Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 03 Juni 2014 12:36

Uislamu Chaguo Langu (82)

Uislamu Chaguo Langu (82)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huwaangazia watu ambao baada ya utafiti wa kina huamua kufuata njia ya haki na iliyojaa nuru katika maisha ya dunia na akhera yaani Uislamu. Ni matumani yangu mtakuwa nami hadi mwisho ambapo leo tutamuangazia mwanamke Mjerumani aliyesilimu anayeitwa Dora ambaye alivutiwa na kuamua kuufuata Uislamu kupitia Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyoongozwa na Hayati Imam Khomeini MA.

@@@

Kuna matukio mengi ya Kihistoria ambayo hayafungamani moja kwa moja na jiografia ya eneo la kujiri na wala zama au wakati maalumu. Baadhi ya matukio huanza kujiri katika eneo moja na athari zake kuenea na kuhisika kote duniani kwa muda mrefu. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mfano wa matukio kama hayo yasiyokuwa na mipaka ya kijiografia, zama na wakati maalumu. Mapinduzi haya makubwa ni chanzo cha ilhamu na mvuto kwa idadi kubwa ya watu duniani. Pamoja na kupita zaidi ya miaka 35 tokea yajiri mapinduzi haya, bado yanaendelea kuwa chanzo cha kuibuka harakati na mabadiliko.

Wakati ilipotajwa maudhui ya kuyaeneza kimataifa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, vyombo vya habari vya nchi za Magharibi viliibua propaganda potofu kuhusu suala hilo. Ilidaiwa kuwa lengo la Iran ni kuingulia mambo ya ndani ya nchi zingine na kuangusha mifumo ya kisiasa katika nchi hizo. Lakini propaganda hizi zilipata pigo kufuatia hotuba ya wazi ya Imam Khomeini MA ambaye alibainisha kuhusu kuenea Mapinduzi ya Kiislamu kimataifa kwa kusema: "Maana ya kueneza mapinduzi yetu Kimataifa ni kuwa mataifa yote yaamke, serikali zote ziamke na kujikwamua kutoka kwenye matatizo ili watu wapate nusra na kuokoka."

Kwa mtazamo wa Imam Khomeini MA kueneza Mapinduzi ya Kiislamu kimataifa kuna maana ya kueneza thamani za kimaanawi na kubainisha maana ya Uislamu duniani sambamba na kuarifisha ustaarabu na utamaduni wa Kiirani-Kiislamu na pia kuhuisha utamaduni wa Ahul Bait AS kwa kutumia suhula za mawasiliano na habari. Kuenezwa mafundisho na thamani za juu za Kiislamu ni jambo ambalo liliwavutia wengi duniani akiwemo Bi. Dora na kumfanya aanze utafiti wa kina kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu na Uislamu.

Akifafanua zaidi, Mjerumani huyu aliyesilimu anasema: "Kwangu mimi nilivutiwa sana na mafundisho ya Uislamu kutokana na kuwa yaliweza kuwalea na kuibua viongozi huru kama Imam Khomeini."  Bi. Dora ambaye alizaliwa katika familia ya Kikristo nchini Ujerumani anaelezea namna alivyoishi na hatimaye kuujua Uislamu kwa kusema: "Mimi nilizaliwa katika familia ya Kikatoliki. Mama yangu alifungamana sana na mafundisho ya Kikristo. Lakini kwa mtazamo wa baba yangu, dini ilikuwa jambo la pili kwa umuhimu katika maisha. Ni katika mazingira kama haya ndio niliweza kuujua Ukristo. Katika zama za ubarobaro, nilianza kutafuta maana na malengo ya maisha. Lakini la kusikitisha ni kuwa, sikufikia natija katika juhudi zangu za utafutaji kwani kulikuwa na mgongano mkubwa baina ya maisha ya kawaida na mafundisho ya Kikristo. Hali hii ilikuwa mbaya kiasi kwamba nilidhani kuwa iwapo mtu anataka kumuamini Mwenyezi Mungu kikamilifu basi hawezi kuendelea na maisha ya kawaida. Sikuweza kupata njia ya kuridhisha roho na fikra yangu na kila nilivyozidi kuutafuta ukweli ndivyo nilivyozidi kupoteza matumaini. Ni kwa sababu hii ndio sikuwa na budi ila kujisalimisha kwa vigezo ambavyo mwanaadamu alikuwa amewekewa katika jamii ya Kimagharibi. Hivyo nikawa ninaishi maisha ya anasa na starehe  zilizokiuka maadili."

Ni katika kipindi hicho ndipo Bi. Dora alipopata kujuana na mtu kutoka Yugoslavia na hatimaye wakaoana na bwana huyo.

Mume wa Bi Dora, Bw. Chalovich aliweza kumfunza mambo mengi kuhusu dunia. Kupitia mume wake, Dora aliweza kujua mengi kuhusu namna mataifa yalivyokuwa yakidhulumiwa na kukandamizwa na madola makubwa ya kibebebru na namna madola hayo yalivyokuwa yakipora utajiri wa nchi nyingi  duniani.

Bi. Dora anafafanua kwa kusema: "Mume wangu alikuwa na fikra zilizonivutia sana. Alikuwa amefungamana na watu waliotengwa na kudhulumiwa. Ni kwa sababu hii ndio alikuwa akifanya utafiti kuhusu mapinduzi katika maeneo mbali mbali ya dunia. Kwa njia hii aliweza kuleta mabadiliko ya kimsingi katika maisha yangu. Ni katika kipindi hicho ndipo yalipojiri Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini MA. Hapo mume wangu ambaye alikuwa amefanya utafiti kuhusu mapinduzi katika maeneo mbali mbali ya dunia, kwa mara ya kwanza alikumbana na Mapinduzi ambayo chimbuko na mizizi yake ilikuwa ni fikra za kidini. Mume wangu ambaye hadi wakati huo alikuwa akiona dini kama kizingiti katika harakati za kimapinduzi za wananchi na kubakia nyuma jamii, sasa alikumbana na mapinduzi ambayo kiongozi wake alikuwa mwanazuoni wa kidini. Jambo hili lilimpelekea mume wangu abadilishe kabisa mitazamo yake nami hapo nikaamua kuanza kufanya utafiti kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran."

@@@@

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni jambo ambalo lilipelekea wasomi wengi kutambua ukweli kuhusu nguvu na uwezo wa Uislamu katika kuibua harakati za wananchi na kimapinduzi. Moja kati ya mafanikio makuu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kuwa yaliweza kupelekea mataifa yaliyokuwa yamedhoofishwa kuamka na kupata moyo wa mapambano na kujitolea. Mapinduzi hayo yalipelekea kuibuka watu wenye uwezo wa kukabiliana na dhulma na kuwa tishio kubwa zaidi kwa madola ya kibeberu. Harakati kubwa na pana ya Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Hayati Imam Khomeini MA ilikuwa ni harakati yenye kuleta mabadiliko makubwa katika historia ya zama hizi na chimbuko lake lilikuwa ni mafundisho ya kidini jambo ambalo lilipelekea kuwepo changamoto ya kina baina ya nchi za Magharibi na Uislamu. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipelekea kuibuka mwamko miongoni mwa Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu kote duniani. Aidha Mapinduzi ya Kiislamu yalifanikiwa kufichua hadaa ya demokrasia ya kiliberali ya nchi za Magharibi ambazo zilikuwa zikiwahadaa walimwengu kuwa eti ni watetezi wa haki za binaadamu, uhuru na demokrasia. Pale Bi. Dora akiwa na mume wake walipoanza kufanya utafiti kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran walivutiwa sana na harakati hii ya kidini ya wananchi. Kuhusu hili Bi. Dora anasema:

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipelekea tuichunguze dini kwa mtazamo mwingine na hilo lilipelekea tupate mabadiliko makubwa sana katika maisha yetu. Tulianza kutembelea na kuwasiliana zaidi na Waislamu ili tuweze kuujua Uislamu kwa kina. Hali hii iliendelea kiasi kwamba, Uislamu na Waislamu ikawa misamiati yetu ya kila siku na hata kuwa sehemu ya maisha yetu. Tulivutiwa na dini hii ambayo iliweza kuwaleta pamoja watu ambao pamoja na kuwepo upinzani mkubwa wa madola ya kibeberu walifanikiwa kuanzisha mfumo wa utawala uliofuata misingi ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Kutokana na utafiti wetu tuliweza kufahamu kuwa kumekuwepo na propaganda chafu zenye lengo la kuchafua jina la Uislamu katika vyombo vya habari vya Kimagharibi. Tulifikia natija kuwa kile tulichokuwa tukisikia katika vyombo vya habari kuhusu Uislamu kilikuwa ni tafauti kabisa na ukweli kuhusu dini hii tukufu.

Tunashuhudia msimamo mkali wa Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya Uislamu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu Iran kupitia propaganda zilizojaa sumu sambamba na kuibuliwa chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi. Sababu kuu ya propaganda na chuki hizo ni kuwa wanahofu kuwa ustaarbau wa Kiislamu utanawiri tena na kurejea katika zama za ufanisi na mafanikio makubwa ya Waislamu ambapo walikuwa ndio viongozi na wabeba bendera ya elimu na teknolojia duniani. Hivi sasa katika zama zetu mazingira yapo tayari kwa Uislamu kuweza kustawi na kunawiri. Nchi za Kiislamu zina utajiri mkubwa wa kimaumbile, jamii za Kiislamu zina vijana werevu, wataalamu na wenye uwezo katika nyanja mbali mbali. Uislamu ni dini iliyojaa thamani tajiri na mafundisho bora zaidi ambayo yakitekelezwa ipasavyo yanaweza kuleta maisha bora kote duniani.  Ni katika hali kama hii ndio Mapinduzi ya Kiislamu yakawa na taathira kubwa katika kuibua mwamko wa Waislamu duniani. Hivi leo tunaona namna Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyo na nguvu na uwezo katika masuala muhimu duniani. Iran ina azma imara ya kupambana na madola makubwa ya kibebeberu na msimamo huu imara umeweza kuigwa na mataifa mengine duniani," anasema Mjerumani aliyesilimu Bi. Dora na kuongeza kuwa: "Kutambua njama dhidi ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kufahamu ipasavyo mafundisho ya Kiislamu ni nukta mbili ambazo zilipelekea tusilimu. Mabadiliko haya makubwa yalienea katika kila sehemu ya maisha yetu kiasi cha kutambua kuwa tuna majukumu si tu katika maisha yetu binafsi bali pia katika jamii nzima."

Katika kauli yake ya mwisho Mjerumani aliyesilimu Bi. Dora anasema: "Baada ya kusilimu nilichagua jina la 'Halima' na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na kuwa amewapa watu wa Iran zawadi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuniongoza mimi kupitia mapinduzi hayo."

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …