Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 01 Septemba 2014 12:07

Uislamu Chaguo Langu (89)

Msikiti mjini Tokyo, Japan Msikiti mjini Tokyo, Japan

‘Mvuto wa kimaanawi wa misikiti ya Waislamu ni jambo ambalo hatua kwa hatua lilinivutia kuelekea katika Uislamu. Nilihisi pia kuwa sauti ya adhana katika misikiti ilikuwa na mvuto wenye kunipa mwongozo kulekea katika uhakika.” Hiyo ni kauli ya Bi.Khaula Nakata. Mjapani huyo alifikia natija kuwa Uislamu ndiyo dini ya haki baada ya kupitia masaibu mengi ambayo hayangeweza kutabirika.  Kabla ya kuujua Uislamu Bi. Nakata anasema alikuwa hajawahi kutafakari kwa kina kuhusu Mwenyezi Mungu na wala hakuona udharura wa suala hilo. Anaendelea kusema kuwa: “Kila kitu kilikuwa kikienda vizuri katika maisha yangu na nilikuwa nikihisi kuwa mambo yote ni shwari kabisa na hivyo niliona kuwa simhitajii Mungu maishani. Lakini ghafla nilianza kuhisi kuwa maisha yangu yalikuwa ni ya kujikariri pasina kuwepo na mwelekeo maalumu. Nilifikia natija kuwa maisha yangu hayakuwa na maana. Hivyo nilianza kufanya utafiti kwa lengo la kufikia uhakika. Wakati nikiwa mwanafunzi wa chuo kikuu, wahubiri kadhaa walikuwa wakinitembelea nyumbani. Wakati huo kulikuwapo mwanamke mhubiri Mkristo ambaye alikuwa daima anakuja kunitembelea na kunifunza Injili. Pamoja na aliyonifunza lakini sikuweza kupata kile nilichokuwa nikifuata.”.

Bi. Khaula Nakata anaendelea kusema kuwa: “Baada ya muda, niliamua kufuata dini ya Kibudha. Katika mji wa Kyoto niliupokuwa nikiishi Japan kulikuwa na athari nyingi za kihistoria. Karibu na nyumba yangu kulikuwa na hekalu na hivyo nilikuwa nikienda hapo kila asubuhi kwa ajili maombi. Niliendeleza mkondo huo kwa muda wa miezi mitatu. Sikuchelewa hata siku moja kufika katika hekalu hiyo. Nilikuwa nikitafuta ukweli maishani. Ilikuwa ivugmu kwangu kuzingatia kwa kina wakati nikiomba dua. Hatimaye nilifikia natija kuwa yalimokuwa hatika hekalu la kibudha yalikuwa mbali na uhalisia wa mambo katika dunia.”

Katika kipindi hicho Bi. Khaula Nakata aliamua kuendeleza masomo ya juu nchini Ufaransa badala ya Japan. Mwislamu huyo kutoka Japan anabainisha hivi kuhusu moja ya sababu zilizompelekea kuikubali dini tukufu ya Kiislamu: 'Katika zama ambazo nilikuwa bado sijauchagua Uislamu, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu wasichana wanaovaa Hijabu katika shule za Ufaransa na mjadala huo ungalipo. Wengi waliamini kuwa shule za serikali Ufaransa hazipaswi kujihusisha na itikadi za kidini za wanafunzi. Mimi pia wakati huo nikiwa kama mtu asiyekuwa Mwislamu, nilitafakakari na kujiuliza ni kwa nini wakuu wa shule wanachukua msimamo mkali kuhusu suala dogo kama vile mtandio wa wanafunzi.

Wasiokuwa Waislamu wamekuwa na dhana potofu kuwa wanawake Waislamu wanalazimishwa kutii sheria za Kiislamu na ndio sababu wanavaa Hijabu. Kwa msingi huo wasiokuwa Waislamu wamekuwa wakiitazama Hijabu ya wanawake Waislamu kama nembo ya dhulma na kudai kuwa uhuru wa mwanamke unapatikana tu kwa kutovaa Hijabu. Hii ni katika hali ambayo wanawake wengi wasiokuwa Waislamu duniani, baada ya kusilimu, hutazama uvaaji Hijabu kama sheria ya kimantiki ya dini. Mimi pia ni mfano wa wanawake hawa. Hijabu yangu si sehemu ya utambulisho wangu wa kijadi au kirangi wala haina maana ya kisiasa au kijamii; vazl la Hijabu yangu ni utambulisho wangu wa kidini. Nilipoamua kuikumbatia dini ya Kiislamu, kamwe sikudhani kuwa siku moja ningeweza kusimamisha sala tano kwa siku au ningeweza kulinda Hijabu yangu. Raghba na hamu yangu ya kuwa Mwislamu ilikuwa na nguvu kubwa kiasi kwamba sikuwa na wasiwasi kuhusu mabadiliko ambayo yalikuwa yanakuja.'

Bi. Nakata Khaula anasema hivi kuhusu nama alivyosilimu na kuvaa Hijabu: 'Baada ya kusikiliza hotuba katika Msikiti wa Paris, nilifahamu faida za kuchunga vazi la Hijabu kiasi kwamba hata baada ya kuondoka msikitini, niliendelea kuvaa mtandio ambao nilikuwa nimeuvaa kwa ajli ya kuuheshimu msikiti. Hotuba hiyo ilinighirikisha katika aina fulani ya ridhaa ya moyoni. Hii ilikuwa ni hali ya kipekee ambayo nilikuwa sijawahi kuihisi. Kwa hakika hisia hiyo ilinifanya nisitake kuondoka msikitini bila mtandio. Mavazi hayo yangu hayakuzingatiwa na watu wakati huo kutokana na kuwa hali ya hewa ilikuwa ya baridi kali. Pamoja na hayo nilikuwa na hisia nzito iliyoniambia kuwa nilikuwa tofauti na wengine, nilipata hisia ya utakasifu na usalama.'
Ingawa kabla ya kusilimu Bi. Nakata Khaula aliitazama hijabu kama kizingiti, lakini leo yeye ni mwanamke ambaye anaheshimu kikamilifu vazi la Hijabu ya Kiislamu. Anayatazama mavazi yake kuwa yenye thamani ya kimaanawi na yanayoashiria imani yake ya kidini. Kuhusiana na hili hiyo anasema: "Kutokana na kuheshimu vazi la Hijabu ninapata furaha na ridhaa. Suala hili ni ishara ya kutii amri ya Mwenyezi Mungu na imani yangu. Hakuna tena haja ya kuitangaza itikadi yangu kwa sauti kubwa, kwa sababu vazi langu  linawabainishia wote imani yangu. Hijabu inawakumbusha watu kuwa Mwenyezi Mungu yupo na daima inanikumbusha kuwa mwenendo wangu unapaswa kuwa ule wa mwanamke Mwislamu. Ni sawa na maafisa wa polisi ambao wakiwa wamevalia sare zao za kazi, huwa waangalifu zaidi kwa hivyo mimi pia ninapovaa Hijab ninapata hisia zaidi ya kuwa Mwislamu.'

Bik Nakata pia anasema mbali na vazi la Hijabu, anavutiwa sana na Swala katika Uislamu. Anasema Swala ni amali ambayo inaimarisha imani ya mwanadamu. Bi. Nakata anasema baada ya kusilimu, wakati aliposwali na kusujudu kwa mara ya kwanza katika ardhi akimshukuru Allah SWT, hakuweza kuinua kichwa chake haraka kutoka kwenye sijda. Anasema kila mara anaposujudu imani yake inaimarika zaidi. Mjapani huyu aliyesilimu anasema alienda Misri kujifunza lugha ya Kiarabu ili aweze kuufahamu vizuri na kikamilifu zaidi Uislamu. Kuhusu uwezo wake wa kusoma Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Kiarabu anasema: “Hivi sasa naweza kuisoma Qur’ani kwa umaridadi. Mbali na maudhui mbalimbali zinazojadiliwa katika kitabu hiki, mimi pia navutiwa na mtirikio wake wenye mvuto wa kipekee. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunineemesha na kunipa taufiki ya kuwa Mwislamu na nitajitahidi kuwafunza Wajapani Uislamu. Nataka nao pia wapate furaha kama niliyonayo katika Uislamu. Mimi ninaamini kuwa kwa kumwamani kikamilifu na kumtegemea Mwenyezi Mungu, kila tatizo lina weza kutatuliwa”

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …