Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 26 Oktoba 2014 20:40

Maombolezo; Uhuishaji wa Hamasa Adhimu ya Ashura

Maombolezo; Uhuishaji wa Hamasa Adhimu ya Ashura

Assalaamu Alaykum Warahamatullahi Wabarakatuh. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kuanza mwezi wa Muharram na ambacho kitazungumzia falsafa na sababu za kufanyika majlisi za maombolezo kwa ajili ya Imam Hussein (AS). Ni matumaini yangu kuwa mtafaidika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki.

Kwa mara nyengine Muharram imewadia, na mvumo na ngurumo za hamasa ya Kihusseini zinasikika tena. Muharram inapowadia damu iliyokuwa imetuwama ndani ya mishipa huchemka tena, macho yaliyokauka hububujikwa na machozi na mvua ihuishayo mapenzi ya Kihusseini huzinyeshea tena na kuzihuisha nyoyo zilizokuwa kwenye usingizi wa mghafala. Muharram inapowadia huvunja kimya katika nchi, miji na vijiji na kuzipa uhai mpya nyoyo na roho za watu; msisimko wa Muharram unapojitokeza akili hupigwa na mshangao na zikabaki kujiuliza kwa mastaajabu: haya ni majonzi ya aina gani ambayo yangali kama kidonda kibichi licha ya kupita karne zote hizi? Na je maombolezo haya yana taathira gani kwa watu hawa na nini hasa falsafa ya maombolezo ya Imam Hussein (AS)?
Matukio yaliyopita ya kila jamii wapenzi wasikilizaji yanaweza kuwa na athari tofauti katika hatima na majaaliwa ya jamii hiyo au hata jamii nyenginezo. Ikiwa tukio litakuwa lenye faida na taathira nzuri, kulitalii tena, kulihuisha na kulidumisha kunaweza kuendeleza pia faida na taathira zake njema. Kwa upande mwengine kuyasahau na kuyapuuza matukio hayo muhimu huwa ni hasara kubwa kwa jamii ya wanadamu; kwa sababu kutukia matukio kama hayo huyahasiri mno mataifa, iwe ni kimaada au kimaanawi; kama kuondokewa na shakhsia wakubwa, mashaka na mateso au unyongeshwaji linaopata taifa fulani n.k. Matukio makubwa yanayotoa funzo, tajiriba na ibra ya kuzingatiwa na watu, ni miongoni mwa rasilimali adhimu za kila taifa na wanadamu wote kwa ujumla, na kwa mtazamo wa akili timamu, rasiliamali kama hizo ni za kutunzwa, kuhuishwa na kutumiwa kwa faida ya jamii. Hakuna shaka yoyote kuwa tukio adhimu la Ashura ambalo lina vipengele vya ibra na mazingatio kadha wa kadha ni moja ya matukio yaliyoihasiri mno jamii ya wanadamu; kwa sababu liliandamana na kuuliwa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume wa mwisho wa Allah pamoja na wafuasi wake waaminifu na mateso na masaibu yaliyowapata watu wa nyumba yake pamoja na watoto wake. Kwa upande mwengine, chanzo cha kujiri tukio hilo hakikuwa ni kupigania maslahi binafsi ya mtu, kikundi cha watu au hata ya utaifa; lakini ukweli ni kwamba tukio la Karbala na kuuliwa shahidi Imam Hussein (AS) pamoja na wafuasi wake mashujaa ni madrasa ya mafunzo, malengo na ibra yakiwemo ya tauhidi, Uimamu, kuamrisha mema na kukataza maovu, kutetea hakika, kupambana na dhulma, heshima ya nafsi, izza na mfano wa hayo kwa ajili ya wanadamu wote. Maimamu watoharifu (AS) ambao ni Ahlul Bayt wa Bwana Mtume walikuwa wakitilia mkazo kuweka majlisi za maombolezo ya Ashura na kuzifanya majlisi hizo kuwa mhimili mkuu wa umoja baina ya watu na wa kueneza mafundisho na thamani aali na tukufu za Uislamu. Kiasi kwamba leo hii katika masiku ya Muharram, mamilioni ya watu wa matabaka, rangi na madhehebu tofauti wanashiriki kwenye maombolezo ya Imam Hussein (AS) na kujumuika pamoja chini ya bendera ya bwana huyo wa mashahidi. Taathira ya tukio hili adhimu ilishuhudiwa katika harakati ya mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran wakati wa vuguvuvugu la Mapinduzi ya Kiislamu katika miezi ya Muharram na Safar, hususan katika siku za Tasu'aa na Ashura ambalo liliitikisa na kuitetemesha mihimili ya utawala wa kitaghuti, na hivyo kuweka wazi zaidi siri ya sisitizo la Maimamu watoharifu juu ya kuyafanya maombolezo ya Imam Hussein (AS) kuwa kitovu na mhimili mkuu.

Ibada katika madrasa ya Ashura ndio msingi wa mafundisho ya dini na umaanawi katika jamii ya Kiislamu. Izza na utukufu wa Waislamu umefungamana na imani na umaanawi. Ujumbe wa mapambano ya kujitolea kwa roho na damu ya Imam Hussein (AS) huko Karbala, ulikuwa ni kuonyesha kwamba hatari kubwa zaidi kwa jamii ya Kiislamu ni kudhoofika na kushuka imani na umaanawi na kupinduliwa thamani za dini. Katika utamaduni wa madhehebu ya Shia kuweka majlisi za kuwaomboleza viongozi wa dini hususan Imam Hussein na wafuasi wake ni ibada; kwa sababu maombolezo huufanya umaanawi uchanue ndani ya nafsi ya mtu na kumsaidia katika kufikia daraja za juu za utu. Kumlilia Imam Hussein (AS) na kuhuzunika na kuungulika kutokana na masaibu yaliyompata mtukufu huyo huleta mageuzi ya ndani ya nafsi yanayomjenga mtu kiroho, na kuwa utangulizi wa kuwa taqwa na kumkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu. Aidha kwa kufunga bai'a thabiti na isiyolega lega na mja madhulumu anayeitakidi kwamba mauti kwa ajili ya imani na itikadi ndio njia ya saada, na kuridhia dhulma ya dhalimu ni madhila na idhilali, huonyesha jinsi mtu alivyoshikamana na malengo matukufu ya bwana wa mashahidi Imam Hussein (AS) ya kutokuwa tayari kupatana na madhalimu, na kutangaza kuwa atakabiliana na kupambana vikali na kila aina ya madhihirisho ya dhulma na udikteta. Na kwa hakika ni kuwa na moyo wa kujitolea namna hiyo ndiko kunakoyapa kinga mataifa dhidi ya tamaa na uchu wa madola ya kikoloni na ngao inayozuia daima dawamu satua na ushawishi wa madola hayo. Wapenzi wasikilizaji ni hakika isiyo na shaka kwamba miongoni mwa matukio ya historia yenye ibra nyingi, mafunzo mengi na mazingatio makubwa ni tukio lenye kutikisa nyoyo la Ashura. Maombolezo ya Ashura huwa yanafanywa kwa madhumuni ya kulisimulia tena tukio hilo zito ili liwe ibra na mazingatio kwa hadhirina waliopo katika zama hizi na watakaokuja katika zama zijazo. Kwa mtazamo wa Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kuomboleza na kulia kutokana na masaibu yaliyowapata Ahlu bayt watoharifu alayhimus salam wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume ni neema anayojaaliwa mtu na Mwenyezi Mungu, ambayo inastahiki shukrani za mja kwa Mola wake. Ayatullah Khamenei amesema:"Kuna wakati mtu huwa hana neema, na kwa hivyo hawezi kuulizwa chochote kuhusu neema hiyo; lakini pale mtu anapokuwa na neema ndipo huulizwa. Moja ya neema kubwa kabisa ni neema ya kuleta kumbukumbu; yaani neema ya hizi majlisi za maombolezo, neema ya Muharram na neema ya Ashura kwa jamii yetu ya Kishia.... Neema hii na adhama yake hii, inaziunganisha nyoyo na chemchemi ya mchemko wa imani ya Kiislamu. Neema hii imefanya kazi katika kipindi chote cha historia, ambayo imewafanya madhalimu wanaotawala waihofu Ashura na kaburi la Imam Hussein (AS).

Wapenzi wasikilizaji, mapambano ya Karbala ni somo kwa historia ya zama zote na kwa wanadamu wote. Kuienzi na kuiadhimisha hamasa ile, kuiendeleza na kuidumisha katika nyoyo, ndiko kunakodhamini saada ya Waislamu na hata wapigania haki na uhuru wasiokuwa Waislamu, katika zama zote. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …