Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 11 Mei 2014 20:42

Uislamu Chaguo Langu (79)

Uislamu Chaguo Langu (79)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru maishani yaani Uislamu. Ni matumaini yangu kuwa utaweza kunufaika na niliyokuandalia.

@@@

Idadi kubwa ya wasomi wa nchi za Magharibi wanaosilimu baada ya kufanya utafiti kuhusu Uislamu ni nukta yenye kuzingatiwa. Kwa muda wa karne kadhaa sasa kumekuwepo juhudi za makusudi zenye lengo la kuhakikisha kuwa Uislamu hauenei katika nchi za Magharibi na njama hizo zimeshika kasi katika karne mbili zilizopota ambapo tumeshuhudia hujuma za pande zote na za wazi dhidi ya Uislamu na Waislamu. Njama hizo zimejumuisha hujuma za kijeshi, ukoloni, uporaji wa mali asili, hujuma dhidi ya itikadi, utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu sambamba na kuendelezwa chuki dhidi ya Uislamu.

Hivi sasa Uislamu ndio dini ya pili kwa ukubwa barani Ulaya.  Dini hii inawavutia sana wasomi na wanafikra wa nchi za Magharibi ambao wanaukumbatia Uislamu baada ya kufanya utafiti na uchunguzi pasina kupendelea upande wowote. Pamoja na kuwa vyombo vya kipropanganda katika nchi za Magharibi vinaichafua sura ya Uislamu na kuinasibisha dini hii tukufu na ugaidi lakini tunaona namna wasomi wenye kuzingatia mantiki wanavyoyakubali mafundisho ya Uislamu kutokana na kuwa wanapata utulivu halisi wa kiroho na kujaza pengo la umaanawi maishani kwa kuukumbatia Uislamu. Ukweli ni kuwa Uislamu unaenea katika nchi za Magharibi pamoja na kuwa taasisi za utafiti zinazofungamana na serikali za Ulaya na Marekani zinajaribu kuwazuia wasomi kuelekea katika Uislamu. Lakini kutokana na kuwa wananadharia wa serikali za nchi za Magharibi wana ufahamu potofu kuhusu dini na utamaduni wa Kiislamu, wameshindwa kukabilianana wimbi la kuenea Uislamu katika nchi hizo. Baadhi ya wanasaikolojia na wataalamu wa jamii katika nchi za Magharibi wanaamini kuwa mtikisiko wa kiuchumi, kuporomoka  misingi ya familia na hatimaye kuenea ufisadi wa kimaadili ni mambo ambayo yamepelekea watu wengi kuhisi kutokuwa na usalama na utulivu. Kwa msingi huo wanasema hizo ni baadhi ya nukta ambazo zimepelekea Wamagharibi wengi kutafuta ukweli na hivyo kukimbilia Uislamu na kupata humo hifadhi ya kimaanawi pamoja na utulivu.

Bw.Ayyub Axel Köhler Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Ujerumani anasema sababu ya watu wengi kusilimu nchini humo ni mvuto uliopo katika mafundisho ya Kiislamu.  Aidha anaongeza kwa kusema: 'Waislamu nchini Ujerumani wamekuwa na taathira nzuri katika jamii kutokana na harakati zao zenye kuleta mshikamano na umoja baina yao kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kuwa na uhusiano mzuri na kuishi kwa maelewano na wasiokuwa Waislamu. Hali kadhalika Waislamu Ujerumani wamekuwa katika mstari wa mbele wa kupambana na ubaguzi wa rangi na hilo nalo limekuwa na taathira nzuri." Kiongozi huyo wa Waislamu Ujerumani anaongeza kuwa, 'Mafundisho ya Uislamu yana nukta nyingi zinazowavutia Wajerumani na kwamba wengi wanaosilimu nchini humo ni wanawake walio na elimu ya juu, watafiti au wasomi  katika vituo vya kielimu na kiutamaduni.'

@@@

Katika makala yetu ya leo tutamuangazia kwa kifupi mwanamke Mjerumani aliyesilimu Bi. Catherine Hoofer kutoka mji wa Stuttgart ambaye anabainisha kuhusu maisha yake kwa kifupi kwa kusema: "Nilizaliwa mwaka 1968 katika mji wa Stuttgart nchini Ujerumani. Wazazi wangu ni Wakristo wa Kanisa Katoliki. Tokea utotoni nilifungamana sana na mafundisho ya kidini na kila siku ya Jumapili nilielekea kanisani. Lakini nilipofika umri wa miaka 14 nilihisi kutokuwa na raghba wala hamu ya kuendelea kutekeleza mafundisho ya Kikristo. Aidha yale niliyoyasoma kwa jina la 'mafundisho ya Ukristo' yalikuwa kinyume kabisa na yale yaliyokuwa yakishuhudiwa katika maisha ya kawaida na ilikuwa vigumu kwangu mimi kuikubali hali hiyo. Baada ya kupoteza hamu kuhusu masuala ya kidini siku moja nilienda kwa mtabiri wa mambo lakini hakuweza kukidhi mahitaji yangu ya kiroho. Baada ya kupita miaka kadhaa nilijuana na Mwislamu mmoja. Fikra zake pamoja na mtindo wake wa maisha ni mambo ambayo yalinifanya niweze kuvutiwa na Uislamu. Nilianza kufanya juhudi za kuujua zaidi Uislamu."

Alipojifunza kuhusu masuala ya kimsingi katika Uislamu, Bi. Hoofer alivutiwa zaidi na dini hii tukufu na hivyo akaamua kufanya utafiti zaidi kuhusu sala na vile vile vazi la Hijabu katika Uislamu. Baada ya utafiti na uchunguzi wake wa kina, akiwa na ufahamu kamili, Bi. Hoofer aliamua kusilimu na hivyo kufuata dini hii tukufu ambayo ni mfumo kamili wa maisha. Mjerumani huyu aliyesilimu anafafanua zaidi kwa kusema: "Wakati nilipoanza kuvaa hijabu, nilihisi kuwa katika hali ya usalama zaidi. Kwa hakika Hijabu ilinipatia itibari katika shakhsia yangu. Hata hivyo mama yangu hakufurahia aliponiona nimevaa Hijabu na alipinga uamuzi wangu huo. Kutokana na kuwa nilikuwa nikimpenda sana mama yangu, niliamua kuweka kando vazi la Hijabu kwa muda lakini niliendelea kuwa Mwislamu. Lakini dhati ya nafsi yangu haikurudhia hali hiyo na naweza kusema nilikumbana na vita ndani ya nafsi yangu.  Baada ya takribani mwaka mmoja nilikutana na wanawake wawili Wajerumani waliosilimu na ambao walikuwa wamevaa vazi la Hijabu. Nilistaajabu sana kutokana na ujasiri wao wa kuvaa Hijabu pamoja na kuwepo matatizo mengi. Ndani ya moyo wangu niliwapongeza kwa kuwa na ujasiri huo. Kwa msingi huo nilipata motisha wa kuanza tena kuvaa Hijabu ya Kiislamu. Nilimuomba Allah SWT anipe msaada na niweze kumtegemea ili niweze kuvaa Hijabu kamili. Kumkumbuka na kumtegemea Mwenyezi Mungu ni jambo ambalo lilinipa uwezo mkubwa wa kujiamini kinafsi. Wakati mama yangu alipofahamu kuwa nimechukua uamuzi imara na kwamba singerudi nyuma, hakuwa na budi ila kukubali hali ya mambo na hivyo akaacha kunipinga."

@@@

Mafundisho ya Uislamu yamepangika kwa msingi wa kuuganisha dunia na akhera na kumtaka mwanaadamu awe na maisha ya wastani au kati kwa kati.  Mafundisho haya hayapuuzi dunia na wala hayatoi dunia muhanga kwa ajili ya kesho akhera. Katika mantiki ya Uislamu, dunia ni uwanja na fursa ya kufikia ukweli na saada. Ni kwa sababu hii ndio katika hadithi na riwaya za Kiislamu dunia imetajwa kama shamba la akhera. Mantiki hii inaashiria kuwa, pembizoni mwa mahitaji ya kimaanawi, masuala ya kimaisha au kimaada ya mwanaadamu pia yazingatiwe. Ni kwa sababu hii ndio maana wale wanaofahamu vyema Uislamu, hupata mpango wote wa mahitaji yao katika dini hii tukufu na hivyo kutohisi upungufu wowote.  Mjerumani aliyesilimu, Bi. Hoofer anafafanua hisia yake baada ya kusilimu kwa kusema: "Nilipoukumbatia Uislamu maishani nilipata utulivu zaidi kwa sababu nilimtegemea Mola Muumba wa dunia. Maisha yangu yalipata muelekeo na lengo maalumu. Niliweza kupata ukamilifu zaidi katika imani na ufahamu wangu kuhusu Mola Muumba. Ufahamu wangu kuhusu Uislamu ni jambo ambalo limeyafanya maisha yangu yawe na maana ya kina. Sasa najua ni kwa sababu gani naishi na siko tena kama wale waishio bila lengo wakiwa wameghiriki katika maisha ya anasa za kidunia. Nasikitika kusema kuwa dini ina nafasi ndogo sana katika maisha ya kijamii ya watu wa nchi za Magharibi.  Kwa hakika dini imepoteza maana yake katika jamii za Kimagharibi hasa Marekani.  Waislamu wanatafautiana sana na wasiokuwa Waislamu katika nchi za Magharibi. Hii ni kwa sababu katika Aya ya 10 ya Surat Hujurat Mwenyezi Mungu SWT anasema "Hakika Waumini ni Ndugu," akimaanisha kuwa Waislamu waumini wana uhusiano wa karibu baina yao, wanasaidiana na kutatua matatizo ya marafiki na majirani wao.

Bi. Hoofer ana haya ya kusema kuhusu namna ya kuuhubiri Uislamu na hali ya Waislamu duniani: "Iwapo vitabu kuhusu Uislamu vitawafikia wote, basi wataweza kuitambua haki kwa kuvisoma. Lakini hapa nasisitiza kuwa, njia nyingine muafaka ya kuuhubiri Uislamu ni kupitia vitendo. Kila mtu huzingatia zaidi vitendo kuliko maneno. Kwa  hivyo iwapo Waislamu watatekeleza kivitendo mafundisho yote ya Kiislamu, wataweza kuwa na taathira nzuri kwa wasiokuwa Waislamu duniani. La kusikitisha ni kuwa Waislamu leo wanakabiliwa na matatizo mengi kutokana na kuwa madola ya Magharibi yanafahamu kuwa iwapo Uislamu utastawi watu wengi duniani watavutiwa na dini hii  tukufu. Kwa msingi huu Wamagharibi wanatumia kila njama na hila kuzuia kuenea na kustawi Uislamu. Lakini pamoja na hayo, mimi naamini kuwa iwapo Waislamu watasaidiana na kuwa na umoja na mshikamano, basi wataweza kukabiliana na maadui," anasema Mjerumani aliyesilimu Bi.  Hoofer.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …