Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 13 Mei 2013 13:50

Nabii wa Rehma (17)

Nabii wa Rehma (17)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya kumi na saba ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi  yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Mtume Mtukufu wa Uislamu ndiye shakhsia wa juu kabisa katika historia ya wanadamu. Jukumu la kuwaongoza watu kuelekea kwenye kheri na saada lilikuwa kubwa na zito mno, na kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu aliamua kumbebesha jukumu hilo mja wake huyo bora kabisa na mteule, naye Nabii Muhammad SAW akalibeba na kulitekeleza kwa ufanisi. Kwa mafunzo yake ya kumjenga mwanadamu, Bwana Mtume SAW aliukomboa ulimwengu na kuuangazia mwanga wa uongofu. Na kwa hakika watu wenye hekima, wanafikra na wasomi wa fani na taaluma mbalimbali wana uwezo zaidi kuliko watu wengine wa kudiriki na kutambua mchango na nafasi isiyo na mbadala ya shakhsia huyo adhimu katika kuwaongoza wanadamu na kuwafikisha kwenye saada.

Jean Brava, raia wa Ufaransa ni mtaalamu mashuhuri wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki yaani Orientalisti aliyezaliwa mwaka 1907. Baada ya kuhitimu masomo yake Jean Brava alichagua kazi ya uandishi wa habari za magazeti na akafanya safari katika nchi nyingi duniani. Kutokana na shauku aliyokuwa nayo ya kulizuru kaburi tukufu la nabii wa rehma Muhammad SAW huko Madina, mnamo mwaka 1966 alifanya safari kuelekea Makka na kushiriki kwa kujionea kwa karibu jinsi Waislamu walivyokuwa wakitekeleza faradhi ya ibada ya Hijja. Jean Brava ameandika vitabu vingi kuhusu Uislamu na shakhsia wa dini hiyo tukufu, na moja ya vitabu vyake ni kile kinachozungumzia shakhsia ya Bwana Mtume Muhammad SAW ambacho kimetarjumiwa pia kwa lugha ya Kiarabu. Katika faslu ya kwanza ya kitabu chake hicho Jean Bravaameandika hivi:

"Ardhi, ambayo sisi tunaishi ndani yake ni mahala pa maonyesho makubwa, ambapo katika kila zama na kwa irada ya Mwenyezi Mungu hushuhudiwa humo maonyesho ya kuajabiwa na kustaajabisha mno. Baadhi ya maonyesho hayo hudumu na kubakia milele katika ardhi, na baadhi yao, kama ulivyo usingizi, ni ya kupita na kumalizika haraka na wala hayabakishi athari yoyote nyuma yao. Onyesho la kudumu zaidi na lenye adhama kubwa zaidi lililoshuhudiwa katika ardhi ni lile lililoonyeshwa na Waislamu katikati ya karne ya saba miladia kwa kudhihiri Muhammad (SAW)."

Nabii wa rehma Muhammad al Mustafa SAW ni mithili ya kioo chenye kuakisi mazuri yote na mema yote. Na hilo ndilo jambo la kwanza kabisa analolikiri Jean Brava yeye anausifu mwenendo, tabia na akhlaqi za Bwana Mtume kwa kusema:" Akhlaqi za Muhammad (SAW) zilikuwa hazina mfano; alikuwa na huruma na mapenzi makubwa na mafakiri, wanyonge na watoto mayatima. Alikuwa na mazoea nao makubwa, na akiwaondolea shida zao na kukimu mahitaji yao. Muhammad alikuwa karibu na moyo wa kila mtu. Kila mara tabasamu lilionekana midomoni mwake na maneno matamu na ya murua yalitoka kinywani mwake. Hakujilimbikizia kitu chochote kwa ajili ya yeye mwenyewe bali kila alichopata alikitoa kuwagaia wengine. Hakuwa mpenda kusema sana, na alikuwa mtu mwenye muamana, kiasi kwamba ni nadra kuweza kumpata mtu mwenye muamana na mwaminifu mfano wake".

Kwa mtazamo wa Jean Brava sifa mahususi na ya kipekee inayompambanua Mtume wa Allah na shakhsia wengine wakubwa katika historia ni kujiweka mbali kwake na tabia ya uimla, na ulafi wa nguvu na uchu wa madaraka. Analizungumzia suala hilo kwa kuandika hivi:" Katika kuasisi utawala wa Kiislamu, Mtume katu hakuwa na nia ya kutaka kujipatia cheo na ukubwa wa madaraka wala kuishi maisha ya raha, starehe na anasa. Alichokuwa akitaka ni kuunda utawala wa kiutu na wa kiadilifu ambao ndani yake hatoabudiwa yeyote au kitu chochote ghairi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; na katika kumwabudu na kumtukuza Yeye Mola, mwanadamu hatomshirikisha na mtu au kitu chochote kile. Huo ni utawala ambao chini ya kivuli chake, haki za mataifa yote zitachungwa na kuheshimiwa kwa usawa; na kwa kudhamini uhuru wa mtu, yataweza kupatikana mazingira ya watu wote kuwa na maisha mazuri na ya salama. Aliandaa ratiba aali ya maisha na kuasisi sheria na utawala mkuu kwa ajili ya watu wa jamii zilizotawanyika za Waarabu, ambao kwa muda wa karne kadhaa walikuwa wamepoteza umoja na mshikamano baina yao. Ndani ya utawala huo Waislamu walipata nusra na ushindi wa mtawalia kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na kumiminikiwa na ghanima na ngawira chungu nzima. Lakini pamoja na hayo na licha ya Mtume kuwa mshika hatamu kuu za utawala, tabia yake haikubadilika hata chembe bali aliendelea kuishi maisha ya chini na ya kawaida ya kuvumilia tabu na shida za maisha".

Jean Brava anasema, kauli za kifedhuli na matamshi ya matusi yanayotolewa na watu wajinga na wasio na uelewa hayalaiki wala hayastahiki kuelekezwa kwa shakhsia ya Mtume ambaye alikuwa mtu mwenye roho teule na moyo uliotukuka. Analizungumzia suala hilo kwa kuandika hivi:"Inatupasa tukumbuke kuwa Muhammad (SAW) katu hakuwa akidai kuwa ana sifa za ajabu za kimaumbile kinyume na mwanadamu wa kawaida. Alikuwa ni mtu anayeteremshiwa wahyi. Wakati watu wa Makka walipokuwa wakimtaka awaonyeshe miujiza alikuwa akiwaambia muujiza wake yeye ni wahyi wa mbinguni anaoupokea kwa lugha fasaha ya Kiarabu na ambao anautangaza kwa watu wote katika sura hiyo ya Qur'ani isiyo na kifani. Jean Brava anaendelea kusema kuwa Muhammad (SAW) alikuwa akijua kwamba yeye ni wasita na kiunganishi cha kupokea wahyi, na pale watu wake walipomtaka athibitishe ukweli wa ujumbe wake kwa kuwaletea miujiza aliteremshiwa wahyi usemao:"  Sema: Wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur'ani basi (hawawezi) kuleta mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao."

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kukomea hapa na kukuageni hadi juma lijalo inshallah tutakapokutana tena katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …