Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 15 Aprili 2013 13:45

Nabii wa Rehma (13)

Nabii wa Rehma (13)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya 13 ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Nabii Muhammad (SAW) ni shakhsia mkubwa kabisa katika historia ya Uislamu na muongozaji wa wanadamu kuelekea kwenye mwanga na nuru ya uongofu. Aliutoa ulimwengu kwenye giza la ushenzi, ujinga na khurafa na kuuingiza kwenye nuru ya tauhidi, imani, upendo na elimu. Kwa sababu hiyo maisha ya shakhsia huyu mkubwa yamekuwa yakifanyiwa utafiti na uhakiki wa kitaalamu kwa muda wa karne kadhaa. Hata hivyo baadhi ya wapinzani wa Uislamu wamejaribu kwa kila njia kulitia doa jina lenye kung'ara la Mtume adhimu wa Uislamu Nabii Muhammad SAW. Katika karne ya 16 hadi 18 uhakiki uliofanywa barani Ulaya kuhusu Mtume wa Uislamu ulichanganyika na chuki na uadui. Mnamo karne ya 18 uhakiki uliofanywa na watu wa Ulaya ulianza kuzingatia uhakika na uhalisia wa mambo, na mtazamo huo ukazidi kuwa wa kiinsafu zaidi katika utafiti na uhakiki uliofanywa katika karne ya 19 kuhusu nabii wa rehma Muhammad SAW.

Si mtu mmoja au tapo maalumu tu la watu waliofanya utafiti na uhakiki kuhusu maisha ya Mtume wa Uislamu na dini hiyo tukufu aliyokuja nayo. Kwa maneno mengine ni kwamba si watafiti na waandishi pekee bali hata washairi na wanafasihi wa Ulaya pia walivutiwa na suala hilo. Kama ambavyo Alphonse de Lamartine, mwandishi, mwanasiasa na mshairi wa Kifaransa aliamua kuzungumzia maisha ya Mtume wa Uislamu katika faslu ya moja ya vitabu vyake alichoandika mwaka 1854.

Victor Marie Hugo, mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kifaransa wa karne ya 19 ni mtu anayefahamika na wengi kwa kitabu chake maarufu cha The Miserables yenye maana ya Mafakiri au walala hoi. Lakini ni watu wachache wanaojua kwamba mwanafasihi huyo mkubwa wa Kifaransa ameandika mashairi pia chini ya anuani ya "Mwaka wa Tisa wa Hijra" ya kumsifu Nabii wa rehma Muhammad SAW.

Victor Hugo ni mtu aliyekuwa na uelewa wa historia na utamaduni wa Uislamu. Ustadi na umahiri unaoonekana katika kitabu cha mashairi cha "Mwaka wa Tisa wa Hijra" umetokana na utafiti na uhakiki makini aliofanya Victor Hugo kuhusu maisha ya Mtume wa Uislamu. Lugha ya taadhima na mtazamo wa Hugo katika kubainisha sifa za Mtume Mtukufu na kusimulia lahadha ya mwisho ya uhai wake inadhihirisha heshima kubwa ambayo mwandishi huyo mashuhuri wa Kifaransa alikuwa akimpa Bwana Mtume Muhammad SAW na ujumbe wa mbinguni wa Uislamu aliokuja nao. Kitabu kiitwacho "Mwaka wa Tisa wa Hijra" ni athari ya kudumu ya Victor Hugo kuhusu Mtume wa Uislamu ambapo katika kipindi chetu cha leo tutajaribu kudondoa baadhi ya beti za mashairi hayo.

Katika kitabu hicho Hugo amejaribu kuonyesha taswira takatifu na ya kimaanawi ya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa kuifuta taswira isiyo sahihi iliyoonyeshwa kwa muda wa miaka mingi na waandishi wa Magharibi wenye vinyongo au wasio na uelewa kuhusu nabii huyo wa rehma na badala yake kuonyesha taswira halisi na sahihi ya Mtume wa Uislamu.

Tabia ya murua, maneno latifu, hulka njema, huruma na upendo ni sifa wadhiha zilizopamba shakhsia ya Mtume mtukufu wa Uislamu. Sifa hizi zilishuhudiwa katika mwenendo na matendo yake yote. Maneno yake yalikuwa na mvutio na ulimi wake ulikuwa na lugha tamu ya kuburudisha moyo. Uso wake wenye nuru na uliojaa tabasamu ilikuwa ni hidaya aliyotunukiwa na Mola. Kuishi maisha ya chini na kuchanganyika na watu zilikuwa miongoni mwa sifa tukufu za Mtume huyo wa Allah. Victor Hugo anazielezea sifa hizo za nabii wa rehma katika lugha ya mashairi kwa kusema:

Kwa adhama na uungwana wake hakumlaumu mtu,

Alimjibu kwa huruma na upendo kila aliyemsalimu,

Alikula kidogo na hata kukaa na njaa kwa kufunga jiwe tumboni,

Alikama maziwa ya kondoo wake kwa mikono yake mwenyewe,

Alikuwa ni mwenye kukaa chini kama walivyo wanyonge

Na akizitia viraka nguo na libasi zake.

Matunda ya kubaathiwa na kupewa utume nabii wa rehma Muhammad SAW na ya juhudi za ikhlasi alizofanya Mtume huyo wa Allah kwa muda wote wa miaka 23 ya Utume wake ilikuwa ni kuenea tauhidi na imani ya Mungu Mmoja duniani. Kwa kuasisi jamii safi iliyotakasika na ubaguzi na upendeleo aliwatunukia wanadamu hidaya ya huruma na upendo na kuwaonyesha njia ya saada kupitia mafunzo hai ya Qur'ani. Victor Hugo analielezea hili kwa kusema, aliisoma kila upande Qur'ani ambayo aliwaletea watu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na akasema:
Enyi watu,

Ni Mwenyezi Mungu tu anayebaki na aliye Pweke,

Hakuna Mungu ghairi ya Mungu Mmoja.

Enyi watu, kama si irada ya Mwenyezi Mungu, mimi pia ningekuwa mjinga na nisiyejua kitu,

Tambueni kuwa asipofuata mwanadamu njia ya Mwenyezi Mungu, huwa ni hayawani duni na mwenye kuchukiza.

Wapenzi wasikilizaji kutokana na shauku aliyokuwa nayo Victor Hugo ya kumuenzi Bwana Mtume Muhammad SAW na kuakisi hayo kwa sura ya fasihi na hasa mashairi aliamua kutunga beti latifu na za kuhuzunisha kuzungumzia pia lahadha za mwishoni mwa uhai wa mtukufu huyo. Hugo analielezea tukio hilo kwa kusema, hatimaye Mtume (SAW) aliikabidhi bendera iliyokuwa ikipepea ya Uislamu kwa mbebaji wake Ali (AS), na hadi dakika za mwisho wa uhai wake sura yake ilikuwa iking'aa na kumeremeta kama ilivyokuwa siku ya kuzaliwa kwake. Victor Hugo anausimulia wasia wa mwisho wa Bwana Mtume kwa umati wake katika sura ya shairi akisema:

Hivi sasa ni mimi,

Baada ya miaka kadhaa ya jihadi ninakaribia kuelekea kaburini,

Mbele yangu ni Mwenyezi Mungu na nyuma yangu ni dunia yenu nyinyi,

Ninajua kwamba baadhi yenu mmeteseka sana katika kuwa pamoja nami,

Lakini itakuwa furaha mtakapoyaona mapambazuko,

Kuweni wakweli katika imani na usiku kesheni,

Mcheni na mwabuduni Mwenyezi Mungu,

Na tahadharini kubaki nyuma ya ukuta,

Utenganishao Pepo na ukingo wa Jahanamu,

Hakuna yeyote aliyetakasika na makosa,

Lakini jitahidini msijistahikishie adhabu.

Naam wapenzi wasikilizaji, maneno haya ya Victor Hugo ndiyo yanayotukamilishia sehemu hii ya 13 ya kipindi hiki cha "Yaliyosemwa na Wenye Hekima Kuhusu Nabii wa Rehma". Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola nakuageni kutoka hapa studio huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …