Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 12 Novemba 2013 16:09

Pamoja na Imam Hussein AS kutoka Madina hadi Karbala (5)

Pamoja na Imam Hussein AS kutoka Madina hadi Karbala (5)

Assalama Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi katika mfululizi wa makala hizi zinazokukieji katika siku hizi za maombolezo ya kuuawa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali (as). Ni matarajio yetu kwamba mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi chetu cha leo.  

XXX

Katika siku ya tarehe 10 Muharram yaani Ashuraa wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, Imam Hussein bin Ali (as) aliendelea kuwazindua watu na kuwatoa kwenye usingizi wa mghafala. Katika kipindi hicho kigumu Imam Hussein (as) hakusahau wajibu wake kama kiongozi na Imam wa jamii, kwa msingi huo aliwahutubia watu hao ambao nyoyo zao zilikuwa zimepatwa na kutu ya kupenda dunia na kumsahau Mwenyezi Mungu akisema: Enyi waja wa Allah! Mwogopeni Mwenyezi Mungu, kwa sababu dunia imeumbwa kwa ajili ya kuisha, mapya yake huchoka na kuchakaa, neema zake huisha na furaha yake huishia kwenye ghamu na majonzi…. Jichukulieni masurufu kwa ajili ya Akhera yenu, na masurufu bora zaidi ya Akhera ni takwa na uchamungu. Enyi watu! Msihadaike na dunia. Kwa sasa mmeungana katika jambo linalomkasirisha Mwenyezi Mungu na kwa sababu ya jambo hilo mmeghadhibikiwa na Allah SW…”

Katika sehemu hii ya hotuba yake Imam  Hussein (as) anazungumzia dunia ya kupita na kuweka wazi sababu za upotofu wa watu wa Kufa huko Iraq na kuwakumbusha kuwa, wameupa mgongo Uislamu, imana na Mola wao Muumba kwa ahadi na vitisho vya utawala wa Bani Umayyah; na matokeo yake wameamua kupigana vita dhidi ya mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Imam anajiarifisha na kuwapa nasaha watu waliokusanyika kwa ajili ya kupiga vita kizazi cha Mtume (saw). Anasema: Enyi watu! Tazameni mimi ni nani, kisha mujilaumu nyinyi wenyewe. Je, ni halali kwenu kuniua mimi na kunivunjia heshima? Je, mimi si mwana wa binti wa Mtume wenu? Je, mimi si mtoto wa wasii na binamu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu? Je, mimi si mwana wa mtu aliyemwamini Mwenyezi Mungu kabla ya Waislamu wote na kusadikisha utume wa Nabii Muhammad kabla ya watu wote? Je, Hamza, Bwana wa Mashahidi si ami ya baba yangu? Je, Jaafar Tayyar si ami yangu? Je, hamkusikia maneno ya Mtume wa Allah akisema kuwa: Hassan na Hussein ni mabwana wa vijana wa peponi? Na kama mnashuku maneno hayo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu je, hamjui kwamba mimi ni mwana wa binti wa Mtume wetu na kwamba hakuna mwana mwingine wa Mtume wa Allah zaidi yangu mimi? Ole wenu! Je, nimeua mtu wenu ili mutafute kisasi kwa kuniuna mimi? Je, nimekula mali ya mtu yeyote miongoni mwenu au kumdhuru yeyote ili nistahiki adhabu? …

Hoja na maneno hayo ya kimantiki ya Imam Hussein mbele ya jeshi la mtawala dhalimu Yazid bin Muawiya hayakubakisha kisingizio chochote kwa maadui hao wa Allah. Baada ya kusikia maneno hayo, mmoja wa viongozi wa jeshi la Yazid alimtaka Imam Hussein ambayi na kutoa mkono wa utiifu kwa Yazid ili aweze kunusuru nafsi na mali yake. Imam Hussein ambaye lengo lake kuu lilikuwa kunusu dini ya Allah hata kwa kusabilia nafsi na mali, alijibu kwa kusema: “Wallahi sitakupeni mkono wa utiifu kama wafanyavyo watu duni na dhalili, wala sitakimbia medani ya vita kama wanavyofanya watumwa.” 

XXX

Hotuba nyingine ya Imam Hussein (as) ilitolewa siku ya Ashuraa katika ardhi ya Karbala wakati majeshi ya pande mbili yalipokuwa tayari kwa ajili ya vita. Bendera ya jeshi la Yazid iliyokuwa imeshikwa na Umar bin Saad ilipeperushwa na sauti za ngoma na maturumbeta ya jeshi hilo zikaanza kusikika. Imam Hussein alitoka kwenye jeshi lake dogo na kusimama mbele ya safu za jeshi la Yazid na kuwataka watu wanyamaze kimya ili wapete kusikiliza maneno yake. Hata hivyo sauti ziliendelea kusikika. Imam aliwanyamazisha watu kwa kusema: Ole wenu! Kwa nini hamusikilizi maneno yanayowapa saada na ufanisi wa dunia na Akhera. Hakika kila atakayenifuata mimi ameongeka na anayenipinga na kunipiga vita ameangamia…..  Naam, Mumeasi na hamtaki kunisikiliza na Mwenyezi Mungu amepiga muhuri katika nyoyo zenu kutokana na hadia za haramu mulizopewa na vyakula visivyohalali mnivyojaza matumboni mwenu. Ole wenu! Hamuwezi kunyama?!

Baada ya watu kusikia maneno hayo walinyaza kimya na Imam Hussein akaendelea na hotuba yake. Baada ya kuwanasihi, kuwakumbusha na kuwaambia yatakayotokea baada ya kuuawa kwake na madhila makubwa na ukandamiza utakaofanywa na utawala wa Yazid bin Muawiya dhidi ya watu, Imam Hussein (as) aliinua mikono juu ya kuliombea dua mbaya jeshi la mtawala dhalimu akisema: Ewe Mola Mlezi! Wakatie neema ya mvua na uwaadhibu kwa miaka ya mashaka na machungu mengi … kwani watu hawa wametukadhibisha na kutuacha peke yetu mbele ya adui. Wewe ndiye Mola wetu Mlezi, kwako tunatawakali na marejeo yetu sote ni kwako wewe.”

Historia inasema kuwa baada ya kuuawa shahidi masahaba wengi wa Imam Hussein (as) jeshi la Yazid mal’uni lilianza kushambulia mahema ya watoto na wanawake. Wakati huu Imam alisema kwa sauti kubwa kwamba: “Enyi wafuasi wa kizazi cha Banii Umayyah! Kama hamna dini na hamuogopi Siku ya Malipo, basi kwa uchache kuweni watu huru na lindeni heshima yenu ya kibinadamu.”

Maneno hayo ya Imam Hussein kwa hakika yalikuwa na ujumbe mkubwa na azimio la wanadamu wote lililotangazwa kwa walimwengu kutoka katika medani ya Karbala.

Baada ya vita kali na ushujaa mkubwa, watu wa kizazi cha Mtume wa Allah na masahaba wa Imam Hussein (as) walianza kuuawa shahidi mmoja baada ya mwingine. Imam aliingia katika medani ya vita na kuanza kuua maadui wa Allah mmoja baada ya mwingine. Hata hivyo kutokana na kuzingirwa na jeshi dhalimu la Yazid na majeruhi mengi, Imam alianza kudhoofika na katika dakika za mwisho za uhai wake, Imam Hussein alifungua macho na kutazama mbinguni na kwa mara ya mwisho alinong’ona na Mola wake Muumba akisema: “Ewe Mola uliye juu ya kila kitu, shadidi wa ghadhabu na mwenye nguvu kuliko kila kitu. Ninastahamili mbele ya makadirio yako, ewe Mola ambaye hapasi kuabudiwa ila wewe. Mola wangu Mlezi unayepima watu kwa mujibu wa amali na matendo yao, hukumu baina yangu na watu hawa, kwani wewe ndiye mbora wa kutoa hukumu.

Kisha Imam alianguka chini na kuwepa kipaji chake juu ya ardhi huku akisema:

 

  "بِسْمِ اللّه وَ بِاللّه وَ فِى سَبیلِ اللّه وَ عَلى مِلَّةِ رَسُولِ اللّه ."

Kwa jina la Allah, na kwa kumkumbuka Allah na katika njia yake Allah na katika dini ya Mtume wa Allah.

 

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …