Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 04 Julai 2014 21:45

Msimu wa Mavuno (3) [Ibada - 2]

Msimu wa Mavuno (3) [Ibada - 2]

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujumuika nami katika kipindi kingine cha Msimu wa Mavuno ya Ibada ambacho leo kitatupia jicho udharura wa kuunga udugu na kushirikiana sanjari na kuwafanyia mambo mema watu wa familia, nakusihini muendelee kuwa nami hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

Tukiwa bado tuko katika siku za kujitakasa za mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tunataraji kwamba twa na ibada zenu zitakuwa zenyekukubaliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kufahamu thamani ya siku hizi adhimu, ambazo zimejaa faida kemkem na umaanawi. Katika moja ya dua zake kuhusiana na fadhila za mwezi huu wa Ramadhani, Imam Sajjad (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) anasema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Tujaalie katika mwezi huu tufanikiwe kuwafanyia wema watu wa karibu yetu na tuharakie kwenda kuwaona. Na tuwakirimu kwa zawadi majirani zetu. Tuzisafishe mali zetu mbazo huenda tulizipata kwa njia zisizo sahihi kwa kutoa zaka na tujiunge na wale tuliotengana nao...."


******

Punje za tunda la komamanga huwa na maana na kutupa funzo muhimu kutokana na punje hizo kushikamana na kuwa pamoja. Sisi wanadamu pia huwa kama punje hizo. Yaani sisi hupata shakhsia, nguvu na umaanawi wakati tunakuwa pamoja. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib (as) akatuusia kwa kusema: "Jiepusheni na mgawanyiko, kupeana mgongo na kutengana." Kutengana na kupeana mgongo huwafanya watu kupoteza shakhsia zao. Hebuutazameni msumeno! Yaangalieni kwa makini meno yake namna yalivyoshikamana na kufuatana! Yaangalieni ni namna gani yanavyosaidiana! ni kwa ajili hiyo ndio maana msumeno huo unaweza kukata kitu. Hii ni katika hali ambayo kama kutakuwepo mwanya kati ya meno hayo au kila jino likawa limeelekea upande wake bila ya mpangilio, kwa hakika msumeno huo hautaweza kukata wala kufanya kazi zake ipasavyo. Hali hiyo ni sawa kabisa na hali yetu hasa pale tunaposhikamana na ndugu na watu wa karibu yetu. Kinyume chake pindi tunapotengana na kuwacha mwanya baina yetu, tukaacha kufunga udugu na kufanyiana mema, basi wakati huo sisi hukosa nguvu na uwezo na kushindwa kufanya jambo lolote, mithili ya msumeno ambao meno yake yana kasoro fulani. Hivi ndivyo Amirul-Muuminina Ali bin Abi Twalib (as) anavyosema: "Ole wako ikiwa utakata udugu!" Hata hivyo ni vyema ifahamike kwamba, kukata au kuunga udugu hakuna maana pekee ya kukutana au kutokukutana na mtu mwengine. Bali kuna maana ya kufuatilia shida na matatizo ya mtu mwingine kwa nia njema, jambo ambalo linatajwa kuwa kiwango cha juu kabisa cha kuunga udugu kati ya pande mbili. Usiku wa Ashura Imam Hussein (as) aliwambia watu wa familia yake kwa kusema: "Mimi sina mtu mithili yenu aliyeunga nami udugu." Yaani kwamba kuunga udugu hakuna maana kwamba lazima tukae pamoja katika meza ya chakula, bali ni kuunga udugu kwa uthabiti katika mazingira ya vita na katika shida na matatizo mbalimbali ili kuzidisha moyo wa umoja baina ya watu wawili au zaidi.

******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako kipindi kilichoko hewani ni kipindi maalumu kinachohusiana na mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kinachokujieni kutoka Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Imeelezwa kuwa mtu mmoja alimwendea Mtukufu Mtume na kumwambia: "Ewe Mtume! Mimi nina ndugu ambao ninawatendea mambo mema na nina uhusiano mzuri nao. Lakini hata hivyo wao wananiudhi. Kutokana na maudhi yao kwangu, nimeamua nami niachane nao!" Baada ya Mtume Muhammad (SAW) kusikia maneno hayo alimwambia mtu yule: "Ukifanya hivyo naye Mwenyezi Mungu ataachana na wewe." Yule mtu akamwambia Mtume: "Basi nifanye nini?" Mtume akamwambia: "Mpe yule aliyekunyima, unga udugu na yule aliyekukatia udugu huo na kukudhulumu. Wakati wowote utakapofanya hivyo basi naye Mwenyezi Mungu atakusaidia." Kwa hakika moja ya ibada kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kuwatumikia waja wake na kutumia neema alizokupa katika kuwasaidia waja hao. Imam Swadiq (as) anasema: "Jambo lolote linaloweza kutia furaha katika moyo wa ndugu yako muumini, Mwenyezi Mungu Mtukufu hulilipia ujira na thawabu mara 10 zaidi. Na jambo lolote linalotia tabasamu katika moyo wa ndugu yako muumini, litahesabika kuwa jema kwake."
Kuhusiana na suala hilo, kumepokelewa kisa kimoja cha kuvutia kinachosema kwamba, Sheikh Rajab'ali Khayyat, alikuwa mtu mwenye zuhudi ambaye alifikia daraja ya juu ya uchaji-Mungu na ukamilifu. Siku moja kijana mmoja aliyekuwa na huzuni alimwendea sheikh huyo. Kijana huyo alikuwa muhandisi majengo na ambaye kwa wakati huo alikuwa amejenga majengo kadhaa, lakini kutokana na kwamba majengo hayo yalikuwa hayajapata mteja wa kuyanunua, alikuwa na madeni mengi. Wadai hata walifikia hatua ya kumshtaki mahakamani. Hivyo kijana huyo alimwendea Sheikh Rajab'ali Khayyat, na kumwambia: "Mimi ninafuatiliwa na kusakamwa sana, hata siwezi kwenda nyumbani kwangu na kuishi kwa amani." Baada ya Sheikh kusikia vile akafikiria kwa muda na kisha akasema: "Nenda ukamridhie dada yako." Yule kijana akasema: "Dada yangu yupo radhi nami." sheikh akamwambia tena: "Hapana!" Muhandisi akafikiria kidogo kisha akasema: "Ni kweli! Wakati baba yangu alipofariki dunia alituachia urithi. Hata hivyo mimi sikumpa dada yangu fungu lake katika urithi huo." Kisha akasimama na akamwendea dada yake na akampatia fedha zake kisha akarudi tena kwa sheikh na kusema: "Tayari nimemridhisha dada yangu." Sheikh akanyamanza kidogo na akasema tena: "Hadi sasa bado hajawa radhi nawe, je, dada yako anayo nyumba ya kuishi?" Yule muhandisi akasema: "Hapana! Bali anaishi katika makazi ya kupanga." Sheikh akamwambia: "Nenda ukampatie dada yako moja ya nyumba nzuri ulizojenga." Kijana yule akaenda na akachagua nyumba nzuri akampatia dada yake sambamba na kumuhamishia katika nyumba hiyo kisha akamwendea tena Sheikh Rajab'ali Khayyat. Hapo sheikh akasema: "Sasa umefanya vyema." Siku iliyofuata, yule muhandisi akafanikiwa kuuza nyumba tatu kati ya nyumba zile na akafanikiniwa pia kuepuka matatizo ya madeni yaliyokuwa yakimkabili. Mwenyezi Mungu anasema: "Na Mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote, na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa wa karibu, na mayatima na masikini na jirani wa karibu (katika koo) na jirani wa mbali na rafiki wa ubavuni na msafiri na waliomilikiwa na mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi mwenye kiburi, ajivunaye." Suratun-Nisaa aya ya 36.

********

Tukiwa tunaelekea tamati ya kipindi hiki, sasa tutupie jicho moja ya dua za Imam Sajjad (as) mmoja wa wajukuu wa Mtume (saw) akisema: Moja ya matunda ya maarifa na imani kwa Mwenyezi Mungu ni mapenzi. Mtu yeyote mwenye maarifa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anakubaliana na ukweli huu kwamba, neema zote za kimada na kimaanawi ni zawadi na hiba kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mambo yanayomfanya azidishe mapenzi kwa Mola wake ambaye ndiye Mfalme wa kila kitu. Mtu wa namna hiyo hufanya juhudi katika kuvutia mapenzi ya Mola wake. Imam Zainul-Abidin (as) anaitaja nukta hiyo wakati akisoma dua kwa kusema: "Ewe Mola wangu! Ninakuomba uujaze moyo wangu kwa mapenzi yako na unifanye niweze kukuogopa...Mola wangu! Naomba mapenzi yako na mapenzi ya yule unayempenda. Nakuomba matendo ambayo yatanifanya niweze kukufikia wewe...."
Kwa upande mwingine mtu yeyote aliyewahi kuonja ladha ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, anakuhesabu kuwa ni balaa kubwa isiyoweza kuvumilika, kujitenga na kuwa mbali na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana mtukufu huyo akasema katika moja ya dua zake kwamba: "Mola wangu! Ni vipi utamuweka mbali mtu aliye na mapenzi juu yako? Mola wangu! Utaninyima vipi rehema na msamaha wako hali ya kuwa nina matumaini makubwa na vitu hivyo...?"
Licha ya maneno haya kubainisha kwa kina machungu ya moyoni, lakini wakati huohuo yanaweka wazi rehema na mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Ni matumaini yetu kwamba Mwenyezi Mungu ataturehemu na kutusamehe sote madhambi yetu kwa baraka za mwezi huu adhimu wa kuteremshwa Qur'ani Tukufu. Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)