Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 03 Juni 2013 15:21

Nabii wa Rehma (Sehemu ya 20 na ya Mwisho)

Nabii wa Rehma (Sehemu ya 20 na ya Mwisho)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya 20 na ya mwisho ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi  yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Bila ya shaka wapenzi wasikilizaji mngali mnakumbuka kuwa mazungumzo yetu katika juma lililopita katika sehemu ya 19 ya mfululizo huu yaliishia katika kunukuu maneno ya George Bernard Shaw alipouelezea Uislamu kuwa ni dini pekee inayofaa kwa ajili ya zama zote za maisha ya mwanadamu na yenye uwezo wa kukivutia kila kizazi. Baada ya hayo Bernard Shaw anasema:" Mimi nimeyatalii vizuri maisha na kazi iliyofanywa na Muhammad; ninavyoamini mimi, yeye sio tu si mpinzani wa Masihi bali inapasa kumwita yeye muokozi wa wanadamu. Laiti mtu kama yeye angetawala katika zama za sasa angetumia suluhu na urafiki kwa ajili ya kutatua matatizo ya wanadamu. Yeye ni mtu mtukufu zaidi kuwepo katika ardhi. Aliwalingania wanadamu dini na kuasisi misingi ya ustaarabu. Alizirasimisha akhlaqi na kujenga jamii hai na imara ili kuyaweka mafundisho yake kwenye sura ya utekelezaji. Aliubadilisha kikamilifu na kwa hali ya kudumu ulimwengu wa fikra na tabia wa mwanadamu. Jina lake mtu huyu ni Muhammad. Alizaliwa Bara Arabu katika mwaka 570 miladia. Alianza kutangaza ujumbe wake wa kuwalingania watu dini sahihi ya Uislamu akiwa katika umri wa miaka arubaini na akaiga dunia alipotimia umri wa miaka sitini na tatu. Katika muda wa miaka 23 ya utume wake aliwaongoza watu katika kumwabudu Mungu mmoja. Aliwagomboa watu wa eneo la Hijazi kwa kuwatoa kwenye vita na mizozo ya kikabila na kuwafikisha kwenye umoja na mshikamano wa kitaifa. Aliwatoa watu kwenye uasherati na ulevi na kuwaelekeza kwenye taqwa na uwiyano wa matendo; aliwakuta na mfumo usio na kanuni wala sheria akawajengea mfumo wenye nidhamu na sheria zilizokamilika, na akawatoa kwenye hali ya upotofu na kuwaongoza kuelekea kwenye vipimo aali kabisa vya akhlaqi njema. Historia haijawahi katu kuona mageuzi kamili kama haya kufanywa na mtu mmoja, kabla ya Mtume wa Uislamu au baada yake"mwisho wa kumnukuu George Bernard Shaw.

Alphonse de Lamartine, mwanahistoria maarufu wa Kifaransa, yeye anahoji kwa kusema: "Kama ukubwa wa lengo, uhaba wa suhula na kupatikana tija ya kustaajabisha ni vigezo vitatu vya kupimia akili na uhodari wa mtu, kuna mtu gani anayeweza kuwalinganisha watu wakubwa wa historia ya wakati huu na Muhammad? Watu wenye majina yaliyotajika zaidi waliweza kuunda majeshi na kuasisi tawala kubwa kubwa tu. Kama hatutosema kwamba hayo waliyoyaasisi watu hao si lolote si chochote, basi inapasa tuseme kuwa walichoasisi wao ni nguvu za kimaada tu ambazo aghalabu yao kufumba na kufumbua tu zilisambaratika na kutoweka mbele ya macho yao. Lakini mtu huyu (anamkusudia Bwana Mtume) hakuleta sheria na utawala na umma wa watu tu bali aliwabadilisha kikamilifu mamilioni ya watu miongoni mwa wakaazi wa dunia hii. Na zaidi ya hayo aliyabadilisha madhabahu, miungu yao, dini, fikra, imani na nafsi za watu kutokana na Kitabu ambacho kila neno lake moja limekuwa ni sheria. Aliasisi utaifa wa kiroho uliojumuisha kila lugha na kila rangi. Subira yake kwa ajili ya kufikia ushindi, hima kubwa aliyokuwa nayo katika kueneza itikadi yake, sala za kiirfani na kunong'ona kwake kwa siri na Mwenyezi Mungu yote hayo ni ishara ya imani thabiti aliyokuwa nayo. Muhammad alikuwa mwalimu wa kidini, mrekebishaji wa jamii, kiongozi wa akhlaqi za kimaanawi, dhihirisho tukufu la usuhuba na uaminifu, mwenza mwema, mume mwenye mahaba na baba mwenye huba na mapenzi. Alikuwa na yote hayo pamoja. Hakuna mtu mwengine yeyote katika historia aliyemshinda yeye au kuwa sawa naye katika yoyote ile kati ya sifa hizi tofauti za maisha. Alikuwa ni shakhsia huyo tu mpenda watu aliyekuwa amekusanya pamoja sifa hizi za ukamilifu kwa namna isiyo na kifani".

Pierre-Simon Laplace, mwanafalaki na mwanahisabati mashuhuri wa Kifaransa wa karne ya 18 na 19 miladia anasema hivi:"Japokuwa mimi siamini dini za mbinguni lakini dini ya Muhammad (SAW) na mafundisho yake ni mfano wa kijamii kwa maisha ya mwanadamu. Kwa maana hiyo ninakiri kwamba kudhihiri kwa dini yake na hukumu zake zenye hekima, lilikuwa jambo kubwa na la thamani, na ni kwa sababu hii mwanadamu hatoacha kuwa na haja ya kuyakubali mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW)".

Wapenzi wasikilizaji, katika mfululizo wa sehemu 20 za kipindi hiki tumedondoa baadhi ya mitazamo ya wanafikra wa Magharibi ambayo inadhihirisha adhama ya shakhsia na nafasi isiyo na mbadala ya nabii wa rehma Muhammad SAW katika uongofu wa wanadamu mpaka Friedrich Max Müller, mwanafilolojia, mwandishi na Muorientalisti wa Kijerumani aliyepitisha karibu umri wake wote nchini Uingereza akafika hadi kusema kuwa: "Karibu Wakristo watafahamu kwamba Muhammad (SAW) alikuwa mmoja wa wasadikishaji wa dini na mafundisho ya Masihi. Wakati huo wataingiwa na fadhaa kwa sababu ya chuki na uadui walioufanya kwa jina la dini katika karne zilizopita."

Katika kuhatimisha mazungumzo yetu haya turejee sasa kwenye Kitabu Kitukufu cha Qur'ani ili kuona kinamzungumzia vipi nabii wa rehma Muhammad SAW. Aya ya 107 ya Suratul Anbiyaa inasema:"Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote."

Rehma, wapenzi wasikilizaji ni hurumana kuwafikishia kheri wanadamu na kuwaondolea shari na hatimaye kuwafikisha kwenye kheri na saada. Kwa maneno mengine ni kwamba rehma za Mwenyezi Mungu ni kubwa mno na zinavienea vitu vyote na viumbe vyote. Kwa maana hiyo basi ueneaji wa rehma zilizoashiriwa katika aya hii kuhusiana na nabii wa rehma Muhammad SAW ni mithili ya rehma zake Mola.

Naam wapenzi wasikilizaji na hadi hapa ndio tumefika mwisho wa safari yetu ya kudondoa yale yaliyosemwa kwa insafu na wasomi, waaandishi, wanafikra na wataalamu mbalimbali wenye hekima duniani hususan wa Ulimwengu wa Magharibi kuhusu Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni mimi msimulizi wenu Abdulfatah Mussa Iddi ambaye nilikuwa pamoja nanyi kwa muda wote wa safari hii ninayekuageni nikiwa na matumaini kuwa mumeelimika, mumefaidika na kunufaika kwa yale mliyoyasikia katika kipindi hiki.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …