Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 12 Julai 2014 11:00

Msimu wa Mavuno (5) [Matumaini ya rehema za Allah]

Msimu wa Mavuno (5) [Matumaini ya rehema za Allah]

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo mwingine wa makala maalumu za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mwezi uliojaa nuru na ukarimu wa Mola Muumba. Tunamuomba Mwenyezi Mungu SWT atutakabalie sote saumu na ibada zetu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Kufika kileleni roho ya umaanawi na ibada katika mwezi huu mtukufu ni jambo ambalo hutuvutia tumuelekee Mwenyezi Mungu na kutubu madhambi yetu. Katika makala ya leo tutaangazia kwa kifupi maudhui ya kuwa na matumaini na rahma za Mwenyezi Mungu SWT katika maisha ya mwanaadamu.

@@@

Mwenyezi Mungu SWT katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani anawahimiza waja wafuate mkondo ambao utawapeleka katika amali njema na zenye kumridisha Yeye. Aghalabu ya waja wema na wacha Mungu wameweza kupitia njia iliyojaa masaibu na hatimaye kufikia lengo la juu la kumridhisha Mwenyezi Mungu. Saumu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani inatupatia darsa ambazo kila moja wazo imejaa maana na umaanawi unaowafikia waja wema wa Mwenyezi Mungu. Saumu humuwezesha mwanaadamu kuimarisha uwezo wake wa kuweka malengo maishani na kumpa imani kuwa ili kufikia malengo bora, hapaswi kuogopa masaibu na matatizo. Kiwango cha kustahamili wenye kufunga ni cha juu sana lakini lengo na makusudio yao ni mazuri sana hasa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu SWT. Hakuna shaka kuwa, katika batini ya kila ugumu au matatizo hatimaye kuna usahali na wepesi. Ili kufikia utulivu unapaswa kustahamili matatizo na kuwa na matumaini. Kwa hakika matumaini yana nafasi muhimu katika kustawi mwanaadamu hasa matumaini kuhusu msaada wa Mwenyezi Mungu. Kila ugumu hatimaye humpelekea mwanaadamu kupata wepesi. Katika Qur'ani Tukufu Surat Al Inshirah Aya za 5 na 6 Mwenyezi Mungu SWT anasema: Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi, Hakika pamoja na uzito upo wepesi.
Katika hali ya kawaida wakati wa kiangazi ardhi huwa imekauka lakini wakati wa msimu wa mvua za masika ardhi hufufuka, mito hutiririka na mimea huchipua na kuibua mandhari nzuri ya kuvutia ya kijani kibichi.
Wakati mwanaadamu anapozingatia ishara hizi za maumbile huweza kupata matumaini kuhusu dunia yenye furaha na matumaini.
Katika Uislamu, kuwa na matumaini ni jambo lenye nafasi ya juu kiasi kwamba katika riwaya za Ahul Bayt wa Mtume SAW, matumaini yametajwa kama rehma ya Mwenyezi Mungu. Pamoja na hayo mwanadamu anapaswa kuwa na matumaini kwa kiasi maalumu ni si kuvuka mpaka na kuwa na ndoto zisizoweza kufikiwa au ambazo haziko katika uwezo wa mtu binafsi.
Abu Tayyara alikuwa mfanya biashara katika mji wa Kufa ulio katika Iraq ya sasa. Alikumbwa na matatizo ambayo hakuyatarajia na ghafla akapoteza mali zake na hivyo akawa ni mwenye kuchakaa na kukosa matumaini. Alielekea katika mji wa Madina na kukutana na Imam Sadiq AS na kumuomba amsaidie kupata suluhiso la masaibu yake. Imam AS alimnasihi na kujitahidi kuhuisha matumaini na tawakali kwa Mwenyezi Mungu katika nafsi yake. Kisha akamuuliza: "Je, una duka sokoni?", Abu Tayarra alijibu kwa kusema: "Ndio, nina duka lakini sina bidhaa za kuuza." Hapo Imam akasema: "Utakaporejea Kufa nenda usafishe duka lako kisha uketi hapo. Kabla ya kuanza kazi zako sali rakaa mbili na baada ya hapo useme: 'Ewe Mola mimi siwezi kutegemea nguvu zangu zilizopotea, wewe ndiye pekee ninayeweza kutegemea kwani uwezo wako haumaliziki. Nipe nguvu na uwezo. Nakuomba Ewe Mola! Unipe riziki pana katika maisha yangu'." Abu Tayyara alitekeleza nasaha za Imam Sadiq AS na kurejea katika duka lake akiwa na yakini na matumaini. Baada ya saa moja tu akaja muuza vitambaa na kumtaka amkodishe nusu ya duka lake. Abu Tayyara aliafiki pendekezo hilo na kumkabidhi nusu ya duka lake. Muuza vitambaa aliweka bidhaa zake katika eneo la nusu ya duka na kuanza kuuza. Hapo Abu Tayyara alimuomba muuza vitambaa ampe vitambaa kadha ili naye aweze kuuza na akifanikiwa amlipe mshahara na faida itakayosalia imuendee muuza vitambaa. Hapo muuza vitambaa alikubali pendekezo hilo na hivyo Abu Tayyara akaanza kazi. Ilitokea sadfa kuwa siku hiyo hali ya hewa ilikuwa baridi sana na hivyo wanunuzi wengi walifika katika duka hilo kununua vitambaa na ilipofika magharibi walikuwa wameuza bidhaa zote. Abu Tayyara anasema: "Niliendelea kufanya kazi hii hadi nilipopata uwezo mzuri na hatimaye nikafanikiwa kuwa na wafanyakazi na kujenga nyumba."
Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW anasema: "Matumaini ni rehema kwa umma wangu na iwapo matumaini hayangekuwepo, mama mwenye kunyonyesha mtoto wake hangempa maziwa na hakuna mkulima ambaye angepanda miche."

@@@

Katika Mwezi huu mtukufu wa Ramahdani, milango ya rehma za Mwenyezi Mungu imefunguka mbele ya waja wake, kwa hivyo sisi kama waja tumefungua macho ya matumaini ya kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu ili kwa rahma zake aweze kututakasa na kutondolea madhambi. Matumaini kuhusu msamaha wa Mwenyezi Mungu ni jambo ambalo humuondoa mwanaadamu katika mkondo wa kuelekea motoni na badala yake kumuelekeza katika upande wa Mola Muumba. Hivyo iwapo mja ametenda dhambi kubwa zaidi hapaswi kupoteza matumaini kuhusu rehma ya Mwenyezi Mungu kwani kupoteza matumaini ni kati ya madhambu makubwa.
Moja ya dua maridadi zaidi za Imam Zainul Abidin AS ni dua ya 'Kuwa na Matumaini". Katika dua hiyo amewasilisha taswira ya kuwa na matumaini kumhusu Mwenyezi Mungu na rehma zake zisizo na kikomo. Katika dua yake hiyo Imam Sajjad AS anampa mwanaadamu ujasiri wa kumuomba Mwenyezi Mungu mambo makubwa ambayo hukuza na kuimarisha matumaini katika moyo wake. Katika sehemu ya dua hiyo, Imam Sajjad AS anamhutubu Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Ni vipi ninaweza kuwa na matumaini kwa ghairi yako katika hali ambayo kheri zote ni zako Wewe? Ni vipi Mwanaadamu awe na matumaini kwa asiyekuwa Wewe katika hali ambayo Wewe ndiye Mwenye kutawala kila kitu? Ni vipi nikate matumaini yangu kwako wewe katika hali ambayo kutokana na fadhila na karama zako unanipa hata yale ambayo sijakuomba?" Katika Qur'ani Tukufu Sura al Baqara aya ya 186 Mwenyezi Mungu SWT anasema:
Na waja wangu watakapokuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.
Ndugu Waislamu, sasa tukiwa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tuna fursa ya kipekee ambapo milango yote ya mbingu imefunguka, tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu SWT atukidhie hitajio letu la juu zaidi ambalo ni kupata taufiki ya kumuambudu na kupata radhi yake sambamba na kujikurubisha kwake.
Iwapo katika maisha mwanaadamu atakumbana na huzuni na majonzi hapaswi kuterereka bali anapaswa kuwa na matumaini kwa sababu katika mustakbali wa karibu au mbali atapata furaha kama ambavyo Imam Ali AS alivyosema: "Katika kila majonzi kuna furaha."

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)