Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 29 Juni 2014 18:07

Msimu wa Mavuno (1) [Ibada - 1]

Msimu wa Mavuno (1) [Ibada - 1]

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa vipindi vyetu maalumu vinavyokujieni katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani vinavyobeba jina la Msimu wa Machipuo wa Ibada. Ni matarajio yetu kuwa mtaendelea kuwa kando ya redio zenu kusikiliza tuliyokuandalieni.

>>>

Wapenzi wasikilizaji mwezi huu wa Ramadhani umetajwa katika mafundisho ya Uislamu kuwa ndio mwezi bora zaidi kuliko yote na kwamba siku na usiku zake ndiyo bora zaidi. Imenukuliwa kutoka kwa Mtume wetu Muhammad (saw) kwamba amesema: "Milango ya mbingu hufunguliwa katika usiku wa kwanza wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na haifungwi tena mpaka usiku wa mwisho wa mwezi huo."
Sisi sote tunajua kwamba aghlabu ya dawa tunazotumia kwa ajili ya kutibu maradhi mbalimbali huwa chungu, hata hivyo dawa hizo chungu huwa na tamu kwa mwanadamu ambayo ni kumpa uzima, ahuweni na kumponya kwa sharti kwamba, dawa hizo zitumiwe kwa wakati wake maalumu bila ya kutangulizwa au kucheleweshwa. Sharti jingine la dawa kuponya ni kuchunga kiwango maalumu anachopasa kunywa mgonjwa na kisipungue au kusizidi kile alichoambiwa na daktari na mganga.
Ibada ya Swala mpenzi msikilizaji, inashabihiana kwa kiasi fulani na dawa na ibada hiyo huwa kama dawa chungu kwa baadhi ya watu. Wakati mwingine mwanadamu hulazimika kuamka mapema alfajiri wakati wa baridi kali au kushuka kwenye gari akiwa safarini na kuchukua udhuu kwa ajili ya Swala huku akitetemeka kwa baridi. Kazi hii huwa na machungu yake makubwa kwa mwanadamu. Au mara nyingine utamuona mtu anayetazama filamu ya kuvutua au mchezo anaopenda lakini anaposikia sauti ya muadhini husimama mbiyo na kuelekea msikitini kwa ajili ya Swala.
Hali hii si makhsusi kwa ibada ya Swala bali pia huwa katika ibada nyingine kwa baadhi ya waumini. Hata hivyo pale mwanadamu anapofikia kiwango cha juu cha kuelewa hakika ya Swala na ibada hiyo, chungu na mashaka hayo hubadilika na kuwa tamu na nyepesi. Ndiyo maana tunawaona baadhi ya mawalii wa Mwenyezi Mungu wakisema waziwazi kwamba, Swala ndiyo kipenzi na kipusa chao, kama ilivyonukuliwa kutoka kwa Mtume wetu mtukufu na Ahlibaiti zake watoharifu. Kwa msingi huo tunamuomba Mwenyezi Mungu Karima atuonjeshe na kutupa tamu ya kumtaja na kumkumbuka Yeye na kuturuzuku maarifa ya hakika ya kumwabudu Yeye.
Nukta nyingine ya kutaja hapa ni kuwa Swala ni mithili ya dawa inayopaswa kutumiwa wakati maalumu. Falsafa ya ibada ya Swala ni kuelewa adhama na utukufu wa Mola Muumba na hisia hiyo haipatikani kama inavyotakiwa isipokuwa pale mwanadamu anapotekeleza ibada hiyo mwanzoni mwa wakati wake. Hii ni kwa sababu mtu anayechelewesha Swala yake huwa anatangaza kuwa Mola wangu! Ninafadhilisha na kutanguliza mbele kazi zangu kuliko kukutii na kukuabudu wewe.

>>>

Katika upande mwingine Swala kama ilivyo dawa, inamlazimisha mtu kujiepusha na baadhi ya mambo. Kwa vile Swala ni haki, hivyo mtu anayetekeleza ibada hiyo anapaswa kujiepusha na batili, kwa maana kwamba analazimika kujiweka mbali na ufuska, maovu na madhambi; la sivyo Swala yake itapoteza sifa zake.
Kwa mfano tu mwanadamu anayetia joto nyumba yake wakati wa msimu wa baridi kali analazimika kuziba matundu yote yanayoruhusu baridi kuingia ndani au yanayoruhusu nishati ya joto kuharibika na kutoka nje. Hapa tunajiuliza kwamba, ni kwa nini ibada ya Swala haitupi joto na vuguvugu inayotakikana na kutukurubisha kwa Mola wetu Karima? Jibu ni kwamba, kwa sababu hatufungi madirisha ya masikio, macho, ndimi, tupu, macho yetu na kadhalika. Kwa msingi huo tunatazama, kusema, kula na kufanya kila kitu japo cha haramu. Hali hiyo ya Swala zetu kukosa sifa pia ni mithili ya ghala lililojaa ngano au nafaka nyingine. Pale tunapoacha matundu ya wazi katika ghala hilo, nafaka zetu huharibiwa na mapanya, mchwa, panzi na kadhalika.
Hivyo basi kila mtu anayetaka ibada yake ya Swala iwe na vuguvugu na athari zake anapaswa kufunga madirisha na matundu hayo yote na asiyafungue isipokuwa kwa dharura na katika njia ya haki.

>>>

Wapenzi wasikilizaji, mzee mmoja muumini anasimulia kumbukumbu zake akisema:
Wakati nilipokuwa kijana nilikwenda katika mji mtakatifu wa Mash'had uliopo kaskazini mashariki mwa Iran. Huko nilimkuta marehemu Sheikh Hassan Ali Nukhodaki ambaye alikuwa miongoni mwa magwiji wa irfani na wachamungu wakubwa. Nilimwambia: Bwana wangu! Nina haja tatu muhimu na namuomba Mwenyezi Mungu anikidhie haja hizo zote ujanani mwangu. Nakuomba unifunze amali na ibada itakayonifanya nikidhiwe haja zangu haraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Alhaji Hassan Ali Nokhodaki alisema: Unataka vitu gani kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Nilisema: Kwanza nataka nifanikiwe kwenda Makka kuhiji nikiwa kijana, kwa sababu ibada ya Hija wakati wa ujana ina ladha yake makhsusi. Sheikh Hassan alisema: Tekeleza Swala yako wakati wake wa awali na katika sura ya swala ya jamaa. Nilisema: Haja yangu ya pili namuomba Mwenyezi Mungu aniruzuku mke mzuri na mwema. Sheikh alisema: Tekeleza Swala yako wakati wake wa awali tena katika sura ya jamaa. Nilitaja haja yangu ya tatu na kusema: Namuomba Allah aniruzuku kazi na kipato kizuri. Mwanazuoni huyu mutaabbad alisema: Swali swala zako wakati wake wa awali tena katika Swala za jamaa.
Tangu wakati huo nilifuata maagizo ya mwanazuoni huyo na nikawa natekeleza Swala zangu zote wakati wake wa awali na katika jamaa. Matokeo yake ni kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu nilifanikiwa kwenda Makka kuhiji, Mwenyezi Mungu aliniruzuku mke mwema na mcha Mungu na nilipata kazi yenye heshima na kipato.

>>>

Wapenzi wasikilizaji, Ramadhani ni mwezi wa ibada na kujikurubisha kwa Mola Karima na hakuna ibada inayomkurubisha zaidi mwanadamu kwa muumba wake kuliko Swala. Hivyo basi shime na tushikamane na Swala na kuitekeleza wakati wake wa awali tena misikitini katika jamaa. Jambo hili linapodumu huwa kinga ya wasiwasi wa shetani aliyelaaniwa na vishawishi vya matamanio ya nafsi. Mtume wetu Mtukufu Muhammad (saw) amesema: "Shetani humuogopa muumini wakati wote anapotekeleza Swala tano kwa kuchunga wakati wake, na anapoacha Swala Shetani hupata ujasiri wa kumghilibu na kumtumbukiza katika madhambi makubwa."

>>>

Wapenzi wasikilizaji wakati uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu cha leo unaelekea ukingoni. Tunamuomba Mwenyezi Mungu SW atakabali dua na ibada zetu katika mwezi huu mtukufu ambao ni mwezi wa rehma, baraka na neema tele za Mwenyezi Mungu. Hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine tunakutakieni kila la kheri.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)