Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 12 Agosti 2014 16:28

Uislamu Chaguo Langu (87)

Uislamu Chaguo Langu (87)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru maishani yaani Uislamu. Katika makala yetu ya leo tutamuangazia Mrussia aliyesilimu Afanassiev Sergei. Karibu kujiunga nasi hadi mwisho.

@@@

Sergei Afanassiev ni mwenyeji wa Russia ambaye daima amekuwa muungaji mkono wa malengo matukufu kama vile uadilifu, uhuru, kupambana na umasikini na kupinga dhulma. Akiwa katika mikakati yake ya utafiti, aliweza kugundua ukweli kuwa, serikali au tawala zilizoundwa na wanaadamu katika kipindi chote cha historia hazikuweza kufikia malengo matukufu yaliyotajwa hapo juu. Sergei Afanassiev anafafanua zaidi kuhusu hili kwa kusema: "Tokea kuumbwa dunia hadi sasa, mwanaadmau daima amekuwa akitaka kuona jamii inayoundwa kwa msingi wa uadilifu. Katika historia kutaka uadilifu ndio chanzo cha malalamiko ya umma. Pamoja na hayo historia imekuwa ikishuhudia nmana ambavyo wenye nguvu huwakandamiza walio dhaifu. Ni kwa msingi ndio nilifikia natija kuwa jamii ya mwanaadamu inahitaji utawala wa kijeshi ambao utadhamini utekelezwaji malengo ya mwanaadamu."
Sergei Afanassiev aliendelea na utafiti kwake ambapo ilimbainikia kuwa, katika kipindi chote cha historia kulikuwa na vipindi kadhaa japo vifupi ambapo mwanaadamu alionja utamu wa uadilifu na vipindi hivyo vilikuwa wakati walipokuwa wakiishi mitume wa Mwenyezi Mungu. Suala hili lilimpelekea awe na hamu ya kuijua dini na hasa dini za Mwenyezi Mungu. Utafiti wake ulipelekea afikia natija kuwa, Mitume walikuja kwa ajili ya kueneza uadilifu, usawa na kuwaongoza wanaadamu kuelekea katika Tauhidi na kumuambudu Mungu Moja sambamba na kupambana na madhalimu na hivyo kuleta mabadiliko na marekebisho ya kina katika jamii. Kutokana na kuwa mitume walibaathiwa au kutumwa kwa lengo la kuirekebisha jamii na kuwaondoa wanaadamu katika utumwa; hivyo walipambana vikali na shirki hurafa na dhulma. Qur'ani Tukufu imetubainishia sifa za Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW katika Sura Al A'raaf aya ya 157 ifuatavyo:
Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao. Basi wale walio muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa.
Tauhidi na uadilifu ni msingi wa miito ya mitume wote wa Mwenyezi Mungu. Sergei Afanassiev anaendelea kusema: "Mimi niliweza kupata tawala bora zaidi katika dini za Mwenyezi Mungu. Mitume walikuwa ni watu wenye taathira kubwa kwenye jamii. Walipambana dhidi ya udikteta. Ukandamizaji, dhulma na ukosefu wa uadilifu. Wakiwa wanaadmau waliokuwa wakimuamini Mungu Moja kwa dhati,walitoa wito kwa wanaadamu wajikuruishe kwa Mwenyezi Mungu. Aidha walitekeleza insafu na uadilifu kwa maana yake halisi na ni kwa sababu hii ndio tunaona thamani za kijamii kama vile uadilifu, uhuru na usawa katika mafundisho ya Mitume ya Mwenyezi Mungu. Hayo pia yamebainika waz na kwa njia ya wazi kabisa katika sira ya maisha ya mitume. Kwa hakika Mitume wa Mwenyezi Mungu daima walikuwa wakiwaelekeza wanaadmau katika saada na ufainisi na waliwataka wajiepusshe kutii masnabu na wanaotumia mabavu." Mrussia aliyesililumu anaendelea kusema kuwa Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa hawafuatilii maslahi binafsi au ya kimaada na walitafakari tu kuhusu saada ya mwanaadamu. Sergei Afanassiev anasema katika kuzingatia mafundisho ya Mitume wa Mwenyezi Mungu nilihisi kuwa nimemkaribia Mwenyezi Mungu zaidi na kwamba Mitume wake ni kigezo bora cha maisha ya mwanaadamu.

@@@@

Bw. Sergei Afanassiev katika kufanya utafiti wake kuhusu dini ya Mwenyezi Mungu alifanikiwa kuyapata mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Mtume wa Uislamu SAW kama Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu alikuja kwa ajili ya kutekeleza malengo ya Mwenyezi Mungu katika nyuga mbali mbali za kisiasa, kiuchumi,kijamii na kiutamaduni na kwa msingi huo aliasisi serikali iliyokuwa kamili na iliyostawi zaidi katika zama zake. Pamoja na kuwepo muda mfupi na vizingiti kadhaa, aliweza kufanikisha na kuleta mafanikio bora zaidi katika njia ya kuelekea katika uhuru, uadilifu na ukamilifu katika jamii. Mtume SAW alikuwa muasisi wa jamii ya kwanza kitauhidi katika jamii iliyokuwa imejaa taasubi, chuki, ujahili n.k. Aidha aliweza kuunda udugu baina ya Waislamu katika siku zake za kwanza mjini Madina.
Sera za serikali ya Mtume SAW zilikuwa kwa lengo la kufikia malengo ya juu kabisa. Kati ya malengo hayo ilikuwa ni kuasisi serikali ya kidini, kuleta usalama wa kijamii, kueneza kwa uadilifu na utajiri kupitia njia kama vile Zakat. Aidha aliandaa mazingira ya kustawisha jamii kupitia kuamurisha mema na kukataza mabaya sambamba na kuwapa waumini utawala na wakati huo huo kupambana na mushrikina. Kwa hivyo, utawala wa Mtume wa Uislamu ulikuwa na sifa bora zaidi. Sifa muhimu zaidi ya serikali ya Mtume Muhammad SAW ilikuwa ni imani kwa Mwenyezi Mungu na umaanawi. Kigezo kingine cha serikali hiyo tukufu kilikuwa ni uadilifu na kuwafikishia wote haki pasina kupendelea. Sifa nyingine ya serikali hiyo ilikuwa ni kujenga udugu. Kurekebisha tabia na kuleta tabia na maadili bora zaidi ni sifa nyingine ya serikali ya Mtume SAW. Sira na maisha ya Mtume yalijaa mifano ya kuigwa ya maadili mema na hivyo jamii aliyoiongoza Madina ilikuwa jamii ya kupigiwa mfano kwani ilikuwa jamii halisi ya Kitauhidi. Kwa hakika jamii hiyo inaweza kuwa ilhamu kwa jamii ambazo zinataka kufuata mkondo wa kufikia daraja ya juu ya maisha ya dunia na ya kimaanawi. Hizo ni baadhi tu ya nukta tulizoweza kuziashiria kwa haraka kuhusu serikali iliyoanzishwa na Mtume SAW mjini Madina.
Bw. Sergei Afanassiev anaashiria nukta hizo na kusema hivi kuhusu dini tukufu ya Kiislamu: "Katika Uislamu nimeweza kupata jamii kamili zaidi yenye kumleketa mwanaadamu saada. Kwa hakika Uislamu ndio njia bora zaidi ambayo inaweza kumpelekea mwanaadamu afikia malengo yake matukufu. Mwenyezi Mungu amempa mwanaadamu uwezo na akili ili aweze kuchagua njia inayofaa maishani. Kwa msingi huo mwanaadmau anatakiwa kuchagua njia sahihi na ili kwa kutekeleza maamurisho ya Mwenyezi Mungu, uadilifu, uhuru na amani ambayo ni matakwa ya wanaadmau wote yaweze kufikiwa duniani."
Bw. Sergei Afanassiev anasema hivi kuhusu hisia aliyopata baada ya kuamua kuukumbatia Uislamu katika maisha yake: "Mimi niligeuka na kuwa mwanaadamu muumini. Baadhi ya marafiki zangu hunikosoa kwa uamuazi niliochukua. Pamoja na hayo mimi ninatamani kuwa siku moja nao pia wapate kuongoka ili waweze kuufuata Uislamu na kwa njia hiyo, sawa nami wapate kuonja utamu wa maisha katika kivuli cha kumuamini Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo wangu matatizo yote duniani leo yanaweza kutatuliwa kwa kufuata Uislamu."

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …