Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 06 Mei 2013 14:05

Nabii wa Rehma (16) + Sauti

Nabii wa Rehma (16) + Sauti

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya 16 ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi  yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Katika kipindi chetu cha leo tutatupia jicho fikra na mitazamo ya mwandishi na mtafiti ambaye awali alikuwa na chuki kubwa na Mtume wa Uislamu na hata akaandika makala kadha wa kadha dhidi ya Uislamu na nabii huyo wa rehma. Lakini kwa kuwa sifa anazopaswa kuwa nazo mtafiti wa kweli ni kufanya upembuzi na kutafuta ukweli, uchunguzi wa kina uliofanywa na mtafiti huyo ulikuwa sababu ya yeye kuangaziwa na mwanga mpya ambao hatimaye ulimwezesha kubaini na kutambua makosa yake kuhusiana na Mtume wa Uislamu.

François-Marie Arouet, maarufu kwa jina la Voltaire, ni mwandishi, mwanahistoria na mwanafalsafa wa Kifaransa aliyezaliwa mwaka 1694 na kuaga dunia mwaka 1778. Kutokana na kuathiriwa na propaganda chafu na hasi na simulizi za kutunga za wahubiri wa Kikristo wa zama za Karne za Kati kwa kimombo Middle Ages, mwanzoni Voltaire alikuwa akitumia lugha mbaya na isiyostahiki dhidi ya Uislamu na Bwana Mtume Muhammad SAW katika uandishi wake. Katika tamthilia yake iitwayo: "Fanaticism, or Muhammad" yaani "Ukereketwa Sugu au Muhammad" ambayo ni athari yake ya kwanza kuhusu Uislamu Voltaire aliandika visa na ngano za kubuni na kumnasibishia nazo Nabii Muhammad SAW. Alitumia muda wa miaka minne kuandika tamthilia hiyo lakini aliupuuza na kuufumbia macho ukweli wa wazi kabisa wa historia. Ni kama alivyosema Napoeleone kwamba:" Voltaire ameifanyia usaliti historia na dhamiri ya wanadamu, kwa sababu amezikana sifa njema za Muhammad na kumnasibishia mambo yasiyostahiki shakhsia adhimu ambaye aliwaangazishia walimwengu mwanga wa mbinguni.

Pamoja na kuandika tamthilia hiyo ya "Fanaticism, or Muhammad" lakini kila mara Voltaire alikuwa akiwaza akilini mwake na kujiuliza kwamba ni nini siri ya kuenea mno Uislamu, na ilikuwaje wafuasi wa Muhammad wakaweza kupata mafanikio kiasi hiki ya ustaarabu na maendeleo ya elimu? Katika kutafuta majibu ya masuali yake hayo Voltaire alianza kufanya utafiti wa kina kuhusu Uislamu na nabii wake wa rehma Muhammad SAW kiasi kwamba ufahamu aliopata kuhusu Bwana Mtume kutokana na utafiti aliofanya haukufanana hata chembe na ule aliouakisi kwenye tamthilia yake. Kutokana na mabadiliko yaliyojiri ndani ya nafsi yake alibaini kuwa kinyume na tuhuma za makasisi na wahubiri wa Kanisa, sio tu dini ya Muhammad haikutokana na shetani wala haikinzani na mantiki na akili, bali inakaribiana sana na dini ya Ukristo, na kwa mtazamo wa kihistoria imekamilika zaidi kuliko Ukristo. Voltaire anasema:" Muhammad (SAW) amebainisha maana ya Uungu inayojipambanua na Utatu wa Ukristo, na katika kumtambua Mwenyezi Mungu ina hoja imara na zenye nguvu zaidi." Suala jengine kwa mtazamo wa Voltaire ni nafasi ya juu ya kielimu na kimaanawi waliyokuwa nayo Waislamu wa karne za mwanzoni mwa Uislamu kuwapita Wakristo. Utangulizi wa Tarjumi ya Qur'ani iliyoandikwa na George Sale ndio ushahidi muhimu zaidi alioutumia Voltaire kujengea hoja yake juu ya suala hilo.

Katika faslu kamili ya tarjumi yake hiyo, George Sale, Muorientalisti raia wa Uingereza, aliyezaliwa mwaka 1697 na kufariki dunia mwaka 1736 amezungumzia dini, mila na desturi mbalimbali za Waarabu kabla ya Uislamu. Mtazamo wake juu ya suala hilo ni wa kiutafiti, na kutokana na kuathiriwa na kitabu hicho, Voltaire alitalii masuala yanayohusu ujengekaji wa Uislamu moja baada ya jengine, na akabainisha natija aliyofikia kwa kuandika hivi:"Haijawahi kutokea wakati wowote kushuhudiwa sanaa yoyote iliyokamilika katika kaumu ya Mayahudi, lakini katika karne zilezile za mwanzoni mwa Uislamu, Waislamu walikuwa walimu kwa watu wa Ulaya katika elimu na taaluma zote za zama zile". Voltaire anaendelea kuandika kama ninavyonukuu:"Katika zama za ushenzi na ujinga, na baada ya kuanguka ufalme wa Rumi, Wakristo walijifunza kila kitu kwa Waislamu kama vile Unajimu, Kemia, Utabibu, Hisabati na mengineyo na waliwaelekea wao tokea zama hizo." Kisha anaendelea kuwakosoa vikali waandishi wa Kikristo kwamba kwa nini wameunyamazia kimya ukomboaji wa ardhi uliofanywa na Waislamu pamoja na maendeleo yao ya kimaanawi na kielimu na kusema kama ninavyonukuu tena:"Mimi ninachukizwa mno na taasubi za kijinga za Wakristo walioshindwa na wanahistoria wasio na hoja ambao wameupindua ukweli wa historia na kumnasibishia Muhammad chungu ya tuhuma zisizostahiki".

Mwaka 1763 ulikuwa mwaka wa mageuzi makubwa na muhimu zaidi ya kifikra kwa Voltaire. Katika mwaka huo, hatimaye taswira mpya ya nabii wa rehma Muhammad SAW pamoja na wafuasi wake ilijengeka ndani ya akili ya mwandishi huyo. Baada ya miaka hamsini ya maisha ya uhakiki na utafiti wa historia, kutokana na kubainikiwa na haki na ukweli Voltaire aliandika haya yafuatayo:"Bila ya shaka yoyote Muhammad alikuwa mtu mkubwa mno, na aliandaa pia watu wakubwa waliokulia kwenye mafunzo yake ya fadhila na sifa za ukamilifu. Alikuwa mtungaji sheria mwenye hekima, kiongozi mweza na mwadilifu, mtume mchajiMungu na mleta mapinduzi makubwa zaidi katika ardhi."

Athari ya kwanza ya maandishi ya Voltaire na ambayo ina maelezo wadhiha na ya wazi kabisa ya kuutetea Uislamu na Qur'ani inaitwa "Sharia za Mtu Mtukufu". Katika kitabu hicho Voltaire ameandika kuwa dini zote nyengine zimeenea katika ardhi kwa kutumia njia za ulaghai wa maneno na kuwahadaa watu wa kawaida isipokuwa dini ya Uislamu ambayo kati ya dini zote walizokuja nazo watu inaonekana kuwa ndio pekee ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu baada ya kupita karne kadhaa sheria zake zingali zinatekelezwa ulimwenguni kote. Voltaire anasema:"Tauhidi ya kifitra na kimaumbile, ni mama wa dini zote zilizoko ardhini". Kwa mtazamo wa mwanafikra huyo wafuasi wa Uislamu wako karibu zaidi na tauhidi ya kimaumbile ikilinganishwa na wafuasi wa dini nyenginezo. Huko nyuma Voltaire alikuwa anakubaliana na wahubiri wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu mpaka kwamba wafuasi wa nabii wa rehma Muhammad SAW ni kizazi cha watu majahili na wajinga lakini hatimaye dhamiri ya nafsi yake ikawa inamsakama na kumsuta kila alipokumbuka kuwa kutokana na kuathiriwa na wahubiri hao wa Kikristo kuna wakati aliwahi kutengeneza tamthilia ya kuunasibisha Ukereketwa Sugu yaani Fanaticism na Bwana Mtume SAW. Kwa sababu hiyo mnamo mwaka 1748 aliamua kuchapisha tamthilia yenye utangulizi mrefu na kujaribu kwa njia hiyo kufidia makosa aliyofanya huko nyuma. Katika barua moja aliyomwandikia rafiki yake, Voltaire anasema hivi:"Mimi nilimtendea vibaya sana Muhammad", na kwa sababu hiyo baada ya hapo na kuendelea kitu pekee kilichoishughulisha zaidi fikra na akili ya mwandishi na mwanafalsafa huyo maarufu wa Kifaransa ilikuwa ni kuutetea Uislamu na kumuarifisha na kumtangaza nabii wa rehma Muhammad SAW kama mtu safi zaidi kati ya wanadamu wote aliyekuja na hidaya na tunu adhimu kwa ajili ya maisha ya watu.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 16 ya kipindi hiki cha "Yaliyosemwa na Wenye Hekima Kuhusu Nabii wa Rehma" imefikia tamati. Basi hadi hadi siku nyengine na katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki panapo majaaliwa ya Mola nakuageni kutoka hapa studio huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …