Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 16 Juni 2014 14:37

Uislamu Chaguo Langu (84)

Uislamu Chaguo Langu (84)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru  na ufanisi katika maisha ya hapa duniani na kesho akhera, yaani Uislamu. Ni matumaini yangu kuwa utakuwa nami hadi mwisho ambapo leo tutamuangazia raia wa Austria aliyeamua kuufuata Uislamu, Bi.Clara Lantsel.

@@@

Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia ongezeko kubwa la wasomi wa nchi za Magharibi ambao wanavutiwa na Uislamu. Hivyo hapa swali linaloibuka ni nukta gani ambayo imepelekea Uislamu uwe dini bora mbele ya Wamagharibi hao ikilinganishwa na dini zingine? Swali hili limepelekea wataalamu kadhaa kufanya utafiti kulihusu. Uchunguzi umebaini kuwa kutokana na mtindo wa maisha ya Kiislamu na pia kutokana na kuwa dini hii imeangazia sekta zote za maisha, Wamagharibi wengi wamevutiwa na dini hii tukufu. Wengi wanaosilimu Ulaya na Amerika Kaskazini huwa wamezaliwa katika Ukristo. Kwa hakika Uislamu ni dini ya amani, utulivu, akili, mantiki, heshima na uhuru halisi wa mwanaadamu. Wakristo wenye kuhakiki wanaiona dini yao kama iliyo na upungufu na isiyofuata misingi ya mantiki. Nadharia ya utatu katika Ukristo imewachanganya Wakristo wengi. Aidha nadharia kama ile ya kuwakataza baadhi ya watu kuoa pia imepelekea Ukristo kutiliwa doa na wengi. Hizo ni baadhi tu ya nukta ambazo hupelekea Wakristo kuvutiwa na Uislamu na kuiona dini hii tukufu kuwa ni ya mantiki inayoenda sambamba na maumbile asilia ya mwanaadamu.

Bi. Clara Lantselambaye amechagua jina la Zainab anasema alisilimu baada ya kuwa ameshafanya utafiti wa kina. Ingawa alizaliwa na kulelewa katika familia ya Kikristo lakini anasema Ukristo haukuweza kumpa majibu ya kukinaisha. Akiashiria kile ambacho leo kinaarifishwa kama itikadi ya Kikristo anasema:  "Kwa matazamo wangu, moja ya sababu ambazo zimepelekea dini ya Ukristo ikose mvuto miongoni mwa vijana ni kuwa haina misingi imara. Hili linatokana na kuwa sheria za Ukristo hazina muelekeo maalumu na kila mtu anaweza kuitafsiri dini hiyo anavyotaka."

Zainab Lantsel anaendelea kusema: "Kwa mtazamo wangu, wakati mwanaadamu anapotaka kufikia malengo ya juu, anapaswa kufanya jitihada zaidi na kutekeleza maamrisho na maelekezo ipasavyo. Mfano wake ni kama ambavyo mwanariadha anavyojitahidi na kufanya kila awezalo ili kupata medali. Kwa hivyo ili kuweza kupata umaanawi, mwanaadamu anapaswa kufanya mambo ya kimsingi na ya lazima na mambo hayo ya kimsingi ndio msingi wa dini. Iwapo misingi kama hiyo haitakuwepo, basi umaanawi utatatoweka na hii ndio hali iliyoukumba Ukristo katika nchi za Magharibi. Ukristo ambao unahubiriwa kupitia Bibilia katika nchi za Magharibi ni nadharia za watu binafsi. Nadharia hizo hazina maelekezo ya kina kuhusu namna mwanaadamu anavyopaswa kuishi. Mimi daima nilikuwa nikitafuta mpango kamili wa kunielekeza maishani ili niweze kupata muongozo bora zaidi."

Kwa ujumla ni kuwa, ukarimu na mahaba katika mafundisho ya Kiislamu huwavutia wengi katika dini hii tukufu. Iwapo ukarimu na mahaba hayo yatadhihirika katika tabia za watu, basi hiyo huwa njia bora zaidi ya kuhubiri dini na kuwavutia watu.

Muaustria aliyesilimu Zainab Lantsel anasema akiwa mtoto alipata kujuana na majeruhi wa vita kutoka Iran ambao walipata majeraha yao katika hujuma ya silaha za kemikali ya utawala wa Saddam dhidi ya Iran. Anasema kujuana na Wairani hao ni jambo lililomvutia kuelekea katika Uislamu. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Uislamu na hasa madhehebu ya Kishia, una mvuto mkubwa sana. Hapa ninaweza kuashiri nukta mbili za msingi ambazo kwa matazamo wangu ni maridadi na zenye kupendeza sana: Moja ni kumbukumbu ya zama zangu za utotoni ambapo nilipata kujuana na majeraha wa kivita kutoka Iran waliokuwa wamekuja Austria kupata matibabu. Majeraha hao Walikuwa na mvuto wa kipekee wa kiroho sambamba na kuwa na muamala na tabia nzuri iliyojaa ukarimu. Pamoja na kuwa wengi wao hawakuwa na mikono wala miguu sambamba na kuathiriwa vibaya na gesi za sumu vitani, lakini walikuwa na moyo wa bashasha. Kwa kweli tabia zao nzuri ni jambo lililokuwa na taathira ya kina katika moyo wangu. Maadili yao mema ni nukta iliyoashiria kuwepo fikra na itikadi imara. Uzoefu huu wangu wa utotoni ni jambo ambalo lilinisaidia kupata motisha wa kufanya utafiti zaidi kuhusu Uislamu, dini ambayo ilikuwa imewafanya wafuasi wake wawe na tabia nzuri na hulka njema."

Zainab Lantsel anasema sababu nyingine iliyompelekea auchague Uislamu maishani ni kutokana na kuwa dini hii tukufu ina sheria na mafundisho imara. Anabainisha zaidi kwa kusema: "Kuwepo sheria imara ambazo humuongoza Mwislamu katika kila uga wa maisha ni jambo ambalo lilinivutia sana. Hizi ni sheria ambazo zinaweza kutatua matatizo ya mwanaadamu kwa njia bora zaidi na kumuongoza kufikia ubora."

@@@

Familia ni ndio msingi wa jamii. Ni kupitia familia ndipo vizazi huibuka na hivyo kumuwezesha mwanaadmau kustawi na kupata ufanisi. Ukiangazia historia ya mwanaadamu utaona kuwa tokea mwanzo hadi sasa, familia ndio msingi wenye thamani na umuhimu zaidi katika jamii. Uislamu nao pia umeleta muongozo bora kuhusu familia. Zainab Lantsel anaashiria mitazamo ya Ukristo na Uislamu kuhusu familia na kusema: "Iwapo Mkristo mwenye kufungamana na itikadi yake anataka kuishi maisha bora ya kifamilia hukumbwa na matatizo mengi sana. Hii ni kwa sababu Wakristo wengi hawana mtazamo mzuri kuhusu maisha ya ndoa hasa katika nchi za Magharibi kwani wengi huhimizwa kuishi maisha ya upweke bila kuoa. Katika mafundisho ya Kikristo pia hakuna maelezo ya kina kuhusu masuala ya familia na ndoa. Lakini katika Uislamu tunaona, mafundiho mapana sana na yanayohusu nukta zote kubwa na ndogo za maisha ya kifamilia. Kwa hivyo ni wazi kuwa mafundisho ya Uislamu yako katika kila uga wa maisha ya mwanaadamu na hivyo dini hii humuondoa mwanaadamu kutoka katika upweke wenye kuleta maangamizo." Muaustria huyu aliyesilimu anasema: "Iwapo katika Bibilia kunasisitizwa kuhusu ukarimu na kusameheana, lakini hakuna maelezo kuhusu njia sahihi za kuyatekeleza mafundisho hayo na hivyo yamkini watu wakafanya makosa katika utekelezaji. Nchini Austria hakuna tafauti kubwa baina ya Mkristo na raia mwingine wa kawaida asiyeamini Ukristo. Kuenda Kanisani kila Jumapili au siku nyingine hakuibui tafauti kubwa baina ya Mkristo na asiye kuwa Mkristo katika maisha ya kawaida. Lakini katika Uislamu, iwapo utamuona Mwislamu ambaye anatakeleza ipasavyo mafundisho ya Kiislamu, basi utamuona anatafautiana sana na wengine na natija ya amali zake njema huwa wazi kwa wote."

Baada ya kusilimu, Zainab Lantsel alikumbana na vizingiti na masaibu mengi kutoka kwa familia na jamii alimokuwa akiishi. Pamoja na hayo anasema uzoefu huo ulimfanya apate utulivu na yakini moyoni. Anaongeza kuwa: "Inakuwa vigumu sana kutekeleza sheria za Kiislamu katika maisha ya kila siku. Tunafanikiwa kukabiliana na masaibu kutokana na kuwa Mwenyezi Mungu yuko katika maisha yetu na tunahisi ukuruba na mahaba yake. Kwa hakika Uislamu kwa mafundisho yake yenye thamani yameweza kuwaletea wafuasi wake utulivu na yakini. Huu ni utulivu ambao hauonekani katika jamii za Magharibi."

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …