niliyoweza kuifahamu ni kuhusu upana wa Uislamu na kwamba mafundisho ya Kiislamu yanaweza kutekelezeka." Maria anaendelea kusema: 'Katika utafiti wangu kuhusu Uislamu niliweza kuvutiwa sana na aya za Qur'ani kwani kila nilichokuwa nikikisoma kilikuwa kipya kabisa. Kwa hakika iwapo mwanaadamu atakisoma kitabu hiki kitakatifu kwa makini na uzingatiaji basi hataweza kuacha kikosoma daima katika maisha yake."
Maria ambaye alichagua jina la Zahra (Binti wa Mtume SAW) baada ya kusilimu anasema aliweza kupata hidaya na muongozo maishani kutokana na fikra za Imam Khomeini MA na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Anasema baada ya kusilimu aliamua kusomea taaluma ya udaktari wa meno. Alichagua kuendeleza masomo yake nchini Iran na akiwa na mume wake walifika katika Jamhuri ya Kiislamu kuendeleza masomo. Anasimulia kumbukumbu zake alipokuwa Iran kwa kusema: 'Tulipokuwa Iran tuliweza kustawi sana kwa matazamo wa kiroho na kimaanawi. Ingawa hatukuwa na upungufu kwa mtazamo wa kifedha, lakini upungufu huo haukuwa chochote mkabala wa utulivu na usalama wa kiroho na kisaikolojia. Natija ya ndoa yetu ni binti ambaye tulimpa jina la Zainab. Kwa hakika mafanikio niliyonayo maishani ni kutokana na msaada wake Mwenyezi Mungu SWT ambaye alinipa taufiki ya kuujua Uislamu kupitia Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Imam Khomeini MA."

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …