Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 15 Julai 2014 15:20

Msimu wa Mavuno (6) [Kuwatendea Wema Wazazi]

Msimu wa Mavuno (6) [Kuwatendea Wema Wazazi]

Assalaam Alaykum wasikilizaji wapenzi, na karibuni kuwa nasi katika dakika hizi chache za kuwaleteeni mfululizo mwingine wa kipindi maalumu cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni matumaini yetu kuwa tutapata taufiki ya kuwa wageni wenye kustahili katika ugeni huu wa Mwenyezi Mungu SW.
Vipande vya mkaa uliowashwa huwa na uwezo wa kuleta joto na kudumu vinapokuwa pamoja! Na kama havitakuwa pamoja na kutenganishwa, huwaka na kuzimika haraka; yaani kudumu kwake huwa ni kwa muda mfupi tu na joto lake haliwi kali sana. Ulimwengu huu na kila kilichomo hutoa darsa, funzo na mazingatio kwa wanadamu na watu wenye fikra. Imam Mussa al Kadhim AS mmoja kati ya watu wa nyumba tukufu ya Mtume SAW amesema: 'Unaweza kujifunza kutokana na kila kitu'. Tunajifunza kutokana na mfano huu kwamba, vipande vya mkaa vilivyokusanywa pamoja huwa na joto jingi na kudumu kwa muda mrefu kunatokana na kuwa kwake pamoja. Kwa hivyo siri hapa ni hii kwamba umri mrefu hutokana na vitu au watu kuwa pamoja. Hivyo mtu huwa na furaha maishani anapoishi na wenzake, jambo ambalo pia humuongezea riziki. Natija ni hii kwamba, mtu yeyote asiyekuwa na mahusiano mazuri na ndugu pamoja na watu wake wa karibu, umri wake huwa mfupi na kutokuwa na mlingano wa pato na matumizi katika maisha yake. Kwa minajili hiyo, ili tuweze kuongeza riziki zetu, tunapaswa kuwajali na kuwaangalia kwa jicho la huruma na mapenzi wazazi wetu na tuwaonyeshee tabasamu la upendo na kuwaomba watuombee dua kwa Mwenyezi Mungu SW. Mtume Muhammad SAW amesema: 'Dua wanayoiomba wazazi kwa mtoto wao, ni mithili ya dua anayoiomba Mtume kwa ajili ya umma wake'. Hapa tunawaleteeni kisa kifupi cha kijana aliyemuendea Mtume Mtukufu SAW na kumwambia: 'Ewe Mtume wa Allah, kila dhambi utakayoisema nimeifanya, je kuna matumaini yoyote ya kupata msamaha na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Mtume alimuuliza: 'Je, unaye baba na mama'? Kijana akajibu: Sina mama, lakini ninaye baba. Mtume akasema: Muendee baba yako na umhudumie! Kisha kijana aliondoka na kujisemeza moyoni: Laiti ningelikuwa na mama! Kwani ningelipata matokeo yake haraka zaidi.'
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 23 na ya 24 ya surat Israa: 'Na Mola wako amehukumu kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu. Na (ameagiza) kuwafanyia wema (mkubwa) wazazi. Kama mmoja wao akifikia uzee, (naye yuko) pamoja nawe, au wote wawili, basi usiwaambie hata Ah! Wala usiwakemee. Na useme nao kwa msemo wa heshima (kabisa). Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa (njia ya kuwaonea) huruma (kwa kuwaona wamekuwa wazee). Na useme: 'Mola wangu! Warehemu (wazee wangu) kama walivyonilea katika utoto'.
KASIDA
Mpenzi msikilizaji, siku moja Nabii Mussa AS wakati alipokuwa akiomba dua na kunong'ona na Mola wake, alimuomba Allah SW amfahamishe mtu atakayekuwa pamoja naye huko Peponi. Mwenyezi Mungu alilikubali ombi la Nabii Mussa AS, na kumueleza kwamba jirani yako ni kijana fulani anayekaa mahala fulani. Nabii Mussa AS aliamua kumuendea kijana huyo aliyekuwa muuza nyama na kuanza kuangalia nyendo zake kwa mbali, ili aweze kujua ni amali gani zenye thamani anazozifanya kijana huyo na kufikia daraja hilo la juu huko Peponi. Hata hivyo, Nabii Mussa AS hakuweza kuona nyendo zozote maalumu na zenye mguso kwa kijana yule. Ulipoingia usiku, kijana yule alifunga duka lake na kujiandaa kuelekea nyumbani. Nabii Mussa AS bila ya kujitambulisha aliamua kumuomba kijana yule akubali awe mgeni wake kwa usiku ule. Kijana alilikubali ombi la Nabii Mussa, na kumchukua hadi nyumbani kwake. Mara walipofika nyumbani, kabla ya kufanya jambo lolote lile kijana yule alianza kutayarisha chakula. Nabii Mussa AS alimuona bikizee, aliyepooza mikono na miguu yake akiwa ameketi pembeni. Baada ya kijana yule kumaliza kupika na kuandaa chakula, alimuendea bikizee yule na kuanza kumlisha chakula huku akiwa makini na mwenye subira na furaha kubwa kutokana na kitendo alichokuwa akimtekelezea bikizee yule hadi aliposhiba. Kijana hakuishia hapo, alianza kumsaidia kubadilisha nguo zake, na kisha kumsaidia katika kutekeleza kazi zake nyingine huku akiwa ni mwenye huruma kubwa. Usiku huo, mbali na taklifu zake za kidini, Nabii Mussa AS hakumuona kijana huyo akitekeleza shughuli nyingine za ziada, kama vile kusoma dua wala kusali sala za usiku. Siku ya pili, kabla ya kuondoka nyumbani, kwa mara nyingine tena, Nabii Mussa AS alimuona kijana yule akimuendea bikizee na kumpa chakula, huku akiwa na ari kubwa ya kutekeleza jukumu lake hilo. Wakati wa kuondoka, Nabii Mussa AS alimuuliza yule kijana: 'Yule bikizee alikuwa nani? Mtu ambaye wakati wote ulipokuwa ukimlisha chakula, nilimuona akiuelekeza uso wake mbinguni huku akiwa amefumba macho na kutamka maneno fulani'. Kijana alimjibu Nabii Mussa AS kwa kumwambia: Yule bikizee ni mama yangu, na kila ninapomlisha chakula na kushiba huomba dua akisema 'Ewe Mwenyezi Mungu! Mjaalie mwanangu huyu awe jirani na rafiki wa Mussa bin Imran huko Peponi, kutokana na huduma hizi anazonifanyia'. Wakati Nabii Mussa AS aliposikia maneno hayo alishtuka na kumwambia yule kijana kwamba, Mwenyezi Mungu alikuwa tayari ameitakabali dua aliyokuwa akimwombea mama yake.'
KASIDA
Mpenzi msikilizaji, mwanadamu wakati anapotaka kutekeleza majukumu aliyopewa na Mwenyezi Mungu, kabla ya yote humuomba Mwenyezi Mungu ampe taufiki ya kutekeleza mambo aliyomuamrisha na kuacha yale aliyomkataza. Anaelewa wazi kwamba, ili aweze kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu na daraja ya uchaji Mungu, anapaswa kutekeleza ipaswavyo majukumu yake ya kisheria. Muumini anapaswa kudiriki sababu ya kuwepo saumu na ni kwa nini amefaradhishiwa ibada hiyo muhimu. Imepokelewa kwamba, kila wakati ulipowadia mwezi Mtukufu wa Ramadhani Imam Ali bin Hussein 'Zainul Abidiin' AS alikuwa akimuomba Mwenyezi Mungu ampe maarifa ya kuujua mwezi huu kwa kusema: 'Ewe Mola wangu! Sala na salamu zimfikie Mohammad na Kizazi chake, nijaalie niweze kutambua fadhila za mwezi wa Ramadhani na kulinda heshima yake." Anas bin Malik, sahaba wa Mtume (saw) anasema; "Wakati ulipowadia mwezi wa Ramadhani, Mtume Mtukufu Muhammad SAW alisema: "Subhan'Allah! Tizama unaenda kuukaribisha mwezi upi na utakuletea kitu gani."
Siku moja Mtume SAW aliulizwa: 'Amali bora zaidi katika Mwezi huu ni ipi?' Mtume Mtukufu alijibu kwa kusema: 'Amali bora zaidi ni kujizuia na yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu.' Hii ina maana kuwa mwanaadamu ajizuie kufanya mambo yote yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu.
Naam wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki maalumu umefikia tamati, ni matarajio yetu kuwa mumenufaika vya kutosha.
Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)