Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 03 Juni 2014 12:37

Uislamu Chaguo Langu (83)

Uislamu Chaguo Langu (83)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru maishani na yenye kuleta saada ya dunia na akhera yaani Uislamu. Katika makala yetu ya leo tutamuangazai Mfaransa aliyesilimu anayeitwa Bi. Janet. Ni matumaini yangu utajiunga nami hadi mwisho.

@@@

Pamoja na kuwa vyombo vya habari hasa vya nchi za Magharibi vimekuwa vikijitahidi kwa muda mrefu kueneza propaganda chafu dhidi ya Uislamu, lakini tunashuhudia namna dini hii tukufu inavyozidi kuwavutia watu wengi duniani wakiwemo kutoka nchi za Magharibi na hivyo kuwawezesha kupata utulivu wa kiakili na kujaza pengo la kimaanawi.  Kukosekana usalama na utulivu wa kiakili, kuenea ufisadi wa kimaadili, kusambaratika jamii na familia pamoja na matatizo mengine chungu nzima ni mambo ambayo huwalazimu Wamagharibi kutafuta njia ya kuupata ukweli na kufikia utulivu wa kiroho. Utafutaji wao huo hatimaye huwafikisha Wamagharibi wengi katika Uislamu.  Moja ya sababu zinazowapelekea Wamagharibi kuukumbatia Uislamu ni kuwa, wao huwa hawawezi kutatua matatizo yao maishani kupitia mafundisho ya Ukristo kwani  mafundisho mengi ya dini hiyo yamepotoshwa.

Wanaosilimu wanaamini kuwa mafundisho ya Uislamu ni ya kivitendo na hivyo huweza kuzuia ufisadi katika jamii.

Moja ya nukta za kuvutia katika Uislamu ni kuwa dini hii tukufu imeweka njia ya moja kwa moja ya uhusiano wa mja na Mwenyezi Mung Mkarimu. Katika Qur'ani Tukufu, tunafundishwa kuwa, wakati mwanaadamu anapomkumbuka Mwenyezi Mungu, uhusiano wake na Mola Muumba huwa ni wa daima. Hii ni kwa sababu kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu, mwanaadamu hupata utulivu na yakini moyoni. Hii ndio nukta iliyomvutia Janet katika Uislamu. Anafafanua kwa kusema: "Mimi nilizaliwa katika familia ya Kikristo. Tokea utotoni, daima nilikuwa nikipenda sana kuwa na uhusiano na Mwenyezi Mungu na nilikuwa nikihisi kuwa nampenda Mwenyezi Mungu. Wakati nilipofika ujanani, nilifanya utafiti na kufikia natija kuwa katika jamii ya Kimagharibi nilimokuwa nikiishi, ilikuwa nadra sana kuhisi kuwepo Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo sikutosheka na utafiti wangu. Katika jamii yangu, ilikuwa nadra sana kumpata mtu ambaye daima alikuwa akimkumbuka Mwenyezi Mungu. Hivyo niliendelea kutafuta ukweli na nilikuwa na hamu sana ya kumjua Mwenyezi Mungu na kupata utulivu wa kiroho. Niliendelea kuhangaika hadi pale nilipoujua Uislamu. Nilisoma kitabu kuhusu Uislamu na Mtume Muhammad SAW. Kitabu hicho kiliniathiri sana hasa nilipokisoma kwa makini. Baad ya kukisoma niliweza kushuhudia mabadiliko makubwa katika maisha yangu. Ilikuwa ni kana kwamba nimezaliwa upya. Mabadiliko hayo yalikuwa ni mimi kuanza kuiamini dini tukufu ya Kiislamu."

Idadi kubwa ya watu wanaosilimu wanasema moja ya nukta muhimu zinazowapelekea kuvutiwa na dini hii ya Mwenyezi Mungu ni kuwa Uislamu ni dini yenye muongozo sahihi kuhusu maisha na dini hii inajibu maswali kuhusu sekta zote za maisha ya mwanaadmau. Wanasema hupata majibu ya maswali yao katika Uislamu na hii ndio sababu ya wao kuvutiwa na dini hii. Kwa kifupi ni kuwa Uislamu ni mfumo kamilifu wa maisha ya hapa duniani na kesho akhera. Kwa mfano Uislamu hausemi kuwa iwapo unataka kustawi kimaanawi basi hupaswi kuoa au kuyapa mgongo mahitaji ya dunia. Katika Uislamu hata Mtume Mtukufu SAW pamoja na kuwa na daraja ya juu ya umaanawi, alioa na hata kuwahimiza wengine kuoa.

Maisha ya Mtume SAW, kama kigezo bora zaidi katika Uislamu ni nukta nyingine iliyomvutia Bi. Janet katika dini hii tukufu. Shakhsia ya Mtume na kuijua sira yake hasa mapambano ya mtukufu huyo dhidi ya dhulma, ibada potofu na ubaguzi ni mambo ambayo yalikuwa na taathira kubwa yaliyompelekea Janet kuvutiwa na Uislamu. Watu ambao wanaifahamu ipasavyo shakhsia ya Mtume SAW na Ahul Bayt wake, huvutiwa sana na Uislamu. Hii ni kwa sababu tunaishi katika dunia ambayo hakuna watu wenye sifa bora kama shakhsia hao watukufu kwani wanaofika madarakani sasa hutumia vibaya vyeo vyao. Janet anafafanua zaidi kwa kusema: "Sira na hotuba za Mtume Mtukufu wa Uislamu ni mambo ambayo yamekuwa na taathira kubwa katika fikra zangu. Kwa mfano Mtume SAW katika moja ya hotuba zake alisema: 'Enyi Watu! Mwenyezi Mungu amendoa ghururi ya kijahili na kujifakharisha kwa mababu. Wanaadamu wote ni kutoka kizazi kimoja cha Adam, na hakuna Mwarabu aliye na fadhila zaidi ya Muajemi (au asiyekuwa Mwarabu) ila katika takua.' Janet anasema kauli hii ya Mtume SAW inaondoa mipaka ya kijiografia, kiutamaduni na kirangi. Katika hali kama hii wanaadmau wote wanahisi kuwa karibu na Uislamu na wanaweza kujihusisha na dini hii kwa njia rahisi.

@@@

Historia ya Uislamu inashuhudia kuwa, Mtume Mtukufu SAW alisisitiza kuhusu kuwaita watu wote katika njia ya Uislamu na wala hakuzingatia kaumu au rangi maalumu katika wito wake. Mtume aliwakusudia wanaadamu wote kwa jumla katika kuuhubiri Uislamu na wala hakuzingatia rangi, utaifa au nukta zingine zozote ambazo hutumiwa kuwaonyesha baadhi ya wanaadamu kuwa bora kuliko wengine. Jamii ya kwanza iliyoundwa na Mtume Mtukufu wa Uislamu ilikuwa jamii iliyokuwa na watu kutoka rangi na kaumu mbali mbali. Katika jamii aliyoiasisi Mtume Muhammad SAW walikuwemo watu mashuhuri kama vile Shuayb kutoka Roma, Bilal kutoka Habasha na Salman kutoka Iran.

Janet anasema nukta hii ilimvutia sana kwani tokea mwanzo wa kudhihiri kwake, Uislamu uliweza kuwavutia kwa kasi watu kutoka rangi na mataifa mbali mbali na watu hao walivutiwa na idiolojia ya Kiislamu tu na wala hawakutafakari kuhusu masuala ya utaifa, kabila au rangi zao.

Historia inashuhudia pia kuwa tokea mwanzo wa kudhihiri kwake, Uislamu ulipinga kabisa mielekeo ya ubaguzi wa rangi na ukabila. Hapa tunapaswa kuongeza kuwa, Uislamu kupinga ubaguzi wa rangi na taasubi za kikaumu au kikabila haimaanishi kuwa dini hii inapinga kuwepo mataifa na kaumu mbali mbali. Uislamu unakubali kuwepo mataifa na kaumu kuwa ni ukweli usiopingika na ni jambo la kimaumbile kwani Mwenyezi Mungu SWT amewaumba wanaadamu wenye lugha na rangi mbali mbali. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu SWT anavyosema katika Qur'ani Tukufu Surat al H'ujuraat aya ya 13: Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mcha-Mungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.

Kwa mtazamo wa Uislamu, itikadi ya kidini na mtazamo wa pamoja wa kifikra ni nguzo muhimu na ya kimsingi katika kuwaunganisha wanaadamu. Kwa hivyo wanaadmau wawili ambao wana itikadi moja ni ndugu hata kama watakuwa tafauti kwa mtazamo wa kilugha, kirangi, kitaifa au kijiografia.

Mfaransa aliyesilimu, Bi. Janet anafafanua zaidi kuhusu namna Qur'ani ilivyomvutia katika Uislamu kwa kusema:  "Kwa kuuchagua Uislamu, niliweza kupata ufahamu wa kina kumhusu Mwenyezi Mungu. Nilipata manufaa mengi kwa kuzichunguza kwa kina aya za Qur'ani. Baadhi ya aya za Qur'ani zinazingumza kwa umaridadi kuhusu maumbile ya mbingu na ardhi. Aya hizi kwa hakika zimepelekea nijikuribishe zaidi kwa Mwenyezi Mungu na kutafakari kuhusu uwepo wake. Tokea niliposilimu na kuanza kuisoma Qur'ani, ninahisi Mwenyezi Mungu yupo katika maisha yangu. Hata sasa kila ninapofanya utafiti kuhusu Uislamu mimi huweza kumfahamu Mwenyezi Mungu kwa njia bora zaidi kama muumba wa dunia na hivyo uhusiano wangu naye huwa karibu na wa kirafiki zaidi."

Janet ambaye baada ya kusilimu alichagua jina la Maryam anasema: "Sisi tunapaswa kutumia fursa tulizonazo hapa duniani. Mimi ninaamini kuwa iwapo Waislamu watatekeleza kivitendo na kwa njia sahihi mafundisho ya Uislamu, watu watavutiwa zaidi na dini hii tukufu. Kama ambavyo tunashuhudia, nchi za Ulaya na Marekani zinashuhudia ongezeko la watu wanaosilimu kila siku.  Hivi sasa Uislamu unastawi kwa kasi duniani na hivyo tunapapswa kuwa na matumaini kuhusu mustakabali." Mfaransa aliyesilimu, Bi.Maryam pia anazungumzia taathira ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kusilimu kwake kwa kusema: "Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamepelekea Waislamu duniani kuamka. Tunaweza kusema kuwa kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Uislamu ulipata uhai mpya kwani idadi kubwa ya watu Walisilimu baada ya mapinduzi hayo."

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …