Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 22 Aprili 2013 14:30

Nabii wa Rehma (14)

Nabii wa Rehma (14)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo. Nakukaribisheni kwa furaha na moyo mkunjufu kujiunga nami katika sehemu hii ya 14 ya kipindi hiki  kinachodondoa yale yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Nakutafadhalisheni muendelee kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Wataalamu mbalimbali wanaofanya utafiti na uhakiki kuhusu maisha ya Mitume wa Mwenyezi Mungu kwa kawaida hukabiliwa na suali hili, kwamba watu hawa wana tofauti gani na wanadamu wengine, na ni sababu gani imezifanya shakhsia zao zidumu na kubakia milele katika zama zote za historia? Watafiti hao huwa wanawaza akilini mwao kwamba ni kwa nini licha ya kupita zaidi ya karne 14 tangu zama alipodhihiri Mtume wa Uislamu, nyota ya mtukufu huyo duniani inazidi kung'ara na kuvutia umati mkubwa zaidi wa watu siku baada ya siku? Mvuto wa Nabii Muhammad SAW ni mkubwa na wa ajabu kiasi kwamba mwandishi mmoja wa Magharibi mwenye kiu ya kujua ukweli aliamua kufanya utafiti na uhakiki kuhusu maisha ya mtukufu huyo, na kutokana na mapenzi na mvuto aliopata juu ya akhlaqi na tabia yake iliyotukuka aliamua kuandika kitabu alichokipa jina la "Muhammad: His Life Based on the Earliest Sources", yaani "Muhammad: Maisha Yake Kwa Mujibu wa Marejeo ya Kale". Akijibu suali kwamba kwa nini majina ya Mitume yanabakia milele katika historia, mwandishi huyo wa Magharibi anasema:"Ni kutokana na irada ya Mwenyezi Mungu tu ndio maana hakika za kudumu na zenye taathira huendelea kubaki, na kuna siri zilizojificha kuhusiana na kuendelea kubaki kwao."

Kitabu kiitwacho: "Muhammad: Maisha Yake Kwa Mujibu wa Marejeo ya Kale", kiliandikwa na Martin Lings na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1983, na hadi sasa kimeshachapishwa tena mara zisizopungua sita. Katika faslu ya kwanza ya kitabu chake, Martin Lings anaashiria nasaba ya jadi ya Mtume ambayo watu wake wote walikuwa wafuasi wa imani ya tauhidi na kuandika hivi:" Katika Kitabu cha Kwanza cha Agano la Kale yaani Genesis au Mwanzo imeelezwa kuwa Ibrahim alikuwa hana mtoto, na hakuwa na matumaini moyoni mwake mpaka usiku mmoja Mwenyezi Mungu akamtaka atoke nje ya hema lake na kumwambia: Sasa tizama mbinguni uzihesabu nyota kama utaweza kuzihesabu! Kisha huku Ibrahim akiwa anaziangalia nyota akasikia tena sauti hiyo ikimwambia: kizazi chako wewe kitakuwa kama hivi (kisichohesabika)".

Kisha Lings anaendelea kusema: Hivi ndivyo taqdiri ilivyokuwa, kwamba si umma mmoja bali ni umma mbili kubwa na nyenzo mbili za uongofu, zitokane na kizazi cha Ibrahim kwa ajili ya kuthibiti irada ya Mwenyezi Mungu. Ibrahim akawa chemchemi ya mikondo miwili ya umaanawi, dini mbili, maduara mawili na vitovu viwili. Kitovu cha moja ya mikondo hii miwili kilianzia kwa Amina. Yeye alikuwa na habari za nuru iliyokuwemo ndani ya batini yake. Siku moja aliisikia sauti ikimwambia: Wewe umebeba ndani ya fuko lako la uzazi bwana wa watu hawa, wakati mwanao atakapozaliwa sema ninamkinga kwa Mwenyezi Mungu na shari ya mahasidi, kisha mpe jina la Muhammad".

Martin Lings, ambaye ni Muingereza, alizaliwa mwaka 1909 na kuaga dunia mwaka 2005. Awali alikuwa mkristo wa madhehebu ya Kiprotestanti. Kama walivyokuwa aghalabu ya vijana wa rika lake wakati huo, Martin Lings aliacha kuwa na imani ya Ukristo katika umri wa takribani miaka 20, lakini hakuacha kuendelea kutafuta hakika na ukweli. Katika umri wa miaka 25 alianza kufanya utafiti kuhusu dini mbalimbali duniani na hatimaye akaamua kufuata Uislamu na kuchagua jina la Abu Bakr Siraj Ad-Din. Wakati Lings alipokuwa akisoma athari za René Guénon, mwanafalsafa wa Magharibi raia wa Ufaransa ambaye naye pia baadaye alisilimu alibaini hakika kwamba dini za mbinguni ni dini za kweli na zinao uwezo wa kuongoza kwenye njia ya kumfikisha mja kwenye ukamilifu wa utu na kumfikia Mwenyezi Mungu.

Katika kumzungumzia Bwana Mtume Muhammad SAW akiwa ni nabii na mjumbe wa Allah, Dakta Martin Lings anaanza kwa kuashiria utabiri uliotolewa kuhusu kudhihiri nabii huyo wa rehma kupitia kisa maarufu cha mtawa wa Kikristo Buhaira na kuandika hivi:"Wakati Buhaira alipoona alama za utume kwa Muhammad alimwambia Abu Talib: mrejeshe kwenu mwanao huyu na umlinde na Mayahudi. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa kama watamwona na wakayajua yale ninayojua mimi kuhusu yeye watamfanyia vitimbi tu. Kuna mambo makubwa yanayomsubiri mwana wa nduguyo huyu".

Katika sehemu nyengine ya kitabu chake, Martin Lings anazungumzia aya za mwanzoni za Qur'ani alizoteremshiwa Bwana Mtume na kusimulia kisa cha Waraqah bin Naufal, alim wa Kinasara aliyempa hakikisho Bibi Khadija kwamba mumewe Muhammad ameteremshiwa wahyi na hakuna shaka yoyote kuwa yeye ni Mtume na mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Kisha yeye Waraqa akaonana na Mtume na kumpa bishara ya utume na akamwambia:"Watakuja kukuita mwongo na wataamiliana na wewe kwa ubaya. Watakufukuza na kupigana vita nawe. Kama nitakuwa hai na kuishuhudia siku hiyo, Mwenyezi Mungu anajua kuwa nitaitetea dini yako". Kisha akainama na kukibusu kipaji cha Muhammad".

Katika kitabu chake hicho kiitwacho "Muhammad: Maisha Yake Kwa Mujibu wa Marejeo ya Kale", Martin Lings anaitaja shakhsia ya Bwana Mtume Muhammad SAW yenyewe kama moja ya sababu za watu kuiamini na kuifuata dini tukufu aliyokuja nayo ya Uislamu. Analielezea hilo kwa kusema: "Muhammad alikuwa mtu ambaye watu wote walikuwa wakijua kwamba amepambika kwa haki na ukweli na hivyo ni muhali kwa yeye kuwa na nia ya kumhadaa mtu. Na vilevile alikuwa na akili na hekima kiasi kwamba hangeweza kuwa mtu wa kutaka kuikweza nafsi yake.  Ujumbe wake ulibeba maonyo na bishara. Maonyo yaliwashurutisha na kuwabidiisha watu kufanya amali, na bishara zilizijaza nyoyo zao furaha.

Said Tehrani Nasab, amekitarjumu kwa lugha ya Kifarsi kitabu hicho kiitwacho "Muhammad: His Life Based on the Earliest Sources", yeye anamzungumzia mwandishi wa kitabu hicho yaani Martin Lings au Abu Bakr Siraj Ad-Din kwa kusema:" Lings alivutiwa na Mtume wa Uislamu baada ya kubaini ukweli, na alitumia muda mwingi kumuarifisha shakhsia huyu adhimu. Katika siku za mwishoni mwa msimu wa joto wa mwaka 2004, takribani mwaka mmoja kabla ya kufariki kwake, nilikwenda kuonana naye Lings kwenye nyumba yake ya kuvutia na isiyo na makuu. Alikuwa akimzungumzia Mtume wa Allah kwa heshima na taadhima kubwa akisema kuwa mtukufu huyo ni hidaya adhimu ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Kilichoonekana ndani ya nyumba yake ni jina tukufu la Allah tu lililoandikwa ukutani pamoja na msala. Ni kama kwamba chumba hicho ulikuwa msikiti wa nyumbani kwake aliokuwa akisali ndani yake mara tano kwa siku, na huenda  ndimo alimokuwa akiandikia vitabu vyake. Alaa kulli hal ilikuwa ni wazi kwamba kutokana na kumfuata kiongozi mkubwa wa Uislamu, maisha yake yalikuwa yakienda mithili ya saa inayofanya kazi kulingana na ratiba makini na yenye nidhamu na mpangilio maalumu."

Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu kwa jumla hili kinaishia hapa, basi hadi tutakapokutana tena siku nyingine na katika kipindi kingine nakuageni huku nikikutakieni kila la kheri maishani.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …