Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 23 Machi 2013 09:23

Nabii wa Rehma (10) + Sauti

Nabii wa Rehma (10) + Sauti

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya 10 ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ninakifungua na kukipamba kipindi chetu cha leo kwa dua ya Imam Sajjad AS aliyoomba kuhusu shakhsia ya Bwana Mtume SAW. Katika dua hiyo iliyomo kwenye kitabu cha As Sahifatus Sajjadiyyah, Imam Sajjad anasema:" Na hamdu ni za Allah ambaye ametufanyia fadhila ambayo hazikupata umma zilizopita ya kutuletea Mtume wake Muhammad SAW. Ewe Mola mshushie rehma na amani Muhammad mwaminiwa wako wa Wahyi wako na mteule kati ya viumbe wako na aliyejitolea zaidi kwako kati ya waja wako. Imamu wa rehma na kiongozi wa kheri na ufunguo wa baraka, aliyeitaabisha nafsi yake kutekeleza amri zako na akavumilia mateso mengi kwa ajili ya njia yako...Na akahajiri kuelekea mji wa ugenini na mahala pa mbali na watu wake na jamaa zake... Ewe Mola Muinue kutokana na tabu alizopata kwa ajili yako afikie daraja ya juu kabisa ya Pepo yako, ambayo hatoweza kuwa sawa naye katika cheo wala hadhi si malaika yeyote aliyekurubishwa wala nabii yeyote aliyetumwa."

Haki na ukweli wapenzi wasikilizaji ni mithili ya johari safi na yenye kung'ara, kiasi kwamba hata kama batili itajaribu kuufifiliza mng'aro wake kwa muda lakini mwishowe kiwingu cha batili hutoweka na nuru ya haki hudhihirika mbele ya watu wote. Ni kwa sababu hiyo wasomi wenye busara na wanafikra wenye insafu wanahisi kuwa wana wajibu wa kuitambua haki na kuibainisha kwa wengine. Kuijulisha shakhsia ya Mtume wa Uislamu na taathira alizoacha mtukufu huyo kwa ulimwengu ni miongoni mwa ukweli na uhakika usioweza kukanushika."Muhammad: A Biography of the Prophet" yenye maana ya "Muhammad: Wasifu wa Mtume" ni jina la kitabu kilichoandikwa na bi Karen Armstrong. Katika sehemu ya mbele ya jalada la kitabu hicho imeandikwa hivi:" Kitabu cha mwaka kilichouzwa zaidi nchini Marekani baada ya tukio la Septemba 11". Amma sehemu ya nyuma ya jalada la kitabu hicho kuna maelezo kuhusu bi Armstrong mwenyewe yasemayo:" Bi Karen Armstrong, ni miongoni mwa wanafikra wakubwa wa masuala ya dini katika ulimwengu wa wazungumzaji wa lugha ya Kiingereza ambaye alipitisha miaka saba ya umri wake akiwa katika vazi la utawa wa Kikatoliki....Kilichomshawishi zaidi kuandika kitabu hiki ni kuutetea Uislamu na kubainisha fikra za Wakristo wa Magharibi kuhusu shakhsia ya Mtume wa Uislamu; shakhsia ambayo imekuwa na shubha na utata mkubwa katika ulimwengu wa Magharibi  baada ya kuchapishwa kitabu cha Aya za Shetani kilichoandikwa na Salman Rushdie. Bi Karen Armstrong, mwandishi na mwanakademia raia wa Uingereza aliyezaliwa mwaka 1944 ameandika katika kitabu chake hicho kama ninavyonukuu:" Mimi nimeandika kitabu hiki kutokana na wasiwasi wa kuchelea taswira itakayotolewa juu ya Muhammad (SAW) kwa watu wa Magharibi isije ikawa ni ile tu iliyotolewa na kitabu cha Salman Rushdie. Na sababu, nimebaini kuwa Muhammad ni mmoja wa shakhsia adimu na wa kipekee wa historia ya wanadamu. Maisha ya Mtume wa Uislamu yalitokana na misingi ya Wahyi na yameratibiwa ili kutekeleza maamrisho halisi ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kujenga jamii ya watu. Muhammad (SAW) alipambana kwa lengo la kuutokomeza ujahiliya na akaweza kuiunganisha pamoja Bara Arabu iliyokuwa imegawika vipande vipande, suala ambalo hawakuweza kuliamini wengi katika zama zile."

"Muhammad: Wasifu wa Mtume" ni kitabu chenye faslu kumi. Katika kila faslu ya kitabu hicho mwandishi amejitahidi kutoa sherhe na ufafanuzi wa sehemu mojawapo ya maisha yaliyojaa baraka na umaanawi ya Bwana Mtume kwa kutegemea ukweli wa historia na kuondoa shubha na utata uliozushwa kuhusiana na mtukufu huyo. Kwa mtazamo wa mwandishi wa kitabu hicho uongozi wa Nabii Muhammad SAW katika kueneza utamaduni wa tauhidi na kusimamisha uadilifu duniani ulikuwa na taathira na mvuto mkubwa kiasi cha kuenea katika ardhi ya Hijazi ndani ya kipindi kifupi cha utawala wake. Yeye aliwafikishia wito wa dini yake viongozi wa dunia waliokuwa na nguvu kubwa zaidi. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Mtume Muhammad aliweza kuasisi utawala ambao baada ya kupita miaka thelathini ulienea hadi kwenye maeneo muhimu ya dunia. Katika faslu nyengine ya kitabu chake, Bi Karen Armstrong, anaashiria tukio la Fat-hu ya Makka na kueleza kuwa kupenda amani ni sifa kuu ya dini ya Uislamu. Analieleza hilo kwa kuandika hivi:"Kuepusha makabiliano ya kishenzi kati ya kaumu ndiko alikokupa umuhimu zaidi Mtume kuliko kitu kingine; kwa sababu neno Uislamu lenye maana ya kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu chimbuko lake limetokana na "salam" yenye maana ya suluhu na amani. Mtume Muhammad alikuwa mtu wa jihadi, lakini zaidi ya hivyo alikuwa mpenda amani wa kweli; yeye aliziweka rehani roho za wafuasi wake wa karibu katika kadhia ya suluhu na watu wa Makka ili umoja huo uweze kupatikana bila ya umwagaji damu. Badala ya umwagaji damu, Muhammad alitaka zaidi mazungumzo na suluhu".

Wapenzi wasikilizaji wanafikra wenye insafu wanaitakidi kuwa dunia ya leo inahitajia zaidi shakhsia kama Mtume wa Uislamu kuliko wakati mwengine wowote ule. Miongozo ya Mtume wa Uislamu  kwa ajili ya wanadamu wa leo ina ujumbe wa kujenga uelewa na kuwa na uono wa mbali, kutetea uadilifu, akhlaqi njema na maadili sahihi, heshima ya utu, huruma na upendo, na amani na kuwapenda watu. Yeye ni mhimili mkuu wa huba na upendo kwa ajili ya wanadamu. Kwa mtazamo wa Bi Karen Armstrong, kuna ulazima mkubwa wa kuwa na uelewa wa kisa cha maisha ya shakhsia kama huyu katika kipindi hiki nyeti cha historia. Armstrong anaitakidi kuwa haifai kuwaruhusu watu vichwa ngumu na wenye taasubi walitumie vibaya kwa maslahi yao suala hilo kwa kupotosha historia ya maisha ya Mtume. Anasema, katika dunia hii yenye kubadilika mtu wa Magharibi anapaswa kujifunza masuala muhimu zaidi kwa ajili ya muongozo wake kutokana na historia ya maisha ya mtukufu huyo. Katika sehemu nyengine ya kitabu chake Bi Karen Armstrong ameandika hivi:"Moja ya tatizo la Magharibi ni kwamba kwa muda wa karne kadhaa imekuwa ikimtambulisha Muhammad (SAW) kuwa ni mtu mpinzani wa ustaarabu, hali ya kuwa sisi tulipaswa kumwangalia yeye kama mtu mwenye moyo uliotukuka mno, mtu mkubwa ambaye alifanya jitihada kubwa kwa ajili ya watu yake ya kuleta suluhu, amani na uadilifu. Kama sisi tutamwangalia Muhammad kwa mtazamo huo kama tunavyowaona shakhsia wakubwa wa kihistoria tutaweza kirahisi kufikia kwenye imani kwamba yeye ndiye shakhsia aliyeacha taathira kubwa zaidi katika historia yote ya wanadamu na kuna udharura na ulazima wa kumjua na kumtambua.

Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu kwa jumla hili kinaishia hapa, basi hadi tutakapokutana tena siku nyingine na katika kipindi kingine nakuageni huku nikikutakieni kila la kheri maishani.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …