Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 23 Agosti 2014 09:40

Uislamu Chaguo Langu (88)

Uislamu Chaguo Langu (88)

Katika makala yetu ya leo tutamuangazia Mrussia aliyesilimu Afanassiev Sergei ambaye ni mwenyeji wa Russia. Sergei daima amekuwa muungaji mkono wa malengo matukufu kama vile uadilifu, uhuru, kupambana na umasikini na kupinga dhulma. Akiwa katika mikakati yake ya utafiti, aliweza kugundua ukweli kuwa, serikali au tawala zilizoundwa na wanaadamu katika kipindi chote cha historia hazikuweza kufikia malengo matukufu yaliyotajwa hapo juu. Sergei Afanassiev anafafanua zaidi kuhusu hili kwa kusema: “Tangu kuumbwa dunia hadi sasa, mwanaadamu daima amekuwa akitaka kuona jamii inayoundwa kwa msingi wa uadilifu. Kihistoria, ukosefu wa uadilifu ndiyo chanzo cha malalamiko ya umma. Pamoja na hayo historia imekuwa ikishuhudia jinsi wenye nguvu wanavyowakandamiza walio dhaifu. Ni kwa msingi huu ndipo nilipofikia natija kuwa, jamii ya mwanaadamu inahitaji utawala wa kijeshi ambao utadhamini utekelezwaji wa malengo ya mwanaadamu.”

Sergei Afanassiev aliendelea na utafiti wake ambapo ilimbainikia kuwa, katika kipindi chote cha historia kulikuwa na vipindi kadhaa japo vifupi ambapo mwanaadamu alionja ladha ya uadilifu na vipindi hivyo vilikuwa wakati wa mitume wa Mwenyezi Mungu. Suala hili lilimfanya awe na hamu ya kuijua dini hasa dini za Mwenyezi Mungu. Utafiti wake ulimfikisha kwenye natija kuwa, Mitume walikuja kwa ajili ya kueneza uadilifu, usawa na kuwaongoza wanaadamu kuelekea katika Tauhidi na kumwambudu Mungu Mmoja sambamba na kupambana na madhalimu na hivyo kufanya mabadiliko na marekebisho ya kina katika jamii. Kutokana na kuwa mitume walibaathiwa au kutumwa kwa lengo la kuirekebisha jamii na kuwaondoa wanaadamu katika minyororo; hivyo walipambana vikali na shirki hurafa na dhulma. Qur’ani Tukufu imetubainishia sifa za Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW katika Suratul A’raaf aya ya 157 ifuatavyo:

Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiyesoma wala kuandika, wanayemkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anayewaamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomwamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa.

Tauhidi na uadilifu ni msingi wa miito ya mitume wote wa Mwenyezi Mungu. Sergei Afanassiev anaendelea kusema: “Mimi niliweza kupata tawala bora zaidi katika dini za Mwenyezi Mungu. Mitume walikuwa watu wenye taathira kubwa kwenye jamii. Walipambana dhidi ya udikteta, ukandamizaji, dhulma na ukosefu wa uadilifu. Wakiwa wanaadamu waliokuwa wakimwamini Mungu Mmoja kwa dhati, walitoa wito kwa wanaadamu wajikurubishe kwa Mwenyezi Mungu. Aidha walitekeleza insafu na uadilifu kwa maana yake halisi na ni kwa sababu hii ndiyo tunaona thamani za kijamii kama vile uadilifu, uhuru na usawa katika mafundisho ya Mitume ya Mwenyezi Mungu. Hayo pia yamebainika wazi na kwa njia nzuri kabisa  katika sira na maisha ya mitume. Kwa hakika Mitume wa Mwenyezi Mungu daima walikuwa wakiwaelekeza wanaadmau katika saada na ufainisi na waliwataka wajiepusshe kutii masanamu na wanaotumia mabavu.” Mrussia aliyesilimu anaendelea kusema kuwa, Mitume wa Mwenyezi Mungu hawakufuatilia maslahi binafsi au ya kimaada na walitafakari tu kuhusu saada ya mwanaadamu. Sergei Afanassiev anasema kwa kuzingatia mafundisho ya Mitume wa Mwenyezi Mungu alihisi kuwa amemkaribia Mwenyezi Mungu zaidi na kwamba Mitume wake ni kigezo bora cha maisha ya mwanaadamu.

Bw. Sergei Afanassiev katika utafiti wake kuhusu dini za Mwenyezi Mungu alifanikiwa kuyapata mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Mtume wa Uislamu SAW ambaye ni Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, alikuja kwa ajili ya kutekeleza malengo ya Mwenyezi Mungu katika nyuga mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na kwa msingi huo aliasisi serikali iliyokuwa  kamili na iliyostawi zaidi katika zama zake. Pamoja na kuwepo muda mfupi na vizingiti kadhaa, aliweza kupata mafanikio makubwa zaidi katika njia ya kuelekea kwenye uhuru, uadilifu na ukamilifu wa kijamii. Mtume SAW alikuwa mwasisi wa jamii ya kwanza ya kitauhidi katika jamii iliyokuwa imejaa taasubi, chuki, ujahili n.k. Aidha aliunda udugu baina ya Waislamu katika siku zake za kwanza mjini Madina.

Sera za serikali ya Mtume SAW zilipangwa kwa madhumuni ya kufikia malengo ya juu kabisa. Kati ya malengo hayo ilikuwa ni kuasisi serikali ya kidini, kuleta usalama wa kijamii, kueneza uadilifu na utajiri kupitia njia kama vile Zaka. Vilevile aliandaa mazingira mazuri ya kustawisha jamii kupitia njia ya kuamrisha mema na kukataza mabaya sambamba na kuwapa waumini mamlaka na wakati huo huo kupambana na washirikina. Kwa hivyo, utawala wa Mtume wa Uislamu ulikuwa na sifa bora zaidi. Sifa muhimu zaidi ya serikali ya Nabii Muhammad SAW ilikuwa imani kwa Mwenyezi Mungu na masuala ya kiroho na kimaanawi. Kigezo kingine cha serikali hiyo tukufu kilikuwa uadilifu na kuwapa watu wote haki zao pasina kupendelea. Sifa nyingine ya serikali hiyo ilikuwa ni kujenga udugu baina ya Waislamu. Kurekebisha tabia na kujenga tabia na maadili bora zaidi ni sifa nyingine ya serikali ya Mtume SAW. Sira na maisha ya Mtume yalijaa mifano ya kuigwa ya maadili mema na hivyo jamii aliyoiongoza mjini Madina ilikuwa jamii ya kupigiwa mfano  kwani ilikuwa jamii halisi ya Kitauhidi. Kwa hakika jamii hiyo inaweza kuwa ilhamu kwa jamii ambazo zinataka kufuata mkondo wa kufikia daraja ya juu ya maisha ya dunia na ya kimaanawi. Hizo ni baadhi tu ya nukta tulizoweza kuziashiria kwa haraka kuhusu serikali iliyoanzishwa na Mtume SAW mjini Madina.

Bw. Sergei Afanassiev anaashiria nukta hizo na kusema hivi kuhusu dini tukufu ya Kiislamu: “Katika Uislamu nimeweza kupata jamii kamili zaidi yenye kumletea mwanaadamu saada na ufanisi. Kwa hakika Uislamu ndio njia bora zaidi ambayo humuwezesha mwanaadamu kufikia malengo yake matukufu. Mwenyezi Mungu amempa mwanaadamu uwezo na akili ili aweze kuchagua njia inayofaa maishani. Kwa msingi huo mwanaadmau anatakiwa kuchagua njia sahihi kwa kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu, uadilifu, uhuru na amani ambayo ni matakwa ya wanaadamu wote yaweze kufikiwa duniani.”

Bw. Sergei Afanassiev anasema hivi kuhusu hisia aliyopata baada ya kuamua kuukumbatia Uislamu katika maisha yake: “Niligeuka na kuwa mwanaadamu muumini. Baadhi ya marafiki zangu hunikosoa kwa uamuzi niliochukua. Pamoja na hayo ninatamani kuwa siku moja nao pia watapate kuongoka ili waweze kuufuata Uislamu na kwa njia hiyo, kama nilivyo name, wao pia wapate kuonja tamu wa maisha katika kivuli cha kumwamini Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo wangu matatizo yote duniani yanaweza kutatuliwa kwa kufuata Uislamu.”

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …