Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 22 Juni 2014 21:41

Uislamu Chaguo Langu (86)

Uislamu Chaguo Langu (86)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru katika maisha ya dunia na kesho akhera yaani Uislamu.
Katika makala yetu ya leo tutamuangazia raia wa nchi ya Malaysia aliyesilimu aitwaye Kwan ambaye amepata masaibu mengi baada ya kuukubali Uislamu Maishani. Mmalaysia huyo ambaye aliwahi kuwa mfuasi wa dini za Budhha na Ukristo hatimaye alivutiwa na mafundisho ya Qur'ani na pia jamii ya Kiislamu na hivyo akaamua kusilimu. Jiunge nami katika makala hii fupi tuweze kumuangazia Mmalaysia huyu aliyesilimu.

@@@

Kwan alizaliwa katika familia iliyokuwa ikifuata dini ya Buddha. Akiwa na umri wa miaka 6 alienda katika shule moja ya Kichina na hapo alijifunza kuhusu itikadi za Confucian. Baadaye akiwa na umri wa miaka tisa alijifuza lugha ya Kiingereza katika Shule ya Victoria mjini Kuala Lumpur Malaysia. Baada ya muda usio mrefu aliweza kujifunza Bibilia na kwa miaka kadhaa alikuwa akifuata dini ya Ukristo. Kuan alizama sana katika mafundisho ya Ukristo na kuendelea na masomo ya juu hadi kufikia cheo cha kasisi aliyekuwa akihubiri ndani ya makanisa. Lakini siku moja akiwa anaelekea Kanisani, alikutana na rafiki yake wa zamani ambaye alikuwa amebadilisha mkondo wake wa maisha. Bw. Kwan anafafanua zaidi kwa kusema:
"Siku moja nilikuwa nikienda Kanisani kuhubiri na hapo nilikutana na Mwislamu mwenye asili ya India ambaye nilikuwa najuana naye kwa muda mrefu. Hapo alinikabidhi zawadi ya tarjama ya Kiingereza ya Qur'ani Tukufu. Jina la Mwislamu huyo ni Kaka Mohammad. Alikuwa na hamu sana kuwafunza wengine kuhusu dini yake, yaani Uislamu. Baada ya kupokea nakala hiyo ya Qur'ani, nilikuwa na hamu sana ya kuisoma ili niweze kuyajua mafunzo ambayo Waislamu hufuata. Awali nilivutiwa sana na mtiririko maridadi wa aya za Qur'ani Tukufu. Lakini taathira hiyo haikuwa na nguvu ya kunifanya niache dini yangu. Niliendelea na maisha yangu ya kawaida lakini ilifika wakati ambao nilisikitishwa sana na hitilafu na malumbano ndani ya kanisa. Hali hii pamoja na masuala mengine ni mambo ambayo yalipelekea nizame katika fikra na nitake kuujua Uislamu zaidi. Kwa msingi huo nilianza tena kuisoma Qur'ani lakini mara hii kitabu hicho kiliniathiri sana kutokana na uzingatiaji wa kina niliokuwa nao zaidi ya huko nyuma."
Tokea ilipoteremshwa kwa njia ya Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu SWT, Qur'ani iliweza kupenya katika nyoyo za watu. Kwa hakika mvuto wake maalumu huwaathiri kwa njia ya ajabu wale wanaoisoma kwa uzingatiaji. Hakuna shaka kuwa kitabu hiki chanye maajabu hakiwezi kuwa kimeletwa na mwanaadamu. Inasimuliwa kuwa hata mushrikina wa Makka pamoja na ukaidi wao mkubwa lakini walikuwa wakienda karibu na kuta za nyumba ya Mtume Muhammad SAW ili waweze kusikia akiisoma Qur'ani wakati wa alfajiri.
Washirikina na makafiri walistaajabishwa sana na balagha pamoja na maudhui za Qur'ani. Kutokana na ukaidi wao walidai eti Mtume SAW ni mchawi. Madai yao yenyewe yalikuwa ni kukiri kuwa hawawezi kuleta kitabu mithili ya Qur'ani. Mushrikina hata walikuwa wakiwausia watu waliokuwa wakija pembizoni mwa Masjid Haram kuweka pamba katika masikio yao ili waisikie sauti ya Mtume SAW akisoma Qur'ani.
Kwa hakika Qur'ani Tukufu ni muujiza ambao leo ungali na taathira kama ile ya zama za awali. Hata baada ya kupita zaidi ya miaka 1400, muujiza wa Qur'ani ungalipo na hauna vizingiti vya zama wala jiografia. Mmalaysia aliyesilimu Bw. Kwan anaendelea kusema: "Moja kati ya masuala yaliyonivutia katika Uislamu ni tauhidi au upweke wa Mwenyezi Mungu. Kwa hakika hii ni nukta muhimu zaidi ambayo inautenganisha Uislamu na Ukristo."

@@@

Nukta nyingine iliyomvutia Kwan katika Uislamu ni kuwa mafundisho ya Kiislamu yanaangazia sekta zote za maisha ya mwanaadamu pasina kufurutu mipaka. Kwa mtazamo wa Uislamu, mwanaadamu ni kiumbe cha kimaada na kimaanawi na ana maisha ya milele. Aidha kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, vitendo na amali za mwanaadamu zina uhusiano na hatima yake ya mwisho. Hii ina maana kuwa jitihada na juhudi zote katika maisha ya leo duniani huwa na taathira katika saada na shifaa ya mwanaadamu. Kwa msingi huo mwanaadamu anapaswa kuwa mwangalifu katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Bw. Kwan pia anasema pia alivutiwa na Uislamu kutokana na msimamo wa kati na kati katika dini hii tukufu kwa kusema: "Baadhi ya itikadi za kidini zinaupa mgongo dunia na kuzingatia masuala ya kimaanawi tu huku katika upande mwingine kukiwa na itikadi ambazo zinapinga kabisa umaanawi na maadili bora katika maisha. Hapa nataka kusema kuwa itikadi hizi mbili si tu kuwa zinamuweka mbali mwanaadmau na usalama na utulivu bali pia zinaiweka mbali dunia na usalama na utulivu. Hii ni kwa sababu chanzo cha machafuko na vita duniani ni misimamo mikali na kujitakia makuu."
Bw. Kwan anasema Uislamu umemuweka mwanaadmau mbali na misimamo mikali ya pande zote mbili.
Nukta nyingine iliyomvutia Kwan katika Uislamu ni ukamilifu na upana wa sheria na maamurisho ya Kiislamu kwani katika Qur'ani na riwaya mbali mbali tunaona kuwa lengo la dini ni kumhakikishia mwanaadamu saada na maisha bora ya dunia na akhera.
Mmalaysia huyu aliyesilimu anasema Uislamu unaleta mlingano baina ya umada na umaanawi na kwamba dini hii tukufu ni ya kimantiki. Nukta hizo zilizotajwa ni kati ya sababu zilizompelekea Kwan kusilimu akiwa na umri wa miaka 42 na kuchagua jina la Ibrahim. Katika kumalizia Bw. Ibrahim Kwan anasema: "Kwa hakika nina furaha kubwa kutokana na kuwa nimekuwa Mwislamu na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwani hivi sasa nimeweza kupata mafanikio makubwa maishani."

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …