Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 28 Aprili 2013 17:56

Nabii wa Rehma (15) + Sauti

Nabii wa Rehma (15) + Sauti

(Sikiliza)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo. Nakukaribisheni kwa furaha na moyo mkunjufu kujiunga nami katika sehemu hii ya 15 ya kipindi hiki  kinachodondoa yale yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Nakutafadhalisheni muendelee kuwa nami hadi mwisho wa kipindi chetu kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Bila ya shaka wapenzi wasikilizaji mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulidondoa baadhi ya faslu za kitabu kiitwacho: "Muhammad: His Life Based on the Earliest Sources", yaani "Muhammad: Maisha Yake Kwa Mujibu wa Marejeo ya Kale" kilichoandikwa na Martin Lings mwanafikra na mwandishi raia wa Uingereza. Katika kitabu chake hicho Lings anaizungumzia shakhsia halisi ya nabii wa rehma Muhammad SAW kwa kutumia vionjo maalumu vya sanaa na vielelezo sahihi vya historia; na kwa ushujaa wa kielimu na udhati wa moyo wake anadhihirisha ukubwa wa mapenzi na heshima maalumu anayompa Mtume huyo mteule wa Allah. Wakati watu mbalimbali wanaposoma kisa cha maisha ya Bwana Mtume katika kitabu hicho cha Martin Lings hupatwa na mguso wenye taathira kubwa mno. Ndani ya kitabu hicho, Lings anatilia mkazo nukta kwamba nuru ing'aayo ya Mtume wa Uislamu ambayo Mwenyezi Mungu ameileta iuangazie ulimwengu haina mpaka wa zama bali ni ya kudumu na ya kuendelea. Sambamba na kukosoa dini mpya zinazobuniwa katika zama hizi, anautaja mchango wenye taathira wa dini kuu za mbinguni na kumtaja Nabii Isa AS na Bwana Mtume Muhammad SAW kuwa ni shakhsia wakubwa kabisa wa dini hizo.

Katika kuzungumzia sababu za kutusiwa na kuvunjiwa heshima shakhsia ya Bwana Mtume, Martin Lings anayejulikana pia kama Abu Bakr Siraj Ad-Din anasema suala hilo linahusiana na silsili ya jadi yake Mtume na kuandika kuwa, Mayahudi walikuwa wakisubiri kwa hamu na shauku kubwa kudhihiri nabii aliyeahidiwa kwa matarajio kwamba asaa wataweza kurejesha hadhi na heshima waliyokuwa nayo huko nyuma katika ardhi ya Yathrib. Lakini walichoshuhudia kwa mastaajabu na mshangao mkubwa ni kuwa nabii huyo aliyebaathiwa kuja kufikisha ujumbe wa Mungu mmoja hakutoka kwenye kizazi cha Is-haq bali alitokana na kizazi cha Ismail. Bila ya shaka mafanikio aliyopata mtukufu huyo, anaendelea kuandika Lings, yalitokana na taufiki ya Mwenyezi Mungu. Mayahudi walipatwa na hofu na kiwewe cha kukubali kwamba Muhammad ndiye huyo nabii aliyeahidiwa, na kwa sababu hiyo wakawa wanauonea husuda umati wake. Walikuwa wakitamani kila mara asiwe na sifa anazokuwa nazo mtume wa kweli. Na kwa sababu hiyo wakawa kila mara wakimtaka awaletee miujiza na kutaraji kuwa atashindwa kufanya hivyo.

Katika kuzungumzia miujiza ya nabii wa rehma Muhammad SAW Martin Lings ameandika hivi:" Mtume alikuwa na miujiza kadha wa kadha. Mara moja viongozi wa Makureishi walimtaka athibitishe ukweli wa utume wake kwa kuufanya mwezi upasuke katikati na kugawika sehemu mbili. Mtume aliwatekelezea takwa lao lakini sio tu waliuelezea muujiza huo kuwa ni mazingaombwe bali walidai pia kwamba Mtume amewazuga na kuwaroga kwa uchawi wake. Lings anakumbusha kuwa licha ya Mtume kuwa na miujiza ya aina kwa aina hakuifanya miujiza hiyo kuwa mhimili mkuu wa utume wake. Kwani muujiza wake mkubwa zaidi ulikuwa ni Kitabu cha wahyi kilichokuwa muujiza wake mkuu na dira ya mwongozo wa mbinguni wa kuwaelekeza watu wa zama zote kwenye njia ya uongofu.

Dakta Lings anaielezea shakhsia na ujudi wa Mtume Mtukufu wa Uislamu kuwa ni jambo la asili na la kudumu na kuandika kama ninavyomnukuu:"Ni jambo lenye asili kwa sababu limetokana moja kwa moja na asili au chemchemi, ikiwa ni mithili ya maji safi na halisi ambayo hayaathiriwi na kitu chochote cha kuyafanya yachache au kuharibika. Hii ni kwa sababu Mtume ana mfungamano zaidi na wahyi kuliko kitu kingine chochote kile. Anatafautiana na watu wengine kwa namna ya kustaajabisha kabisa na wakati huohuo amebeba ujumbe wa uongofu. Na sababu ni kwamba anayoyasema yanatoka kwenye dhati moja ya Mungu mmoja. Katika kitabu chake hicho kiitwacho: "Muhammad: Maisha Yake Kwa Mujibu wa Marejeo ya Kale" Martin Lings anasimulia na kuzungumzia sira na mwenendo wa Bwana Mtume na kusema kuwa, wakati mtu anapopiga mbizi kwenye bahari ya Irfani ya Kiislamu na mafundisho ya kidini ya Mtume huweza kuchuma ua kwenye bustani za kupendeza, zenye manukato ya kuvutia na zilizostawi kwa maua ya maneno yake ya hekima. Mfano wake ni haya maneno ya kuvutia yasemayo:"Tafuteni elimu hata kama ni (kwa kwenda) China".

Kwa mtazamo wa Martin Lings moja ya hidaya muhimu zaidi za Bwana Mtume kwa wanadamu ni bishara aliyowapa ya kuwepo muslihi mkuu yaani mrekebishaji wa ulimwengu. Anaielezea nukta hiyo kwa kuandika hivi:" Sehemu kubwa ya jamii ya wanadamu imefikia kwenye kiwango cha juu kabisa cha ukomo wa kupotoka kwa namna inayoiwiya vigumu kupiga hatua mbele zaidi ya hapo. Hata hivyo upotokaji huu hautoenea kote. Kwa sababu kwa ujumla wake ulimwengu ni kitu kitakatifu. Haiwezekani kutasawari na kudhani kwamba Mwenyezi Mungu atauacha ulimwengu kama ulivyo. Mtume alitabiri kuwa licha ya machafu yatakayokuwepo katika akhiri-zaman atatokea muokozi ambaye watu wanamtaja kwa jina la Mahdi. Muslihi mkuu huyu bila ya shaka yoyote atakuja tu."

Wapenzi wasikilizaji, Martin Lings au Abu Bakr Siraj Ad-Din, alikuwa mwandishi asiyechoka ambaye aliendelea kuandika mpaka kwenye umri wa miaka 97, yaani mwezi mmoja tu kabla ya kufariki kwake. Wasomi na wanafikra wengi wamemuelezea Martin Lings raia wa Uingereza kama mtaalamu mkubwa wa masuala ya Metafizikia, na wataalamu wengine wa masuala ya sanaa wamemtaja yeye kuwa ni malenga na mshairi wa daraja ya kwanza. Amma kwa mtazamo wa wanafunzi wake wa karibu jina la Martin Lings linawakumbusha zaidi vitu viwili: Uzuri na utajo wa Mwenyezi Mungu. Mapenzi aliyokuwa nayo kwa uzuri yalimfanya aamue kujitengezea kibustani kizuri mno cha mimea na maua ya kupendeza kwenye ua wa nyumba yake iliyoko mjini Westerham, Kent, na wakati Lings alipoaga dunia mnamo mwezi Mei mwaka 2005, mwili wake ulizikwa kwenye bustani yake hiyo. Mwandishi huyu aliyekuwa na heshima na mapenzi makubwa kwa nabii wa rehma Muhammad SAW amehitimisha uandishi wa kitabu chake cha: "Muhammad: Maisha Yake Kwa Mujibu wa Marejeo ya Kale" kwa aya ya 56 ya Suratul Ahzab isemayo:" Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlioamini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu".

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kukomea hapa kwa leo na kukuageni hadi juma lijalo inshallah tutakapokutana tena katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …