Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 21 Mei 2013 16:42

Nabii wa Rehma (18)

Nabii wa Rehma (18)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya kumi na nane ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi  yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Bila ya shaka wapenzi wasikilizaji mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulizungumzia mitazamo ya Jean Brava, raia wa Ufaransa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki yaani Orientalisti kuhusu nabii wa rehma Muhammad SAW. Akiendelea kubainisha adhama ya Qur'ani tukufu Brava anasema licha ya Waarabu kuwa na fasihi maarufu, mila na utamaduni mkongwe, na historia ndefu ya utungaji mashairi hawakuweza kuleta hata jumla na sentensi moja yenye muundo na muhtawa unaofanana na wa sura au hata aya moja ya Qur'ani."

Katika kitabu chake alichoandika kuhusu Bwana Mtume Muhammad SAW, mwandishi huyo wa habari wa Kifaransa ametumia maneno na misamiati ya kuvutia kumzungumzia nabii huyo wa rehma na anasema:"Mtume wa Mwenyezi Mungu ni kiongozi mkuu na mlezi wa wote, na yeye ni shakhsia mwenye irada huru. Lakini yeye ni mfuataji wa wahyi wa Mwenyezi Mungu ambao ulikuwa ukiteremshwa kwake kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya maslaha, kheri, saada na mshikamano wa watu. Licha ya nguvu na mamlaka yote aliyokuwa nayo, Mtume alikuwa msamehevu mno katika maisha yake, na alisamehe na kufumbia macho adha na maudhi waliyomfanyia watu wa Makka na wa maeneo ya kandokando yake."

Katika kuzungumzia sifa ya usamehevu ya Bwana Mtume, Jean Brava anasimulia mfano mwengine wa suala hilo kwa kuandika hivi:"Siku moja Mtume alikuwa amefua kanzu yake na kuianika juani, kisha akajipumzisha chini ya mti na usingizi ukamchukua. Mmoja wa maadui zake aliyekuwa akiitwa Athur aliitumia fursa hiyo ya kumwona Mtume yuko peke yake akamfuata ili kumshambulia. Huku akiwa ameinua upanga wake juu alimwamsha Mtume na kumwambia:" Ewe Muhammad! Ni nani sasa anayeweza kukuokoa? Katika hali ya utulivu kamili Mtume alimjibu kwa kumwambia:"Allah". Jibu hilo la Mtume liliutetemesha mkono wa Athur, na upanga aliokuwa ameushikilia mkononi mwake ukamponyoka na kuanguka chini. Mtume aliuokota upanga huo na kumuelekezea Athur huku akimuuliza:" Ni nani sasa atakayeweza kukuokoa wewe kutokana na mimi? Jibu la Athur lilikuwa hili:"Ni usamehevu na msamaha wako". Mtume alimsamehe kumuua Athur, na kwa hatua yake hiyo akamfunza adui yake huyo somo kubwa na bora kabisa la kuwa na moyo wa kusamehe".

Jean Brava anawashangaa na kuwakosoa wale waandishi wanaomtuhumu nabii wa rehma Muhammad SAW kwamba alikuwa mtu mpenda vita. Analizungumzia hilo kwa kuandika hivi:"Muhammad hakuwa mtu mwenye kujuzisha mambo yanayokinzana na akhlaqi njema. Lengo kuu zaidi la Muhammad lilikuwa ni kutangaza na kufikisha ujumbe wake kwa watu wote ulimwenguni. Mazonge ya kifamilia na mashughuliko ya masuala ya maisha hayakumzuia kutekeleza wajibu wa kufikisha risala na ujumbe huo. Japokuwa Makureishi na watu wa Makka walianzisha uadui dhidi yake, wakapanga na kula njama ya kumpiga vita kwa kuyashawishi na kuyahamasisha makabila yote yaungane nao katika vita hivyo lakini pamoja na hayo hakuamua kupigana nao vita tokea mwanzo, na wala hakuamua kutoa jibu la uadui kwa uadui aliotendewa! Ilikuwa ni baada ya uadui na uchokozi huo kurudiwa tena na tena ndipo ulipoteremka wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba sasa ni ruhusa kwako kupigana vita na watu wanaokufanyia uadui na uchokozi. Wahyi huo ulisema hivi:"Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu!

Katika sehemu nyengine ya kitabu chake, Jean Brava anazungumzia sifa za dini tukufu ya Uislamu na sababu za kuenea kwake kwa kuandika hivi:"Mafundisho ya Uislamu ni mepesi na sahali, na wala hamna ndani ya mafundisho hayo kitu kinachopingana na akili, elimu na mantiki. Uislamu unatilia mkazo utekelezaji Sala kwa sura ya jamaa ili kudumisha mshikamano na umoja wa jamii. Katika mafundisho ya dini ya Muhammad watu walikuwa ndugu, na utawala wa Kiislamu uliasisiwa juu ya msingi wa uadilifu, usawa wa matendo na uhuru wa mtu. Wasio Waislamu pia waliishi chini ya hifadhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika hali kamili ya amani, salama na utulivu. Watu hao walikuwa huru kufuata itikadi na imani za dini zao na wakadhaminiwa na kupewa hakikisho na Waislamu juu ya suala hilo, na wakachanganyika nao katika majonzi na furaha yao"... Jean Brava anaongeza kwa kusema kuwa "Mwenyezi Mungu alitaka utawala wa kwanza wa Kiislamu uasisiwe na Mtume wake".

Kwa mtazamo wa mwandishi huyo wa Kifaransa Mwenyezi Mungu alimpa izza Mtume wake. Jina lake limeadhimishwa na kutukuzwa kwa namna ambayo linajulikana na kutambulika duniani kote. Jean Brava anasema, Muhammad alikuwa Mtume mkubwa, mtekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu, mtawala muadilifu, mzungumzaji mahiri na jemedari mweledi na mwenye hadhi ya juu. Hata kama hakuwahi kuingia kwenye chuo kikuu chochote cha Rumi wala madrasa yoyote ile ya elimu ya Uajemi lakini pamoja na hayo jina lake limetukuka kwa namna ambayo hakuna mtu yeyote katika jamii ya Waarabu aliyepata umaarufu na umashuhuri kama wake.

Naam wapenzi wasikilizaji, maneno haya ya Jean Brava, Muorientalisti wa Kifaransa ndiyo yanayotukamilishia sehemu hii ya 18 ya kipindi hiki cha "Yaliyosemwa na Wenye Hekima Kuhusu Nabii wa Rehma". Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola nakuageni kutoka hapa studio huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …