Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 11 Mei 2014 20:44

Uislamu Chaguo Langu (80)

Uislamu Chaguo Langu (80)

Hamjambo Wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika kipindi hiki ambacho huwaangazia watu ambao baada ya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru maishani yaani Uislamu. Ni matumaini yangu kuwa utakuwa nasi hadi mwisho kusukiliza tuliyokuandalia.

@@@

Kwa dhati yake ya maumbile, mwanaadamu huwa anapenda vitu vya kuvutia. Kwa mfano kila mmoja hufurahia kutazama mandhari nzuri na ya kuvutia ya maji safi katika ziwa. Kila mmoja hupenda kutazama bustani iliyojaa maua ya kuvutia au mchoro maridadi. Baadhi ya wakati hisia ya kuvutia na vitu maridadi huwa ni ya juu sana kiasi cha kuwa chimbuko la athari ya sanaa. Qur'ani Tukufu inatoa wito kwa mwanaadamu atafakari wakati wa kuanglia mazingira ya maumbile. Hii ni kwa sababu kupitia maajabu ya maumbile mwanaadamu huweza kutambua mambo mengi ya kiakili. Katika Aya ya 190 ya Sura Aal Imran tunasoma kama ifuatavyo:  Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kuhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili,...

Kwa hivyo kutafakari kuhusu maumbile ni jambo ambalo linaweza kuhuisha na kuleta mabadiliko katika fikra za mwanaadamu.

Katika ustaarabu wa zama zetu, ingawa kidhahiri mwanaadamu anaonekana kuwa katika harakati mpya lakini maisha ya kimashine yamemfanya ajisahau na kughafilika.

Katika maisha ya kujikariri katika dunia ya leo, watu wamekuwa ni wenye kurudiarudia ada na hivyo kusahau uhakika wa juu na wadhifa wao wa kuwa makhalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi. Leo tunashuhudia taathira mbaya za kutozingatiwa misingi ya jamii iliyostaarabika.

Ulf Karlsson, ni Msweden aliyesilimu. Kabla ya hapo alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu wala kufuata dini yoyote lakini wakati huo huo alikuwa akitafuta uhakika. Maajabu ya maumbile ni jambo ambalo lilikuwa likimfanya atafakari sana. Karlsson anaendelea kusema: "Sikua namwamini Mwenyezi Mungu na nilikuwa nikipuuza masuala yote ya kidini. Moja ya vitu vinavyonivutia ni upiga picha. Kwa msingi huo mimi hutilia maanani sana mazingira ya maumbile na umaridadi wake.  Siku moja nilikuwa katika msitu nikipiga picha na nikaanza kutafakari na kuhisi kuwa mimi nimeumbwa na nguvu kubwa na adhimu na kwamba mimi ni sehemu ndogo tu ya maumbile. Nilikuwa na uhakika kuwa umaridadi wote huu uliojaa maajabu hauwezekani kuwepo pasina kuwa na muumba wake. Fikra hii ilipelekea nianze kumtafuta Mungu wangu ili niweze kudiriki ukweli wa maumbile."

Ingawa Karlsson hakuwa mtu mwenye kufungamana na dini lakini kutokana na kuwa familia yake ilikuwa ya Kikristo alikuwa anaufahamu kwa kiasi fulani. Pamoja na hayo hakuweza kupata majibu ya baadhi ya maswali yake katika Ukristo. Kwa msingi huo alianza kujitahidi kuzijua dini zingine. Anaendelea kusema: "Sikumbuki ni muda gani nilikuwa nikijishughulisha kufanya utafiti kuhusu dini lakini kile kilichonibainikia ni kuwa Ukristo haukuweza kukidhi mahitaji yangu. Sikuweza kuamini kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa na washirika wengi na pia sikukubali kumuabudu mtu ambaye alitakiwa kuwa nusu Mungu na nusu mwanaadamu. Kwangu mimi itikadi kama hii ilikuwa ni itikadi isiyokubalika. Nilianza kufanya utafiti na hapo niliweza kuzijua dini mbali mbali. Lakini dini nilizozichunguza si tu kuwa hazikujibu maswali yangu bali maswali mengi zaidi yaliibuka akilini. Hali hii iliendelea hadi wakati ambao kwa kutumia internet niliweza kupata rafiki Mwislamu ambaye alinifahamisa kuhusu imani na itikadi yake imara. Yakini yake kuhusu Uislamu ni jambo lilinonivutia sana. Imani yake imara kuhusu Uislamu ilinivutia kufanya utafiti zaidi kuhusu Uislamu."

Kwa mtazamo wa Qur'ani dunia ni tawi tu la maumbile na hivyo inatoa mwito kwa mwanadamu afanya taamali na aitazame dunia kwa mtazamo wa kufanya utafiti. Leo tunashuhudia namna Qur'ani Tukufu, kitabu cha mwisho kutoka mbinguni' kilivyo na maudhui ambazo ndio kwanza zimeanza kuvumbuliwa na Wanasayansi. Kwa msingi huo kila ambaye anafanya utafiti kuhusu Qur'ani Tukufu atapata majibu ya maswali yake mengi. Karlsson aliweza kuujua Uislamu na hivyo baada ya hapo akaamua na kuendeleza utafiti wake kwa kuisoma Qur'ani. Anafanua zaidi kwa kusema: "Nilivutiwa kila siku katika utafiti wangu kuhusu Qur'ani na tafsiri ya aya zake. Nilihisi kwamba maswali yangu mengi yalikuwa na majibu katika Qur'ani. Kwa msingi huo Uislamu ilinivutia zaidi.  Qur'ani ina dalili na mantiki katika aya zake, uhakika wa kivitendo pia unadhihirika katika aya zake tukufu. Hizo ni baadhi ya nukta ambazo zilinipelekea niamini kuwa kitabu hiki si maneneo ya mwanaadamu bali ni ya Mola Muumba. Kwa msingi huo niliamini kikamilifu kuwepo Mwenyezi Mungu na pia niliamini kuwa Mohammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Wakati nilipopata yakini kuhusu hayo mawili, niliukumbatia Uislamu maishani."

Wakati Ulf Karlsson alipoamua kuwa Mwislamu, alikuwa na wasiwasi kuhusu masaibu ambayo angekumbana nayo katika maisha yake mapya. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Wakati nilipoamua kusilimu niliingiwa na hofu.  Nilikuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wangu. Nilikuwa nikiishi katika jamii ambayo Waislamu walikuwa wachache sana na hata katika baadhi ya maeneo hapakuwa na Waislamu. Katika eneo langu ilinibidi niende kwa muda wa saa moja ili kufika katika mtaa wenye Waislamu. Hivyo singeweza kuwapata Waislamu kila nilipowahitajia. Pamoja na hayo, mvuto wa itikadi ya Kiislamu na mafundisho yake matukufu ni mambo ambayo yalinipelekea nisahau hofu hiyo na kuamua kusonga mbele. Nilitawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na hivyo hatimaye nikasilimu. Mwenyezi Mungu alinisahilishia na kunisaidia katika kukabiliana na masaibu yaliyonikumba".

Kufikia utulivu wa kweli ndio takwa la daima la wanaadamu kiasi kwamba katika kipindi chote cha historia wanaadamu wamestahamili masaibu mengi ili kufikia uhakika. Wengine hufanikiwa na wengine hushindwa kupata utulivu. Kutokana na kuwa Uislamu ndio dini ya mwisho na kamili zaidi, dini hii ndio chimbuko asili la utulivu na kila anayesilimu hupata utulivu wa daima. Bw. Ulf Karlsson naye pia baada ya kuujua na kuukumbatia Uislamu anasema aliweza kupata utulivu na furaha zaidi kuliko huko nyuma: "Hivi sasa nahisi kuwa ni mwenye furaha zaidi, sina mfadhaiko wa nafsi na vishawishi vibaya kama siku za nyuma. Kutokana na uamuzi wa kusilimu na msaada wa Mwenyezi Mungu nimeweza kufikia utulivu. Marafiki zangu wananiambia kuwa nimetulia sana na maisha yangu yamekuwa mazuri zaidi kuliko siku zilizopita." Msweden huyu aliyesilimu anamaliza kwa kusema: "Hatimaye Uislamu ulipelekea niweze kustawi katika sekta zote za maisha. Hivi sasa nimepata utulivu na naweza kusema hii ndio kati ya tafauti kubwa zaidi kabla na baada ya kusilimu.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …