Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 08 Aprili 2013 17:42

Nabii wa Rehma (12)

Nabii wa Rehma (12)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo. Nakukaribisheni kwa furaha na moyo mkunjufu kujiunga nami katika sehemu hii ya 12 ya kipindi hiki  kinachodondoa yale yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Nakutafadhalisheni muendelee kuwa nami hadi mwisho wa kipindi chetu kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Baada ya kudhihiri Uislamu katika ardhi ya Hijazi na kuandaliwa watu waliotaalamika katika chuo cha Bwana Mtume SAW nuru ya Uislamu iling'ara na mwanga wake kutanda hadi nje ya mipaka ya kijiografia ya Bara Arabu na kupelekea kujengeka utamaduni na ustaarabu mpya duniani. Ustaarabu huo uliathiri staarabu nyengine zote, na baada ya muda zikaanza zile zilizojulikana kama "Zama za dhahabu za Ustaarabu wa Kiislamu".

Wanafikra mbalimbali wameuhakiki ustaarabu wa Kiislamu katika pande tofauti, na kuna vitabu na makala kadha wa kadha zilizoandikwa kuhusiana na maudhui hiyo. Amma kile walichoghafilika nacho wanafikra hao na ambacho hawakukifanyia insafu ni nafasi kuu na isiyo na mbadala ya Bwana Mtume Muhammad SAW katika kuweka msingi na kuasisi jengo la ustaarabu huo adhimu. Mche wa mti huo imara na uliostawi ulipandwa na mikono mitukufu ya nabii huyo wa rehma, na shina na mizizi yake ikajizatiti na kuamirika zaidi kutokana na hijra ya mtukufu huyo ya kuhama Makka na kuhamia Madina. Nafasi ya Bwana Mtume katika kuasisi ustaarabu wa Kiislamu na kustawisha ustaarabu wa wanadamu kwa ujumla haijaweza kufichika mbele ya macho ya Will James Durant, mwanahistoria, mwandishi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kimarekani. Katika kitabu chake maarufu kiitwacho:" The Story of Civilization" yenye maana "Kisa cha Ustaarabu", Will Durant ambaye alizaliwa mwaka 1885 na kuaga dunia mwaka 1981 amezungumzia mchango wa Bwana Mtume katika kuleta amani na utulivu, mshikamano wa kitaifa, akhlaqi, umoja na ustawi wa jamii, ambazo ni miongoni mwa sababu athirifu za kuchipua na kustawi kwa staarabu.

Will Durant anaamini kuwa kuna mambo kadhaa yanayochangia kuchipuka na kustawi kwa ustaarabu wowote ule. Katika kuizungumzia nukta hiyo ameandika hivi:" Kudhihiri kwa ustaarabu kunayumkinika pale machafuko na hali ya mchafukoge inapotoweka katika jamii. Kwa sababu ni pale tu hofu inapotoweka ndipo hisia za udadisi na za ugunduzi na ubunifu zinapofanya kazi ndani ya nafsi ya mwanadamu. Na hapo ndipo yanapojitokeza mazingira ya mtu kuwa na hamu ya kujifunza elimu na maarifa na kustawisha hali yake ya maisha. Will Durant anasema, Mtume alikuwa mtu aliyeandaa mazingira ya kupatikana hali hiyo. Muhammad alifanya jitihada za kufikisha kwenye daraja ya juu kabisa kiwango cha maarifa na akhlaqi za kaumu ya watu waliokuwa wametingwa na giza la ushenzi kutokana na athari za hali ya hewa ya joto kali na ukavu wa ardhi ya jangwa. Yeye alifanikiwa katika suala hilo, na mafanikio hayo yalikuwa makubwa zaidi kuliko yale waliyopata warekebishaji wote wa jamii duniani. Ghairi yake yeye ni watu wachache ambao wameweza kuyafikia matarajio yao yote katika njia ya dini. Will Durant anaendelea kusema:"Kutoka ndani ya makabila ya waabudu masanamu na yaliyotawanyika kwenye jangwa, Muhammad alijenga umma mmoja ulioungana na uliotukuka na wenye hadhi ya juu zaidi kuliko wafuasi wa dini ya Uyahudi, dini ya Ukristo na dini ya kale ya Bara Arabu. Yeye alileta dini nyepesi, ya wazi na imara... kiasi kwamba katika muda wa chini ya karne moja ilijenga utawala mkubwa na adhimu. Katika zama zetu, dini yake ni nguvu moja muhimu yenye ushawishi katika upande wa nusu moja ya dunia." Kwa maana hiyo, Will Durant anasema, "kama tutapima kiwango cha taathira iliyoachwa na mtu huyu mkubwa kwa watu, tunalazimika kusema kuwa Nabii Muhammad (SAW) ni mmoja wa watu wakubwa zaidi katika historia ya mwandamu."

Katika kitabu chake cha "Kisa cha Ustaarabu", mwanahistoria huyo wa Kimarekani amezungumzia pia kasi ya ukuaji wa elimu kutokana na athari ya mafundisho ya Mtume wa Uislamu. Kuhusiana na nukta hiyo anasema:"Ustaarabu wa Uislamu ulifikia kwenye kilele cha ustawi na maendeleo katika anuai za elimu na fani za ufundi kuanzia mwaka 81 hadi 598 Hijria sawa na mwaka 700 hadi 1200 Miladia. Elimu za amali na tajiriba zikiwemo za utabibu, kemia, fizikia, jiolojia, biolojia na botania zilifikia kilele cha ustawi, ambapo wanasayansi na wavumbuzi wakubwa kabisa walioenea katika Ulimwengu wa Kiislamu walikuwa wakisomesha, wakiandika na kufanya utafiti katika elimu hizo. Wao walifanya kazi ya kuzifikisha na kuzifunza elimu hizo kuu za msingi kwa majirani na watafutaji wa elimu katika nchi mbalimbali... Will Durant anaendelea kuandika:" Katika kipindi cha kung'ara kwa Uislamu ulimwengu wa Magharibi ulikuwa umezongwa na fikra za Zama za Kati (Middle Ages), ushenzi na mgando wa kifikra wa Kanisa, na kuwa mbali kikamilifu na utumiaji akili na utaalamu wa ufundi. Na kinyume chake katika Ulimwengu wa Kiislamu kulikuwepo wataalamu wa kupigiwa mfano kama vile Ibn Sinaa, Kharazmi, Farabi, Muhammad bin Zakariyya Razi, Abu Raihan Biruni, Hakim Omar Khayyam, Ibn Khaldun na wengineo ambao walikuwa wakishughulika na uenezaji elimu duniani bila ya mpaka wala kizuizi chochote."

Katika kuzungumzia shakhsia ya Mtume wa Uislamu, Will Durant ambaye ni msomi mwenye kutajika katika ulimwengu wa Magharibi ameandika hivi:"Muhammad alitokana na ukoo mashuhuri na mtukufu... neno Muhammad lina maana ya msifiwa. Kuna mfungamano wa kimaanawi baina ya neno hili na baadhi ya ibara zilizomo kwenye Kitabu Kitakatifu ambao unaweza kuwa ni bishara iliyotolewa na Kitabu Kitakatifu juu ya kudhihiri kwa Muhammad...Inavyoonekana, hakuna mtu yeyote aliyefikiria kumfunza kusoma na kuandika, lakini pamoja na hayo yeye aliyatambua mambo kwa umakini zaidi kuliko watu waliosoma. Wakati ule fani ya kusoma na kuandika haikuwa na umuhimu kwa mtazamo wa Waarabu. Na ndiyo maana kati ya makabila ya Makureishi watu waliokuwa wakijua kusoma na kuandika hawakuzidi 17. Pamoja na hayo kitabu maarufu zaidi na chenye balagha ya juu zaidi cha Kiarabu kilisomwa kupitia kwenye kinywa cha Mtume. Yeye alionyesha umahiri wa kuelewa masuala yanayohusu maisha ya watu kiasi kwamba hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfikia katika suala hilo. Ndani ya kitabu chake cha Qur'ani, Will Durant anasema, sheria na akhlaqi zina uzito sawa, ndani ya Qur'ani mwenendo wa kidini unajumuisha pia mwenendo wa masuala ya kidunia, na mambo yake yote yaliteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Muhammad kwa njia ya wahyi. Ndani ya Qurani, kuna taratibu zinazohusu adabu, afya, ndoa na talaka, namna ya kuamiliana na watoto, watumwa na wanyama, biashara, siasa, mikopo na riba, mikataba na wasia, masuala ya ufundi, masuala ya mali, faini na adhabu, vita na suluhu n.k".

Wapenzi wasikilizaji, moja ya sifa tukufu za Bwana Mtume Muhammad SAW ilikuwa ni kuwajali na kuwahurumia masikini na mayatima. Alielekeza hima na bidii zake zote katika kukidhi mahitaji ya watu hao. Kwa kutilia mkazo sifa hii ya Bwana Mtume, Will Durant ameandika:" Katika historia zote za watu waleta marekebsho katika jamii hatuwezi kumpata mtu aliyetoza kodi matajiri kwa manufaa ya mafakiri kama alivyofanya Muhammad. Muhammad (SAW) alikuwa akiwashajiisha watu kutenga sehemu ya mali zao kwa ajili ya mafakiri na wahitaji. Mtume alikuwa alikuwa akitumia muda mwingi kufanya safari za kuwatembelea watu wanyonge, kukaa na kuzungumza nao."

Kwa kumalizia, Will Durant anakiri kuhusu ukweli anaoueleza kama ifuatavyo:" Kwa kutoa wito wa kulingania Uislamu, Muhammad (SAW) aliweza kuleta mapinduzi mapya ya kiroho katika maisha ya mamilioni ya watu. Na watu hao waliisikia sauti murua ya Muhammad na kuikubali kwa roho na nyoyo zao".

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kukomea hapa kwa leo na kukuageni hadi juma lijalo inshallah tutakapokutana tena katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …