Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 01 Septemba 2014 12:11

Uislamu Chaguo Langu (90)

Msikiti katika mji wa Toronto, Canada Msikiti katika mji wa Toronto, Canada

Uislamu ni dini ambayo ina sifa za kipekee na kila mojawapo ya sifa hizo ni nukta yenye nguvu ambayo huwavutia wale wenye kufanya utafiti. Kila anayefanya utafiti kuhusu Uislamu huvutiwa na moja ya sifa hizo na hatimaye kuukumbatia Uislamu maishani. Mkanada aliyesilimu Bw. Kart alivutiwa na suala la maumbile na kuwepo muumba moja wa ulimwengu. Kuhusu hili anasema: "Daima nilikuwa nikitafakari na kuwaza kuwa, ulimwengu hauwezi kuwepo pasina kuwepo muumba mwenye uwezo. Tukitazama yote yanayotuzunguka tunaona mbingu maridadi, nyota za kustaajabisha na kuvutia, ardhi pana pamoja na maajabu mengine mengi ya maumbile. Hayo yote humfanya mwanaadamu atumbukie katika kutafakari na jambo hili humpa matumaini na kumfanya aweze kumhisi muumba wa umaridadi wote huu.  Wakati nilipokuwa nikitafakari kuhusu maumbile sikuweza kughafilika kuhusu siri ya maumbile. Kwa msingi huo nilifanya utafiti kuhusu dini mbali mbali ili niweze kugundua siri za ukweli wa maumbile ya ulimwengu."

Mkanada huyu aliyesilimu anaongeza kusema: "Ingawa leo watu wengi katika nchi za Magharibi wanakana kuwepo Mwenyezi Mungu, wakati huo huo wanajinasibisha na Ukristo. Lakini Ukristo wao ni turathi tu waliyoipata kutoka vizazi vilivyotangulia. Mimi sikutaka kuwa kama Wakristo waliowengi ambao hufuata mafundisho wakiwa wamefunga macho pasina kuuliza kuhusu misingi na lengo la Ukristo. Hivyo awali nilifanya utafiti kuhusu Ukristio ili niujue zaidi.  Kabla ya utafiti wangu sikuwa nikilipa umuhimu mkubwa suala la utatu. Katika utafiti wangu sikuweza kukubali kuwa dunia adhimu kama hii inaendeshwa na miungu kadhaa. Nilifikia natija kuwa maumbile ya ulimwengu yalikuwa ya kipekee na juu ya uwezo wa mwanaadamu; hii ni kwa sababu iwapo kungekuwa na miungu kadhaa inayosimamia dunia hatungekuwa na nidhamu hii ya kipekee.  Nilikaa vikao na makasisi na kujadili masuala hayo lakini kadiri tulivyosonga mbele ndio shaka yangu kuhusu Ukristo ilivyozidi kuongezeka jambo ambalo lilinikosesha usalama na utulivu wa kiroho. Hatimaye niliamua kuuacha Ukristo na nikaanza kufuata Uyahudi."

Wapenzi wasikilizaji Uislamu ni dini ambayo haiwahusu Waarabu tu bali ni dini ya dunia nzima na wanaadamu wote. Hii ni tafauti moja kabwa kati ya Uislamu na Uyahudi wa sasa.  Bw. Kart alianza kufanya utafiti kuhusu Uyahudi na anasema hivi kuhusu utafiti wake huo: "Katika Uyahudi unaweza kupata nukta za kuvutia za umaanawi. Lakini nukta hizo ni chache sana kiasi kwamba haziwezi kukidhi kiu ya kiroho. Kadiri nilivyofanya utafiti kuhusu Uyahudi ndio nilivyofahamu kuhusu mtazamo potofu wa Mayahudi kuhusu dunia. Tatizo kubwa la Mayahudi ni kuwa wao wanajitazaama kama kaumu bora kuliko watu wengine wote na wanadai kuwa ndio wateule wa Mwenyezi Mungu duniani na hivyo wanawatazama wasiokuwa Mayahudi kama watu ambao wamekuja duniani kuwahudumia. Katika itikadi za Kiyahudi, Mwenyezi Mungu ni wa Mayahudi tu na wala hayuko kwa ajili ya wanaadamu wengine. Ni mwanaadmau yupi mwenye akili salama anayeweza kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni wa Mayahudi pekee pamoja na kuwa yeye ndiye Muumba wa ulimwengu huu wote mkubwa na kila chote kilichomo. Hivyo nilifikia natija kuwa Uyahudi hauna mantiki na uhakika ambao mimi nilikuwa nikiutafuta," anasema Mkanada huyo aliyesilimu.

Baada ya uchunguzi wa kina Bw. Kart aliamua kufanya utafiti kuhusu Uislamu. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Niliendeleza utafiti wangu kwa kuuchunguza Uislamu. Lakini nilikuwa na mushkili katika kuanza utafiti wangu kuhusu Uislamu. Hii ni kwa sababu ufahamu niliokuwa nao kuhusu Uislamu ulikuwa ufahamu potofu niliokuwa nimeupata katika vyombo vya habari vya Kimagharibi. Lakini pamoja na hayo wakati nilipoanza utafiti wangu kuhusu Uislamu kwa mara ya kwanza nilifungua marejeo makuu ya elimu za Kiislamu yaani Qur'ani Tukufu. Baada ya kuisoma Qur'ani nilijipata katika mkondo mpya. Katika Qur'ani nilikumbana na masuala ya kina na uhakika thabiti na imara. Kila aya ya Qur'ani niliyoisoma iliongoza maarifa yangu.  Katika Qur'ani nilipata ukweli na uhakika ambao nimekuwa nikiutafuta kwa muda mrefu sana. Kila aya ya Qur'ani ilituliza moyo wangu uliokuwa umekumbwa na tufani."

Wapenzi wasikilizaji Qur'ani Tukufu ni kitabu ambacho kila siku huwaongoza watu wengi ambao wana hamu ya kuujua na kuufuata ukweli. Waislamu wote karibu bilioni mbili duniani na hata idadi kubwa ya wasiokuwa Waislamu husoma matini ya Qur'ani kwa lugha yake asili ya Kiarabu au tarjama ya Qur'ani kwa lugha nyinginezo.

Jules la Boum msomi Mfaransa anaamini kwamba, kutokana na kuwa Qur'ani inaenda sambamba na akili na hekima, jambo hili limepelekea kitabu hiki kupata mvuto maalumu na hivyo kuwa muongozo wa maisha ya kila siku ya Waislamu duniani. Msomi huyo wa Ufaransa anaandika: "Kwa yakini Qur'ani itabakia hai daima na katika kila zama, wasomi na watafiti watanufaika nayo kwa kadiri ya elimu yao."

Mkanada aliyesilimu Bw. Kart anasema umaridadi wa Qur'ani ulimvutia sana. Anaongeza kuwa: "Qur'ani inazungumzia Mwenyezi Mungu Mmoja, Muumba wa mbingu na ardhi, Msimamizi asiye na mshirika. Qur'ani ni neno la kweli la Mwenyezi Mungu na si neno la mwanaadamu. Katika mafundisho ya Qur'ani mwanaadmau anaweza kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu na hivyo hahitajii baba wa kiroho. Qur'ani imezungumza kuhusu Issa na Musa (amani ya Mwenyezi Mngu iwe juu yao) Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu ambao waliwaita watu kuelekea katika Tauhidi yaani kumuabudu Mungu Mmoja. Katika Qu'rani sijaona aya inayoelekeza watu katika ugaidi au utumiaji mabavu. Hilo ni kinyume cha propaganda potofu za vyombo vya habari vya Kimagharibi ambavyo vinawanasibisha Waislamu na ugaidi. Uislamu ni dini ya amani, udugu na mshikamano. Hii ni dini ambayo niliamua kuikumbatia na kuifuata baada ya utafiti wa muda mrefu," anasema Mkanada aliyesilimu Bw. Kart. Anaendelea kusema alipokutana na Waislamu kwa mara ya kwanza kabisa aliweza kufahamu maana ya neno ukarimu kwani walimkaribisha kwa moyo mkunjufu na kwa udugu. Anaongeza kuwa kabla ya kusilimu alipofika msikitini awali alikuwa na hofu lakini alipoingia Waislamu walimkaribisha kwa ukarimu mkubwa  na kwamba walijibu kikamilifu maswali yote aliyokuwa nayo na hivyo aliweza kukinaika. Hatimaye aliamua kufuata njia ya saada na nuru maishani yaani Uislamu. Bw. Kart anasema alisilimu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na hivyo alianza ibada katika mwezi huo uliojaa rahma za Mwenyezi Mungu. Anasema maisha yake yalibadilika na kuchukua muelekeo bora na uliojaa nuru baada ya kusilimu. Mkanada huyu aliyesilimu anasema kila ambaye anatafuta ukweli na uhakika pasina kupendelea upande wowote hatimaye huweza kupata muongozo na hidaya ya Mwenyezi Mungu. Anamaliza kwa kumuomba Mwenyezi Mungu SWT awape wanaadamu wote taufiki ya kuutambua Uislamu kama dini ya haki.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …