Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Julai 2014 11:22

Msimu wa Mavuno (4) [Kuwaheshimu wenzako]

Msimu wa Mavuno (4) [Kuwaheshimu wenzako]

Assalaam Alaykum wasikilizaji wapenzi, ni wakati mwingine tena wa kuwa nanyi katika dakika hizi chache za kukuleteeni kipindi hiki maalumu cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambacho leo kitazungumzia ulazima wa kuhifadhi na kutunza heshima za wengine kwa mtazamo wa dini ya Kiislamu. Ni matarajio yetu kuwa mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ili kusikiliza yale tuliyokuandalieni kwa leo, karibuni.
Mwenyezi Mungu SW amewapa waja Wake neema maalumu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, kwani katika mwezi huu mtukufu, Mwislamu anapaswa kufikiri na kutekeleza amali ambazo zitamuwezesha kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu SW. Mwenyezi Mungu amewapa fursa waja Wake wote katika mwezi huu kufanya mambo mema na kuepuka kutenda dhambi zinazosababishwa na matamanio ya kidunia. Katika mwezi huu mtukufu, shetani mpotevu huangamizwa. Kwa ibara nyingine tunaweza kusema kuwa, shetani maluuni hufungwa minyororo katika mwezi huu, ili waja wema wa Allah waweze kutekeleza amali zao kwa wepesi na ufanisi mkubwa. Mtume Mtukufu SAW amesema: 'Shetani hutembea kwenye mwili wa mwanadamu mithili ya damu. Basi zibeni njia zake kwa kufunga saumu'. Hadithi hii inatupatia mazingatio haya kwamba, kwa kawaida saumu ya mwezi mtukufu inamwezesha mwanadamu kutodhibitiwa na nguvu za shetani. Saumu licha ya kumzuia shetani, inamuokoa mwanadamu kutokana na misukosuko, mabalaa na nafsi inayoamrisha maovu. Imam Ali bin Abi Talib AS anasema, 'Saumu ni msaidizi mzuri wa kuidhibiti nafsi na katika kuzuia ada yake'.
Mpenzi msikilizaji, bila shaka mwanadamu anapaswa kuchukua tahadhari kubwa iwapo ataamua kupita kwenye njia iliyojaa mashimo nyakati za usiku tena kwenye giza totoro. Iwapo atakuwa na jambo ambalo hana elimu nalo na halielewi, basi bora asilizungumze! Anyamaze na wala asilitolee maamuzi ya pupa. Mwenyezi Mungu anasema katika sura Israa aya ya 36: 'Wala usifuate (ukipita ukiyasema au kuyafanya) usiyo na ilimu (ujuzi) nayo. Hakika masikio na macho na moyo; hivyo vyote vitaulizwa'.
KASIDA
Mpenzi msikilizaji, inawezekana umeshawahi kunyunyuziwa mikononi mwako matone kadhaa ya maji ya waridi yenye harufu nzuri, ingawa matayarisho yake yanahitajia uvumilivu mkubwa! Mtu anayekwenda kuchuma maua ya waridi, huelekea shambani asubuhi na mapema na huko huchomwa na miba ambayo humsababishia majeraha mikononi na mwilini mwake. Baada ya usumbufu wote huo na kuchomwa miba, maua hayo huchukuliwa na kumiminwa kwenye sufuria kubwa lililojaa maji na kuchemshwa. Maji hayo yakichemshwa hutoa mvuke, ambao hukusanywa na kuwa matone matone na mwishowe hupatikana maji ya waridi. Inawezekana kabisa akatokea mtu asiyejali nguvu za wenzake na kuamua kupiga teke sufuria na kumwaga maji ya waridi, yaliyopatikana baada ya taabu na misukosuko mingi. Mpenzi msikilizaji, hebu fikiria kwa makini iwapo utakumbana na mkasa kama huo utajisikiaje?
Bila shaka, heshima ya mwanadamu ni mithili ya maji ya waridi ambayo huanza kwa kujikusanya matone matone, baada ya kupitia hatua ngumu za upatikanaji wake. Lakini baadhi ya watu huwa hawajali heshima za wenzao na mara moja huamua kuwavunjia heshima katika jamii bila kujali lolote. Dini tukufu ya Kiislamu iko makini katika suala la uchungwaji wa heshima ya mwanadamu. Kuhusiana na suala hilo Amirul Muuminin Ali AS amesema: 'Kila mtu anayefichua aibu za watu wengine, Mwenyezi Mungu naye humfichulia aibu zake'. Uhakika wa mambo ni kwamba, Mwenyezi Mungu humfahamisha na kumtanabaisha mwanadamu kwamba, ni uchungu ulioje anaoupata mtu aliyevunjiwa heshima na mwanadamu mwenzake. Qurani Tukufu inasema katika aya ya 112 ya surat Nisaa: 'Na mwenye kufanya khatia (ndogo) au dhambi (kubwa), kisha akamsingizia (nayo) asiye na kosa, basi kwa yakini amebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri'.
Bila shaka mpenzi msikilizaji umeshawahi kusikia usemi huu unaosema kwamba, ulimi ni kama mshale, ambapo ukishatoka kwenye upinde haurudi tena! Hapa tunakuleteeni kisa chenye mazingitio kuhusiana na maudhui hii. Siku moja mwanamke mmoja alimtuhumu jirani yake na kuanza kusambaza tuhuma hizo kwa watu wengine. Baada ya muda mfupi tu, watu wote na majirani walizipata habari zile. Bwana yule aliyetuhumiwa tuhuma hizo nzito alijisikia vibaya mno na kuumia moyo wake. Baada ya kupita muda mrefu kidogo, mwanamama yule alijuta kutokana na kosa alilofanya la kumtuhumu jirani yake, na hivyo akaamua kumuendea bwana mmoja mwenye hekima na busara kwa lengo la kupata mawazo na msaada wake, ili aweze kufidia kosa lake. Bwana yule alimuambia mwanamke yule: "Nenda sokoni na ununue kuku, kisha umchinje na baadaye uyasambaze manyoya yake katika mtaa ilioko karibu na mahala unapoishi". Mwanamke yule alishangazwa na kauli hiyo, lakini aliamua kutekeleza kama alivyoambiwa. Siku iliyofuata, bwana mwenye hekima alimwambia yule mwanamke: 'Sasa nenda uyakusanye manyoya yote na uniletee ". Mwanamke yule alikwenda katika eneo alilotupa yale manyoya, lakini hakuweza kukusanya zaidi ya manyoya manne, kwani manyoya yote yalikuwa tayari yameshapeperushwa na upepo. Bwana mwenye hekima alimwambia yule mwanamke: "Kitendo cha kutupa manyoya kilikuwa rahisi na chepesi mno, lakini kuna ugumu na uzito mkubwa wa kuyakusanya manyoya yaliyokwishatupwa. Kwa hivyo, kitendo cha kumtuhumu jirani yako kilikuwa chepesi, lakini kukirekebisha ni jambo gumu na lisilowezekana. Tuhuma yoyote inayotolewa dhidi ya mtu mwingine, bila shaka inaweza kuharibu maisha ya mtu huyo.
KASIDA
Mpenzi msikilizaji, mwanadamu daima anakabiliwa na maadui wawili wa hatari; mmoja ni nafsi inayoamrisha maovu ambayo ni adui wa batini, na mwingine ni shetani ambaye ni adui wa dhahiri. Kuhusiana na adui wa nafsi inayoamrisha, Mtume Mtukufu Muhammad SAW anatahadharisha kwa kusema: 'Adui mbaya zaidi yuko ndani ya nafsi, ambaye amejikita baina ya pande mbili'.
Amma kuhusiana na uadui wa shetani kwa mwanadamu, moja kati ya baraka kubwa za Qurani Tukufu, ni kumtanabaisha mwanadamu kutokana na uadui wa shetani unaodhihirika katika sura mbalimbali na kumtahadharisha asitumbukie kwenye mtego wa adui huyu hatari, ambapo mwisho wake ni majuto na masikitiko. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 6 ya suratul Faatir: 'Kwa hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni adui (yenu; kwa hivyo msimtii) kwani analiita kundi lake liwe katika watu wa Motoni'.
Kwa vile shetani hawezi kuzuia chaguo na azma ya mwanadamu, basi huamua kumjia kwa kutumia mbinu na vitimbi mbalimbali ili aweze kumhadaa na kumpoteza. Shetani huingia kwenye moyo wa mwanadamu na kumtia wasiwasi, hupotosha fikra zake sahihi na kumtumbukiza kwenye upotevu, hatimaye humuondoa kabisa kwenye njia iliyonyooka na kwenye njia safi ya fitra ya mwanadamu. Katika hali ya kawaida, mwanadamu hujisikia kuwa ni mwenye kupenda ladha na matamanio ya kidunia, na shetani naye hutumia fursa hiyo na udhaifu huohuo wa mwanadamu kumtumbukiza kwenye maasi na mambo machafu. Baadhi ya wakati shetani humuonyesha sura nzuri, ili amuongoze kwenye dhambi, na baadhi ya wakati huteta vitisho, hofu na uvivu ili ashindwe kutekeleza majukumu aliyopewa na Mwenyezi Mungu. Baadhi ya wakati mwanadamu hujutia makosa yake aliyoyafanya baada ya kufuata hadaa, hila na ghiliba za shetani, lakini mara hurudia kutenda makosa yaleyale au mengineyo. Kwa utaratibu huo tunaona kwamba, shetani humfuata mwanadamu hatua kwa hatua na humrubuni kwa tamaa na ladha zisizoelezeka, ili awe mbali na Allah SW na hatimaye kumzuia kabisa kutekeleza maamrisho ya Muumba wake.
Naam mpenzi msikilizaji, kipindi chetu maalumu cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kimefikia tamati hapa. Ni matarajio yetu kuwa mumenufaika vya kutosha na yale tuliyowaandalia kwa siku hii ya leo.
Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)