Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 20 Julai 2014 14:32

Msimu wa Mavuno ( 7) {Kuwa na Subira}

Msimu wa Mavuno ( 7)  {Kuwa na Subira}

Assalaam Alaykum wasikilizaji wapenzi. Ni wakati mwingine tena wa kuwa nanyi katika kipindi hiki maalumu cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ni matumaini yetu kuwa mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ambacho leo hii kitazungumzia taathira za kufanya subira, karibuni.
Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS mmoja kati ya Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad SAW anasema: 'Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wenye adhama kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na ni sikukuu ya marafiki na waja Wake maalumu'. Kwenye mwezi huu mtukufu, mja hupata taufiki ya kutekeleza ibada ikiwemo funga ambayo ni hidaya na zawadi kubwa kutoka kwa Allah SW aliyomtunuku mja Wake. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe nguvu na taufiki ya kusimama imara ili tuweze kujikusanyia umaanawi ulioko kwenye mwezi huu.

*****

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa subira na kusimama imara mkabala wa kiu na njaa, kusimama imara mkabala wa dhambi, subira mkabala wa machungu na matatizo, bila shaka hayo yote yamo katika saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa kawaida, maisha ya kidunia huwa yamechanganyika na matatizo na mushkeli mbalimbali ambayo kama mwanadamu atakuwa na subira na kusimama kidete katika kukabiliana nayo, bila shaka atafanikiwa na kupata ushindi, lakini kama hatofanya subira na badala yake kuamua kusalimu amri mbele ya masaibu na matukio mbalimbali, kamwe hatoweza kufika kwenye malengo uliyoyakusudia.
Bila shaka msikilizaji mpenzi unaelewa kwamba kahawa ni chungu, na uchungu wake hauondoki kwa sukari lakini unaweza kuustahamili. Kahawa inapochanganywa na sukari, huwa ni ya kuvutia na hivyo uchungu wake kuvumilika na kutoa ladhaa maalumu kwa anayeitumia. Matatizo pia ni machungu, na kamwe hayawi matamu. Lakini unaweza kuyastahamili kwa kufanya amali fulani. Subira ndiyo inayokuwezesha kuyastahamili matatizo hayo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Surat Asr kwamba: "Naapa kwa Zama! Hakika mtu bila ya shaka yumo katika hasara. Ila wale walioamini, na wakatenda mema, Na wakausiana haki, na wakausiana kusubiri". Subira ni mfano wa alkemia, yaani mwanadamu huwa mfano wa dhahabu kwa thamani iwapo atasimama kidete na kupambana vilivyo na matatizo. Jambo hilo humpa nguvu na thamani kubwa, na hasa iwapo subira hiyo mbele ya matatizo itaandamana na sala, yaani kuwepo mawasiliano na Mwenyezi Mungu SW. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 45 ya Surat al Baqarah: "Na takeni msaada kwa kusubiri na kwa kusali". Mitume wa Mwenyezi Mungu walishuhudia mateso na usumbufu mkubwa kutoka kwa wapinzani na washirikina; kwani walikuwa wakiwaita wateule hao wa Allah kuwa ni wachawi na waongo na kuwakadhibisha, lakini Mitume hao wa Allah walikuwa na subira na kutekeleza kwa ufanisi mkubwa maagizo na ujumbe wa Mwenyezi Mungu.

*****

Siku moja Mtume Muhammad SAW alielekea katika mji wa Taif, karibu na Makka kwa lengo la kuwalingania watu wa mji huo katika dini tukufu ya Kiislamu. Mtume wa Allah alikutana na wazee wa mji huo na kuwaelezea kwa kina masuala yanayohusu dini ya Kiislamu. Lakini wazee wale licha ya kukataa kusikiliza maelezo yake, baadhi yao walianza kuwashawishi watu wamchokoze kwa makusudi Mtume wa Allah. Watu hao waliochochewa walianza kumrushia mawe na kumsababishia majeraha mwilini. Mtume wa Mwenyezi Mungu baada ya kujeruhiwa na uchovu aliokuwa nao wakati ule, alikata shauri kuelekea kwenye shamba lililokuwa jirani. Aliamua kuketi chini ya kivuli cha mti na kumshtakia Mwenyezi Mungu matatizo na masaibu yaliyomkuta. Wakati mwenye shamba alipomuona Mtume katika hali ile, alihuzunishwa mno na kumuamuru mfanyakazi wake mmoja ampelekee kikapu cha zabibu. Mfanyakazi alichukua kikapu cha zabibu na kumpelekea Mtume Mtukufu SAW. Mtume alimshukuru yule bwana kutokana na ukarimu wake. Mtume wa Allah alichukua kishada au kishuke cha zabibu na kabla ya kuanza kula alisema: 'Bismillahir Rahmanir Rahiim'. Yule mfanyakazi wa shambani alishangazwa pindi aliposikia maneno hayo na kusema: 'Umesema nini?' Maneno uliyoyasema ndiyo mara ya kwanza kuyasikia!' Mtume Muhammad SAW akasema: 'Nimelitaja jina la Mwenyezi Mungu.' Kisha Mtume SAW alimuuliza yule mfanyakazi: 'Wewe ni mwenyeji wa wapi?' Mfanyakazi alijibu: 'Mimi ni mwenyeji wa Neinawah (Iraq)'. Mtume SAW alitabasabu na kusema: 'Mji wa Yunus, mja wa Mwenyezi Mungu aliyetakasika!' Mfanyakazi akasema: 'Kwani wewe unamjua Nabii Yunus?' Mtume Muhammad SAW aliangalia juu na kwa upole kabisa akasema: 'Naam, nami pia ni mithili ya Nabii Yunus, ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Allah SW ametuhabarisha juu ya shakhsia huyo mtukufu.' Kijana yule aliibusu mikono ya Mtume Mtukufu na kusema: 'Mimi ninakuamini wewe na Mungu wako'. Mtume Mtukufu SAW aliingiwa na furaha mno kutokana na maneno ya kijana yule, aliyekuwa akifanya kazi shambani. Wakati Mtume SAW alipokuwa akirejea Makka, alisahau kabisa kama alikuwa amepata maumivu na majeraha mkononi na mguuni mwake. Kwani alifanikiwa kumpata mtu mmoja aliyemlingania kwenye dini ya haki kutokana na moyo wake wa subira na kustahamili machungu yaliyomkuta. Tunaweza kusema kuwa, moja kati ya mambo yaliyochangia kupiga hatua kubwa dini ya Kiislamu na kuwavutia washirikina kwenye dini hiyo tukufu, ni moyo wa subira aliokuwa nao Mtume Mtukufu SAW.

*****

Wapenzi wasikilizaji, Imam Ali bin Hussein Zainul Abidiin AS mmoja kati ya Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume Muhammad SAW alifanikiwa kupata ushindi akiwa katika hali na mazingira magumu mno kwa kutumia mbinu za mahubiri na mapambano kama vile kusoma visomo na dua mbalimbali za kuwaangamiza maadui zake. Miongoni mwa urithi mkubwa wa kiutamaduni wa Imam Zainul Abidiin AS ni dua zilizokusanywa katika kitabu kinachoitwa Swahifatu Sajjadiyya. Mkusanyiko wa dua hizo za kiirfani na zenye thamani, ni mithili ya bahari iliyojaa maarifa ya Kiislamu, kama vile masuala ya kiitikadi, kiutamaduni, kijamii na kisiasa. Uchunguzi wa kina wa dua hizo unathibitisha kuwa, dua hizo hazikuwa dua za kawaida, bali zilibeba ujumbe mzito zaidi. Imam Sajjad AS alitumia dua hizo kubainisha sababu za kuumbwa ulimwengu na mwanadamu humu duniani, masuala ya kiitikadi, akhalaki ya mtu binafsi na ya hadhara, kijamii na kisiasa. Wafuasi wa dini tukufu ya Kiislamu wanaitumia fursa hii ya mwezi mtukufu na katika miezi mingineyo katika kusoma Qurani Tukufu, dua na nyuradi mbalimbali kutoka katika kitabu hicho, wakiwa na matumaini ya kupata maghufira na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na yale waliyoyatenda kwa kujua au kutojua.
Naam, muda wa kipindi chetu cha leo umefikia tamati, tunakuombeni mujiunge nasi katika kipindi chetu cha wiki ijayo panapo majaaliwa yake Allah SW.

Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)