Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 25 Mei 2014 20:38

Uislamu Chaguo Langu (81)

Uislamu Chaguo Langu (81)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huwaangazia watu ambao baada ya utafiti wa kina na wa muda mrefu huamua kufuata njia iliyojaa nuru maishani yaani Uislamu. Augustine Julius ambaye sasa anajulikana kwa jina la Khalil alizaliwa nchini Argentina katika familia ya Kikristo. Baba yake ni wakili naye binafsi amehitimu katika taaluma ya sanaa ya uchoraji. Alipata bahati ya kuujua Uislamu miaka kadhaa iliyopita na baada ya kusilimu aliamua kufuata madhehebu ya Kishia. Khalil Julius hivi sasa anaendeleza masomo katika taaluma ya Maarifa ya Kiislamu ili akihitimu aweze kuendeleza shughuli zake za sanaa kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu. Ni matumaini yangu kuwa utakuwa nasi hadi mwisho wa makala hii upate kusikiliza tuliyokuandalia kuhusu Muargentina huyu aliyesilimu.

@@@

Uislamu unataka kuwepo na dunia takasifu ambayo itawaleta pamoja watu wa kaumu na mataifa yote chini ya kivuli cha Uislamu. Kwa mtazamo wa Uislamu hakuna kaumu au kundi lolote la watu lililo bora zaidi kuliko jingine. Tokea mwanzo wake, kivutio muhimu zaidi katika Uislamu kilikuwa ni mafundisho yake ya kimaadili, kimalezi na kimaanawi. Mhimili mkuu wa mvuto huu ni Qur'ani Tukufu ambayo kutokana na fikra zake zenye mafundisho yenye thamani za juu na yenye nguvu inawaongoza wanaadamu kuelekea katika saada. Kwa hakika kuna nguvu zilizofichika katika batini ya Uislamu ambazo zimepelekea kuenea dini hii tukufu. Uislamu unawapa wanaadamu uhuru na haki ya kutafakari na hivyo kuwawezesha kufika katika upeo a mbali. Daima Uislamu unamhimiza mwanaadamu atafakari na ajitahidi kuvumbua uhakika. Khalil Augustine naye pia ni kati ya wale ambao wametumia fikra za kina na utafiti ili kufikia uamuzi wa kuchagua na kufuata dini. Anaelezea zaidi kuhusu namna alivyoukumbatia Uislamu kwa kusema: "Sababu kuu iliyopelekea nisilimu ni uchunguzi na utafiti wa kina nilioufanya. Pamoja na kuwa nilikuwa Mkristo lakini kamwe sikuwahi kurihdhika na hali hiyo. Kwa msingi huo nilianza kufanya utafiti kuhusu utamaduni na dini nyinginezo. Ni kwa sababu hii ndio nilianza utafiti kuhusu dini ili kuongeza maarifa yangu. Nilikuwa nikiifahamu misingi ya Ukristo lakini ilikuwa vigumu kwangu mimi kuikubali. Hivyo nilielekea katika Ubudha. Nilisoma vitabu vingi kuhusu itikadi hii na hatimaye nikawa mfuasi wa Ubudhha kwa muda wa miaka mitano ambapo niliacha kula nyama na badala yake nilikuwa mlaji mimea tu. Lakini hatua kwa hatua nilianza kuhisi dini hii haina misingi imara na sikuweza kupata majibu ya kuridhisha kwa maswali yangu mengi. Nilikuwa nakihangaika huku na kule hadi pale nilipokutana na rafiki yangu wa zamani. Nilikuwa nikimfahamu vizuri lakini nilishangaa kuona namna tabia na shakhsia yake ilivyobadilika. Alinifahamisha kwamba alikuwa ameshabadili dini yake na kuwa Mwislamu. Hapo alinifahamisha zaidi kuhusu Uislamu, dini ambayo ilikuwa imembadilisha na kuwa mtu mwenye sifa bora za kimaadili."

Augustine alihisi sauti ya ndani ya nafsi yake ikiwa inamuita kuelekea katika njia halisi ya Mwenyezi Mungu. Augustine naye aliitikia sauti hiyo na kuelekea ilikokua ikitokea. Hapo alianza kuhisi cheche za kuongezeka mapenzi ya kutaka kumjua Mwenyezi Mungu na hivyo kuelekea katika uhakika. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Niliamua kufanya utafiti kuhusu sababu iliyopelekea rafiki yangu ashuhudie mabadiliko makubwa katika maisha yake. Kila wakati tulipokutana, tulifanya mjadala na mazungumzo naye kuhusu Uislamu. Mikutano yangu naye ilizidi kuongezeka na hivyo mahusiano yetu yakaimarika zaidi. Kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu niliweza kuujua zaidi Uislamu pamoja na mafundisho yake. Aliweza kujibu maswali mengi niliyokuwa nayo."

@@@

Wapenzi wasikilizaji, familia katika Uislamu ina nafasi ya juu sana na watoto ambao wanaishi na wazazi wao kwa njia sahihi huwa mbali na ufisadi na madhambi. Nukta hii ya familia huwa sababu ya watu wengi wasiokuwa Waislamu kuvutiwa na Uislamu na mafundisho yake. Uchunguzi umebaini kuwa idadi kubwa ya watu wanaosilimu katika nchi za Magharibi huwa ni  wasomi katika jamii. Ukweli ni kuwa kutokana na kuenea ufisadi, utovu wa maadili na kuharibika jamii katika dunia ya leo, wanaadamu wameanza kutafakari kuhusu namna ya kurekebisha maadili.  Mwanaadamu kwa dhati yake huwa anataka maadili mema na kuimarisha upeo wa uwezo na mafanikio yake. Idadi kubwa ya watu wenye kutafakari wamefikia natija hii kuwa, Uislamu ndio njia muafaka maishani yenye kukidhi mahitaji ya mwanaadamu na kumuelekeza katika saada. Baada ya kusilimu Khalil Julius anasema: "Familia yangu iliingiwa na hofu kubwa baada ya kusilimu kwangu na waliingiwa na wasi wasi sana. Kutokana na propaganda shadidi za vyombo vya habari vya Marekani na Kizayuni dhidi ya Uislamu, waliutazama Uislamu kama dini ya vita na ghasia. Lakini kutokana na tabia yangu kama Mwislamu waliweza kufahamu na kudiriki kuwa Uislamu si dini mbaya na hivyo hawakuwa na wasi wasi tena. Hivi sasa si tu kuwa familia yangu haina wasi wasi bali hata wanajifakharisha kutokana na kuwa mimi ni Mwislamu. Jambo hilo limepelekea nipate furaha kubwa sana."

Khalil Julius anasema tokea utotoni alivutiwa sana na sanaa na ndio sababu aliendeleza masomo ya juu katika uga huu. Hivi sasa baada ya kuwa amesilimu anajitahidi kueneza Uislamu kupitia taaluma ya sanaa. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Sanaa ina uhusiano na dhati ya mwanaadamu. Watu wengi hadi sasa hawaufahamu vizuri Uislamu. Kwa hivyo kwanza tunapaswa kuwaonyesha wanaadamu umaanawi na haki ya Uislamu kwa njia inayofahamika. Kwa mtazamo wangu sanaa ni moja ya njia bora zaidi za kuuhubiri Uislamu. Kwa mfano filamu inaweza kuwa na taathira kubwa sana katika kueneza Uislamu. Kwa hakika kueneza mafuhumu ya kidini kupitia sanaa ni mbinu inayoweza kupelekea kupatikana matokeo mazuri kwani hudumu na kubakia katika nyoyo za watu kwa muda mrefu. Aidha kuhusu utamaduni wa tukio la Karbala na kuuawa shahidi Imam Hussein AS na wafuasi wake watiifu katika siku ya Ashura, kutumika mbinu za sanaa hupelekea kupatikana taathira kubwa kuhusu tukio hilo kwani sanaa ni lugha ya kimataifa. Tukitegemea hotuba na mihadhara tuu yamkini ujumbe usiweze kufikisha kikamilifu utamaduni wa Ashura. Mimi ninajitahidi kutumia sanaa kuuarifisha Uislamu halisi kwa walimwengu." Raia huyo wa Argentina aliyesilimu anaendelea kusema: "Lugha ya wasanii kote duniani ni moja na haina tafauti, iwe ni Iran, Argentina au nchi nyingine yoyote ile. Wataalamu wa sanaa hutumia lugha ya moyo wa mwanaadamu kuibua hisia na hivyo kuleta uhusiano baina ya wanaadamu. Malenga, wachoraji, wanamuziki, watengeneza filamu n.k wanaweza kuwa na nafasi muhimu sana katika kueneza mafundisho na utamaduni wa Kiislamu. Mimi binafsi ninajitahidi kuhakikisha kuwa ninatumia uchoraji kueneza ufahamu wa ustaarabu wa Kiislamu kama vile utamaduni wa Ashura au visa vingine vya maisha na shahada ya Maimamu maasumu kwa watu kote duniani. Ninajitahidi kutumia sanaa kuwaelimisha watu wa Amerika Kusinikuhusu Uislamu na nina yakini kuwa taathira ya sanaa inaweza kuwa ya kina zaidi."

Wapenzi wasikilizaji, imani ina nafasi muhimu katika maisha ya mwanaadamu. Wanaadamu wanaoingia katika uga wa imani halisi ya Mwenyezi Mungu hushuhudia tafauti kubwa na siku za nyuma. Imani humbadilisha mwanaadamu kutoka ndani na kuujenga upya moyo wake. Tunaweza kusema kuwa kumwamini Mwenyezi Munguni ni nukta muhimu katika maisha ya mwanaadamu. Abu Mohammad Ghazali mwanafikra maarufu Mwislamu anaamini kuwa kutathmini mabadiliko ya mwanaadamu kifikra si jambo rahisi. Kwa hivyo inakuwa vigumu kubainisha kikamilifu msisimuko na nishati anayopata mwanaadamu ambaye ameweza kudiriki ukweli. Pamoja na hayo idadi kubwa ya watu waliosilimu huweza kuidiriki hali hii. Wengi wao wanasema huweza kuukubali Uislamu kutokana na nuru ambayo Mwenyezi Mungu huwa ameiangaza katika nyoyo zao na hivyo kukidhi kiu yao katika chemi chemi ya haki.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …