Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 30 Juni 2014 12:00

Msimu wa Mavuno (2) [Uchaji Mungu]

Msimu wa  Mavuno (2)  [Uchaji Mungu]

Assalaam Alaykum wasikilizaji wapenzi, ni wakati mwingine tena wa kukuleteeni kipindi maalumu cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, kipindi ambacho kitaangazia masuala ya uchaji Mungu katika mwezi huu mtukufu; ni matarajio yetu kuwa mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki karibuni.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni mwezi wa kujipinda katika kusoma Qurani na kumuomba Mwenyezi Mungu atupatie rehema na baraka Zake. Mwezi ambao, Mwenyezi Mungu SW huwasamehe waja na kuwapatia rehema Zake zisizo na ukomo. Hivi sasa Allah SW kwa mara nyingine tena amekikunjua kitanga hiki chenye adhama kwa ajili ya waja Wake na kuwaalika wote kwenye ugeni huu uliojaa kheri na baraka. Tunawapongeza Waislamu wote kwa kuwadia mwezi huu mtukufu, mwezi unaotakasa nafsi na nyoyo zao, na mwezi ambao mja anapasa kuacha kujiegemeza na kukumbatia mambo batili na ya kimaada na badala yake amuelekee Mola wake.
KASIDA
Msomi mmoja anasema: Ni bahati iliyoje kwa udongo ulioko katika sehemu inayopita mkondo wa maji, kwani udongo huo hutoa rutuba na kukuza mimea ambayo ukiketi pambizoni mwake hupata burudani na furaha ya moyo. Amma bahati mbaya iko kwenye maua na mimea iliyo mbali na mkondo wa maji. Hivyo mwanadamu ni mithili ya maua au mimea, na Mwenyezi Mungu SW ni mithili ya maji ambayo huuisha mimea na maua hayo. Ni bahati iliyoje kwa mtu anayefuata njia ya uongofu, na bahati mbaya iliyoje kwa mtu ambaye amejiweka mbali na Mwenyezi Mungu SW, anabaki akitangatanga na kuwa mithili ya ua lisilopata maji au mwanga wa jua.
Mpenzi msikilizaji, neno taqwa ni neno la Kiarabu lenye maana ya mtu kujilinda kupitia kitu au ngao fulani. Na katika fani ya dini, neno hili kitaalamu, lina maana ya kule mtu kujiweza au kuimiliki nafsi yake, kunakomfanya awe nje ya maasi au ajitenge na maasi. Kwa ibara nyingine ni kwamba, taqwa ni zile nguvu maalumu ambazo hugeuka na kuwa kipaji kilichomo ndani ya nafsi ya mwanadamu alichojichumia kupitia fikra na matendo maalumu, nguvu ambazo humuwezesha kumiliki nafsi yake pale anapokutana na vishwawishi au pale nafsi inapotaka kumuelekeza katika maasi kwa namna moja au nyingine. Mwenyezi Mungu anasema kwenye aya ya 2 ya surat Twalaaq: "Na anayemcha Mwenyezi Mungu, Yeye humtengenezea njia ya kuokoka (katika kila balaa)". Hii haina maana kwamba tutaepukana na mambo magumu, hapana! Yaani hatutahisi ugumu wala matatizo kwenye mambo yetu na badala yake tutapita kwenye mambo mepesi mepesi tu. Hayo tuliyoyaeleza ni mithili ya farasi anayepita kwa amani kwenye vizuizi na mazingira magumu, bila shaka mnyama huyo huhisi furaha kubwa anapopita kwenye vizuizi hivyo bila matatizo. Taqwa ni mithili ya kumjenga mwanadamu kuwa kama mpanda farasi mahiri ambaye uhodari wake humuwezesha kupita kwenye vizuizi. Taathira na baraka nyingine za taqwa ni kutomuweka mwanadamu kwenye hali ya hofu na woga au kumuweka kwenye njia na mazingira ya kukimbia. Qurani Tukufu inasema: "Na anayemcha Mwenyezi Mungu, Yeye humtengenezea njia ya kuokoka (katika kila balaa)".
KASIDA
Mpenzi msikilizaji, hivi sasa tunaweleteeni kisa cha kweli ambacho kilimtokea mmoja kati ya wanafunzi wa chuo kikuu kimoja cha kidini au kwa jina jingine 'hawza' hapa nchini. Kisa hicho kinaelezea jinsi mwanadamu anavyopasa kumtegemea na kumcha Mungu, na kujiepusha na mambo machafu yawe ni ya dhahiri au batini. Muhammad bin Baqer mwanafunzi kijana wa hawzah, akiwa anajishughulisha na kutalii na kupitia masomo yake, ghafla aliingia chumbani mwake msichana ambaye alikuwa akionyesha dalili za hofu na wasiwasi mwingi usoni mwake. Msichana huyo alionyesha wazi kuwa anatoka katika familia ya kifalme, na mara alipoingia kwenye chumba cha Muhammad Baqer alimtolea ishara za kumtaka anyamaze kimya bila ya kupiga kelele zozote. Msichana huyo alianza kwa kumuuliza Muhammad Baqer alikuwa ameandaa nini kwa ajili ya chakula cha usiku. Mwanafunzi yule alimletea chakula chote alichokuwa amejiandalia usiku ule. Msichana alikula chakula chote na kisha akaelekea kwenye kona ya chumba na kulala, huku Muhammad Baqer akiendelea na kutalii na kudurusu masomo yake. Wakati hayo yakiendelea, nje kulikuwa na pirikapirika na juhudi kubwa za kumtafuta msichana huyo ambaye alikuwa binti ya mfalme. Ilipofika asubuhi, wafanyakazi na walinzi wa mfalme walimkamata Muhammad Baqer pamoja na binti yule na kuwapeleka mbele ya mfalme, kwani walimuona wakati akitoka ndani ya chumba cha mwanafunzi huyo wa kidini. Mfalme Abbas wa Kisafavia, aliyekuwa na nguvu kubwa alighadhabika mno na kumuuliza mwanafunzi wa kidini: 'Kwa nini hukutoa taarifa kwamba, binti yangu yuko chumbani kwako?' Muhammad Baqer alisema: 'Binti wa mfalme alinitishia kwamba kama ningemueleza mtu yeyote habari za kuwepo kwake chumbani kwangu, angehakikisha ninapelekwa kwa mnyongaji ili aninyonge.' Baada ya kufanyika uchunguzi wa kina, Mfalme Abbas alitambua kwamba mwanafunzi huyo alikuwa akijishughulisha na kutalii na kudurusu masomo yake hadi asubuhi, na wala hakumfanyia kitendo chochote kibaya binti yake. Alishangazwa na kustaajabishwa mno na kitendo cha kijana huyo. Alimuuliza: 'Ni vipi uliweza kukabiliana na nafsi yako? Mwanafunzi huyo wa kidini alimuonyesha mfalme vidole vyake kumi vya mikononi ambavyo vyote vilikuwa vyeusi na vikionyesha alama ya kuungua katika sehemu za kucha. Mfalme Abbas alimuuliza mwanafunzi sababu ya kuungua vidole hivyo, naye alimjibu: 'Baada ya binti yako kupatwa na usingizi, shetani aliniingia na kunishawishi kufanya tendo baya naye; lakini kila mara niliposhikwa na matamanio ya kishetani ya kufanya tendo hilo, nilikuwa nikichukua kidole changu kimoja na kukichoma kwenye mshumaa uliokuwa ukiwaka chumbani kwangu, ili niweze kuhisi walau kwa uchache tu uchungu wa moto wa Jahannam, hali iliyoendelea hadi asubuhi bila ya kumkaribia binti yako. Namshukuru Mwenyezi Mungu, shetani hakuweza kunipotosha kwenye njia sahihi na kuiteketeza imani yangu'. Mfalme Abbas alifurahishwa mno na imani na uchajiMungu aliokuwa nao Muhammad Baqer na hatimaye akatoa amri ya kuozeshwa binti yake huyo. Mfalme Abbas alimpa Muhammad Baqer lakabu ya 'Mirdamad' na msomi huyo akatokea kuwa miongoni mwa wanafalsafa na wanazuoni wakubwa katika zama zake na hadi leo hii shakhsia huyo bado anakumbukwa kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya wakati wa zama zake.
KASIDA
Mpenzi msikilizaji, mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi bora zaidi kati ya miezi ya Kiislamu, ambapo hujulikana kama mwezi wa wageni wa Allah. Mwezi huu mtukufu, licha ya muumini kufunga saumu na kujipinda katika kusoma Qurani Tukufu, ni fursa nzuri ya kusoma na kuomba dua, huku akitarajia kutakabaliwa amali zake. Kwa minajili hiyo, Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu daima walikuwa wakijipinda zaidi katika kusoma dua ili hatua kwa hatua waweze kumkaribia zaidi Mwenyezi Mungu SW. Imam Ali bin Hussein bin Ali AS ni mmoja wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu na kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW ambaye anajulikana kwa lakabu ya Zainul Abidiin yaani 'pambo la wafanya ibada', ameacha athari zake kubwa za dua kwenye kitabu kinachojulikana kwa jina la Sahiifat Sajjadiyyah.
Imam Sajjad AS katika dua ya 20 ya Sahiifat Sajjadiyyah anamuomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Ewe Mola! Nijaalie nije kwako wakati wa matatizo na niombe msaada wako kwa ninayohitajia na wala nisishawishike kuomba msaada kwa yeyote isiyekuwa wewe....."
Dua hii inasisitiza kuwa, mwanaadamu kwa dhati yake huelekea kwa Mola wake wakati akiwa na matatizo na akiwa muhitaji.
Imam Sajjad AS pia katika dua zake, mbali na masuala ya malezi pia anazingatia masuala ya neema za Mwenyezi Mungu. Anakumbusha kuhusu neema za Mwenyezi Mungu ambazo mwanadamu huwa anaghafilika nazo kutokana na kujishughulisha na maisha ya kidunia.
Katika mfumo wa malezi wa Imam Sajjad AS, kukumbuka neema kunapaswa kuwa katika fremu ya kumhimidi na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, katika dua ya kwanza ya Sahiifat Sajjadiyyah, Imam Sajjad AS anakumbusha kuhusu neema kwa kumhimdi Mwenyezi Mungu na kisha kusisitiza kuhusu kutubu mja na kurejea kwa Mola wake.
Mtukufu huyo katika dua hiyo anamsifu Mwenyezi Mungu kwa kuweka wazi mlango wa toba kwa wanaadamu. Anamtaja mwanaadamu aliyefikia ubora na ufanisi kuwa ni yule ambaye anarejea kwa Mola wake. Toba katika Sahiifat Sajjadiyyah imetajwa kuwa msingi muhimu katika malezi ya mwanaadamu. Kwa mtazamo wa Imam Sajjad AS, toba kwa maana yake halisi haihusiani tu na madhambi na maasi, bali kujiweka mbali na lile duara la kumridhisha Mwenyezi Mungu ni jambo linalohitajia toba.
Naam wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu maalumu cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kimefikia tamati. Tunakuombeni mjiunge nasi tena katika vipindi vyetu vingine vya mwezi mtukufu wa Ramadhani, huku tukiwatakia Waislamu wote duniani funga njema ya mwezi huu mtukufu.
Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)