Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 25 Juni 2015 13:10

Katika Msafara wa Ramadhani (1)

Katika Msafara wa Ramadhani (1)

Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia katika maisha ya wanadamu baadhi ya siku, miezi na nyakati zilizojaa baraka na hadhi kubwa. Katika siku na nyakati hizo upepo mwanana kama ule wa alfajiri, hupuliza nafsi na roho ya mwanadamu na kuipa uhai mpya. Katika nyakati hizo roho iliyochoka na kupatwa na kutu ya mghafala ya mwanadamu hujitenga kidogo na anasa za dunia na kuhisi zaidi rehma na neema za Mola Muumba. Ni katika siku kama hizi ndipo mwanadamu anapoweza kupaa na jikurubisha zaidi kwa Muumba.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni miongoni mwa nyakati hizo adhimu na za dhahabu katika maisha ya mwanadamu. Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Mwenyezi Mungu na mwezi wa Qur'ani. Milango ya mbingu na pepo ya Firdaus hufunguliwa katika mwezi huu na milango ya moto wa Jahannamu hufungwa ndani yake. Ibada na dhikri katika mwezi wa Ramadhani huwa na ujira na baraka tele na ndio mwezi wenye usiku ya Lailatul Qadr ambao Mwenyezi Mungu Mannani anasema, ni bora kuliko miezi elfu moja.
Mtume Muhammad (saw) amesema katika hotuba yake kuhusu utukufu wa mwezi huu kwamba: Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Umekujieni mwezi wa Mwenyezi Mungu kwa baraka, rehma na maghufira; mwezi ambao ndio bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Siku zake ndizo siku bora zaidi na usiku zake ndizo bora zaidi na saa zake ndizo saa bora zaidi. Mumealikwa katika ugeni na mahfali ya Mwenyezi Mungu na kuwa miongoni mwa watu wa karama yake katika mwezi huu. Pumzi zenu katika mwezi wa Ramadhani ni tasbihi, usingizi wenu ndani yake ni ibada, amali zenu ni maqbuli na dua zeni ni mustajabu. Hivyo basi muombeni Mwezi Mungu kwa nia safi na nyoyo zilizotwahirika akupeni taufiki ya kufunga siku zake na kusoma Qur'ani ndani yake. Mtu mbaya na muovu ni yule aliyekosa kupata maghufira na msamaha wa Mwenyezi Mungu katika mwezi huu mtukufu. Kumbukeni njaa na kiu ya siku ya Kiyama kutokana na njaa na kiu yenu katika mwezi huu. Toweni sadaka kwa watu fakiri na maskini, waheshimuni wakubwa miongoni mwenu, warehemuni na kuwaonea huruma wadogo zenu na ungeni ndugu na jamaa zenu..." >>
Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kutakasa nafsi na kuiondoa katika kutu la dunia na minyororo ya Shetani. Mwezi huu unaleta bishara njema kwa Waislamu hususan wale wanaoanza kufunga mwaka huu. Marcos ni kijana wa Kifipino ambaye baada ya kusilimu amechagua jina la Ahmad Muumin. Kijana huyu ambaye amekuwa akiusubiri kwa hamu kubwa na isiyo na kifani fursa ya mwezi mtukufu wa kwanza wa Ramadhani katika maisha yake anasimulia hisia zake akisema: Awali nilikuwa nikifanyia maskhara mwezi wa Ramadhani na maana ya funga na swaumu katika Uislamu. Nimeishi kipindi cha miaka kumi nchini Imarati na wakati huo funga ya mwezi wa Ramadhani ya Waislamu ilikuwa janga na kero kubwa sana kwangu. Katika mwezi huo watu wote tulikuwa tukibakia majumbani na maduka yote yalikuwa yakifungwa. Nilikerwa mno na mambo mengi ya mwezi wa Ramadhani na niliamini kuwa, funga na swaumu ni mateso ya kiroho na kimwili kwa mwanadamu.
Mtazamo huo wa Marcos ulibadilika kabisa baada ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu dini ya Uislamu na kutambua maana halisi na falsafa ya swaumu. Baada ya kusilimu Marcos ambaye sasa alikuwa akiitwa Muhammad Muumin, alifunga mwezi wa Ramadhani na anahadithia tajiriba yake akisema: Hadi sasa sijawahi kupata utulivu mkubwa kama huu wa kiroho katika maisha yangu. Sasa naelewa taathira kubwa za kiroho za ibada ya swaumu kwa mwanadamu na mbali na kuwa funga ya Ramadhani si mateso kwa mwili na roho ya mwanadamu kama nilivyokuwa nikiamini, vilevile ni uzima na tiba yenye faida kubwa kwa mwili na nafsi ya kiumbe huyo.
Amina, ni Mwislamu mwingine mpya ambaye mwaka huu alikuwa akiisubiri kwa hamu kubwa funga ya mwezi wa Ramadhani. Amina ambaye awali alikuwa akiitwa Caroline na anaishi Jordan, anasema kufunga swaumu ni somo la kuwa na subira, uvumulivu, kudhibiti nafsi na kupeleka juu masuala ya kiroho na kimaanawi. Caroline au Amina ambaye ni mwenyeji wa Afrika Kusini anasema kuhusu swaumu ya Ramadhani kwamba: Swaumu ni njia nzuri ya kuzidisha utulivu wa kiroho na kinafsi. Katika mwezi wa Ramadhani Waislamu hujizuia kula, kunywa, kuvuta sigara na mengine mengi ya halali katika kipindi cha baina ya kuchomoza jua na kuzama kwake na kujikurubisha zaidi kwa Mola wao Muumba." >
Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa Mwenyezi Mungu na mwezi wa kumkumbuka na kumtaja Yeye. Daima dalili ndogo zaidi ya mahaba na mapenzi ni kumkumbuka kipenzi na mahbubu. Mtu ashiki na aliyetumbukia katika nyonda na penzi hujulikana kutokana na kumtaja mara kwa mara mpenzi na maashuki wake. Mawalii wa Mwenyezi Mungu na wale waliobobea katika maarifa wanakutambua kumtaja na kumkumbuka Allah kuwa ni sharti kuu la kupaa kwa muumini hadi kufikia radhi za Mwenyezi Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, dhikri si kukariri maneno kwa ulimi tu, bali ni kuhudhuria na kuwepo daima mtu ashiki mbele ya mahbubu na kipenzi chake. Dhikri ni kuwa pamoja daima na kipenzi na mja kuwa karibu zaidi na muumba wake.
Magwiji wa irfani na maarifa wanasema, kama ambavyo mwili unahitajia chakula na maji kwa ajili ya kudumisha uhai, vivyo hivyo roho ya mwanadamu inahitaji chakula cha kiroho kwa ajili ya kudumisha uhai wake na kukwea ngazi na daraja za juu zaidi. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anakutaja kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu kuwa ndiyo nishati na nguvu ya roho ya mwanadamu. Mjukuu wake, Imam Zainul Abidin (as) anaomba dua akisema: Ilahi Mola wangu Mlezi! Huisha roho yangu kwa dhikri na kukutaja Wewe, na zima moto na ghamu na maumivu yangu kwa kunomg'ona na Wewe."
Miongoni mwa sifa makhsusi za kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ambazo zimetajwa katika dua za mwezi huu wa Ramadhani ni ladha na utamu wake. Mtume (saw) anasema katika dua inayosomwa katika mwezi huu wa Ramadhani kwamba: Mola wangu Mlezi! Nionjeshe mimi utamu wa kukukumbuka Wewe.." Mtu ambaye hajaonja utamu wa kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu hawezi kuelewa maana halisi ya ibada, na bila shaka hatapata baraka na taathira zake hapa duniani na huko Akhera.
Tunakamilisha makala hii kwa kumuomba Mwenyezi Mungu atughufirie madhambi yetu na kusamehe makosa yetu. Mola wetu Karimu! Takabali toba zetu na ujibu dua na maombi yetu. Tulinde na maasi katika mwezi huu na baada yake, na utukurubishe zaidi kwako, hakika Wewe ndiye dunia, pepo na akhera yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)