Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 20 Julai 2013 12:14

Ramadhan, Mwezi wa ibada na toba (5)

Ramadhan, Mwezi wa ibada na toba (5)

As-Salamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujumuika nami katika kipindi kingine maalumu cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kipindi hiki ni katika mfululizo wa vipindi maalumu vilivyotayarishwa kwa ajili ya mwezi huu mtukufu na ambavyo vinazungumzia mambo mengi yanayosaidia katika malezi ya nafasi zetu, karibuni…

Tukiwa bado tumo ndani ya siku hizi bora za kupata rehma na maghfira ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, tunataraji kwamba, twaa na ibada zenu zitakuwa zenye kukubalika.

Kwa mara nyingine tunaangazia sehemu nyingine ya dua ya Makarimul-Akhlaq ya Imam Sajjad (as), inayosema. “Mola wangu! Ikamilishe nia yangu kwa upole wako, isahihishe yakini yangu kwa uwezo wako, na yakamilishe yale yote yaliyoniharibikia kwa uwezo wako wa milele.”

Hakuna shaka kuwa, ikhlasi na usafi ni alama ya kwanza ya ukamilifu wa nia. Kadri nia itakavyokuwa salama, ndivyo inavyozidi kuwa kamilifu. Nia timilifu na kamili ni ile ambayo humpelekea mja hufanya ibada kwa ajili ya shukurani na kutekeleza wadhifa wa uchaji Mungu kwa ajili tu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hii ina maana kwamba, mtu afanye ibada kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu, si kwa ajili ya kupata malipo mema wala kusalimika na adhabu yake. Katika hadithi imenukuliwa kutoka kwa Imam Sajjad (as) akisema: “Sipendi nimwabudu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kupata pepo. Kadhalika sipendi kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa kukhofia adhabu na mateso (ya siku ya Kiama).” Wakati huo mtukufu huyo akaulizwa swali: "Basi unamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kitu gani?" Imam akasema: “Ninamwabudu Mwenyezi Mungu kwa kuwa yeye ni mstahiki na mbora wa kuabudiwa, kwa neema alizonipa na kwa baraka zake mbalimbali alizonienezea.” Ibada ya aina hiyo, ndiyo ibada bora na ya hali ya juu na ndio nia kamili iliyotimilifu. Hiyo ndiyo nia ambayo Imam Sajjad alimwomba Mwenyezi Mungu kwa kusema, “Mola wangu! Ikamilishe nia yangu kwa upole wako na isahihishe yakini yangu kwa uwezo wako.”

Baada ya hapo imam Sajjad (as) anamwelekea Mwenyezi Mungu kwa kusema: “Mola wangu! Ikamilishe yakini yangu kwa elimu na uwezo wako.” Baada ya hapo anaongeza kwa kusema: “Mola wangu! Nisahihishie kwa uwezo wako wa milele, kila kile ambacho kimeniharibikia na kimeniondoa kwenye hali nzuri na njia iliyonyoka na kunipeleka kwenye uovu.” Katika kipengele hicho cha dua Imam Sajjad (as) anakusudia kusema kwamba: “Mola wangu! Kamwe usinipe kisogo na kuniacha. Nisaidie na kuniongoza katika matendo yangu yote ya kimaada na kimaanawi.” Ibara hii fupi inaweza kurekebisha hali zote za mwanadamu, kama vile kudhoofika mwili, msongo wa mawazo, wasiwasi wa na jambo jingine lolote ambalo linamwendea mrama maishani. Ni wazi kuwa, ufisadi wa maadili, itikadi na matendo na kwenda kinyume na njia iliyonyoka ya Mwenyezi Mungu, ndio ufisadi ulio na madhara makubwa zaidi kwa mwanadamu.  Ikiwa Mwenyezi Mungu atakukubali dua za waombaji wanaotaka kurekebishwa mabaya yao, ni wazi kuwa mabaya hayo yataondoka na mahala pake kuchukuliwa na wema pamoja na saada. Hii ni kwa sababu Mola Mlezi anaujua ukweli wote na kufahamu kila jema na baya lililo na manufaa kwa mja. Hata hivyo nukta hii inapaswa kuzingatiwa kwamba, kuomba dua kwa ajili ya kutaka marekebisho kutokana na machafu na aibu za mtu binafsi na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hakusababishi kuondolewa wajibu wa kidini wala majukumu yanayowakabili Waislamu. Uislamu unawataka wafuasi wake kurekebishana kutokana na machafu na aibu, baina yao kwa njia ya kukumbushana ili kuandaa mazingira ya kupatikana saada na wokovu kwa jamii ya mwanadamu.

******************************************

Moja ya mambo yanayomzuia mwanadamu kufikia ukamilifu, ni kusema uongo na kufanya hila na khiana. Kusemea uongo na kuwafanyia unafiki wanadamu, ni vitendo vibaya na hatari ambavyo huvunja kabisa misingi ya kuaminiana katika jamii. Katika maisha ya kijamii, uaminifu na ukweli ni misingi miwili muhimu. Ikiwa hakutakuwa na kuaminiana, basi kila mmoja atakosa utulivu wa moyo na kupelekea jamii kusambaratika. Imepokewa kuwa Mitume wote wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakisisitiza juu ya mambo makuu mawili, ambayo ni uaminifu na ukweli.

Siku moja mfanyabiashara mmoja mwaminifu na mwema aliamua  kufanya safari mbali na mji wake. Hivyo alimuweka pahala pake mfanyakazi wake mmoja ili aendelee na shughuli za uuzaji katika duka lake. Yahudi mmoja akaja dukani na kununua kutoka hapo nguo ambayo kidogo ilikuwa na kasoro. Wakati mfanyabiashara yuele aliporejea kutoka safarini na kwenda dukani kwake hakuikuta nguo ile na hivyo akaanza kuitafuta. Mfanyakazi akamwabia tajiri wake: “Ile nguo niliiuza kwa Myahudi mmoja kwa dirham 3000 na sikuwa na habari yoyote kuwa ilikuwa na dosari.” Yule mfanyabiashara akakasirika na kuuliza: “Huyo mtu aliyeinunua yuko wapi?” Mfanyakazi akajibu: “Amesafiri.” Mfanyabiashara huyo wa Kiislamu akachukua zile pesa na haraka akatoka nje ya mji ili auwahi msafara ambao alikuwamo yule Yahudi. Baada ya kupita siku tatu, akaweza kuufikia msafara ule na kumpata yule Yahudi. Baada ya kumpata akamwabia: “Ndugu yangu! Ulinunua nguo kutoka dukani kwangu ambayo ilikuwa na dosari ambayo imejificha. Basi chukua pesa zako nawe unipe nguo yangu.” Yule Yahudi akastaajabishwa saana na hali ile na ndipo akauliza: “Kwa nini umefanya hivi na kutembea safari yote hii kunifuata?” Mfanyabiashara akajibu: “Dini yangu imeniamuru kuwa mwaminifu na kutofanya khiyana.” Mtume wetu anasema: “Mtu yeyote atakayesema uongo, basi si katika mimi.” Yule Yahudi akapigwa na butwaa na hivyo akakiri mbele ya mfanyabiashara yule kwamba, pesa alizompatia mfanyakazi wake zilikuwa bandia na hivyo akampa pesa sahihi na kisha kusema: “Nimemwamini Mungu na Uislamu wenu. Ninashuhudia kuwa hapana Mola apaswaye kuabudiwa kwa haki, ila Mwenyezi Mungu na ninakiri kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.”

***********************************************

Baada ya kuyasikia hayo, sasa tunakukaribisheni kwenye sehemu ya pili ya kipindi hiki, inayohusu usia wa Imam Ali (as). Imam anasema: “(Mwanangu)! Fahamu kuwa, kujigamba, ni kinyume cha mambo mazuri na maafa ya hekima. Jitahidi sana katika kujiboresha na usiwe muweka hazina wa wengine na unapoainisha njia yako, basi tembea kwenye njia ya Mola wako kwa unyenyekevu na upole.”

Tunafahamu sote maana ya kujiona na kujigamba. Kujiona kuna maana ya mtu kujiona kuwa mbora zaidi kuliko wenzake au kwa istilahi nyingine ya kileo, ni kujipa asilimia 100. Imam Ali (as) anaitaja hali hiyo kuwa ni kwenda kinyume na njia sahihi na ya kweli na kwamba ni maafa ya akili na utambuzi. Mtu yeyote anayejiona kuwa mwenye nadharia safi na kamilifu hawezi kuona njia sahihi. Madhara haya ya kujiona, huua akili na hisia za mwanadamu. Aidha wakati mtu anaingiwa na hali hiyo, basi huwa haoni kitu kingine zaidi yake, huku akiiona nadharia yake kuwa juu ya kila kitu. Kuhusiana na hilo Imam Ali (as) anasema: "Wakati unapohusudu nadharia yako kupita kiasi, utapotea njia sahihi na kushindwa akili yako kuainisha mwelekeo sahihi. Ukijiona basi hutoweza kuona mambo mengi na huko ni kujitenga na ukweli." Ni kwa ajili hiyo ndipo mtukufu huyo akakutaja kujiona kuwa sifa mbaya inayoangamiza akili na kuingiza gizani fikra ya mwanadamu.

Aidha Imam Ali (as) anamsihi mwanadamu kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kufikia saada na utukufu. Kwa ibara nyingine ni kuwa, kazi na jitihada za mwanadamu ndizo humfanya afikie utukufu. Madhumuni ya Imam katika kufikia utukufu, ni kufikia ukamilifu wa kiroho na kimaanawi. Yaani mwanadamu anapasa kufanya juhudi kwa ajili ya kuinua kiwango chake cha kiroho. Aidha kwa ibara nyingine ni kwamba, anatakiwa kufanya juhudi kubwa ili kufikia itikadi iliyo sahihi na hivyo kujitenga na itikadi potofu na zisizo sahihi, na wakati huohuo kuweza kufahamu ukweli na kujitenga na akhlaqi mbaya. Baada ya hapo Imam anaendelea kumnasihi mwanawe asiwe mweka hazina wa watu wengine na kuuweka umri wake rehani ukatumiwa na wengine kwa maslahi yao wenyewe na kwa madhara yake yeye.

*******************************************

Ikiwa mtu ataghafilika na ibada ya Mwenyezi Mungu na kujishughulisha na ukusanyaji mali na utajiri wa kidunia tu, kwa hakika juhudi zake hizo ni sawa na kujaza mifuko ya wengine. Amma ikiwa atamuelekea Mwenyezi Mungu na akafanya juhudi za uchaji Mungu kwa ajili ya Mola wake, basi atakuwa amewekeza fungu kwa ajili ya Akhera yake. Aidha Imam anamalizia kwa kusema kuwa, unaposhika njia yako, basi tembea kwa unyenyekevu kwa ajili ya Mola wako.

Nam! Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu hiki kinaishia hapa kwa leo. Ni matumaini yangu kuwa mmenufaika vya kutosha na kuweza kufahamu njia sahihi za malezi ya nafsi zetu. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, basi hadi wakati mwingine, ninakuageni kwa kusema, kwaherini…../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)